Abu 'Ubaydah 'Aamir Bin Al-Jarraah - Muaminifu Wa Ummah Huu

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’y

 

 

YALIYOMO

Nasaba Yake.. 1

Sifa Zake.. 1

Kusilimu Na Hijra Yake.. 2

Mitihani Yake.. 2

Hakimu Muaminifu.. 3

Ustahamilivu Wake.. 4

Uaminifu Wake.. 5

Kifo Chake.. 6

 

 

Nasaba yake

Jina lake kamili ni ‘Aamir bin ‘Abdillaah bin Al-Jarraah bin Hilaal bin Uhayb bin Swabbaah bin Al-Haarith bin Fihri bin Maalik bin An-Nadhar bin Kinaanah bin Khuzaymah bin Mudrikata bin Ilyaas bin Madhar bin Nizar bin Maad bin ‘Adnaan kutoka katika kabila la Quraysh. Uhusiano wake na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) unakutana kwa Fihri

 

 

Sifa Zake

 

Huyu ni Swahaba ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimpa jukumu la kuliongoza jeshi lililokwenda kumsaidia ‘Amru bin Al-‘Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) katika vita vilivyojulikana kwa jina la 'Dhaatus Salaasil'.

Katika vita hivyo alipewa uongozi wa jeshi ambalo ndani yake alikuwemo Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhum).

Huyu ni Swahaba ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisema juu yake:

"Hakika kila umma una mwaminifu wake, na mwaminifu wa umma huu ni Abu ‘Ubaydah ‘Aamir bin Al-Jarraah."

Na hii haina maana kuwa Maswahaba wengine hawakuwa waaminifu, bali hizi ni sifa ambazo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kuwahusisha nazo Sahibu zake (Radhiya Llaahu ‘anhum), mfano aliposema:

"Mwenye huruma kupita wote kwa umma wangu ni Abu Bakr."

Hii haikuwa na maana kuwa wengine hawakuwa na huruma.

 

Na aliposema:

"Mkali kupita wote katika kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu ni Umar"

Hii haikumaanisha kuwa wengine walikuwa wakisahilisha katika kufuata maamrisho.

 

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mwenye uso mkunjufu, mwembamba, mrefu, mwepesi, na jicho hutulia na kufurahi kila linapomuona. Alikuwa mpole mwenye huruma.

‘Abdullaah bin ‘Umar bin Al Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhuma) alisema juu yake:

"Watatu katika Makureshi walikuwa wenye nyuso kunjufu, mwenendo na tabia njema, wingi wa hayaa, na hawasemi uongo wanapozungumza na wala hawakukadhibishi unapozungumza nao; Abu Bakr Asw-Swiddiyq, ‘Uthmaan bin ‘Affaan na Abu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah."

 

Imepokelewa pia kuwa siku moja ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwaambia watu waliokuwa naye:

"Kila mtu atamani anachokitaka."

Kila mmoja akasema anachotamani, mwisho ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema:

"Ama mimi natamani nyumba iliyojaa watu mfano wa Abu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah."

 

Hata hivyo, katika vita dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu, Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mkali na hatari kama simba.

 

 

Kusilimu Na Hijra Yake

 

Alisilimu siku iliyofuata baada ya kusilimu Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kwa ajili hiyo alikuwa miongoni mwa wachache wa mwanzo walioingia katika dini hii tukufu ambao Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta’ala) Alisema juu yao:

 

"Na kumbukeni mlipokuwa wachache, mkionekana wanyonge katika nchi, mnaogopa watu wasikunyakueni, naye Akakupeni pahala pazuri pa kukaa, na Akakutieni nguvu kwa nusura Yake, na Akakupeni riziki nzuri ili mpate kushukuru." Al-Anfaal: 26.

