012-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Sita

SURA YA SITA

 

HUKUMU

 

 

Hukumu

 

Hukumu (hukm) inatolewa tafsiri kuwa ni kile ambacho kinasuluhisha au kinamaliza mgogoro. Hukumu inaweza kuwa ni ya maelekezo, inayomuelekeza yule aliyeshindwa (judgement-debtor) kumpa chochote kwa aliyeshinda (judgement-creditor). Au kuzuia, kama pale kesi inapoamuliwa dhidi ya mdai ikiwa kwamba hana mamlaka ya kupatiwa haki aliyodai. Hukumu na amri za Mahkama ni lazima ziheshimiwe.

 

Pale hukumu inapotolewa, suala linaibuka, nani inayemshika hukumu ama amri hiyo? Ni kwamba inawashika wadaawa na pia wale ambao Shari'ah inawaruhusu kuwakilisha, lakini sio kwa wengine. Ama baina yao, suala linaamuliwa kuwa limekhitimishwa na kwamba haiwezi kusikilizwa baadaye (res judicata), isipokuwa kwa kesi maalum. Hivyo, hukumu kwa mnasaba wa mali dhidi ya mtu mwenye kuihodhi hiyo mali, inamshika huyo anayehodhi mali hiyo yeye peke yake na wale wanaopata manufaa nayo hiyo mali kutoka kwake lakini sio wengine.[1]

 

Hata hivyo, kwa mujibu wa Rukuu’l-Islaam, hukumu dhidi ya mtu mwenye kuhodhi mali anayedai kwamba mali hiyo ni waqf inawafunga watu wote. Lakini sio hivyo kwa maoni ya Abu Layth na Sadnu’sh-Shahiid.[2] Na kama ilivyotajwa, hukumu dhidi ya mrithi wa wasia, kuzungumza ukweli, inaifunga mali ya urithi.

 

Hukumu ya Mahkama inaweza kuwa batili katika mazingira fulani. Kwa mfano, kama imekwenda kinyume na Shari'ah maalum kama haki za msingi (mfano haki ya kusikilizwa) au kama imeegemezwa katika ushahidi usiokubalika kutumika Mahkamani au kama imempendelea mtu ambaye Hakimu ana faida naye, kama vile baba, mama, mke au watoto.

 

Sheria kwa upande wake pia inaweka pingamizi ya kufunguwa kesi ambayo imeshatolewa hukumu hapo kabla. Pingamizi hii ni kwa wadaawa wale wale na madai yale yale yaliyofunguliwa kwenye Mahkama nyengine.[3] Kwa mfano, A mdai na B ni mdaiwa, A anadai B kuvunja makubaliano ya mkataba. Mahkama X ikaamua B kumlipa fidia A kutokana na kuvunja mkataba huo. Mahkama Y ambayo ina hadhi sawa na Mahkama X (kwa mfano zote ni Mahkama za Wilaya) haiwezi kuisikiliza tena kesi baina ya A na B kwani imekwishatolea ufumbuzi. Isipokuwa B anaweza kukata rufaa katika Mahkama ya juu (kwa mfano Mahkama ya Mkoa).[4]

 

 

Kutoa Hukumu

 

Hukumu iwe kwa maandishi kwa mujibu wa mawazo ya wanavyoni. Al-Bayhaqiy amenukuu Hadiyth inayosema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha kuandikiwa wakfu kwa ajili ya Ansaar (wasaidizi wa Muhajiriyn huko Madiynah). Waliomba kwamba hiyo iandikwe kwa ndugu zao wa Ki-Quraysh. Hivyo al-Bayhaqiy amesema kwamba Hakimu anaweza kuandika hukumu yake kwa upande wenye kesi pale anapoombwa.[5]

 

Ibn Qudaamah, hata hivyo, ana mawazo ya kwamba nakala mbili za hukumu zitayarishwe, moja itunzwe chumba cha kumbukumbu (diwaan) na nyengine kama ikiombwa ipelekwe kwa aliyeshinda kesi.[6]

 

Al-Kasaniy, ameeleza tabia ya mwenendo wa Kimahkama enzi za leo, kumbukumbu ya madai pamoja na tarehe iandikwe kwanza, kisha majina ya mashahidi na kisha majibu. Kumbukumbu hii inawekewa mtindo wa mwezi au mwaka, kwenye mkoa au kesi au faili (linaloitwa qimatrah) ikiwa na muhuri wa Mahkama.[7]

