Rumayswaa Ummu Sulaym Al-Answaariyah (Mama Wa Anas Bin Maalik)

 

Kutoka Kitabu Cha: Sayyidaatu Mubashiraatu bil-Jannah (Wanawake Waliobashiriwa Pepo)

 

 

Mwandishi: Muhammad Jabliyy

 

Mfasiri: Binti Ahmadah

 

 

ALISEMA MTOTO WANGU: NA NANI YULE AMBAE ALIYEBASHIRIWA PEPO VILEVILE EWE BABA?

 

Nikasema: Hakika huyo ni Ummu Sulaym al-Answaariyah ewe mwanangu. Baba yake ni Milhaani mtoto wa Khaalid mmoja kati ya Answaari katika kabila la Khazraji. Na mama yake anaitwa Malika mtoto wa Maalik.

 

Ama mumewe anaitwa Maalik mtoto wa Nadhar, na walikuwa na watoto wao kwa majina ya Anas na Baraa waliokuwa Swahaba zake Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

AKASEMA: EWE BABA NIHADITHIE KUHUSIANA NA UISLAMU WA UMMU SULAYM NA LIPI LILIKUWA JINA LAKE?

 

Nikasema: Alikuwa jina lake ni Rumaysaa au Ghumayswaa. Alisilimu baada ya ubalozi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uliposafiri kwenda Madiynah, ili kuwafundisha watu wake Uislamu, kuwapa utambuzi kuhusiana na Diyn na kuwasomesha juu yao Qur-aan. Kisha wakafungamana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na wanawake wa ki-Answaar. Kuingia kwake katika Uislamu kulitimia pale mumewe (Maalik) aliposafiri katika biashara zake. Wakati aliporejea katika safari yake, alijua kuhusiana na Uislamu wa Ummu Sulaym akamshambulia.

 

Akasema mumewe: Umefanya ujinga (gani)?

 

Akarejesha juu yake kwa maneno yake: Hapana, lakini nimeamini.

 

Alikuwa akimchezesha kitoto Anas, akimtamkisha shahada mbili huku akimwambia aseme: Ewe Anas sema: Ash-had ann laa ilaaha Illa Allaah.

 

Anas akawa anarejesha juu yake: Ash-hadu alaa ilaaha Illa Allaah.

 

Naye mama mtu akasema kumwambia Anas, sema: Ash-hadu anna Muhammadan rasuuluLLaah.

 

Anas naye akaiga kwa kusema: Ash-hadu anna Muhammadan rasuuluLLaah. Mpaka ikamkaa vizuri.

 

Wakati wote huo mumewe alikuwa akimsikia Ummu Sulaym akimsemeza mwanawe maneno hayo.

 

Mumewe akasema kumwambia Ummu Sulaym huku akimkodolea macho ya hasira: Usinifisidie mwanangu juu yangu.

 

Ummu Sulaym akarejesha kauli kwa maneno haya: Mimi simfisidii.

 

Uislamu ulikuwa ni sababu ya ugomvi ambao ulisimama baina yao. Hadi siku moja akaondoka Maalik katika safari zake huku akiwa mwenye kuuweka ugomvi ndani ya moyo. Yakamfikia mauti kwa kuuliwa.

 

Akapambazukiwa Ummu Sulaym akiwa kizuka, akaendelea kumlea Anas huku akiwa anasema: Sitomuachisha mpaka atakapoliwacha chuchu kwa nafsi yake, na wala sitoolewa mpaka atakaponiamrisha Anas.

 

Akaanza Anas kukua mkubwa na akaenda Ummu Sulaym kumpeleka Anas kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akamuomba amuombee du'aa Anas. Wakati huo huo akimuomba Mtume amfanye mwanawe kama ni mfanyakazi wake.

 

Akamkabili Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuombea du'aa Anas kwa Allaah Amzidishie mali na watoto. Na akapambazukiwa ni mmoja kati ya matajiri wa Madiynah wenye kuhisabiwa. Akapata Anas watoto na kumpatia mama yake wajukuu wengi. Hii ilikuwa baraka ya du'aa ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

AKASEMA: KULIKUWA NA NINI BAADAYE KWA UMMU SULAYM EWE BABA?