 

Alisilimishwa na Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu) siku moja yeye pamoja na ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf na ‘Uthmaan bin Madh’uun na Al-Arqam bin Al-Arqam (Radhiya Llaahu ‘anhum), kisha Abu Bakr (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawapeleka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ambako mbele yake walizitamka shahada mbili, na kwa ajili hiyo wakawa miongoni mwa nguzo madhubuti za mwanzo zilizoisimamisha dini hii tukufu.

 

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) Alihajir (alihama) kwenda nchi ya Uhabeshi (Ethiopia) katika hijra ya pili kisha akarudi na kuhajir tena, mara hii kuelekea Madina.

 

 

Mitihani Yake

 

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipambana na mashaka, huzuni na mitihani mingi mikubwa alipokuwa Makkah sawa kama Waislamu wenzake, lakini mtihani mkubwa aliopambana nao usioweza kusahaulika na hata masikio hayakubali kusadiki wala moyo hauwezi kuustahamilia ulikuwa siku ya vita vya Badr.

Katika vita vya Badr, siku ambayo Mwenyezi Mungu Alitaka aihakikishe haki kwa maneno Yake, na Aikate mizizi ya makafiri. Siku hiyo Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliingia vitani akipambana kwa ushujaa mkubwa huku akikata kila kichwa cha kafiri aliyemkaribia. Hofu iliingia ndani ya nyoyo za Makureshi, wakawa wanamkimbia kila anapowasogelea huku yeye akisonga mbele bila ya kuhofia mauti. Lakini mtu mmoja katika jeshi la maadui alikuwa akimsogelea na kusimama mbele yake huku akimshambulia akijaribu kumzuia asisonge mbele. Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alijaribu kumuepuka na kuelekea kwengine, lakini mtu huyo aliendelea kumfuata huku na kule akimzonga na kumshambulia kwa upanga wake ili amzuie asiendelee kupambana na adui wa Mwenyezi Mungu, na hatimaye mtu huyo akageuka kuwa ngome isiyopitika baina yake na baina ya adui.

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliposhindwa kustahamili na alipoona kuwa akitaka kuendelea kuipigania dini ya Mwenyezi Mungu hana budi kupambana na mtu huyo, akaamua kufanya hivyo. Na kwa pigo moja la upanga wake alimkata kichwa.

Usijishughulishe sana kutaka kumjua ni nani huyu, kwani mtu huyo alikuwa ni ‘Abdullaah bin Al-Jarraah baba yake Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa akipigana upande wa washirikina.

Mwenyezi Mungu kwa ajili yake Akateremsha aya inayosema:

 

"Huwakuti watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na Amewapa nguvu kwa Roho itokayo Kwake. Na Atawaingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu Awe radhi nao, na wao wawe radhi Naye. Hao ndio HizbuLlaah, Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa." Al-Mujadaalah: 22.

 

 

Hakimu Muaminifu

 

Haya si ya kushangaza kwa Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye wengi katika Maswahaba wakubwa (Radhiya Llaahu ‘anhum) walitamani kuifikia daraja ya imani yake iliyoshuhudiwa hata na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Ulipokuja ujumbe kutoka Najraan (Yemen) kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kumtaka awape mtu aliyeridhika naye katika Maswahaba wake ili awe hakimu baina yao wanapohitalifiana katika mambo mbali mbali ya maisha yao pamoja na yale yanayohusu mali zao, aliwaambia:

"Rudini mchana nitakupeni mwenye nguvu na muaminifu afuatane nanyi."

Anasema ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu):

"Siku hiyo niliwasili mapema sana Msikitini kuswali Adhuhuri (ili nipewe mimi jukumu hilo), na sikupenda kupewa jukumu hilo isipokuwa kwa sababu ya kuitamani kwangu ile sifa ya uaminifu."

Baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kumaliza kutuswalisha akaanza kutazama kulia na kushoto akitafuta, na mimi nikawa najisogeza mbele apate kuniona. Akawa anaendelea kutafuta huku na kule mpaka alipomuona Abu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah, akamuita na kumuambia:

"Fuatana nao uwe hakimu katika waliyokhitalifiana baina yao."

