Anataka Kusilimu Lakini Anataka Kwanza Aonyeshwe Wapi Kwenye Qur-aan Kuna Amri Kumi Za Muusa, Na Kwa Nini Waislam Wanaswali Ijum

SWALI:

Assalam alaikum.kuna rafiki yangu anataka kusilimu. Yeye ni msabato, na amekuwa karibu miezi miwili anajifunza uislamu. Mambo yanayomtatiza anataka aoneshwe wapi kwenye quran wameandika amri kumi alizopewa nabii Musa (as). Na kwa nini waislamu wanasali ijumaa badala ya jumamosi. Naomba mnisaidie majibu


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu amri kumi za Nabii Musa (‘Alayhis Salaam) katika Qur-aan na kuswaliwa Swalah ya Ijumaa.

Kwanza amri hizi kumi ambazo zipo katika Agano la Kale zinapatikana katika ‘Kutoka’ 20: 1 – 17 na ‘Kumbukumbu la Sheria’ 5: 7 – 21. Bila shaka Uislamu ukiwa ni mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu, amri hizo zilizo nzuri zinapatikana katika machimbuko muhimu ya Uislamu nayo ni Qur-aan na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nasi tutajibana katika Aayah za Qur-aan kuhusu amri hizo kumi. Nazo ni kama zifuatazo:

1.     Usiwe na miungu mingine:

2.     Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga:

3.     Usivisujudie wala kuvitumikia:

Hizi nukta tatu za juu zinahusiana na ushirikina ambao umepigwa vita vikali sana. Muislamu anafaa amuabudu, kumsujudia, kutofanya masanamu ya kuchonga au mengine na kutomshirikisha. Kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa madhambi makubwa sana katika Uislamu ambayo inafanya amali zako zote ziharibike. Miongoni mwa Aayah kuhusu hilo ni kama zifuatazo:

a. Amepitisha Mola wako Mlezi usimuabudu ila Yeye (17: 23).

b. Muabuduni Allaah wala msimshirikishe Yeye na chochote (4: 36).

c. Na miongoni mwa watu wapo wenye kuchukua miungu washirika wanaowapenda kama kumpenda Allaah. Na wale Waumini wanampenda Allaah zaidi (kuliko yeyote mwengine)” (2: 165).

d. Na hakika Tumewatuma kwa kila Ummah Mitume, na Tukawaambia: Muabuduni Allaah tu na mjiepushe na Twaaghuuti (anayeabudiwa asiyekuwa Allaah) {16: 36}.

e. Sema: Allaah ni Mmoja tu. Allaah ndiye Mwenye kukusudiwa. Hakuzaa wala Hakuzaliwa na hakuna anayefanana Naye (112: 1-4).

f. Mwenyezi Mungu Hasamehe dhambi ya kushirikishwa (4: 48, 116)

 

4.                 Waheshimu baba na mama yako: Kuwaheshimu wazazi imekuja katika Qur-aan baada ya kumuabudu Allaah. Kutowaheshimu wazazi ni katika madhambi makubwa.

a. Anasema Aliyetukuka: Na kuwafanyia wema wazazi. Na wanapofikia uzee mmoja wao au wote wawili, usiwaambie uff (neno ndogo hata kusema ah!) ... na uwaambie maneno mema (17: 23-24).

b. Wafanyie wema wazazi wako (4: 36).

c. Mnishukuru Mimi na wazazi wako. Na wakikulazimisha kunishirikisha kwa usilokuwa nalo elimu usiwatii (wazazi wako) lakini suhubiana nao duniani kwa wema (31: 14 – 15).

 

5.     Usizini: Uzinzi ni dhambi kubwa katika Uislamu kiasi ambacho mwenye kuzini akiwa ameoa au hajaoa au kuolewa ana adhabu kali. Mwenyezi Mungu anatuamuru hata tusije karibu na zinaa (17: 32).

6.     Usiue: Kuua pia ni katika madhambi makubwa ambayo anapata adhabu mwenye kufanya kitendo hicho. Mwenyezi Mungu Asema kuwa yeyote mwenye kuua nafsi moja ni kama ambavyo ameua walimwengu wote na kuhuisha nafsi moja ni kama ambavyo amehuisha walimwengu wote (5: 32). Na pia msiue watoto wenu kwa kuhofia ufakiri (17: 31).

 

7.     Usiibe: Kuiba ni katika dhambi kubwa na mwenye kufanya hilo inabidi aadhibiwe na sheria ya Kiislamu. Na mwizi mwanamme na mwanamke, kateni mikono yaokama malipo kwa wanayochuma (5: 38). Kufanya hivyo ni kumkwaza anayetaka kuiba asiwe ni mwenye kutenda tendo hilo baya.

8.     Usimshuhudie jirani yako uongo: Jirani ni mtu muhimu katika jamii. Uislamu umehimiza sana ujirani mwema. Zipo heshima na adabu ambazo majirani wawili kila mmoja analazimika kumfanyia mwenzake na kumpa haki zake zikiwa kamili. Na kutomshuhudia jirani uongo ni miongoni mwa adabu. Na Allaah Anasema: “Na kuwafanyia wema wazazi wawili … jirani ndugu na jirani asiye ndugu” (4: 36). Na Mtume (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) amesema: “Anayemuamini Allaah na siku ya Mwisho basi amkirimu jirani yake” (Muslim, Ahmad).

 

9.      Usimtamani mke wa jirani yako wala vitu vyake: Kufanya hivyo ni kutoka katika ujirani mwema na kuvunja ujirani mwema. Maelezo tayari tumeyaandika hapo juu. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Na kumwekea mshirika wakati Yeye ndiye Aliyekuumba, kumuua mwanao ili asile nawe na kuzini na mke wa jirani yako” (al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaa’iy).

 

10.      Adhimisha siku ya Sabato: Sabato ya Waislamu ni siku ya Ijumaa wala sio Jumamosi. Hiyo ni kuwa siku ya Ijumaa ni siku bora na tukufu hapa duniani. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Siku bora iliyochomoza jua ni Ijumaa, kwani ndani yake aliumbwa Aadam (‘Alayhis salaam) na siku hiyo aliingizwa Peponi na kwayo alitolewa, na Qiyaamah hakitasimama ila Ijumaa” (Muslim). Siku hii ni sikukuu ya Waislamu ulimwenguni. Hiyo ni siku ambayo inafaa kwa Muislamu kuiheshimu, hivyo kwenda Msikitini mapema na kufanya Ibadah. Japokuwa sikukuu kwa Muislamu anaruhusiwa kufanya kazi kabla ya Ibadah hiyo mahsusi au baada yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: “Na itakapokwisha Swalah, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Allaah, na mkumbukeni Allaah kwa wingi ili mpate kufaulu” (62: 10).

Ama kuhusu kipengele cha pili cha swali lako kuhusu kwa nini Waislamu huswali Ijumaa, ni kuwa sisi Waislamu tunaswali siku ya Ijumaa badala ya Jumamosi kwa kuwa tumeagiziwa hilo na Muumba wetu, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

Enyi Mlioamini! Kukiadhiniwa kwa ajili ya Swalah ya Ijumaa, nendeni upesi kumtaja Allaah na acheni biashara. Kufanya hivi ni bora kwenu ikiwa mnajua” (62: 9).

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share