 

Sheria inaeleza kwamba, Hakimu atatamka hukumu pale kesi itakaposikilizwa. Baadaye itafuatia amri ya hiyo hukumu.[8] Masharti mengine muhimu yanayoeleza namna ya kutayarisha hukumu ni kama yafuatayo:

 

  1. Ni lazima itamkwe hadharani (open court)
  2. Iwe kwa maandishi
  3. Hakimu hana ruhusa ya ya kuiacha hukumu kusomwa na msaidizi wake
  4. Iwe na tarehe
  5. Isainiwe na Hakimu
  6. Iwe na maelezo ya kesi
  7. Namna alivyofikia kwenye hukumu hiyo (maoni ya Hakimu)
  8. Ioneshe maamuzi aliyofikia
  9. Sababu ya maamuzi hayo kufikiwa hivyo
  10. Hoja za msingi na namna ilivyozichunguza hoja hizo[9]

 

 

Athari Ya Maoni Binafsi Ya Hakimu

 

Kwa mujibu wa wanachuoni walio wengi, Hakimu anaweza kuihukumu kesi kulingana na uelewa wake binafsi wa ukweli wa kesi. Abu Haniyfah anasema kwamba, uamuzi kama huo unakubalika kwenye kesi tu ambapo ukweli ulitambulika kwenye uelewa binafsi wa Hakimu baada ya kuteuliwa kushika ofisi.[10]

 

Hakimu Abu Yuusuf ana mawazo kwamba, uamuzi huo ni sahihi isipokuwa katika kesi za jinai (kama uzinifu, wizi n.k.)[11]

 

Maalik kwa upande wake, anakataa Hakimu kutumia uelewa wake binafsi wa kesi.[12]

 

Al-Mawardi ametoa mawazo kwamba, Hakimu aitamke ndani ya hukumu iwapo amefikia uamuzi wa kesi hiyo kwa mujibu wa uelewa wake binafsi wa kesi hiyo.[13] Wanachuoni wengine wanakubali Hakimu kutumia uelewa wake binafsi bila ya kikwazo au lawama.[14]

 

Sheria kwa upande wake inaruhusu kuwepo maoni binafsi ya Hakimu. Hata hivyo, wakati wa kuisoma hukumu ni lazima Hakimu aeleze maoni hayo na sababu ya kuyaingiza hadi kufikia hukumu hiyo anayoitoa.[15]

 

 

Kikaza Hukumu (Execution Of Decree)

 

Hii ni hati inayotolewa baada ya hukumu kusomwa ili kuifanyia kazi hukumu hiyo kwa vitendo. Mfano hukumu ya kuruhusu kuvunja nyumba, kikaza hukumu chake ni hati ya kuivunja nyumba hiyo.

 

Hukumu bila ya kufanyiwa kazi, haina nguvu kama alivyosema ‘Umar kumwambia Abu Muusa al-Ash’ariy kama ilivyoelezwa mwanzo wa kitabu hiki. Kwa mujibu wa al-Marghinani, kikaza hukumu kitolewe na Mahkama hiyo hiyo iliyotoa hukumu. Kwa sababu hukumu bila ya kuifanyia kazi haikutani na haki inayostahiki. Kama Hakimu ametoa kikaza hukumu na kuiacha izagae ofisini, Hakimu atakayerithi ataifanyia kazi, kuwa nayo na kuipa nguvu kikaza hukumu hicho kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na waliomtangulia kwa lengo la kufanyiwa mapitio.

 

Pale hukumu inapotolewa kwa upande wa kesi, Shari’ah pia inatoa ruhusa ya kuifanyia kazi na kuiwasilisha kwa wakala wa Mahkama hiyo kwa kuipa nguvu (tafiydh). Hukumu ni lazima ikaziwe kwa kumlazimisha aliyeshindwa kuifuata na ulazima huo kwa kawaida unafanyiwa kazi kwa kumpeleka jela mshindwa hadi atii.

