Wakwe Wanataka Kumuozesha Mke Mwengine Mtoto Wao Kisha Asiwe Ananipa Haki Kwa Sababu Ya Kuwa Mimi Sio Kabila Lao La Kihindi

 

SWALI:

Assalam Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Ningependa mwanzo kuwashukuru sana kwa kazi yenu nzuri, Mashallah na kuwatakia nyote ndugu katika Islam mwaka mpya wa 1430 mwema wenye Barka na uwe mwaka wa kheri na uongofu kwetu sote, tumkurubie na kumtakasa Allah "Subhana Huwat' Allah" na tufuate yale yote aliyotufunza kipenzi chetu na Mtume wetu Muhammad, "Swalallahu Alaihi Wasallam".

Ndugu katika Islam, ningependa kuuliza swali ambalo ni ndefu na natarajia Insha'Allah mutanisaidia kwa jibu kwa haraka kadri ya Allah Subhana Huwat'Allah atakavyowaezesha.

Mimi nimeolewa na mume Muislamu wa kihindi na sasa tuna mtoto mmoja. Ndoa yetu hii imekuwa na mitihani mingi kwa sababu ingawa upande wa familia yangu hawana shida nayo, upande wa mume wangu haswa mamake mume wangu (mavyaa) amekuwa hana raha nayo kwa kile anachosema kuwa ndoa yetu haitodumu kwa sababu mwanawe (mume wangu) hakuoa mhindi mwenzao bali kanioa mimi. Tumekuwa na subra siku nyingi na kwa vile mume wangu anamheshimu mamake ambaye toka hapo waliishi pamoja, tuliamua mimi niishi kando naye aishi na mamake lakini huja kututembelea kila wiki kwani sote wawili twafanya kazi. Mimi naishi na mwanangu mchanga na msaidizi wangu ambaye humwangalia mtoto wetu wakati niko kazini. Nimestahamili haya kwa kuwa sitaki vita na mamake, lakini ni subra tu na kumpenda mume na mtoto wangu.

Hivi karibuni yule mama ambaye sasa ni mzee amekuwa na hasira nyingi kwa mume wangu kwa sababu hanitaki mimi na yeye na jamaa zako wanamwambia aoe mke mwingine wa kihindi na awachane nami lakini mimi na mume wangu hatuna matatizo yoyote, ni wao tu wenye mambo hayo mengi. Sasa hivi mume wangu yuko katika hali ya pressure nyingi kutoka kwa jamaa zake na ananiambia kuwa yeye hataki kuniwacha lakini tu kwa sababu ya kuwaridhisha watu wake haswa mamake anayehofia atamnyima radhi zake kwa kutomtii, ananiambia nimkubalie amuoe huyo mke atakaye lazimishwa kumuoa na jamaa zake. Sasa mimi nakubali kuwa Allah Subhana huwat'Allah amewaruhusu wanaume kuoa hadi wake wanne, lakini je ni haki katika hali kama hii. Mume wangu kwa muda alikuwa kazi yake imeharibika na sasa alipata kazi nyingine ingiwa pato lake si kubwa, kwa hiyo mahitaji ya nyumba ninayoishi mimi najilipia mwenyewe kwa kuwa naelewa hali yake. Sasa vipi leo alazimishwe kuoa na labda baadaye kulazimishwa kuniacha na huku haweze kutuhitajia vyema mimi mke na mtoto wake? Yule mke wa kihindi atamuoa na akae naye pamoja huku mimi nikiishi kando naye kwa subra, lakini haya yote kwa sababu ya kumuogopa mamake. Kwa wakati huo huo anasema kuwa hii ni pale itakapofika kuwa hana budi na amelazimishwa basi ataoa, lakini mimi hilo sikubaliani nalo kwa sababu hata pale Allah Subhana huwat' Allah alipoamsrisha kuoa wake hadi wanne, aliamrisha kuwe na uadilifu. Je ni haki baada ya kustahamili yote hayo, aje mke mwingine kwa kuwa ni kabila lao aishi naye kila siku nami anione tu mara moja kwa wiki? Ingawa mume wangu anapinga na kusema haombi yafikie hapo naona ana unyonge kujitetea kwa mamake na kusema haweze kuwahitajia wake wawili ki hali na mali. Yeye asema kuwa mimi nafanya kazi kwa hivyo tutaendelea kuishi kama tulivyokuwa lakini mimi nimemwambia akitaka kuoa mke kwa kulazimishwa, basi anipe talaka yangu, na hili hataki kusikia. Naomba tafadhali munipe ushauri bora kwa hali yangu hii ngumu. Je ni haki mume wangu kuoa mke wa pili kwa kutaka tu kuwaridhisha watu wake na huku mimi haki zangu hanikamilishii inavyotakikana hata sasa? Kama kweli sote ni waislamu, mbona jamaa zake kuingilia ndoa yetu?

Nitashukuru sana kupata jibu kwa haraka;.

 

Shukran, Wajazakallahu Khair


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ndugu yetu Allaah Akupe kila la kheri inaonyesha katika maneno yako karibu yote kuwa unaelewa mengi kuhusu dini yako ni jambo la kujivunia na Allaah Awape kila la kheri waliokufiksha hapo. Umesema, Mimi nimeolewa na mume Muislamu na hili ndio litakiwalo kwa kila mwanamke Muislamu ama kusema, wa kihindi, hili halina haja katika Uislamu wala kwa Muislamu.

Umeeleza kuwa, tuliamua mimi niishi kando naye aishi na mamake. Kama mlikubaliana na kuwa haki zako ulikubali zisipatikane kama mke na mume hilo ni katika maamuzi yako na hakuna atakayekulazimisha kwa haki yako.

