07-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Fadhila Za Ahlul-Bayt

 

Fadhila Za Ahlul-Bayt

 

Tunaweza kugawa fadhila za Ahlul Bayt katika mafungu mawili:

1.     Fadhila za ujumla

2.     Fadhila makhsusi

 

 

Kwanza Fadhila za ujumla

Fadhila za ujumla mfano wa hadithi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema:

 

{ وأهل بيتي، أذكركم الله في أهل بيتي، أذكركم الله في أهل بيتي }.

 

«Na watu wa nyumba yangu. Nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu, Nakukumbusheni Allaah juu ya watu wa nyumba yangu.» Muslim

 

Na fadhila zilizotajwa katika Suratul Ahzaab:

 

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيراً

 

"Hakika Allaah anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba (ya Mtume), na kukusafisheni barabara."

 

Ndani yake fadhila hizi wanaingia wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa sababu wao ndio waliokusudiwa, na pia wanaingia ‘Aliy na Bibi Faatwimah na Al-Hasan na Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum) kupitia hadithi ya Al-Kisaa.

Fadhila za ujumla zinapatikana pia katika kutoa shahada ndani ya Swalah wakati wa kusoma Tahiyatu, tunaposema:

 

اللهم صل على محمد وعلى آل محمد

 

"Mola wangu mswalie Muhammad na Aali yake Muhammad”

 

Na yote haya yanatokana na fadhila zao na daraja yao mbele ya Allaah.

 

Fadhila Makhsusi

Wafuatao ni baadhi ya watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na hawa ni Maimamu kumi na mbili wa Shia:

 

1. ‘Aliy bin Abi Twaalib

2. Al-Hasan

3. Al-Husayn

4. ‘Aliy bin Al-Husayn (Zaynul ‘Abidiyn)

5. Muhammad bin ‘Aliy bin Al-Husayn (Al-Baaqir)

6. Ja’afar Asw-Swaadiq

7. Musa Al-Kaadhwim

8. ‘Aliy Ar-Ridhwaa

9. Muhammad Al-Jawwaad

10. ‘Aliy Al-Haadiy

11. Al-Hasan Al-Askariy

12. Muhammad (Imamu wa kumi na mbili wanayemsubiri)

 

Hawa tunaweza kuwagawa makundi manne.

1-    Kundi la mwanzo ni Masahaba (waliomuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)), nao ni ‘Aliy na Al-Hasan na Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum).

2-    Kundi la pili ni Maulamaa wachaji Allaah miongoni mwa Maulamaa wa Ahlus Sunnah wal Jama’ah nao ni:

 

1- ‘Aliy bin Al-Husayn

2- Muhammad Al-Baaqir

3- Ja’afar Asw-Swaadiq

4- Muusa Al-Kaadhim

5- ‘Aliy Ar-Ridhwa

6- Muhammad Al-Jawwaad

 

3-    Kundi la tatu; hawa ni wachaji Allaah lakini si katika Maulamaa na inawatosha fahari ya kuwa wanatoka katika nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na wanayo haki ya kwenda penye kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kusema:

‘Assalaam ‘alayka ewe baba yangu.’

Na hawa ni: ‘Aliy Al-Haadiy na Al-Hasan Al-Askariy.

4-    Sehemu ya nne ni mtu asiyezaliwa wanayemsubiri, naye ni Muhammad bin Al-Hasan.

 

 

‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

Wa mwanzo wao ni ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni mtoto wa ‘ami yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na mume wa Bibi wa mabibi wa Peponi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) binti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni Khalifa wa nne muongofu, na ni katika wale kumi waliobashiriwa kuingia Peponi.

Ndani ya Al-Bukhaariy na Muslim ipo hadithi kutoka kwa Abul ‘Abbaas Sahl bin Sa’ad As-Sa’idiy (Radhiya Allaahu ‘anhu), aliyesema kuwa siku ya vita vya Khaybar, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:

 

(لأعطين هذه الراية غدا رجلا يفتح الله على يديه، يحب الله ورسوله ويحبه الله ورسوله)

 

"Nitampa bendera hii kesho, mtu ambaye atatupa ushindi Allaah kwa mikono yake. (Mtu huyo) Anampenda Allaah na Mtume Wake na anapendwa na Allaah na Mtume Wake".

 

Anaendelea kusema Sahl (Radhiya Allaahu ‘anhu):

 

"Usiku kucha watu walikuwa wakiwaza wakitaka kujua ni nani huyo mwenye kupendwa na Allaah na Mtume Wake atakayepewa bendera hiyo. Asubuhi yake watu wote wakaamkia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kila mmoja akitamani apewe yeye bendera siku hiyo".

