Mashairi: Toa Sadaka

 

 Toa Sadaka

‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu Allaah)

Alhidaaya.com

                

 

Salaamu kwa mahabubu, zivuke yote mipaka,

Walo mbali na karibu, nawaombea fanaka,  

Nimefungua kitabu, na kalamu nimeshika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Hapo siku ya hesabu, hukuokoa Sadaka,

Utakusanya thawabu, marundo hujirundika,

Inapunguza ghadhabu, ya Mwenyezi Mtukuka,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Inakua ni kivuli, ona inakufunika,

Utamkuta Jalali, na wewe Ameridhika,

Umetoa kwa halali, radhi za Allaah kutaka,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Khasa Sadaka ya siri, hakika imetajika,

Ina baraka na kheri, kwa Allaah hukubalika,

Huitoi kwa fakhari, ili upate sifika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Akhera na duniani, mambo yanasahilika,

Utaona mitihani, kwa wepesi unavuka,

Nuru yazidi nyumbani, riziki huongezeka,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Toa Sadaka upesi, kabla kufilisika,

Utoe hata kiasi, kwa jina la Msifika,

Utoe kwa ikhlasi, huku umefurahika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Usifanye kusimanga, thawabu itafutika,

Wala hapana kuringa, kudharau na kufoka,

Dini yetu inapinga, masikini kumcheka,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Kwa maiti ndio nzuri, Sadaka inamfika,

Mpaka ndani ya kaburi, thawabu humiminika,

Tena inakusitiri, siku ya kujumuika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Duniani kwenye mali, inazidisha baraka,

Usifanye ubakhili, mwisho utahangaika,

Utakwenda na amali, mali yote hukatika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Kwanza waliokaribu, lazima kuwakumbuka,

Kina bibi kina babu, kina dada kina kaka,

Hawa wote ni wajibu, wapate kunufaika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Halafu ni mafakiri, kwa shida wanasumbuka,

Amewanyima Qahari, hivyo Allah Ametaka,

Kagawa rizki Jabari, yote Ameshaandika.

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Usisahau yatima, ona wanavyoleleka,

Mapenzi yale ya mama, wamekosa kwa hakika,

Kwa macho ukitazama, kweli utasikitika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Toa kwa mambo ya kheri, yote Mola Anaweka,

Utazikuta tayari, thawabu kukusanyika,

Akhera wewe tajiri, hapo utafaidika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Nawasihi ndugu zangu, ipate kueleweka,

Haipotei kwa Allaah, Kwake inahifadhika,

Iwe ndogo kama chungu, kwa Mola husajilika,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Sote tuwe Wakarimu, kabla ya kuondoka,

Tumridhishe Rahimu, mwisho tutapumzika,

Tuepushwe jahanamu, moto unaolipuka,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Ona Sadaka si Zakaa, Zakaa imefaridhika,

Usipoitoa Zakaa, mengi yataharibika,

Madhambi yatakufika, nguzo tano kupunguka,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

                                                                  

Amma Sadaka khiari, hapo hukulazimika,

Ukitoa ni vizuri, akiba yako kuweka,

Mbele itakunawiri, kama taa itawaka,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

Hapa nafunga shairi, mwisho sasa nimefika,

Atuepushe na shari, Mola wetu Mtajika,

Tupo ndani ya safari, toa Sadaka haraka,

Hukuokoa Sadaka, hapo siku ya hesabu.

 

 

 

 

Share