 

Nikasema: Alikuwa Ummu Sulaym ni mwanamke mwenye fadhila, na kwake yeye pia alikuwa na utimamu wa akili na sifa za fadhila kwa yale aliyojaaliwa. Alikuwa ni tegemeo la watu wengi, wanawake watukufu wa ki-Answaar na wanaume baada ya kufa mumewe.

 

Bwana Zayyid bin Sahli alitokea katika kabila la mafundi wa mbao (seremala), akipewa jina la kupanga la Abu Twalha. Alipotambua ya kwamba Ummu Sulaym amepambazukiwa na ujane (hana mume), alifanya haraka asitanguliwe na mmoja kati ya waposaji.

 

Kwa hakika Abu Twalha aliona hatokataliwa kwani alishtadi kwa mali nyingi anayeweza kutanguliza kutokana na manjano au nyeupe – dhahabu na fedha. Anachohitaji mtu kupitia kwa AbuTwalha huweza kukipata kama vile anavyoomba. Akaja kwa Ummu Sulaym bila ya kufikiri katika akili yake na kumrejesha kutokana na udhaifu wake. Kwani Abu Twalha alikuwa ni mpambaji na mrembeaji mzuri mwenye kujua usanifu wa vitu.

 

Akakazania Abu Twalha jambo lake la kumposa Ummu Sulaym. Akatoka tena kuelekea kwenye nyumba ya Ummu Sulaym, akapiga hodi na kukaribishwa kupitia kwa mwanawe Ummu Sulaym (Anas). Akamruhusu kuingia wakati alipoweka wazi Abu Twalha nia ya ndoa yake.

 

Alisema Ummu Sulaym: Je unadhani mfano wa mtu kama wako anarejeshwa ewe Abu Twalha? Lakini kwako kuna kitu kimoja kinanizuia nisiolewe na wewe. Na unadhani Abu Twalha ya kwamba amebakia juu yako mposaji wa mwisho na ameweka juu yako mahari makubwa ambayo hayatoweza kwa yeye kuyatoa au kuzidisha juu yako?

 

Akasema Abu Twalha: Ewe Ummu Sulaym, hakika mimi ni mtu niliyemiliki mali nyingi, na nitajaalia kuwa sadaka yako (yaani mahari yako) kutokana na dhahabu na fedha, na watashindwa wengine kutanguliza mfano wa mali hiyo.

 

Akatabasamu Ummu Sulaym, ya kwamba huwenda fikra za Abu Twalha zilimpeleka katika biashara, lakini ni kinyume na alivyofikiria Abu Twalha. Isipokuwa kilichokuwa kinamzuilia yeye kukubali jambo hili ni kinyume na mali ya Abu Twalha.

 

Alisema Abu Twalha: Una nini? Nitakupa lolote lililokuwa muhimu bila ya kujikalifisha kwa hayo kutokana na thamani yoyote.

 

Alisema Ummu Sulaym: Ewe Abu Twalha, hakika wewe ni mtu mshirikina, na mimi ni mwanamke Muislamu, haisihi kuwa pamoja kwa mfano huo.

 

Kisha akaendelea kwa maneno yake: Je hutambui ewe Abu Twalha unaye kwako unayemuabudia juu yake, na unafanya ibada kinyume na Allaah ambaye amekuumba?

 

Akasema Abu Twalha: Hapana.

 

Akasema Ummu Sulaym: Huoni vibaya ewe Abu Twalha ya kwamba kigogo cha mti kimekuwa mungu wako. Na kinyume chake wanatengeneza juu yake unga au kufanyia kuni kwa kupikia chakula au kuwashia moto siku za baridi kali.

 

Hatimaye Abu Twalha yalimuingia kwenye moyo wake maneno ya Ummu Sulaym pamoja na ugumu wake na yanaelekea kwenye ukweli. Wala hayarejei kwenye njia ya haki.

 

Kisha akasema Abu Twalha: Na yepi mahari ambayo unayaridhia ewe Ummu Sulaym?

 

Akasema: Ikiwa utasilimu nitakubali kuolewa na wewe kinyume na dhahabu wala fedha.