Nikajisemea nafsini mwangu:

"Abu ‘Ubaydah keshaichukua (daraja ile)."

 

 

Ustahamilivu Wake

 

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakuwa muaminifu tu, bali alikuwa mwenye nguvu na mstahamilivu pia.

Siku moja alipotakiwa kuongoza jeshi litakalokwenda kuuteka msafara wa Kikureshi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwa na chakula cha kutosha cha kuwapa isipokuwa mfuko wa tende. Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) akawa anawagawia watu wake kila mtu tende moja kwa siku. Mtu anainyonya tende hiyo kama mtoto mchanga anavyonyonya ziwa la mama yake, na akishaimaliza anakunywa maji.

 

Siku ya vita vya Uhud baada ya maadui kufanikiwa kulizunguka jeshi la Waislamu na kuwapiga vibaya, Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa miongoni mwa watu kumi waliobaki katika uwanja wa vita waliomzunguka Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) wakimlinda na kumkinga na mikuki ya makafiri iliyokuwa ikirushwa kutoka huku na kule, huku makafiri wakisonga mbele na kupiga kele:

"Tuonesheni alipo Muhammad, tuonesheni alipo Muhammad!"

 

Wakati huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa keshajeruhiwa vibaya sana; jino lake lilivunjika, kipaji cha uso wake kilipasuka na shanga mbili za ngao yake zilikatika na kuzama ndani ya shavu lake tukufu, huku uso wake ukivuja damu.

Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa karibu alijaribu kuzitoa shanga zile, lakini Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuambia:

"Nakula kiapo juu yako uniachie mie."

 

Akamuchia, na Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) akihofia kuzitoa kwa mikono asije akamuumiza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliamua kuzitoa kwa meno yake.

Akaibana shanga ya mwanzo kwa meno yake ya upande wa kulia kwa nguvu zake zote na ustadi, akafanikiwa kuitoa lakini jino lake moja liling'oka na kuanguka.

Kisha akaibana shanga ya pili kwa meno yake ya upande wa kushoto akafanikiwa pia kuitoa na jino lake la pili likang'oka na kuanguka.

 

 

Uaminifu Wake

 

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alishuhudia vita vyote alivyoshiriki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) tokea alipokuwa sahibu yake mpaka alipofariki dunia.

 

Kama alivyokuwa muaminifu wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliendelea kuwa muaminifu wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr na pia wakati wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhum).

Bila kujali akiwa ni kiongozi au askari wa kawaida, alipigana chini ya bendera ya Uislam kwa ajili ya kulinyanyua neno la Mwenyezi Mungu kila bendera hiyo ilipokwenda

Abu ‘Ubaydah ((Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa askari wa kawaida wakati Khaalid bin Al-Waliyd (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokuwa akiongoza majeshi ya Waislamu katika mapambano makubwa na muhimu sana dhidi ya makafiri katika nchi ya Shaam. Khalifa wa Waislamu ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) alituma mjumbe amkabidhi Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) barua yenye amri ya kumpa yeye uongozi wa jeshi hilo.

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimtaka mjumbe huyo asimjulishe mtu juu ya amri hiyo mpya mpaka baada ya vita kumalizika, kwa sababu usiku huo jeshi lilikuwa katika mapambano yake ya mwisho yatakayoupa ushindi mkubwa jeshi la Waislamu.

Baada ya vita kumalizika na Waislamu kushinda, Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimuendea Khaalid (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kumkabidhi barua.

Khaalid akamuambia:

"Mwenyezi Mungu Akurehemu ewe Abu ‘Ubaydah, jambo gani lililokuzuia usinionyeshe barua tokea ulipoipokea?"

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamuambia:

"Sikupenda kukuharibia vita vyako. Sina haja ya ufalme wa kidunia mimi Wala siitumikii dunia. Sisi sote ni ndugu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."