 

Kama hukumu inaweza kuthibitishwa kwa kupelekwa mali maalum au kwa uuzaji wa mali ya aliyeshindwa, Mahkama itatoa amri kwa kupelekwa jela au kuuzwa. Hili litafanywa, pale tu, mshindwa kwa hali nyengine hatimizi hukumu.[16] Kwenye ukazaji wa hukumu ya pesa, mshindwa atafungwa jela iwapo atarudisha nyuma jitihada za kuifanyia kazi hukumu; lakini kama ataweza kuithibitisha Mahkama kwamba hana mali au uwezo, hakutakuwa na sababu ya kufungwa jela. Kama Mahkama hiyo itatambua kwamba mshindwa ameficha mali yake au amekataa kulipa kiwango kilichotajwa ndani ya hukumu, ingawa ana uwezo wa kulipa, basi atafungwa jela hadi alipe. Lakini, kama Hakimu anaona kwamba aliyeshindwa amesota sana jela, ataachiwa huru.

 

Kwa upande wa Sheria, tunaona kwamba mshindi anahitajia kuandika barua ya maombi kwa Hakimu ili kuifanyia kazi hukumu iliyotolewa. Barua hiyo ioneshe mambo yafuatayo:[17]

 

  1. Nambari ya kesi
  2. Majina ya pande za kesi (mdai na mdaiwa)
  3. Tarehe ya hukumu
  4. Iwapo imependekezwa rufaa yoyote
  5. Iwapo yamefanywa malipo kwa Mahkama au baina ya wadaawa
  6. Iwapo kuliwahi kufanywa ombi kama hili hapo kabla
  7. Kiwango cha pesa (malipo au fidia) kilichotozwa
  8. Jina la yule aliyeshindwa kesi
  9. Msaada wa mahkama katika kuifanyia kazi hukumu hiyo:

a)    Iwapo kwa kufikisha mali Mahkamani

b)    Kuiuza mali

c)     Kuteuliwa kwa mpokeaji

d)    Iwapo Mahkama tayari imeshatoa maelekezo

 

 

Marejeo (Reference) Na Mapitio (Review)

 

Shari’ah inaruhusu mapitio ya hukumu kwenye kesi ambapo imekiuka kanuni za Shari’ah, hapo kesi itasikilizwa tena kwa mara nyengine.

 

Wanachuoni hawakujihusisha na marejeo za kesi kwenda Mahkama nyengine au mapitio kwa chini zaidi. Muongozo kuhusiana na hili, unaweza kuchukuliwa kutokana na simulizi refu iliyopokewa na Waki’ katika Akhbaar-al-Qudhaah ambapo ‘Aliy ameripotiwa kusema kwa wenye kugombana ambapo kesi ilihukumiwa na yeye:

 

Ikamateni hukumu yangu kwa muda, mpaka mukutane mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuhukumu kesi yenu.[18]

 

Kutokana na mapokezi haya, tunaweza kuamua kwamba:

 

1)  Amri ya muda inaruhusika (ad interim injuctions), na

2)  Hakimu anaweza kuwasilisha kesi kwenye mamlaka ya juu ikiwa haiangukii kwenye uwezo wake wa Kimahkama au ameona ni vyema kuamuliwa na mamlaka ya juu.

 

Maneno ya ‘Umar katika barua yake kwenda kwa Abu Muusa al-Ash’ariy inasema:

 

Jiepushe na hukumu yako ya jana, ambayo umetanabahi kwenye akili yako na ukaongozwa njia sahihi kurudi kwenye hukumu ya haki, kwa sababu haki inasimamishwa, na hakuna chochote kinachobatilisha kuliko haki, kwa sababu ni bora kurejea kwenye usahihi kuliko kuendelea na lisilo sahihi.

 

Kwa mujibu wa al-Marghinani, ni mzigo juu ya kila Hakimu kusimamia na kuipa nguvu kikaza hukumu cha Hakimu mwengine, isipokuwa kama ama hicho kikaza hukumu kitakuwa ni kinyume na hukumu za Qur-aan au Sunnah, au maamuzi dhidi ya makubaliano ya wanachuoni.[19]

 

Kwa ujumla, si vizuri kumpinga Hakimu aliyetangulia kutoa hukumu nyengine juu ya kigezo cha tofauti za mawazo kwa mnasaba wa mada ya Kishari'ah kama ilivyoshauriwa ndani ya al-Jaami’ as-Saghiyr ya Muhammad na kunukuliwa na al-Marghinani ndani ya al-Hidayah.[20]

 

Al-Hilli anasema kwamba Hakimu aliyemrithi Hakimu aliyeondoka, akiona makosa fulani ndani ya maamuzi ya baadhi ya Mahakimu, Hakimu aliyerithi anaweza kufanyia kazi kikaza hukumu kwa niaba yake.[21]

