Zingatio: Ni Haki Ya Muumba Kutoa Laana

 

Naaswir Haamid

 

 

Miongoni mwa wakuu wa utwaaghuti hapa duniani ni Ibilisi (Laana za Allaah Ziwe juu yake). Ibilisi amelaanika kutokana na kukaidi amri ya Mola kwa kumsujudia baba yetu Aadam (‘Alayhis Salaam). Hata baada ya kufukuzwa mbinguni, amechukua ahadi ya kuwapotosha viumbe na uhakika ni kwamba anaifanyia kazi ahadi hiyo na amewakumba wengi.

 

Ibilisi amelaanika kutokana na Aayah zifuatazo:

 

{{(Mwenyezi Mungu) Akasema: "Ewe Ibilisi! Imekuwaje? Hukuwa pamoja na waliotii?"}}

 

{{Akasema: "Siwezi kumtii mtu Uliyemuumba kwa udongo mkavu unaotoa sauti, unaotokana na matope yaliyovunda."}}

 

{{Akasema (Mungu): "Basi toka humo, na hali ya kuwa wewe (sasa) ni mwenye kufukuzwa na kubaidishwa na rehema.}}

 

{{"Na kwa yakini itakuwa juu yako laana mpaka Siku ya Malipo."}}

 

[Suratu-Hijr: 32-35]

 

Hivyo ndivyo namna alivyolaanika Ibilisi kwa kukosa rehema za Muumba tokea siku hiyo alipokataa kutii amri ya Mola (Subhaanahu wa Ta’ala), na kwa yakini itaendelea laana juu yake Ibilisi mpaka Qiyaamah.

 

Rehema Za Mwenyezi Mungu zipo mbali kabisa na laana, na huruma Zake kwetu ni kubwa kuliko ghadhabu Zake. Hata inapomfikia kiumbe hizo laana, hakika anastahiki kabisa kabisa kama huyo Ibilisi. Tendo la kulaani viumbe ni haki Yake Mola Mlezi pekee wala sisi hatuwezi kujua ni binaadamu gani haswa amelaanika! Wala hatustahiki kukaa kutupiana laana kama vile tunavyotupa taka majumbani mwetu. Huo sio mwenendo wa aliyeamini nguzo sita za iymaan. Na huenda hizo laana anazotoa mwanadamu zikamrudia yeye mwenyewe kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Pekee Ndie Ajuaye ni nani wa kulaaniwa.

 

Tabia ya kulaaniana ndani ya maisha yetu imekuwa ni tabia ya kawaida kabisa. Hata mzee tunashuhudia kutoa kauli za laana kwa mwanawe mzazi kabisa. Tunalaumu nini pale mtoto anapofurutu ada kwa vitimbi viovu kabisa kama kuvuta bangi, kuiba na kulewa? Huyo mtoto si tumemlaani sisi wenyewe au sio?! Cha ajabu nini hapo?

 

Na kuna waliovuka mipaka kwa kiwango cha juu kabisa na kuwalaani Maswahaba watukufu ambao ndio waliotufikishia hii Dini yetu, na kuwatukana watukufu wa Maswahaba ambao ni Abu Bakr Na ‘Umar na imekuwa ni ada ya watu hao kuwalaani hao katika Swalah zao na vikao vyao! Hakika watu hao Iymaan yao ina mashaka na wana khasara kubwa katika maisha ya duniani na Akhera wana mwisho mbaya kabisa.

 

Baadhi ya wazee tunawashuhudia wakiwa vibarazani wakiwalaani watoto wao kutokana na maovu yao. Na mzee anapoulizwa: "huyo mtoto wako unamlaani kwani sio mtoto halali?" anajibu kwa kuinamisha kichwa chini kama vile ameonewa: "ndivyo alivyonambia mamake." Yaani uaminifu haupo kabisa baina ya mume na mke, inafika wakati mtoto umemzaa na kumlea mwenyewe, unamwita ni wa haramu kwa lengo la kuburudisha baraza tu! La hawla wala quwwata illa bi Llaah.

 

Maneno kama khabiythi, mwanaharamu, laana iwe juu yako na mengineyo ni maneno yasiyofaa kabisa kutamkwa na Muislamu wa kweli. Seuze yanapotamkwa kwa mzee juu ya mwanawe, hapo tatizo linakuwa kubwa zaidi. Hakika haingii akilini kwa mzee kutamka mfano wa maneno hayo.

 

Tuzingatie na tuelewe kwamba ni Ibilisi tuliye na uhakika wa kwamba amelaanika, yeye ndie aliyekosa rehema za Muumba. Sisi tupo hai wala haifai kulaaniana baina yetu, wala haifai kwa Muislamu kumlaani kafiri kwa kumtaja jina. Ila tu tunaweza kusema kwa jumla "Mola Awalaani Mayahudi". Cha kusema hapo unapoghadhibika na kukerwa ni يهديك الله "Allaah Akuongoze" au kama ni mwanao wa kumzaa basi mwite يا إبن الحلال "Ewe mtoto wa halali."

 

Share