Na hivi ndivyo walivyokuwa - Mwenyezi Mungu awe radhi nao; hawakuwa wakijishughulisha na vyeo wala dunia, bali walikuwa watu waliojitolea nafsi zao na roho zao na mali zao kwa ajili ya kulinyanyua neno la Mwenyezi Mungu.

 

 

Kifo Chake

 

Wakati Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipokuwa Shaam akiongoza majeshi ya Kiislamu yaliyokuwa yakiendelea kuteka nchi baada ya nchi; kutoka Euphrates upande wa mashariki hadi Asia minor kaskazini, maradhi ya tauni yasiyopata kuonekana mfano wake yaliivamia nchi ya Shaam na kuua watu wengi sana.

Alipoona maisha ya Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) yamo hatarini, ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa Khalifa wa Waislamu wakati ule, alimtuma mjumbe kwa Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) akiwa na barua iliyoandikwa yafuatayo:

"Ninakuhitajia sana. Itakapokufikia barua hii wakati wa usiku, usingoje asubuhi iingie ufunge safari kuja kwangu. Na ikikufikia wakati wa mchana usiungoje usiku uingie, uifunge safari ya kuja kwangu."

 

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alifahamu kusudi la barua ile, nayo ni kumtaka aondoke Shaam asije akapatwa na maradhi ya tauni.

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) akamjibu ifuatavyo:

"Ewe Amiri wa Waumini, nishaijua haja yako kwangu. Mimi ni askari katika askari wa Kiislamu na sipendi kujiepusha na kile kinachowasibu wenzangu. Na sitaki kuachana nao ndugu zangu, mpaka pale Mwenyezi Mungu Atakapoipitisha amri Yake.

Itakapokufikia barua yangu hii, unipe udhuru katika haja yako na uniruhusu nibaki."

‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipoisoma alilia sana, hata walio karibu naye wakamuuliza:

"Amekwishafariki dunia Abu ‘Ubaydah?"

Akasema:

"Hapana. Lakini kifo chake kipo karibu."

 

Hakukosea ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu), kwani Abu ‘Ubaydah (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipata maradhi ya tauni, na alipokuwa akikata roho aliwausia waliokuwepo kwa kuwaambia:

"Hakika mimi nakupeni usia wangu, mukiufuata mtakua katika kheri;

Simamisheni Swalah, fungeni mwezi wa Ramadhaan, toeni Sadaka, msiache kufanya ibada ya Hija na ya ‘Umrah. Mupeane usia mwema baina yenu, na muwape nasaha njema viongozi wenu na msiwaghushi, na isikubabaisheni dunia kwa sababu mtu hata aishi miaka elfu, lazima siku moja atakuwepo juu ya njia hii mnayoiona niliyopo mimi hivi sasa juu yake. Was-Salaamu ‘Alaykum wa RahmatuLlaahi wa Barakaatuh."

Kisha akageuka kumtizama Mu’aadh bin Jabal (Radhiya Llaahu ‘anhu), akamuambia:

"Swalisha watu."

Kisha akafariki dunia. Na Mu’aadh (Radhiya Llaahu ‘anhu) akainuka na kuwahutubia watu akasema:

"Enyi watu! Tumeondokewa na mtu ambaye WaLlaahi sijui kama nimewahi kumuona mwenye ustahamilivu na upole kupita yeye, na mwenye kujiweka mbali na shari kupita yeye. Wala sijapata kumuona mtu mwenye kuipenda Akhera yake na mwenye kupenda kuwanasihi watu kupita yeye.

Kwa hivyo muombeeni rehma Mwenyezi Mungu Akurehemuni."

 

Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka hamsini na nane kwa ugonjwa wa tauni uliojulikana kwa jina la 'Twa’uun Amuwaas' kutokana na jina la mji wa Amuwaas (Jordan) ulioshambuliwa na maradhi hayo. Na hii ilikuwa katika mwaka wa kumi na nane, na wengine wakasema kuwa amefariki katika mwaka wa kumi na saba Hijra.

 

Share