Sigara Na Tumbaku: Mtazamo wa Uislamu - 3

 

Sigara Na Tumbaku: Mtizamo Wa Uislamu - 3

 

Imetafsiriwa na Naaswir Haamid

 

Fatwa Kutoka Kwa

Shaykh 'Abdur-Rahmaan Bin An-Naaswir As-Sa'diy

 

Alhidaaya.com

 

 

Utangulizi Umefanywa Na 'Abdur-Razzaaq Al-'Afiyfiy (Rahimahu Allaahu)

 

 

Utangulizi:

 

 

Sifa zote ni Zake Allaah, Bwana wa Ulimwengu wote, Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya Nabiy wetu, Muhammad, na juu ya watu wake wa nyumbani na Swahaba zake.

 

Hakika wanachuoni kwenye wakati wetu wa leo ni wengi, lakini  ni wachache wanaotolea hukumu kutokana na chanzo chake na wakiegemeza kutokana na msingi, wenye kufuatanisha matamshi yao kwa vitendo, na wakikusudia kutafuta ukweli kwa yale yote yanayotokea na kuibuka kutoka kwenye kiini. Na kutoka hapa, miongoni mwa walio wachache alikuwa ni 'Abdur-Rahmaan bin Naaswir Sa'adiy (Rahimahu Allaahu), kwani hakika iwapo mtu atazipigia mbizi kazi zake, kukutana naye na kumchunguza mtindo wa maisha yake katika siku za uhai wake, atakuja kutambua kwamba alikithiri katika utumishi wa elimu, iwapo ni kwa uchunguzi au kutolea fafanuzi. Atakuja kumkutia kwamba yupo juu katika tabia, ucha Mungu katika shughuli zake, na muadilifu na mwenye kupenda haki kwa watu wake na wanafunzi wake, akihimiza umoja kwenye migogoro ambayo inaweza kupelekea mparaganyiko na ugomvi, Allaah Awe radhi naye.

 

Na miongoni mwa kazi zake ni haya maelezo mafupi lakini yaliyo makini kwenye barua aliyoiandika kujibu suala lililoulizwa na ndugu 'Aliy al-Hamd as-Swaalihi kuhusiana na hukumu ya uvutaji sigara. Achilia mbali ukakamavu wake hiyo barua, hakika imefanikisha malengo yake kwa uwazi, kwa uwazi ikiwathibitishia ukweli. Kwa barua hiyo, uchaguzi umewekwa bayana kwa wale wanaoshikamana (na ukweli) na wale wanaofuata matakwa yao kuliko Uongofu kutoka kwa Allaah, kama alivyotumia maandiko mengi kutoka Qur-aan na Sunnah kuwa ndio msingi wa ushahidi wa kuharamisha sigara, na pia israfu inayosababishwa na hali ya mtu kifedha, kimwili, na kijamii kwa jumla.

 

Wala haijuzu kwa mtu yeyote kukaidi kwa kutaja ushahidi mahsusi unaoharamisha uvutaji sigara, huku akiacha maandiko ya jumla, isipokuwa kama akiwa ni mwenye uoni mdogo, dhoofu wa elimu, na mjinga kwenye vyanzo vya Diyn na namna ya kufahamu manufaa kutokana nayo. Hakika ushahidi ndani ya Diyn, kama zinavyojitokeza kuwa na hukumu mahsusi, lakini pia unajitokeza kama ni hukumu za jumla zenye kuvisha zile za mahsusi. Mambo haya ya mashaka na dhana mbovu hazipati nafasi kwa wale wenye kutafuta na kuchunguza ukweli. Mtu atatumia tu aina hizi za hoja iwapo matashi yake yamezidi roho yake na kumtawala, hapo basi atakuwa ni mfungwa wake. Shaytwaan anamlaghai, akimpambia mambo ya kikhabithi, na akiuheshimu ukhabithi; anamfanya Shaytwaan kuwa ni Imamu wake, akimuongoza kwenye upotofu kwa minong’ono na shaka anazozitengeneza.