Kisha ukasema, wanamwambia aoe mke mwingine wa kihindi, kuambiwa au kushauriwa aoe mke mwengine si jambo baya kama atalimudu na maelezo yako yanathibisha hayo na huu ndio Uislamu hata kama wewe utaona kuwa wewe ndio unapaswa umtafutie huyo mke basi hilo ni katika iymaan ya Waislamu wenye kheri nyingi.

Ama kumshauri awachane nami, hili si katika mafundisho ya Uislam kwani kumchukiza mtu kwa mume wake au mume kwa mkewe ni jambo lenye kumtoa mtu katika kuwa miongoni mwa Waislamu wachilia mbali kumuachisha mtu kwa mumewe au kumtaka mume amuache mkewe haya ni katika yasiyokubalika katika Uislamu

Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hayuko pamoja na sisi mwenye kumchukiza mwanamke kwa mume wake, au mtumwa kwa bwana wake.” Imepokelewa na Al-Haakim, kitabu cha twalaaq, amesema Hadiyth hii ni sahihi kwa sharti ya Imaam Al-Bukhaariy lakini Al-Bukhaariy hakuitoa kwenye Kitabu chake.

 

Ukasema, lakini tu kwa sababu ya kuwaridhisha watu wake haswa mamake anayehofia atamnyima radhi zake kwa kutomtii, Wazee hawana radhi za kumuachia wala chochote hayo ni maneno tu yaliyozooleka, mwenye radhi ni Allaah na kama yuko na heshima na anawahudumia wazee wake na kuwatii katika maarufu basi hakuna dhambi atakayoipata mtu kwa Mola wala hakuna wa kumuachia radhi; hivyo la muhimu ni yeye kumfanyia wema   hasa huyo mama kama anavyotaka Allaah basi radhi zake Atapata mumeo kwa  Allaah kwani Yeye ndiye mwenye kutoa na kuwachia radhi sio wazee wala mtu yeyote.

Ukaeleza, ananiambia nimkubalie amuoe huyo mke atakaye lazimishwa kumuoa na jamaa zake  wewe kama unampenda huyo mumeo kama unavyodai basi huna haja ya kumkatalia lakini ni vyema wewe kama ni mkewe ambaye mmeshaishi pamoja na kuelewa matatizo ya maisha yenu leo mmepata na kesho hakuna kitu na hali yake inaielewa wewe na yeye mwenyewe basi mshauri na kumwekea wazi kila kitu kuhusu maisha yenu na namna ulivyokuwa ukimstahamilia kupata na kukosa; yawezekana mke huyo wa kihindi amepewa zawadi na hatakiwi kitu ila shughuli ya kitandani tu, sasa kukataa si jambo zuri ametunukiwa na anao uwezo wa kitanda lakini hana uwezo wa kinyumba kula kuvisha na kadhalika yote atasimamia mama au huyo mke au jamaa zake, na kama huyo mumeo ana akili zake na anaelewa ukweli kuhusu maisha na kuwa hana mbele wala nyuma basi ataweza kuwashauri jamaa zake kuhusu hali yake.

Ukaendelea kueleza, Sasa vipi leo alazimishwe kuoa, Hakuna mtu anayelazimishwa kuoa kwani kuoa siyo kupeleka mkono na kusema nimekubali kumuoa binti fulani, bali kuoa ni kumuingila huyo binti na kama kweli kalazimishwa basi hata huko kumuingilia watamlazimishwa.  Ndugu yetu tumia akili yako Aliyokutunuku Mola wako na shauriana na huyo mumeo kuhusu hukumu na haki za wake kwa mume wao kama wako wawili na sio kufikiria jambo ambalo halipo wala halitakiwi kufikiriwa kama hivi ulivyosema, baadaye kulazimishwa kuniacha na huku haweze kutuhitajia vyema mimi mke na mtoto wake? La kumshauri ni kumueleza ukweli kuhusu hali yenu ambayo ni maisha yenu ya kila siku ambayo unadai kuwa hawezi kukuhudumia, sasa hali hii itakuwa pia kwa huyo bibi mpya au ni vipi? Mkumbushe kuwa anatakiwa kumuogopa Allaah.

Umesema, lakini mimi nimemwambia akitaka kuoa mke kwa kulazimishwa, basi anipe talaka yangu, na hili hataki kusikia, Ndugu yetu hutakiwi kuomba talaka kwa sababu tu mumeo ameoa mke iwe kwa kulazimishwa au hata kwa kutunukiwa au kwa sababu yoyote ile isiyokubalika lakini wewe kama uko mkweli katika malalamiko yako basi unayo haki ya kumnasihi huyo mumeo sio kumtaka akuache wewe. Mnasihi na umuwekee wazi kuwa kama hatokuwa muadilifu baina yenu wewe na mke atakayetunukiwa basi atakuwa anajitengezea pahala pabaya pa kufikia huko tuaminiko kuwa tutakwenda inshaAllaah; hivyo basi huna haki ya kuomba talaka wala kumshikia akupe wala kumchagiza iwe kaoa kwa hiari yake au kaolewa na mwanamke au katunukiwa.

Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke yeyote atakayeomba talaka kwa mume wake bila ya sababu (inayokubalika) basi Allaah atamuharamishia kunusa harufu ya Pepo” Imepokelewa na Al-Haakim, kitabu cha twalaaq, amesema Hadiyth hii ni sahihi kwa sharti ya Shaykhayn -Imaam Al-Bukhaariy na Muslim- lakini wote wawili hawakuiweka kwenye vitabu vyao.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share