Nilikumbwa Na Majini, Nikapona, Mchumba Anayetaka Kumuoa Anazuiliwa Na Kaka Na Mama Yake

 

Nilikumbwa Na Majini, Nikapona, Mchumba Anayetaka

Kumuoa Anazuiliwa Na Kaka Na Mama Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum,

 
Napenda kuwashukuru kwa mchango mkubwa munaoutoa kwa jamii kuhusu dini yetu, hakika nimefaidika kwa mengi, na kwa leo napenda kuwauliza  swali kuhusu nikaah,  na kama itawezekana mukinijibu wa kutumia email hii itakuwa vizuri zaidi, mimi ni msichana mkubwa nakaribia miaka 34, sijaolewa  nilikuwa nasumbuliwa na majini na katika kipindi hicho cha matatizo nilikuwa nikipanda jini mara kwa mara na anasema kuwa hataki niolewe, lakini kwa uwezo wa Allaah na kwa elimu aliyowapa waja wake nimefanyiwa visomo na rukya nyingi, wametulia kiasi, tatizo jengine ni kuwa kila ambapo akija mtu kutaka kunioa nikikubali tu, mtu anakuwa harudi tena mara nasikia kaoa, mpaka nikajiona tafrani, lakini baada ya kufanyiwa visomo na ruqya niliweza kupataa mchumba ambae alidhamiria kunioa, baada ya miezi miwili alipopeleka shauri kwao, mtoto wa ami yake ambae atakuwa ni sawa ni kaka yake mkubwa alikataa na alimjaza maneno mabaya kuhusu mimi, pia alimjaza maneno mama yake na ami yake (kwa vile mchumba mwenyewe baba yake kafariki) jambo hilo walilipinga kwa nguvu zao binafsi, maneno na pia kutumia nguvu za giza, kwa upande wangu Allaah alinipa subra, kila mara huyo mchumba alipokuja kunieleza kuwa kwao wamekataa nilimshauri asubiri na ajaribu tena, kajaribu mpaka tumefikisha mwaka na nusu, mpaka mara hii ya mwisho baada ya kukataa kwao alinijulisha tu kwa sms kuwa wamenikataa tena na wamempatia mchumba ambae yeye hakumtaka, ila huyu mchumba kakata mawasiliano kabisa na kawa mkali kiasi nashindwa kumwambia chochote, siwezi kumpigia simu wala kumtumai sms ha yeye ndio kakata mawasiliano, sasa naomba ushauri wenu, kwanza nifanyeje? Kwa sababu huyu mchumba nampenda na yeye ananipenda sana, pia ana msimamo wa dini ndio akanivutia, lakini inavoonyesha kawezwa kwa nguvu za kawaida na zisizo kawaida, pili nini hukumu ya wazee wanaozouia watoto kutooa wanawake wanaowapenda wao, tatu huyu kaka yeye kaenda maka lakini anatumia kila aina ya mbinu kuzuia hii ndoa, nini hukumu yake, nne naweza kumshauri vipi ili aweze kurudi katika haoli yake ya kawaida? Au kuna kisomo chochote naweza kumfanyia ili atokane na hali ya uzuzu aliotiwa nao kwa muda? Tano jee huyu mchumba angezalimisha kunioa hata kama mama yake hajaridhia japokuwa mama yake kamwambia atamtenga akinioa atakuwa kafanya kosa? (Mama yake hajawahi kuniona ila ananisikia tu) nakuombeni munijibu kwa uwezo wa Allah, Assalam alaykum

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika mwanzo twashangaa kuwa umetufahamisha kuwa huyo mchumba ni mtu aliyeshika Dini vilivyo ilhali maelezo uliyotueleza ni kinyume na hivyo. Hiyo ni kuwa mahusiano na mawasiliano baina ya wanaadamu katika Uislamu yana mipaka yake. Na hasa watu wakiwa ni jinsia tofauti hawawezi kuwa wanawasiliana kwa mwaka na nusu kabla hata posa haijapelekwa kwenu katika njia za kisheria huo ni utovu wa kufuata sheria ya Allaah Aliyetukuka. Ilikuwa ungojee mpaka itakapokuja posa kutoka kwa mchumba wako na kuoana rasmi. Mara nyingi wanawake au wasichana hudanganywa kwa maneno ya kuwa nakupenda kisha baada ya hapo wakatupwa pwaa bila ya kutekelezewa hilo. Jambo hilo huwatweza sana dada zetu kwa kiasi ambayo huwa ni shida au tatizo kubwa kwao kupata mchumba mwengine.