 

Imekuwa wazi kwamba uvutaji sigara una hatari na madhara mengi, madaktari wa tiba wamethibitisha ukweli huu. Nitanukuu kwa yale waliyoyasema, ingawa, kwa upande mwengine uharamu wa kitu unaharamishwa kutokana na amri ya Allaah na mtu yahitaji kutosheka ndani ya Kitabu chake na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani hizo ndio zilizo wazi na za moja kwa moja na ndio njia iliyo sahihi na humo ndiko kwenye hoja za kuthibitisha kwa wale ambao Allaah Amewapa uongofu na kuelekea njia sahihi. Nimetaja tu kwa wale walio wapofu wa kufuata watu wanaowafikiria kuwa ni wenye elimu, wastaarabu, na wenye kufahamika, wakitafuta njia za kuthibitisha kwamba wale wanaowaiga wamekubali na madhara yake lakini hawayajali.

 

Yafuatayo ni maelezo kutoka kitabu cha Kitaab-ul-Bayaan, kilichoandikwa na Shaykh Ibraahiym 'Abdul-Baawi (Rahimahu Allaahu). Tabibu aliyeeleza ndani ya Adaab al-Muhalla, uk. 122:

 

 

Tumbaku Na Sigara: Kutoka Kwa Afisa Wa Afya Wa Magharibi Bwana Ismaa'iyl Rushdiy

 

Ni mmea ambao Waarabu wanauita: "at-tabaaq" (tumbaku). Kwa muoni wa kikemikali, inaonesha kuwa una chembe chembe za sumu ambazo iwapo yakirambishwa matone mawili kwenye mdomo wa mbwa, hapo hapo atakufa, na matone matano yanatosha kumuua ngamia. Watu makatili hapo kale walikuwa na mazoea ya kuuchakua chakua. Hii ni aina mbaya kabisa inayotumika yenye madhara, kwani inaingia tumboni kupitia kwenye mate. Juu ya upana ulionao wa madhara inayosababisha, matumizi yake yameendelea kukuwa miongoni mwa mataifa mengi.

 

Matababibu wamethibitisha kwamba tumbaku inaathiri moyo na kuufanya moyo kupweta, kusababisha mapafu kukohoa, kulifanya tumbo kukosa hamu, kuyafanya macho kukunjana na mfumo wa ubongo kuutuliza.

 

Tabibu Damardaash Ahmad ameeleza yafuatayo: 

ولم أرى في عيوب الناس عيبا كنقص القادرين على التمام

"Na wala sioni ndani ya makosa ya watu kosa, Kama uoni mdogo unaopatikana ndani ya jambo lililo timu."

 

Siamini kwamba makabila ya watu, tokea kuumbwa kwao, yamejidhoofisha na kujinyanyasa wenyewe mbele ya adui wake kuliko walivyojisalimisha mbele ya uvutaji wa sigara, kwa vile tabia hii imeenea, kujitia minyororo na kujinyanyasa yaliyo mazuri. Imethibiti kwa aina zote za watu, kuanzia watumishi wa maabara wanaochafua hali yao ya hewa na ya familia zao, hadi kwa matabibu wakubwa, wanafalsafa, na wasomi walibatilisha akili zao kwa kujiweka mbali (na madhara yake) huku wakijipamba na mambo ya sanaa na sayansi.

 

Ukweli wa mambo uliyoyathibitisha uchunguzi huu (ni uchunguzi) uliofanywa na Profesa  Diamond Palmer aliyefanya uchunguzi wa mada kwa miaka ishirini, miongoni mwa aliowachunguza kwa pamoja walikuwa ni wasioweza kuacha kuvuta sigara, wenye kuvuta kwa wastani, na wale walioacha kuvuta. Alitengeneza jalada (profile) huko Chuo Kikuu cha Hopkins akieleza ndani yake kila kitu kuhusiana na afya zao, maradhi na mitindo ya maisha yao. Alianza uchunguzi wake mwaka 1919 na kuikamilisha mwaka 1940 akiwa na hitimisho lifuatalo:

 

"Uvutaji wa sigara unafupisha maisha ya mtu kulingana na kiwango anachotumia; wale walioacha wanaishi zaidi kuliko wale wanaovuta kwa wastani, na wale wanaovuta kwa wastani wanaishi zaidi kuliko wale waliokithiri katika kuvuta sigara."