 

Sheria inaeleza kwamba Hakimu anaweza kumuomba Hakimu aliye juu yake kuipitia kesi. Kwa mfano Hakimu wa Wilaya kumuomba Hakimu wa Mkoa kumpatia maoni.[22]

 

Iwapo upande mmoja wa kesi umeona kwamba haujatendewa haki, unaweza kuomba mapitio katika Mahkama iliyoitoa hukumu yake. Utaratibu huu unaweza kufanywa iwapo hukumu yake ilitoa nafasi ya rufaa au haikutoa.[23]

 

Mahakama Kuu inaweza kuamrisha kupatiwa jalada la kesi kutoka Mahkama zilizo chini yake. Mahkama Kuu inaweza kuamrisha vyenginevyo iwapo itatambulika mambo yafuatayo:

 

  1. Iwapo Hakimu ametumia nguvu zisizo zake (unauthorized jurisdiction)
  2. Ameshindwa kutumia ipasavyo nguvu aliyopatiwa
  3. Amefanyia kazi nguvu zake kwa njia zisizo sahihi[24]

 

 

Amri Ndogo Ndogo (Ancillary Orders)

 

Mahkama imepewa nguvu ya kutoa amri ndogo kwa malengo ya kukitunza kiini kikuu cha mzozo. Kwa mfano inawezekana kutokea kwamba wadaawa wote wana malengo ya faida katika mali fulani, waweza pia kuwa hawapo mbele ya Mahkama na pirika zao hazijulikani. Kwa kadhia kama hizo, Mahkama inalinda hifadhi za faida za wengine kwa kuteuwa mpokeaji au kwa kuchukua ulinzi kutoka kwa upande wenye kuihodhi. Kwa mfano, kama mali imehodhiwa na mtu, na mtu mwengine anatoa ushahidi kwamba ni mali ya baba yake aliyefariki na kumuacha yeye na ndugu aliyepotea. Hakimu anapotengeneza hukumu kuhusiana na nyumba hiyo kwa faida ya mdai, ni lazima, kwa mujibu wa Abu Haniyfah, awache gharama nyengine kwenye mikono ya mtu aliyeihodhi, bila ya kuchukua ulinzi kutoka kwake.[25] Lakini kwa mujibu wa wafuasi wa Abu Haniyfah, kama mtu mwenye kuihodhi mali atatoa ukweli wa mgogoro kwamba ilimilikiwa na aliyefariki, ni lazima iondoshwe kutoka kwenye mikono yake na ikabidhiwe kwa mtu muadilifu ili kuikamata kwa niaba ya mrithi asiyekuwepo.

 

Hivyo hivyo, ni lazima Mahkama ichukue ulinzi pale inapoamrisha mume kulipia huduma kwa mwanamke anayedaiwa kumkimbia mke huyo.

Hakimu ndani ya Sheria anaweza kutoa amri nyengine ndogo ndogo ambazo anaamini zinafaa. Kwa mfano amri ya kuizuia mali, kufanya jambo, kumuamuru mtu kula kiapo juu ya mtu fulani anayehusiana na mali.[26]

Kuna kesi ambazo zinatolewa amri ya kuuzwa mali kabla ya kumaliza kesi (interlocutory orders). Hizi ni mali ambazo zinaweza kuhamishika. Kwa mfano katika kesi ya gari baina ya A na B, ambayo kwa amri ya Mahkama gari hiyo imehodhiwa kabla ya hukumu (attached before judgement). A ambaye gari hiyo imesajiliwa kwa jina lake, anakhofu kwamba kwa kipindi ambacho kesi itakuwa imesimama, gari hiyo inaweza kuharibika au kufisidika thamani yake. Katika hali kama hiyo, A anaweza kuomba kwa Hakimu kwamba gari hiyo iuzwe mara moja.[27]

 

Kizuizi (Time Barred)

 

Ni utaratibu wa nchi nyingi kuweka kipindi cha kuzuia kusikiliza kesi. Ili kwamba; kama mdai atakuja Mahkamani baada ya kumalizika kipindi kilichotajwa, kesi yake haitosikilizwa.