 

Akaelekea Abu Twalha kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujitambulisha Uislamu baina ya mikono yake.

Ikatimia ndoa nzuri kabisa na wakasema wanawake wa ki-Answaar: Hatukutambua mahari makubwa kuliko mahari ya Abu Twalha kwa Ummu Sulaym. Kwa hakika mahari yake yalikuwa ni Uislamu.

 

Haki! Hakika ilikuwa neema katika ndoa hiyo. Maadamu imejengwa na msingi madhubuti. Na je lipo jambo lenye maslahi kuliko Uislamu kuwa msingi wa ndoa madhubuti na mtukufu?

 

Hakika Uislamu ni kisaidizi na ni fadhila za chemchem za mambo yote. Wala usidhani hakika Diyn hii ni ya haki kwa watoto wako tu, bali ni tukufu kwa wote kama ilivyochaguliwa. Na ipi ajabu kwa hayo? Kwa hakika Amesema Allaah Mtukufu:

 

{{Leo nimekukakamilishieni Diyn yenu, na kukutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislamu uwe Diyn yenu.}} [Suratul - Maidah: 3]

 

 

AKASEMA: JE HUNIPI HABARI YA KITU KILICHO KUWA BORA KWA UMMU SULAYM EWE BABA?

 

Nikasema: Hapana ewe mwanangu. Alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haingii katika nyumba ya mmoja kati ya waliooana ila kwa Ummu Sulaym. Mtume akaulizwa kuhusu jambo hilo. Akajibu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((Hakika mimi namrehemu, ameuliwa ndugu yake pamoja nami.)) [Imepokewa na Muslim: 04, 2455]

 

Pia kutokana na masimulizi ya Anas kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Aliingia Peponi akazisikia sauti – Ni sauti ipi – akasema – Nani huyu? Pakasemwa kuambiwa yeye (Mtume): Huyu ni Ghumayswaa binti Milhaan mama wa Anas bin Maalik.)) [Imepokewa na Muslim: 105, 2456]

 

Na Ummu Sulaym ameudiriki ubora, na baraka hizi zimemsibu pia Abu Twalha kupitia ndoa hii yenye baraka ya Bibi Ghumayswaa mama yake Anas (Radhwiya Allaahu ‘Anhum).

 

 

AKASEMA: JE HUNIPI HABARI EWE BABA YA KWAMBA UMMU SULAYM ALIKUWA NI MWENYE AKILI MADHUBUTI AMBAZO ZIMEMUANDALIA YEYE WEMA NA MAHANGAIKO NA MIPANGILIO YAKE YA USANIFU, NA IPI DALILI AMBAYO IMEKUPELEKEA KUMSIFU KWA HAYO EWE BABA?

 

Nikasema: Naapa kwa Allaah, hakika vile vile ilipambika akili yake Ummu Sulaym kwa hikmah katika kujaalia (khayr) mahangaiko yake na kuweka mbali aibu zake na upungufu wa kitu. Na hii mifano inatosheleza kwako kwa hikmah zake kwa yale yaliyomtokezea juu yake.

 

 

AKASEMA: NA ALITUMIA VIPI HIKMAH NA UONGOZI WAKE KUTENGENEZA MAMBO?

 

Nikasema: Abu Twalha alikuwa ana mtoto mdogo aliyempenda katika nafsi yake kuliko kitu chochote. Na alikuwa Ummu Sulaym akimlea na akimchunga. Siku moja alitoka Abu Twalha katika kutafuta rizki. Muda si mrefu mwanawe huyu alifariki bila ya Abu Twalha kuelewa hilo. Akausia Ummu Sulaym kwa watu wa nyumba yake kwamba asipewe habari Abu Twalha kuhusiana na kifo cha mtoto wake.

 

Wakati alipomaliza Abu Twalha kazi yake, akaswali Swalah ya 'Ishaa Msikitini, akaelekea nyumbani na kumkuta Ummu Sulaym hakika amemuandalia yeye chakula na amezidisha mapambo juu yake kuliko anavyojipamba.