 

Ninamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuongoze kwenye njia sahihi, na kwamba Atupatie uongofu wa kukubali ushauri, na kwamba Atuweke mbali kutokana na yale yote yenye madhara na hatari. Tunamuomba kwamba Atupatie rahmah kwa mwandishi, izae manufaa kazi yake, na itufanye sisi kukutana na ustahamilivu wa hali ya juu.

 

Na Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya Nabiy wetu Muhammad, na watu wake wa nyumbani na Swahaba zake.

 

'Abdur-Razzaaq al-'Afiyfiy

 

 

Hukumu Kuhusiana Na Sigara

 

Ifuatayo ni barua kutoka kwa mheshimiwa, Shaykh, 'Abdur-Rahmaan an-Naaswir as-Sa'adiy (Rahimahu Allaahu), ambayo ameandika akijibu suala ambalo nililiulizia kutokana na mjadala uliofanyika baina yangu na Muislamu mwengine kuhusiana na hukumu ya uvutaji sigara. Na kwa kuwa maelezo haya hayakupatikana kwa mtu mwengine yeyote, nimehisi kuwa na jukumu la kuiweka mbele, nikikhofia adhabu na dhambi ya kuficha elimu, na halikadhalika kutaraji kutoka kwa Allaah kwamba Anijaalie mimi, mwandishi na Waislamu wengine kunufaika nayo.

 

Yafuatayo ni maandiko ya suala hilo na jibu kama lilivyoandikwa na mnukuaji (Rahimahu Allaahu).

 

Kutoka: Mwanao, 'Aliy bin Hamd as-Swaalihi.

Kwa: Wako Mheshimiwa, Shaykh muadhamu, 'Abdur-Rahmaan an-Naaswir as-Sa'adiy.

 

 

Assalamu 'Alaykum wa RahmatuLlaahi wa Barakaatuh:

 

Ninakuomba utunufaishe kwa kutuelezea hukumu kwa nji za wazi kuhusiana na uvutaji sigara na biashara yake, je ni haraam au makruuh[1]? Tafadhali tupatie hukumu.

 

 

Jibu:

 

Na kwa Allaah kuna Tawfiyq, tunamuomba kwamba Atuongoze na ndugu zetu Waislamu.

 

Uvutaji sigara, biashara yake na vinavyonasibiana navyo hakuna shaka yoyote ni haramu. Si ruhusa kwa Muislamu kujinasibisha nayo, iwapo kwa uvutaji au kwa biashara, na ni wajibu wa yule mtu anayefanya hivyo kurudi kwa Allaah kwa kutubia kikweli kweli, kwani ni wajibu wa kutubu kwa madhambi yoyote. Hii ni kwa sababu ya ukweli kwamba yapo maandiko ya jumla kuhusiana na uharamu wake, kwa matini yake ya jumla na kilugha. Uharamu huu ni kwa sababu ya madhara yake kwa Diyn ya mtu, maendeleo, hali yake ya kifedha, na sababu yoyote kati ya hizi yatosha kuiharamisha.

 

Ama kwa madhara yanayomsababishia mtu kwenye Diyn yake na ushahidi wa maandiko kuhusiana na uharamu wake, zinaweza kupatikana kwa njia tofauti:

 

Kutokana na ushahidi wa maneno Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ

Na anawaharamishia maovu..[Al-A'raaf: 157]

 

Na Tamko Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ ۛ

Wala msijitupe katika maangamizi kwa (kuzuia) mikono yenu (isitoe). [Al-Baqarah: 195]

 

Na Tamko Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا ﴿٢٩﴾

Wala msijiue. Hakika Allaah ni Mwenye kuwarehemuni. [An-Nisaa: 29]

 

Kwa kupitia Aayah hizo hapo juu na nyenginezo zinazofanana nazo kwenye maana, Allaah Ameharamisha vitu vyote ambavyo ni khabiithi na vyenye kusababisha hasara, na khubth na hasara vinatambulika kutokana na athari na madhara yake kutokana navyo. Sigara ina athari nyingi mbaya ambazo watu wote wanazielewa, haswa wale wanaonasibiana nayo. Lakini nguvu zao zimehimilikiwa; ingawa wanatambua madhara yake, matashi yao yanawabeba juu. Wanachuoni wameeleza kwamba vyakula na vinywaji vyote vyenye madhara hakika ni haramu.

