002-Talbiys Ibliys - Ufunikaji (Uhadaifu) Wa Ibilisi: Wasiwasi Katika Kutia Niyah Na Utulivu (At-Twumaaniynah)

 

Wasiwasi Katika Kutia Niyah

 

Katika kutia Niyah ya Swalah, Shaytwaan hupata upenyo pia wa kuwachezea watu na kuwakosesha thawabu nyingi sana.

 

Utamuona mtu anafunga Swalah kisha anaivunja. Na mwengine huendelea hivyo mpaka Imaam anaporukuu, hapo ndipo huifunga Swalah kwa haraka na kurukuu pamoja naye.

 

Ameweza kuihudhurisha Niyah kwa haraka pale Imaam aliporukuu, wakati alishindwa kufanya hivyo tokea mwanzo wa Swalah.

 

Hii ni njia moja wapo ya Shaytwaan kumkosesha thawabu nyingi kama anglifunga Swalah pamoja na Imaam.

 

Wengine kabla ya kufunga Swalah utawasikia wakinyanyua sauti zao wakitamka maneno Fulani na kushadidia maneno hayo, kisha husema; “Allaahu Akbar”, kisha huivunja Swalah na kuanza kutamka tena maneno hayo akidhani kuwa amekosea kuyatamka, na akidhani pia kwamba maneno hayo yamepangwa na Mtume wa  Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwamba akiyakosea Swalah yake inabatilika.

Utamuona akiendelea kukubali kuchezewa na Shaytwaan na kumkosesha thawabu nyingi za kujiunga na Imaam mapema.

 

Ukweli ni kuwa maneno hayo anayotamka, anayodhani kuwa ndiyo Niyah ya Swalah, hayajapata kutamkwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wala na Swahaba zake watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Anasema Ibnul Qayyim:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotaka kuswali husema:

“Allaahu Akbar”, kisha hufunga Swalah. Hakuwa akisema kitu kabla yake kama vile; “Uswaliy fardha sSwalaatil Ishaa...” Au kauli zozote katika zile wanazozitamka watu hivi sasa. Hapana Hadiyth Sahihi wala hata dhaifu inayotujulisha kuwa kitendo hiki kimetendwa na Sahaba yeyote au Taabi'i au mmojawapo wa maImaam wanaojulikana kwa ucha Mungu wao. Hapana hata mmoja wao aliyewahi kutamka kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo kabla ya kufunga Swalah….” (Kitabu ‘ Al-Qawlul Mubiyn Fiy Akhtwail Muswalliyn)

 

Anasema Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotaka kuswali huanza kwa kusema:

“Allaahu Akbar.” Muslim – 1/357 na 498

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu), anasema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona mtu mmoja akikosea katika Swalah alimwambia:

“Unapotaka kuswali, tia udhu kisha elekea kibla kisha sema, “Allaahu Akbar”, kisha soma utakachoweza kusoma katika Qur-aan”. Al-Bukhaariy na Muslim

 

Ama ‘Abdullaah bin ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alisema:

“Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akianza kuswali kwa kusema “Allaahu Akbar.” Al-Bukhaariy 2/221 na 738.

 

Hizi ni dalili chache katika nyingi zinazotujulisha kuwa kitendo cha kuitamka Niyah hakikuwepo katika mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa ajili hiyo tusimpe fursa Shaytwaan kutuingilia na kutufisidia Swalah zetu au kutukosesha thawabu za kujiunga mapema na Imaam kwa kupitia mlango huo.

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Aqiyl, kuwa siku moja aliulizwa na mmoja katika watu wenye maradhi haya ya wasiwasi:

“Mimi kila ninapotawadha, huhisi kama kwamba sijatawadha vizuri, na kila ninapofunga Swalah huhisi kama sikuifunga vizuri, nifanye nini?”

Ibn ‘Aqiyl akamjibu:

“Wacha kuswali, kwa sababu wewe huna lazima ya kuswali”.

Alipoulizwa kwa nini alijibu hivyo, alisema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

‘Haandikiwi dhambi wala thawabu mwendawazimu mpaka awe na akili …” na mtu aliyetawadha akahisi kuwa bado hajatawadha, kisha akafunga Swalah akahisi kuwa bado hajaifunga, huyo akili zake si sawa. Huyo ni mwendawazimu, na mwendawazimu halazimiki kuswali”. (Talbiys Ibliys – Ibn Taymiyyah Uk.169)

 

 

 

 

Utulivu (At-Twumaaniynah)

 

Utulivu (At-Twumaaniynah) ni nguzo muhimu sana katika nguzo za Swalah, na bila ya utulivu Swalah haiwi kamilifu.

Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa Msikitini, akaingia mtu mmoja na kuswali. Baada ya kumaliza akainuka na kwenda kumsalimia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swallah Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamuambia:

“Rudi kaswali tena, wewe bado hujaswali.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimrudisha mtu huyo mara tatu, na kila anapomaliza kuswali alikuwa akimuambia:

“Rudi kaswali tena, wewe bado hujaswali.”

Yule mtu akamuambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Sijui kuswali vizuri kuliko hivi, (bora) nifundishe.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia:

“Unapotaka kuswali tia wudhuu, kisha elekea Qiblah, kisha soma utakachoweza kusoma katika Qur-aan, kisha rukuu mpaka utulie (tatwmaina - At-Twumaaniynah) na uwe na uhakika kuwa umerukuu (sawa), kisha inuka usimame sawa sawa (At-Twumaaniynah), kisha usujudu mpaka utulie (At-Twumaaniynah) na uwe na uhakika kuwa umesujudu sawa, kisha kaa vizuri mpaka utulie katika kikao chako (Tumaaniyna), kisha sujudu na utulie (At-Twumaaniynah) mpaka uwe na uhakika kuwa umesujudu sawa, kisha ufanye hivyo hivyo mpaka umalize kuswali.” Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah.

 

Hadiyth hii na nyingi kama hizi zinatujulisha kuwa Swalah haiwi kamili bila ya utulivu (At-Twumaaniynah). Nako ni kutulia katika kila kitendo cha Swalah. Mtu anatakiwa atulie mpaka awe na uhakika kuwa ametulia.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amempa jina la ‘Mwizi’ mtu anayeswali bila utulivu.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Katika wezi wabaya kabisa ni wale wanaoiba katika Swalah zao, hawarukuu kwa ukamilifu wala hawasujudu kwa ukamilifu na hawawi na khushuu.”

 

Na katika riwaya nyingine amesema juu ya ‘Mwizi wa Swalah’:

“Na wala haunyoshi mgongo wake sawa pale anaporukuu na anaposujudu.”

Imaam Ahmad, Al-Haakim na imesahihishwa na Imaam Adh-Dhahabiy.

 

 

Share