 

Wakati alipomuuliza hali ya mtoto, akampa habari ya kwamba ni nzuri kuliko ilivyokuwa. Kisha Ummu Sulaym akatanguliza Swala ya 'Ishaa. Abu Twalha akala mpaka akashiba, ukasimama usingizi juu yao.

 

Wakati walipoamka alisema Ummu Sulaym kumwambia Abu Twalha kuhusiana na kitendo cha jirani yake juu yao: Ewe Abu Twalha, jirani ameazima cha kuazima, wakati alipotakiwa yeye akirejeshe, alichukizwa na alijizuilia juu ya kurejesha. Je amefanya kosa kwa jambo hilo na anaweza kujitetea kwa kujizuilia?

 

Akastaajabu Abu Twalha: Hana udhuru kwa jambo hilo na ubaya ulioje kwa kujizuilia!

 

Akasema Ummu Sulaym: Kwa hakika ilikuwa kwa mtoto wako ni kiazimo cha kitu kutoka kwa Allaah na kukirejesha (ni haki), ikiwa utafanya (subra) basi kitarejea.

 

Akaendelea Ummu Sulaym kwa kusema: Hakika sisi sote tunamtegemea Allaah na kwake Yeye tutarejea.

 

 

Abu Twalha akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumsimulia kutokana na aliyoyafanya Ummu Sulaym.

 

 

Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia Abu Twalha: ((Akubarikieni Allaah usiku wenu))

 

Ikajibiwa du'aa hiyo na akabeba mimba Ummu Sulaym kisha akazaa kitoto cha kiume. Akamuamrisha mwanawe Anas kumbeba ndugu yake mdogo ili kwenda nae kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili amfungue koo na ampatie jina.

 

Akaelekea Anas na ndugu yake huku akiwa na tende. Alipowaona Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanakuja alisema kumwambia Anas: ((Je unayo pamoja nawe tende?)) Alisema Anas kumwambia Mtume "ndio". Akaichukua tende huku akisoma du'aa na kuilainisha kwa kuitafuna tafuna. Kisha akakifungua kinywa cha mtoto na kumlisha baadhi ya tende hiyo. Akaanza kitoto kuramba ramba utamu tamu katika midomo yake miwili. Akasema Mjumbe wa Allaah: ((Wamekanusha Answaar juu ya mapenzi ya tende)) Kisha akamwita jina la 'AbduLlaah. Anas akamrejesha kwa mama yake.

 

 

ALISEMA MTOTO: NIAMBIE UKWELI KUHUSIANA NA JIHAAD YA KILA MMOJA BAINA YA WATU WAWILI HAWA, WANA NDOA NA MASWAHABA WAZURI ZAIDI. NA NI VIPI ULIKUWA UKARIMU WAO?

 

Nikasema: Kwa kila furaha ewe mwanangu, walikuwa na mwenendo wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukoo wa Abu Twalha uliokuwa na nguvu sana. Kwa hakika aliutumia vizuri Abu Twalha upanga katika kumlinda Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyoweka mali yake kwa ajili ya maandalizi ya vita na kutilia mkazo haja za Waislamu. Na alikuwa Abu Twalha ni mwenye kutaraji juu hayo kwa radhi za Mola wake na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kwa hakika alikuwa nayo bustani kubwa iliyojaa miti mizito mizito na aina tofauti za matunda. Siku moja alikuwa anaswali ndani ya bustani hiyo na alimuona ndege akiimba juu ya mti, alikuwa ana rangi tofauti. Akavutiwa juu ya kumuangalia kwa ukali wa uzuri wake, ikashughulika akili yake Abu Twalha mpaka hakuweza kukumbuka rakaa ngapi ameweza kuswali.

 

Wakati alipomaliza Swalah yake alikimbilia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akamsimulia kwa kile kilichomtokea juu yake, na vipi aliweza kumshughulisha ndege mzuri ndani ya Swalah yake.

 

Kisha akasema: Nishuhudie ewe Mjumbe wa Allaah, hakika mimi nimeijaalia bustani yangu hii ni sadaka kwa ajili ya Allaah Mtukufu na ifanye unavyotaka.