 

Kutokana na madhara yake yanayosababisha kwa Diyn ya mtu, inakuwa ni tabu kwa mja kufanya matendo ya 'Ibaadah na kutimiza yale aliyoamrishwa, haswa kwa upande wa Swawm, na ukweli ni kwamba chochote kitakachotengua matendo mazuri basi hicho wenyewe ni ovu. Uvutaji sigara pia unahamasisha mtu kujiweka karibu na watu waovu kuliko watu wema. Hii ni miongoni mwa hasara kubwa, kwani inasababisha uadui na uchukivu kwa watu wema na majadiliano ya namna ya kufuata mitindo yao ya maisha. Na hii ndio kesi haswa ya watoto na vijana wakubwa, kwani pale wanapoathirika na mtihani huu, hapo hapo wanajigeuza na kujiingiza kwenye mishughuliko ya kihuni. Uvutaji sigara unaenda mbali hadi kuharibu tabia, inakuwa ndio mlango wa kuingilia kwenye maasi makubwa.

 

Ama kwa hasara unazosababisha kwa mwili, ni ukweli ulio wazi, kwani unapitia kwenye mirija na kujitengenezea njia ya kuenea mwili mzima. Inadhoofisha uoni wa macho, inadhoofisha uzima wa mwili, na kuzuia mwili kunufaika ilivyo na manufaa ya chakula. Pale sifa hizi zinapokutana kwa pamoja, inaongeza ukubwa wa madhara.

 

Tunaposema madhara yake mabaya ni kwamba inadhoofisha moyo, kuparaganya kazi zake za kawaida za mfumo wa ubongo, na kusababisha ukosefu wa hamu ya kula. Pia inasababisha ukohozi wa hali ya juu hadi kuweza kusababisha ukosefu wa pumzi na msongo wa pumzi (suffocation), na waathirika wengi imewadhuru na kusababisha uharibifu!

 

Matabibu bingwa wamehitimisha kwamba uvutaji wa sigara ni sababu kuu za maradhi yanayohusiana na kifua, kwa mfano kifua kikuu na maradhi mengine yanayotokana nayo. Pia ina nafasi kubwa ya kusababisha saratani, maradhi ambayo ni yenye kuumiza sana na mabaya mno.

 

Pia inashangaza kwamba tunawaona watu wenye vipaji vya akili ambao wanalenga kuzilinda afya zao wakiendelea kuvuta sigara, wakati madhara mengi kama haya yametambuliwa na yanajulikana. Na ni maradhi mangapi yamejikusanya kutokana na sigara hii na hadi kuwa taabu kwa matabibu kutibu? Na ni watu wengi wangapi wamedhoofika haraka kutoka hali ya kuwa na nguvu?!

 

Na pia inashangaza sana kwamba watu wengi wanafuata ushauri wa matabibu kwenye masuala yasiyokuwa makubwa kama haya. Ni kwa namna gani wanachukulia jambo hili la hatari kuwa ni jepesi? Hili bila ya shaka ni kwa sababu ya kuyasalimisha matashi yao yachukuwe hatamu ya mawazo yao, udhoofu wa kushindwa kuidhibiti, na kuiacha kuwa ni mtindo wa maisha yao, hata baada ya kuelewa madhara yake yalio mengi.

 

Na wala sio jambo la kushangaza kwamba matabibu wengi pia wanavuta sigara, wakati wanakubali kwa matamshi yao wenyewe kwa hali zao na kuanguka kwa afya zao, kwani matakwa yao yanawabeba kuliko utaalamu wao na upambanuzi; ingawa wanaelewa fika madhara yake, bado tu wanaendelea kuivuta.