 

Ni kawaida kuwepo uteuzi wa Hakimu ambaye anakuwa na mamlaka fulani tu kwenye kutolea hukumu. Kwa mfano Hakimu kwa ajili ya migogoro ya ndoa, mirathi tofauti na yule wa masuala ya nyumba, ardhi, jinai nk. Hali kadhalika, amri ya kumzuia Hakimu asisikilize kesi itakayovuka kipindi kinachotakiwa ipo ndani ya mamlaka yake. Kwa mfano, A kudai kuibiwa mazao yake miaka 15 iliyopita.

 

Wasomi wa leo, wamekubaliana kwamba amri kama hiyo ni kwa mujibu wa kanuni za Shari’ah za Kiislamu.[28] Dhana ya kale ya Shari’ah, hapana shaka ilikuwa kwamba haki ya mtu haitopotea kwa sababu ya kupita muda na kwamba ni mashaka kwa Hakimu kusikiliza dai lake.[29] Hata hivyo, inawezekana kwamba, kuanzishwa kwa Shari’ah ya kizuizi ni kielelezo cha nguvu kwa ukweli kwamba Shari’ah kwa kipindi kirefu, imekuwa inatafuta njia za kujifananisha na mazingira ya wakati na Shari’ah haijakataa kanuni hii.[30]

 

Sheria ya Kuzuia Kufunguliwa Kesi[31] Mahkamani imeweka jedwali ambalo linaonesha aina tofauti ya kesi, na kizuizi cha idadi ya siku kwa ajili ya kufungulia kesi. Kwa mfano A ameingiliana mkataba wa ujenzi na B, B ameshindwa kuondosha mabaki ya vifaa vilivyotumika katika ujenzi. A akitambua kwamba ni wajibu wa B kuifanya kazi na bila ya kufungua kesi ndani ya siku tisiini (90) atazuiliwa kumdai fidia B katika Mahkama.[32]

 

 

Ushauri Wa Wanachuoni

 

Hakimu anaweza kuwaendea wanachuoni kwa ajili ya ushauri kama vile Mufti na Maulamaa kuhusiana na vifungu vya Shari’ah. Jambo hili sio tu linaruhusiwa bali kupendekezwa na wanachuoni. Fikra hii pia inathibitishwa na mapokezi kutoka kwa Maswahaba ambayo inawekwa hapa chini kwa manufaa zaidi:

 

‘Uthmaan bin Affaan alimuomba ‘Abd Allaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhuma) akamate nafasi ya kuwa Hakimu kwa ajili ya watu. Lakini ‘Abd Allaah akamuomba mkuu wa majeshi kumuweka mbali na kazi hiyo. Khaliyfah alimuuliza sababu kuu itakayomkubalisha kukubali cheo hicho ambapo baba yake amekuwa nacho. Ibn ‘Umar alisema:

 

“Kama kulikuwa na hitilafu yoyote kwa baba yangu, alikuwa akimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini mimi sioni mtu yeyote wa kumuuliza.”[33]

 

Tumeona kwamba Shari'ah inaruhusu Hakimu kumuomba Hakimu mwenziwe kupata ushauri wa kesi aliyonayo mkononi. Lakini pia Sheria inaruhusu kuwepo kwa washauri ama wazee wa busara katika jopo la Mahkama.[34]

 

Mahkama inaruhusiwa kwa nguvu ilizopatiwa, kumteua mtu yeyote atakayefaa kuishauri katika kesi. Pia pande za kesi zinaweza kutoa ombi kama hili. Mshauri wa Mahkama anaweza kuwa ni mmoja au zaidi. Hakimu ni lazima aweke kumbukumbu ya ushauri huo. Hata hivyo, mshauri huyo hatokuwa na sauti katika maamuzi (hukumu) ya Mahkama.[35]

 

 

Suluhu (Arbitration)

 

Suluhu ni kinyume cha hukumu, kwani suluhu ni maridhiano ya kumaliza kesi kwa pande zote mbili bila ya kutezwa nguvu. Ama hukumu hutolewa ikiushinikiza upande ulioshindwa kuifuata.

 

Shari’ah ya Kiislamu inaruhusu pande za kesi zinazogombana kuhusu madai juu ya mali fulani na haki binafsi nyengine kupeleka malalamiko yao kwa msuluhishi/mpatanishi (arbitrator). Kwa maarufu, inajulikana kama ni tahkiym. Msuluhishi ni lazima awe na sifa zinazofanana na kuchukua kiti cha Uhakimu, kwani hakika, anafanya kazi kama ya Hakimu, lakini dhimmi[36] anaweza kuteua mtu wa imani kama zake kuwa msuluhishi.