Baada ya watu kujikusanya mbele yake, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akauliza:

"Yuwapi ‘Aliy bin Abi Twaalib?...."

Al-Bukhaariy na Muslim

 

Na akasema pia (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu):

 

لا يحبك إلا مؤمن، ولا يبغضك إلا منافق

 

«Hakupendi isipokuwa Muumini na hakuchukii isipokuwa mnafiki »

 

Na sisi Wallahi tunampenda na kumuenzi na kumheshimu yeye na mkewe na watoto wake wote (Radhiya Allaahu ‘anhum). Hadithi zake zimejaa ndani ya vitabu vyetu. Hekima yake tunaitumia na tunawafunza watoto wetu. Mashairi yake yaliyojaa mafunzo ya kheri na busara tunayasoma na kuyarudia na tunamfunza kila mmoja wetu.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema pia:

 

{أما ترضى أن تكون مني بمنزلة هارون من موسى} وزاد مسلم: { إلا أنه لا نبي بعدي}

Al-Bukhaariy

«Hutoridhika ukiwa wewe kwangu upo katika daraja ya Haaruun kwa Muusa» na Muslim akaongeza: «Isipokuwa hapana Mtume baada yangu».

 

Hadithi zote hizi na nyingi nyingine zimo ndani ya vitabu vya Ahlus Sunnah zikituhakikishia kuwa hatuna uzito wowote kwetu katika kuzitaja au kuziandika ndani ya vitabu vyetu na hata kuzisema hadharani, bali ni fahari kwetu kufanya hivyo, kwa sababu hawa ni watu wa nyumba ya Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

 

Faatwimah (Radhiya Llahu ‘anha)

 

Bibi Faatwimah (Radhiya Llahu ‘anha) binti yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Kipenzi chake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Manukato yake mazuri aliyesema juu yake :

 

{إن فاطمة بضعة مني يؤذيني ما آذاها}

 

«Hakika Faatwimah ni sehemu inayotokana na mimi kinaniudhi kinachomuudhi» Muslim

 

Na akasema kumuambia Faatwimah:

 

{أما ترضي أن تكوني سيدة نساء المؤمنين، أو سيدة نساء هذه الأمة}

 

«Huridhiki ukiwa wewe ni Bibi wa wanawake waumini, au Bibi wa wanawake wa umma huu»

 

Na katika Al-Bukhaariy:

 

فاطمة سيدة نساء أهل الجنة

 

« Faatwimah ni Bibi wa wanawake wa Peponi»

 

 

Al-Hasan na Al-Husayn

 

Tunawaheshimu na kuwapenda pia Al-Hasan na Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum), na ndani ya vitabu vya Ahlus Sunnah utakuta maelezo mengi juu ya wajukuu hawa wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliyokuwa akitamka mbele ya Masahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). Alikuwa akisema:

 

اللهم إني أحبهما فأحبهما

 

‘Mola wangu kwa hakika mimi ninawapenda na Wewe wapende’

At-Tirmidhiy

 

Na akasema:

 

الحسن والحسين سيدا شباب أهل الجنة

 

‘Al-Hasan na Al-Husayn ni mabwana wa vijana wa Peponi’

At-Tirmidhiy na Ahmad na Al-Haakim na wengine

 

 

Al-‘Abbaas bin ‘Abdil-Muttwalib (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

Huyu ni ‘ami yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliyesema juu yake:

 

عم الرجل صنو أبيه

 

‘Ami yake mtu ni sawa na baba yake

At-Tirmidhiy

 

 

 

Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma)

 

Huyu ni mtoto wa ‘ami yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliyemuombea dua nzuri aliposema:

 

{اللهم علمه التأويل وفقهه في الدين}

 

“Mola wangu mpe elimu ya kujua uhakika wa mambo na mjaalie awe na fiq-hi katika dini."

Ahmad

 

 

‘Aliy Zaynul ‘Aabidiyn (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

Huyu ni ‘Aliy bin Al-Husayn bin ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhum) ambaye amesema Imam Az-Zuhry juu yake:

 

‘Sijapata kumuona mtu kutoka kabila la Quraysh aliye bora kupita yeye.’

 

Na alisema Sa’iyd bin Musayib:

 

‘Sijapata kumuona mcha Mungu kupita huyu.’

  

 

Muhammad bin ‘Aliy bin Al-Husayn ‘Al Baaqir’ (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

Amesema juu yake Abu Na’iym:

 

‘Alikuwa mtu wa kuaminika, mwingi wa elimu na hadithi.’

 

 

Ja’afar bin Muhammad (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

Huyu ndiye Ja’afar Asw-Swaadiq bin Muhammad Al-Baaqir ambaye Imam Abu Hanifa alisema juu yake:

 

‘Sijapata kuona mtu mwenye elimu ya fiq-hi kupita Ja’afar bin Muhammad.’