 

Hakika tumebainisha kwa ufupi yale madhara yanayonasibiana na sigara, pamoja na ukweli kwamba inasababisha uchafu kubakia kwenye mdomo na kupiga weusi, pia ukingo wa midomo yake (lips) na ulimi, na kusababisha ubovu na uozo wa meno.

 

Pia inasababisha mnyororo wa maradhi ya kutisha, na iwapo mtu atafanyia uchunguzi madhara yake, atakuja kugundua mengi zaidi kuliko yale tuliyoyaeleza.

 

Na kwa hasara inayosababisha kwa hali ya mtu kifedha, imesimuliwa kwa njia sahihi kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Kwamba ameharamisha ufujaji wa pesa."

 

Na lile linaloweza kuwa uharibifu zaidi kuliko kuziunguza katika sigara kwamba: "Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa.[2]"na hakika hakuna manufaa yoyote kwa mnasaba wake (sigara). Wale waliojikita katika uvutaji sigara wanakutana na maumivu makali ya kupoteza viwango vikubwa vya pesa kwa sababu yake, hadi kufikia kwamba wanaweza kuacha kutumia pesa zao kwa lile lililo wajibu juu yao. Hakika hili ni upotevu wa hali ya juu na kusababisha madhara zaidi. Kutumia pesa kwa lile ambalo halina manufaa hakika limeharamishwa, hivyo ni kwa namna gani mtu anatumia kwa lile linalojulikana kuwa na madhara?

 

Kutokana na ukweli kwamba sigara hizi zinaleta madhara kwa Diyn ya mtu, mwili, na hali ya kifedha, basi pia biashara yake ni haramu, na ni jambo lisilofaa, lisilo na faida. Watu wengi wameshuhudia kwamba wale wanaojinasibisha na biashara yake, hata kama watafaidika nayo pale walipoanza biashara zao, hatima yake wamekumbana na upotevu wa mali. Na kwa hakika watu wa Najd, na shukrani zote ni za Allaah, wanachuoni wote wanakubaliana kuhusiana na uharamu wake, na watu wasio na elimu wanawajibishwa kufuata wanachuoni. Hairuhusiwi kwao kufuata matakwa yao, kubadili maana au kutoa hoja kwamba kuna wanachuoni kutoka ardhi nyengine wanaoeleza kuhusu uhalali wake na sio uharamu wake. Aina hii ya hoja hairuhusiwi na ijmaa[3] ya wanachuoni, kwani watu wajinga ni lazima wafuate wanachuoni; hawapo huru dhidi yao. Si ruhusa kwao kukataa matamko ya wanachuoni wao, na hili ndio lililo miongoni mwao, kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliposema ndani ya Qur-aan:

 

 فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٧﴾

Basi ulizeni watu wa ukumbusho mkiwa hamjui. [Al-Anbiyaa: 7]

 

Na wala hakuna usawa kwenye hoja hii mbovu, ambayo imejaa katika ndimi za baadhi ya wajinga kwa kufuata matakwa yao badala ya ukweli na uongofu, isipokuwa ni wenye kusema: "Kuna baadhi ya wanachuoni ndani ya ardhi nyengine ambao hawaoni kuwa ni wajibu wa itmi'naan[4]ndani ya Swalah, kwa hivyo msitukatalie pale tunapowafuata." Au, "Kuna baadhi ya watu wanaoona uhalali wa riba, kwa hivyo ni chaguzi yetu kuwafuata au laa." Au, "Kuna baadhi wasioharamisha ulaji wa ndege wenye kucha (za kuwindia), kwa hivyo ni chaguzi yetu iwapo inatuwajibikia kuwafuata." Iwapo mlango huu umefunguliwa, maasi mengi yatafanywa ruhusa kwa watu, na itakuwa ni sababu ya mgawanyiko wa Diyn. Kila mtu anaelewa fika kwamba matamko kama hayo hakika yanapelekea mgongano kwa lile ambalo limeshaelezwa ndani ya Diyn pamoja na matamko ya wanachuoni, na ni kutokana na mambo hayo ambayo hairuhusiki.