 

 

Na pia ni ajabu kuwa mchumba wako atashurutishwa kumuoa mwanamke ambaye hamtaki. Kukubali yeye kufanya hivyo ni kujitia katika dhuluma ambao Uislamu umekataza kabisa. Vipi atafanya dhuluma? Dhuluma itaingia kwa yeye kutompenda kumfanyia mambo ambayo mke hafai kufanyiwa na hiyo itampeleka mahali pabaya hapa duniani na kesho Aakhirah. Kwa hakika, twaona ni bora yeye kukata mawasiliano nawe kwani mlikuwa katika madhambi baina yenu kwa hayo mawasiliano yenu na zinaa ya mdomo ni mazungumzo. Na kupatikana hilo ni kheri kwako kwani Allaah Aliyetukuka hamfanyii mja wake kitu isipokuwa inakuwa ni kheri kabisa kwake. Kwa kuwa wewe umesubiri kwa muda mrefu zidi kusubiri kwani kheri yote ya kila mja inajulikana na Yeye mwenyewe Aliyetuumba. Hivyo usikate tama kabisa kuhusu hilo wala ujitie katika huzuni kwa kuwa hukumpata huyo aliyekuwa mchumba wako. Allaah In shaa Allaah Atukapatia mwengine aliye wa kheri na bora zaidi kuliko huyo uliyemkosa. Cha kufanya wewe ni kusubiri na subira huvuta na kuleta kheri. Mapenzi si hoja bali huja na kuondoka, na ukweli ni kuwa mapenzi ya uhakika hupatikana tu baada ya nyinyi wawili kuoana bila hivyo hayawezi kupatikana hayo unayosema. Na fahamu kuwa nguvu zote zinatoka kwa Allaah na si mwanaadamu, na ni juu yako kumtegemea Yeye, Naye Atakuongoza katika njia iliyo nzuri na bora.

 

 

Wazee wema ni wale wenye kuwasaidia watoto wao katika kutekeleza ndoto zao njema. Na hakuna ndoto nzuri za kusaidiwa kama kusaidiwa katika kuoa mke unayempenda. Ilikuwa ni vyema wazazi wamsaidie mtoto wao aweze kukuoa wewe ambaye anakupenda. Wazazi kumkwaza katika hilo ni kufanya dhuluma ya hali ya juu. Hata hivyo, inaonyesha mchumba wako hajui haki zake kama Muislamu katika ndoa, kwani mwanamume hahitaji ruhusa ya wazazi kumuoa mwanamke anayemtaka bali ni heshima tu kuwaambia kuwa mimi nimefikia umri wa kuoa na naona mwanamke fulani ndiye atakayenifaa basi mambo huwa hapo yamekwisha. Hivyo, makosa katika hilo yanarudi kwa mchumbako kwa kutokuwa na msimamo katika hilo.

