Mwanamke Ana Rafiki Mwanaume Mkristo, Anaweza Kumuombea Duaa Asilimu?

SWALI:

 

Je ukipata mchumba mkristo inaruhusiwa kumuombea dua ili asilimu? Na kama unaruhusiwa ni zipi hizo dua?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu du’aa ya kutaka mchumba Mkristo asilimu. Hakika hili limekuwa ni tatizo sugu kwa Waislamu kwa wasichana kutaka kuolewa na Wakristo na wavulana Waislamu kuwa na mahusiano na kuoana na wasichana wasiokuwa Waislamu. Huu ni msiba katika jamii na tusipobadili mienendo huenda tukaingia katika shimo ambalo itakuwa vigumu kutoka.

 

Mwanzo msichana Muislamu haifai kuna na urafiki, uchumba wala kuolewa na asiyekuwa Muislamu. Hata hivyo, urafiki baina ya msichana na mvulana haufai hata baina ya Waislamu. Lile ambalo unatakiwa kufanya mwanzo ni kuepukana na huyo mchumba Mkristo. Ama kuomba du’aa, Muislamu anafaa awaombee wote wasiokuwa Waislamu ili wapate kuingia katika ini ya haki, Uislamu. Hili ni jambo ambalo linafaa na linatakiwa.

 

Sasa ikiwa unaona kuwa mwanamme fulani ana baadhi ya sifa ambazo ni nzuri ambazo zinafaa kuwa kwa Waislamu waweza kumuombea mtu huyo hasa apate hidaaya na kuingia katika Uislamu. Hakuna du’aa maalumu kuhusu hilo bali unaweza kumuombea na kuwaombea wengine katika nyakati ambapo du’aa huwa ni yenye kukubaliwa na Allaah Aliyetukuka kama katika nyakati zifuatazo:

 

1.    Baina Adhana na Iqaamah.

2.     Aliyefunga.

3.     Wakati wa kufungua kwa aliyefunga.

4.     Msafiri.

5.     Ukiwa katika Sijdah.

6.     Kuinuka saa za usiku na kumuomba Allaah.

7.     Na kadhalika.

 

Na kwa mfano akiwa mvulana huyo atasilimu kwa kuwa umeweka sharti ya kwamba kuolewa naye mpaka afanye hivyo basi chunga sana kwani matatizo ya ndoa hizo ni makubwa. Huyo mvulana husilimu kwa ajili ya kukupata wewe, akisha kukupata huwa basi atarudi katika Ukristo na hapo utaanza kuona matatizo na itawiwa shida kurudi na kurekebisha kosa hilo. Tahadhari sana kabla ya athari mbaya kukufika.

 

Ni jambo la busara kama atasilimu, basi apatiwe mafunzo juu ya Uislamu na aachwe katika hilo kwa muda usiopungua mwaka. Katika muda huo anaweza kuonekana zile tabia zake na maadili yake, na hapo kuamua kuhusu suala la ndoa baada ya kuswali Swalah ya Istikhaarah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share