 

Njia sahihi ya kutathmini ni kupitia misingi mikuu ya Diyn, na zinakubaliana juu ya uharamu wa sigara. Hii ni kwa sababu zilizo nyingi katika kusababisha madhara yake mabaya. Chochote chenye kumletea madhara mja, iwapo ndani ya Diyn, mwili, au hali ya kifedha, na wala hakina manufaa yoyote inaharamishwa. Na ni kwa namna gani kwa kesi ambayo madhara yasiyohesabika yatapatikana ndani ya ovu moja? Je hakuna uwajibikaji, kidini, kielimu, na kiafya, kwamba iachwe na kuwa ni onyo dhidi yake, na kwamba ushauri upelekwe kwa wale wenye kuikubali?

 

Ni jukumu la wale ambao ni wenye kujitakia mema juu yao na kuipatia miili yao chenye maana na faida, kwamba warudi kwa Allaah kwa njia ya kutubia, na kwamba waombe kujifunga bila ya kurudi nyuma na kuomba msaada kutoka kwa Allaah, kwani yeyote anayefanya hivyo, Allaah Atawasaidia na kuwafanyia wepesi kufanikisha lile waliloazimia.

 

Kinachohamasisha hiki ni kuelewa kwamba yeyote anayeacha jambo kwa Allaah, Anabadilisha kwa lililo bora. Pia, kama yalivyo malipo ya matendo ya utiifu kwamba ni yenye taabu kuyatekeleza ni bora zaidi kuliko yale yasiyokuwa na taabu, hayo pia ni kwa kuacha madhambi yaliyokuwa magumu kuyaacha. Kwa hivyo, yeyote aliyepatiwa Uongofu na Msaada wa Allaah, basi atakumbana na mashaka mwanzoni mwa siku zake, lakini baadaye inapandishwa kidogo kidogo, hadi Allaah Anakamilisha msaada Wake juu ya mja Wake na kumliwaza kwa Mapenzi ya Allaah na Ulinzi Wake na Msaada. Anakuwa muaminifu kwa ndugu zake kama alivyokuwa muaminfu kwake mwenyewe, na Tawfiyq (mafaniko kutoka kwa Allaah) yapo Mkononi mwa Allaah. Na yeyote anayemuamini Allaah ndani ya moyo wake na kumtaka msaada kwa dhati kutokana na yale Aliyoamrisha na kuacha yale Aliyoharamisha, Allaah Atamfanyia njia ya Jannah (Pepo) na yote mema yatakuwa mepesi kwake, na Atamuweka mbali kutokana na Moto. Hivyo tunamuomba Allaah kwamba Atuongoze kwenye mema, na Atulinde kutokana na maovu, hakika Yeye ni Mkarimu, Mwingi wa Rahmah na Mwenye Mapenzi.

 

'Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa'diy Rabi'ul-Awwal, 1375 AH Imenukuliwa na: 'Aliy al-Hamd as-Swaalihi.

 

 

Namna 'Abdul-Laatwiyf Bin Ibraahiym Aalish-Shaykh (Mwenyekiti Wa Idara Na Vitivo) Alivyoiunga Mkono Fatwa ya Shaykh Sa'diy

 

Sifa zote ni Zake Allaah, Bwana wa Dunia zote, Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya Nabiy wetu, Muhammad, na juu ya watu wake wa nyumbani na Swahaba zake.

 

Nimepitia kile ambacho ameandika al-Allaamah ash-Shaykh 'Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa'diy katika kujibu suala lililoulizwa kuhusiana na hukumu ya uvutaji sigara na biashara yake. Nimeona kwamba amejibu kwa njia sahihi na yenye manufaa, na kwamba amelifafanua jibu kwa njia ya wazi na mtindo wa moja kwa moja akiwa na ushahidi sahihi kutoka Qur-aan Tukufu, Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kutoka matamko ya wanachuoni wanaotuliza nyoyo, wakifichua madhara yanayosababisha maisha ya mtu kiafya na kiroho na pia kile kinachonasibiana kutokana na hiyo sigara kuanzia israfu ya pesa na kukosa heshima kutoka kwa watu. Na pia ameelezea uharamu wa matumizi na biashara, na kwamba imeshakubaliwa na wanachuoni walio wengi, insha Allaah Amlipe, Amsamehe na kuwa radhi naye.