 

 

Dada yetu mpendwa, kwenda kwa mtu Makkah hakumaanishi chochote katika sheria ya Allaah Aliyetukuka. Lililo muhimu ni ile nia na lengo ya Muislamu yeyote kwenda huko. Je, alikwenda kwa nia ya kutafuta radhi ya Aliyetukuka au amekwenda kutafuta mabaya kwa njia moja au nyingine. Habari nyingi zinapatikana kwa Waislamu wengi wanaokwenda kwa ajili ya Hajj au ‘Umrah, lakini ukapata ya kwamba wapo wanaoibiwa wakiwa katika Twawaaf au kwenye kutupa mawe, na yapo mengine mengi hata hayasemeki. Kwa Uislamu wetu, tunamchukulia kwa dhana nzuri kuwa amekwenda huko kufanya mema na mazuri. Mbali na hilo, mtu baada ya kurudi Makkah kwa ajili ya Hija huenda akabadilika na akawa pengine muovu zaidi kuliko alivyokuwa kabla ya safari yake kuelekea huko. Hata hivyo, ikiwa atakuwa ni mwenye kutumia mbinu kinyume na sheria ya Kiislamu kuwatenganisha atakuwa anapata madhambi na anafanya dhuluma. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuelezea kuwa dhuluma itakuwa ni giza kwa aliyefanya Siku ya Qiyaamah.

 

 

Ama kumshauri na kumpatia nasaha aliye mchumba wako zipo njia nyingi. Na kama tulivyosema awali ni kuwa mawasiliano yenu baina nyinyi wawili ni aina ya uzinzi hivyo tunakunasihi usiwe ni mwenye kuwasiliana naye moja kwa moja.

 

 

Sasa njia ambazo twaziona kuwa zinaweza kuleta natija iliyo nzuri ni kama zifuatazo:

 

1.     Mwanzo ni wewe kuswali Swaalah ya Istikhaarah, kumtaka ushauri Muumba wako, Allaah. Ushauri wenyewe ni kuwa je, kwa mitihani yote haya kweli huyu mwanamme ana kheri nawe? Jibu utakalolipata kwa Swalah hiyo ndiyo litakufanya uweze kuchukua mwelekeo mmoja au mwingine.

2.     Tumia watu wenye busara na hekima na hasa Mashaykh waliobobea katika elimu ya Dini ya Kiislamu, wacha wa Allaah na wenye nia njema waende wakazungumze naye mchumba wako kuhusu suala la ndoa na waweze kumpatia nasaha kwa njia ya uwazi na bora. Huenda akatia akili na akarudi nyuma.

3.   Ashauriwe kusoma Suwrah, Aayah na nyiradi za Ruqyah (kinga) kwa mambo ambayo anaweza kuwa kafanyiwa katika uchawi na mazingaombwe. Pia anaweza kupelekwa kwa Shaykh anayesoma Ruqyah za kisheria ili kumtoa katika uchawi ikiwa kweli atakuwa amefanyiwa hivyo kama unavyodhania.

 

 

Ama kuhusu swali lako la mwisho tayari tumelijibu hapo juu/ awali. Na kusisitiza ni kuwa mwanamme ana khiyari yeye mwenyewe na wala hahitaji walii au mlezi kwa ndoa yake kusihi. Na kwa kutekeleza haki yake hiyo angeweza kukuoa bila idhini yake japokuwa kumwambia kuhusu suala hilo ni katika wajibu wako. Mbali na haki hiyo ya mwanamme, hata hivyo ni muhimu asiwe ni mwenye kumuudhi mama yake. Inatakuwa mwanamme aweze kumkinaisha mama yake kuhusu uchaguzi wake. Lau itakuwa kweli uchaguzi wake ni katika Dini na pingamizi ya mama ni kutotaka mtoto wake asioe aliyeshika Dini basi hapo kijana atamvunja mama yake katika hilo lakini itabidi amuwekee heshima yake kwa kumtazama na kumfanyia wema. Ikiwa mama hatotaka uhusiano huo atakuwa na dhambi mbele ya Allaah Aliyetukuka lakini kijana atalazimika kujenga uhusiano kwa njia moja au nyingine.

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akutimizie lile ambalo litakuwa ni kheri kwako katika Dini na amali yako na hatima yako na Akuepushie kila la shari.

 

 

Na utambue kwa sababu moja au nyingine ikiwa hukuweza kuolewa na huyo mwanamme huenda ikawa ndio kheri yako. Usihuzunike bali subiri mpaka kheri nyingine itakapokujia.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share