01-Jihaad: Maana Ya Jihaad Na Kuwekewa Shari'ah

 

Maana ya neno Jihaad

 

Neno Jihaad, asili yake linatokana na juhudi, tabu, mashaka. Kwa mfano tunasema; ‘Amejitahidi’, ‘amefanya juhudi’, yaani amezitumia nguvu zake na uwezo wake wote katika kutimiza jambo fulani, na haya yote yanapatikana katika mapambano ya kivita.

 

 

Sheria ya Jihaad

 

Allaah Alimtuma Mtume wake (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam) kwa watu wote, akamuamrisha kuwalingania katika uongofu na katika dini ya haki, na wakati wote alipokuwa Makkah alikuwa akiwalingania watu kwa hekima na kwa mawaidha mema, na kwa ajili hiyo ilibidi apambane na kila aina ya uadui, udhia na mateso kutoka kwa watu wa kabila lake baada ya kuuona utukufu na uluwa wao umo hatarini.

 

Wakati wote huo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alimtaka awe akipambana na uadui huo kwa subira, uvumilivu na kwa kusamehe msamaha mzuri.

 

Allaah Anasema:

 

فَاصْفَحِ الصَّفْحَ الْجَمِيلَ

 

“Basi msamehe msamaha mzuri (kila anayekufanyia ubaya).”

Al Hijr – 85

 

Na Akasema:

وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا

“Na ungoje hukumu ya Mola wako, na hakika wewe uko mbele ya macho Yetu.”

At-Twuur: 48

 

Na Akasema:

فَاصْفَحْ عَنْهُمْ وَقُلْ سَلامٌ

“Basi wasamehe wewe na uwambie (maneno ya) salama.”

Az-Zukhruf: 89

 

Na Akasema:

قُل لِّلَّذِينَ آمَنُوا يَغْفِرُوا لِلَّذِينَ لا يَرْجُون أَيَّامَ اللَّهِ

“Waambie wale walioamini wawasamehe wale wasioziogopa siku za Allaah (za kuwatia adabu wabaya).”

Al-Jaathiyah: 14

 

Allaah Hakumtaka Mtume wake (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam) aukabili ubaya wao kwa ubaya, wala udhia kwa udhia na wala Hakumuamrisha kuwapiga vita wanaoipiga vita da’wah hiyo, au kuwapiga vita wale wanaowatesa Waislamu, bali alikuwa Akimwambia Mtume Wake (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam):

 

ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ السَّيِّئَةَ نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَصِفُونَ

“Ondosha mabaya (unayofanyiwa) kwa (kulipa) mema; Sisi tunajua wanayoyasema.”

Al-Muminuun: 96

 

Muda wote huo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alimuamrisha Mtume wake (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam) apigane Jihaad kwa Qur-aan na kwa hoja zilizo wazi.

 

Allaah Anasema:

وَجَاهِدْهُم بِهِ جِهَادًا كَبِيرًا

“Na ushindane nao kwa (Qurani) hii mashindano makubwa.”

Al-Furqaan: 52

 

Lakini baada ya kupita miaka kumi na tatu huku mateso yakiongezeka, na makafiri kuzidisha uonevu na kuwadhalilisha Waislamu, na hatimaye kufanya njama za kumuua Mtume wa Allaah (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam) hata akalazimika kuhamia Madiynah na kuwaamrisha Masahaba wake (Radhiya AAllaahu anhu) pia kuhamia huko, hapo ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alipoteremsha kauli Yake isemayo:

 

وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُواْ لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللّهُ وَاللّهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ

“Na (kumbuka ewe Muhammad) walipokufanyia hila wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe, na wakafanya hila (zao barabara) Na Allaah akazipindua hila hizo. Na Allaah ni mbora wa kupindua hila (za watu wabaya).”

Al-Anfaal: 30

 

Kisha Akasema:

 

إِلاَّ تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللّهُ

“Kama hamtomnusuru (Mtume wa Allaah (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam), basi Allaah Alimnusuru.”

At-Tawbah: 40

 

Baada ya kuhamia Madiynah, makao makuu ya dola mpya ya Kiislamu, na baada ya makafiri kuwaendea huko huko na kuwafanyia mbinu na hila mbali mbali, ndipo Allaah Alipotoa amri ya kupigana Aliposema:

 

أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا وَإِنَّ اللَّهَ عَلَى نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ 39 الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ بِغَيْرِ حَقٍّ الا أَن يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّهُ وَلَوْلا دَفْعُ اللَّهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّهُدِّمَتْ صَوَامِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَاتٌ وَمَسَاجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا اسْمُ اللَّهِ كَثِيرًا وَلَيَنصُرَنَّ اللَّهُ مَن يَنصُرُهُ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ 40 الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ وَلِلَّهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ 41

“Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa, kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa yakini Allaah ni Muweza wa kuwasaidia.

Ambao wametolewa majumbani (mijini) mwao pasipo haki ila kwa sababu wanasema “Mola wetu ni Allaah.”

Na kama Allaah Asingaliwakinga watu, baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangalivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyengine za ibada na Misikiti ambamo jina la Allaah hutajwa kwa wingi. Na bila shaka Allaah Humsaidia yule anayesaidia dini yake. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda.

Wale ambao tukiwamakinisha (tukiwaweka uzuri) katika ardhi husimamisha Swalah na wakatoa Zakaah na wakaamrisha yaliyo mema na wakakataza yaliyo mabaya. Na marejeo ya mambo ni kwa Allaah.”

Al-Hajj: 39-41

 

Katika aya hizi zimetajwa sababu tatu ambazo kwa ajili yake Allaah Ametoa ruhusa ya kupigana vita:

 

Ya kwanza - Kwa sababu ya kudhulumiwa kwa kushambuliwa na kutolewa majumbani mwao pasipo haki kwa sababu wanasema “Mola wetu ni Allaah”.

 

Ya pili – Lau kama Allaah Asingaliwakinga kwa kuwaamrisha kupigana Jihaad, bila shaka yangalivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyengine za ibada na Misikiti ambamo ndani yake jina la Allaah hutajwa kwa wingi.

 

Ya tatu – Sababu ya Waislamu kupewa nusura ya Allaah na kumakinishwa (kuwekwa uzuri) katika ardhi ni kwa ajili ya Kusimamisha Swalah na Kutoa Zakaah na Kuamrisha mema na Kukataza mabaya.

 

 

 

 

Share