 

Imeelezwa na: 'Abdul-Laatwiif bin Ibraahiym Aal-ish-Shaykh.

 

Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya Muhammad.

 

 

Namna Shaykh 'Abdul-Muhaymin Abu Samh (Imaamu Wa Al-Masjidul-Haraam) Alivyounga Mkono Fatwa ya Shaykh Sa'diy

 

BimsimiLlaahir Rrahmaanir Rahiym, Rahmah na Amani za Allaah ziwe juu ya kiongozi wetu Muhammad, aliyesema:

 

"Sikuacha chochote ambacho kitamkurubisha mtu karibu na Allaah isipokuwa kwamba nimekieleza na kukiamrisha, na wala sijaacha chochote ambacho kitamweka mtu mbali na Allaah isipokuwa kwamba nimekieleza na kuwazuia, hivyo chochote nilichowaamrisha, fanyeni kadiri ya utakavyoweza, na chochote nilivyowazuia, acheni."

 

ni mfano wa:

 

Nimesikia jibu ya Shaykh 'Abdur-Rahmaan bin Sa'diy (Rahimahu Allaahu) na Amsamehe, ndani ya hukumu, kuhusiana na uvutaji sigara. Ukweli ni kwamba ni jibu maridhawa na lenye manufaa, na iwapo mtu angependelea kuzungumzia kuhusiana na jibu hilo kwa kusherehesha kuliko Shaykh huyo (Rahimahu Allaahu), ataona kuna mengi ya kuzungumza na ushahidi mwingi unaofungamana nayo, kama vile tamko la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Mguu wa mwanaadamu hautaondoka Siku ya Hukumu kutoka katika kisimamo mbele ya Rabb wake hadi aulizwe kuhusu mambo matano: maisha yake – namna alivyoyatumia, ujana wake – namna alivyoutumia, mali yake – wapi alipoipata na vipi aliitumia, na namna gani alifuata kile alichokuwa anakijua." [Imesimuliwa na Ibn Mas'uud na Abu Barzah. Imepokewa na at-Tirmidhiy. Imesahihishwa na al-Albaaniy].

 

… au Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾

Na kuleni na kunyweni; na wala msifanye israfu. Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu. [Al-A'raaf: 31]

 

Aayah hii ni mnasaba wa yale mambo ambayo yamehalalishwa yasiyokuwa na shaka, iweje kwa lile ambalo maandiko na ushahidi wa wenye akili unakubaliana kila moja katika kukubali uharamu wake, pamoja na kuwa ina harufu mbovu, ukosefu wa hamu ya kula, kutoweza kuzaa, kudhoofika afya, na mengi mengineyo mfano wa hayo!!!

 

Imeelezwa na: 'Abdul-Muhaymin Abu Samh, Imaamu wa Masjid al-Haraam.

 

 

Itaendelea In shaa Allaah…

 

 

 

 


 

 

 

[1] Makruuh: Kama ilivyofasiliwa ndani ya Uswuulul-Fiqhi (Msingi wa Maarifa ya Shari’ah), ni lile tendo ambalo lina malipo iwapo litaachwa, na halina adhabu kwa mwenye kulifanya.

[2]  Utajo ndani ya Suwraah Al-Ghaashiyah: 7.

[3] Ijmaa: Mawafikiano ya wanachuoni, ambayo yanatambulika kuwa ni ushahidi wa kisheria kwa tamko la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Ummah wangu hautakutana pamoja kwenye (kwa lile lenye) upotofu."

[4] Itimi'naan: Hali ya kuwa na utulivu katika kila nguzo ya Swalaah, ili kuruhusu mifupa kubakia kwenye sehemu yake ya asili kabla ya kuendelea katika nguzo nyengine.

 

 

Share