Ameoa Kisha Ameacha Kwa Vile Mke Hana Maadili – Anataka Kumrudia Mkewe Lakini Mama Hayuko Radhi

SWALI:

 

Assalam aleykum Werahmatolah Wabarakatuh.

Shukrani nyingi sana kwa Al-Hidaaya kwa kutusaidia katika kutujibu maswali yetu.

Ningependa kuuliza kama ifuatavyo. Ikiwa mzazi atakwambia usimuoe mtu fulani kwa sababu hana maadili au ulikuwa ushamuoa ukamwacha akakwambia usimrudie hana maadili na ukimrudia siko radhi na wewe. Nini hukmu ya mzazi na ya mtoto endapo hatamsikikiliza mzazi wake na je ikiwa anayoyasema mzazi kuhusu mwanamke muolewaji au mrudiwaji ni ya kweli je radhi itampata mtoto wa kiume? Natumai mtanijibu kwa ufasaha na kwa ufafanuzi.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mama kutokuwa radhi kwako kumuoa au kumrudia mkeo. Hakika mara nyingi vijana huchukulia mambo mengine kuwa sahali na hivyo kukiuka maadili ya Kiislamu katika suala hilo.

 

Wazazi na hasa mama wana haki kubwa kwa watoto wao. Hii ni kwa jinsi pindi kijana mmoja alipokwenda kumshitakia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa babake amechukua baadhi ya mali yake, alimwambia kuwa wewe na mali yako ni ya baba yako. Na pale ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomtaka mtoto wake amuache mkewe, mtoto alikataa kwani alikuwa anampenda. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtoto afuate agizo la baba yake, naye akafanya hivyo. Kwa hiyo, mama ana haki na inatakiwa kijana awe ni mwenye kumfuata katika mambo yasiyo na madhambi au maasiya ndani yake. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na Mola wako Mlezi Ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyonilea utotoni” (17: 23 – 24).

Unatakiwa uwasikilize katika wema na kutowasikiliza ni thibitisho kuwa uko hasarani hapa duniani na kesho Akhera. Kufanya hivyo, utakuwa umekiuka maagizo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amekuagiza na kukuamuru uchague binti katika ndoa yako mwenye Dini na maadili. Ukitazama kwa mujibu wa swali lako ni kuwa wewe unamtaka binti au kumrudia mkeo ambaye hana maadili. Ukosefu wa maadili ni kumaanisha kuwa na Dini hatokuwa nayo. Mama yako anatakutakia wema kwa kukuepusha katika janga hilo nawe unataka kujiingiza huko huko. Kumfuata mama yako ndio kumtii Allaah Aliyetukuka na hivyo kupata ridhaa ya wote na kukosa kumtii ni kujiingiza katika adhabu na kuchukiwa.

Nasaha yetu ni kuwa mama anakuelekeza kwema nawe unatakiwa ufuate anayokwambia na uyashike kwa magego yako. Tunakutakia kila la kheri na Allaah Mtukufu Akuwezeshe pamoja na kukupatia hima ya kuweza kumfuata mamako bila tatizo lolote.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share