 

Hakika mfano wa kitu hichi kilichotolewa ni kizuri, hakipatikani kitendo hichi ila kwa yule mwenye mapenzi ya kweli kwa Mola wake na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kuyakinisha kwamba mbele ya Allaah kuna khayr na ni yenye kubakia.

 

Ama kwa upande wa Jihaad, Abu Twalha hakika alifikia nafasi ya mbele katika vita vya Uhud. Hivi ni vita ambavyo walikwenda kinyume (kukhalifu) warembeaji wa mishale wa Kiislamu amri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakaacha sehemu zao na kutaka kuokota na kunyang'anyiana ngawira ambazo zilienea kwenye uwanja wa mapambano. Kwa hakika ilikuwa hapana budi kubadilika muelekeo wa ushindi kwa maslahi ya washirikina badala ya kuwa ni kwa maslahi ya Waislamu. Wakakimbia Waislamu pale alipoeneza mmoja wa washirikina ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwisha uawa.

 

Na kilikuwa kichwa cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kimepasuka, zimevunjwa taya zake na amejeruhiwa midomo yake. Ikaanza damu kumtiririka mtukufu, na alikuwa amezungukwa mbele yake na kikundi cha Maswahaba watukufu (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) kama vile bangili zinavyozunguka mkono. Sio hivyo tu, bali wamezitoa panga zao, wakamzunguka na kuvitoa vifua vyao bila ya kupita mmoja kati ya washirikina baina yao.

 

Naye hakuwa nyuma, kwani Abu Twalha alikuwa ni mmoja kati ya wale walioweka ngome kwa Mtume siku hiyo. Akaanza Abu Twalha kuwarushia washirikina mishale isiyo na idadi.

 

Abu Twalha alimwambia maneno yafuatayo pale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kujinyanyua kutoka sehemu aliyokaa, kwa ajili ya kuona wapi imeangukia mishale: Kwa baba yangu na mama yangu, ewe Mtume, usiwachungulie yakaja kukupata maudhi yao, nijaalie mimi kwa Allaah ni fidia yako.

 

Mara aliiingia kwao wao mmoja wa Waislamu akisema kwamba washirikina wanakimbia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kumwambia: ((Rembea mshale wako baina ya mikono ya Abu Twalha na wala usipite (mshale) kutokana na wao ukakimbia))

 

Aliendelea Abu Twalha kurembea na kumlinda kutokana na hayo Mjumbe wa Allaah mpaka akavunja mipinde mitatu. Na akauwa idadi kubwa ya maadui wa Allaah na maadui dhidi ya Diyn moja, ikafikia idadi yake watu ishirini (20).

 

Ikaja siku ya vita vya Hunayn, wakatoka wanandoa hao watukufu pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Jihaad dhidi ya washirikina. Na alikuwa Ummu Sulaym juu ya ngamia wa Abu Twalha, wakati alipomuona Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ummu Sulaym alinadi: Kwa baba yangu na mama yangu ewe Mjumbe wa Allaah, nitawauwa hawa wote waliokimbia mlimani (Uhud), kwa ajili yako wewe kama walivyouawa wale ambao walitaka kukuuwa wewe. Mjumbe wa Allaah akasema: ((Akutosheleze Allaah ewe Ummu Sulaym))

 

Hakika Ummu Sulaym alikuwa ni jemedari aliye tayari kwa mapambano. Kwani katika vita hivyo vya Hunayn, Abu Twalha alimuona na kitu mikononi mwake, akamuuliza: Nini hichi ulicho nacho ewe Ummu Sulaym.

 

Akasema Ummu Sulaym: Panga nimeichukua pamoja nami, atakaponikurubia mmoja kati ya washirikina nitalichoma tumbo lake.

 

Akasema Abu Twalha: Hivyo hukusikia yale aliyoyasema Mjumbe wa Allaah?!

 

Alisema Jubayr bin Mutwghama: Kwa hakika niliona kabla ya kushindwa kwa watu (yaani washirikina) huku watu wanapambana mfano wa mkusanyiko wa guo kubwa jeusi, limetanda kutoka mbinguni mpaka likaanguka baina yetu na baina ya watu. Nikaliangalia nikaona kana kwamba (hao wapiganaji) ni wadudu chungu weusi wametawanywa na wameenea katika jangwa. Basi nikawa nina shaka kwamba hao ni Malaika, na wala hawakuwa Malaika isipokuwa ni kushindwa kwa watu.