 

Amesema pia juu yake Ibni Hibbaan :

 

‘Mwenye kuaminika asiye na mfano.’

 

Amesema Imam Adh-Dhahabiy :

 

« Imam Asw-Swaadiq ni Sheikh katika Masheikh wa Kikureshi anayetokana na ukoo wa Bani Hashim na ni miongoni mwa Maulamaa wao.»

 

 

Muusa bin Ja’afar ‘Al-Kaadhwim’ (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

Huyu ni mtoto wa Ja’afar Asw-Swadiq (Radhiya Allaahu ‘anhu)

Amesema juu yake Ibni Taymiyyah:

 

« Mashuhuri kwa kufanya ibada na kuhiji.»

 

Akasema Abu Haatim Ar-Raazi:

 

« Ni mwenye kutegemewa msemakweli, Imam katika maimamu wa Kiislamu.»

 

Amesema juu yake Ibni Kathiyr:

 

« Alikuwa mwingi wa kufanya ibada na mwenye kuheshimika.»

 

Anasema Adh-Dhahabiy katika ‘Siyar’ kuwa siku moja Haaruun Ar-Rashiyd alipokuwa katika Hija alikwenda mbele ya kaburi la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na alikuwa pamoja naye katika safari hiyo Muusa bin Ja’afar Al-Kaadhwim (Radhiya Allaahu ‘anhu). Haaruun Ar-Rashiyd alipofika penye kaburi la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema kwa ufahari mbele ya watu: “Assalaam ‘alayka ewe mtoto wa ‘ami yangu.” Haaruun Ar-Rashiyd anatokana na ukoo wa Al-‘Abbaas bin ‘Abdil Muttalib (Radhiya Allaahu ‘anhu). Muusa bin Ja’afar naye akasogea mbele ya kaburi hilo kisha akasema: “Assalaam ‘alayka ewe baba yangu.”

Uso wa Haaruun Ar-Rashiyd ulibadilika. Akamtizama kisha akamuambia: “Hili Wallahi ni la kujionea fahari.”

 

 

‘Aliy bin Muusa ‘Ar-Ridhwaa’

 

Amesema juu yake Ibni Hibbaan:

 

« Huyu ni miongoni mwa mabwana wa Ahlul Bayt na katika wenye hekima.»

 

Na Adh-Dhahabiy amesema juu yake :

 

« Alikuwa mwenye shani kubwa mwenye kustahiki ukhalifa.»

 

 

Muhammad bin ‘Aliy bin Muusa ‘Al-Jawwaad’

 

Amesema juu yake Ibni Taymiyyah:

«Alikuwa miongoni mwa watu wema na mkarimu sana, na kwa ajili hii alipewa jina la Al-Jawwaad. Na alikuwa mwenye kuheshimika sana.»

 

Yote haya yanabatilisha zile kauli kuwa Masunni hawawapendi watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Alipotuhumiwa ‘Abdullaah mwana wa Imam Muhammad bin ‘Abdil-Wahaab kwamba alisema kuwa watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hawana haki yoyote” akajibu:

“Subhana Allaah huu ni uongo mkubwa. Waliotuzulia haya au kutunasibisha nayo wamesema uongo mtupu juu yetu.”

 

Na hivi ndivyo ilivyo kwa wote wanaotokana na ukoo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na pia wajukuu wote wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), wote tunawapenda bila kuwafarikisha na wote wamepewa sifa wanazozistahiki ndani ya vitabu vya Sunni ikiwa ni dalili wazi kuwa watu hawa tunawaenzi na kuwaheshimu.

 

Shia juu ya kudai kwao kuwa wanawapenda na kufuata mwenenendo wa watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), lakini ukweli ni kuwa wao wanawafarikisha na kuwatenga wengine. Kwa sababu watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwao ni ‘Aliy na Faatwimah na Al-Hasan na Al-Husayn na watoto wao na wajukuu zao peke yao, na wengine wasiokuwa hao wamewatoa katika sifa hii.

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alioa wake wengine akazaa nao watoto wengi, lakini Mashia hawahesabu watoto hao kuwa  ni Ahlul Bayt.

 

Watoto wengine wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kama vile Muhammad bin AlHanafiyah, Abu Bakr bin ‘Aliy, ‘Umar bin ‘Aliy na ‘Uthmaan bin ‘Aliy na ‘Abbaas, wote hawa ni watoto wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Wamewatoa pia mabinti wengine wa ‘Aliy kama walivyowatoa mabinti wengine wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), nao ni Zaynab na Ruqayah na Ummu Kulthum, kama walivyowatoa wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hapo mwanzo.

 

 

 

Share