 

Kwenye makosa ya jinai yanayoadhibiwa kwa hadd na kisasi, suluhu hairuhusiwi. Msuluhishi amepewa nguvu ya kusikiliza ushahidi na kuapisha viapo kama ilivyo Mahkamani na kwa suluhu ya msuluhishi iliyopelekwa Mahkamani ili kupata ridhaa na usajili wa Mahkama. Hukumu ya suluhu hiyo itatolewa kwa mujibu wa vifungu vyake ikiwa tu haipingani na Shari’ah.

 

Kwa upande wa Sheria, Mahkama katika hali ambayo wadaawa hawajateua msuluhishi, inaweza kuteua msuluhishi wa kesi ya wadaawa pale inapoona inafaa.[37]

 

Pale ambapo wadaawa wameafikiana, wanaweza kuteua msuluhishi kabla ya kutamkwa hukumu katika Mahkama. Maombi hayo yanatakiwa kuwa kwa maandishi, na yanatakiwa kutiwa saini na msuluhishi. Msuluhishi huyu anateuliwa kwa makubaliano ya wadaawa. Mahkama inaweza kuweka muda wa kufikia suluhu hiyo.[38]

 

 

[1] Fataawa ‘Alamgiri, Juzuu ya III, uk. 525.

[2] Fataawa ‘Alamgiri, Juzuu ya III, uk. 526.

[3] Sheria ya Mwenendo wa madai, S. 6 (1).

[4] Sheria ya Mwenendo wa madai, S. 72.

[5] Al-Bayhaqiy, as-Sunan al-Kubra, X, uk. 131.

[6] Ibn Qudaamah, Akhbar al-Qudat, IX, uk. 75.

[7] Al-Kasaniy; K. Bada’ia as-Sanaia, VII, uk. 12.

[8] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 25

[9] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXIII, r. 2-3

[10] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, II, uk. 369.

[11] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, II, uk. 370.

[12] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, II, uk. 370.

[13] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, II, uk. 377.

[14] Muhammad Sangalaji, Qadhaa daar Islam, uk. 140.

[15] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXIII, r. 3 (2)

[16] Fataawa ‘Alamgiri, Juz. ya 3, uk. 501-502.

[17] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXIV, r. 7-8

[18] Waki’, Akhbaar-al-Qudhaah, I, uk. 97.

[19] Al-Marghinani; al-Hidayah, II, uk. 144-145.

[20] Al-Marghinani; al-Hidayah, II, uk. 144-145. Kwa maelezo angalia as-Sarkhasi; K. al-Mubsuut, XVI, uk. 84.

[21] Al-Hilli, K. Sharai’ al-Islam, uk. 315.

[22] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 88

[23] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 89

[24] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 90

[25] Al-Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 430.

[26] Commonwealth Consolidated Acts, Proceeds of Crime Act 2002, section 39.

[27] B. D. Chipeta, Civil Procedure In Tanzania, Dar es Salaam University Press Ltd, Tanzania, 2002.

[28] Raddu’l-Mukhtaar, Juzuu ya IV, uk. 377-371.

[29] Raddu’l-Mukhtaar, Juzuu ya IV, uk. 377-379.

[30] Abdur-Rahiym, The Principles Of Islamic Jurisprudence, toleo la mwanzo, (1991), uk. 356.

[31] Rudia Limitation Decree, chapter 12

[32] Limitation Decree, S. 3, jedwali I, uk. 10. Angalia pia Sheria ya Mikataba – Contract Decree, chapter 149.

[33] Mapokezi hayo yamepokewa na at-Tirmidhiy lakini mapokezi yaliyotolewa hapa yamepokewa na al-Khaatib at-Tibriyz ndani ya Mishkaat al-Masaabih, uk. 325. Hata hivyo, Tibriyz hakutoa chanzo.

[34] Rudia Sheria ya Mahkama ya Ardhi – Zanzibar, no. 12 ya 1994, S. 4 (1), 5 (1), 6 (2) na 37.

[35] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 118; Angalia pia Sheria ya Mahkama, Sura ya 3, O. XXII

[36] Raia asiyekuwa Muislamu anayeishi katika taifa la Kiislamu.

[37] Sheria ya Usuluhishi, S. 7

[38] Rudia Sheria ya Mwenendo wa Madai, kifungu 66, Jedwali ya Tatu, S. 1-5, uk. 350

Share