 

Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

{{Bila shaka Allaah Amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunayn (pia); ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni chochote, na ardhi ikawa dhiki juu yenu; ingawa ilikuwa yenye wasaa, kisha mkageuka mkarudi nyuma (mnakimbia).}}

 

{{Kisha Allaah Akateremsha utulivu Wake juu ya Mtume Wake na juu ya walioamini. Na Akataremsha majeshi (ya Malaika) ambayo hamkuyaona, na Akawaadhibu wale waliokufuru; na hayo ndiyo malipo ya makafiri.}}

 

{{Kisha baada ya haya Allaah Atawasamehe Awatakao (katika wale makafiri maadamu watasilimu watubie). Allaah ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.}}

[Suratu-Tawbah: 25-27]

 

Vile vile alimkunjulia Allaah Mjumbe Wake kwa (kumteremshia majeshi ya) Malaika na ushindi ukawa kwa Waislamu. Wakawashinda makafiri, shukurani zote ni za Allaah Mola wa viumbe vyote.

 

 

 

ALISEMA MTOTO: EWE BABA NIZIDISHIE MIMI MASIMULIZI JUU YA FADHILA ZA UMMU SULAYM.

 

Nikasema: Ummu Sulaym alihifadhi Hadiyth ambazo alizisikia kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha akisimulia, na akawa amechukua juu yake idadi ya Hadiyth na baadhi ya Maswahaba wamesimulia kutoka kwake.

 

Jumla ya wapokezi waliosimulia kupitia kwake ni: mwanawe – Anas bin Maalik, 'AbduLlaah bin Abbaas, Ghamra bin Ghaaswim Answaari, Zubayr bin Thaabit, 'Abdur-Rahmaan bin 'Awf. Hizi ni fadhila za Allaah, Humpa Amtakae.

 

Amepokea Ghatwaa kutoka kwa Ummu Sulaym Al-Answaariy: Alisema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza Ummu Sulaym: ((Kwa nini Ummu Sulaym hujaja kuhiji pamoja nasi mwaka huu?)) Akasema Ummu Sulaym: Ewe Mtume kulikuwa kwa mume wangu kuna watu wawili, ama mmoja amehiji juu yake, ama mwengine amemuacha akimwangalia juu yake mitende. Akasema: ((Pindi itakapokuwa Ramadhaan au mwezi wa kufunga, fanya 'Umrah ndani yake, kwani hakika ya 'Umrah ni mfano wa Hijja, au huchukua nafasi ya Hijja))

 

Akabaki Ummu Sulaym akikata masiku ya uhai wake baina ya funga na kisimamo na kupigana kwa ajili ya Allaah mpaka ikamfikia kikata ladha na kufarikiana na jamaa zake. Akalala katika ulinzi wa Allaah, ambao hakuna hata mmoja anaeweza kuwarehemu waja wake sawa sawa.

 

Akaishi Abu Twalha hadi kukutana na kipindi cha ukhalifa wa mwenye nuru mbili - 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu). Alimtaka Abu Twalha kutoka pamoja na jeshi la vita vya baharini aliloliandaa 'Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu). Abu Twalha aliweza kutanguliza kwa hilo upanga wake.

 

Wanawe wakamwambia: Tuache sisi tuende badala yako wewe, unahitaji kwa sasa mapumziko.

 

Walipokuwa katikati ya bahari yakamsibu maradhi Abu Twalha akafariki. Akawa miongoni mwa Maswahaba waliofariki ambao walitafutiwa sehemu ya kuzikwa miili yao kwa muda wa siku saba. Hatimaye wakakipata kisiwa. Na alikuwa amefunikwa kama vile amelala, na wala hakubadilika kitu chochote.

 

Amrehemu Allaah Abu Twalha na Ummu Sulaym na Awakutanishe wawili hao mbele Yake wakiwa ni wenye kung'ara na kufurahi.

 

 
Share