Zingatio: Vitu Vya Duniani Vinapungua Ladha, Pepo Haipo HivyoNaaswir Haamid

 

 

Tafuta riziki ya halali uitie tonge kinywani, mwishowe itayeyushwa na kutolewa tumboni. Jenga nyumba nzuri ya ghorofa uzipendazo, mwishowe utahitaji nyumba iliyojengwa kwa lulu. Jaza fanicha ndani ya nyumba yako, mwishowe utataka kuzibadili zote kwani machoni mwako zimechoka kuangaliwa. Nunua gari iliyo brand new (mpya) uipendayo, siku chache zinaingia nyengine mpya, nawe wahitaji.

 

Juu ya raha zote hizi za dunia, ni matajiri wangapi waliohodhi kila kitu wamejidhulumu nafsi zao kwa kujitia vitanzi? Ni matajiri wangapi ambao wanakosa kupata usingizi usiku? Hio sio hali waliyokuwa nayo Swahaabah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambao walipata kichache wakakinai, na walipopata kingi wakikitumia katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Hiyo ndio ladha ya dunia ambayo inapungua na kumalizika, inakosa ladha kwa ulimi, inakosa nuru katika macho na inakwisha muda kwenye nafsi. Kutwa roho ya mwanaadamu ni yenye kutamani na kutapatapa kama mfa maji. Iwapo hali ndio hiyo, kumbuka maneno ya wahenga:

 

"بانوا بانوا وما سكنوا, ساروا ساروا وما رجعوا"

 

(Wamejenga na kujenga bila ya kukaa, Wamekwenda na kwenda bila ya kurejea))

 

Juu ya raha zote hizi za dunia, ni matajiri wangapi waliohodhi kila kitu wamejidhulumu nafsi zao kwa kujitia vitanzi? Ni matajiri wangapi ambao wanakosa kupata usingizi usiku? Hio sio hali waliyokuwa nayo Swahaabah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambao walipata kichache wakakinai, na walipopata kingi wakikitumia katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Dunia ndugu zangu ni ya kupita tu, maisha yapo Akhera huko. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametuandalia mambo mazuri ambayo macho hayajapata kuona, wala sikio kusikia, wala moyo kuwahi kufikiria na unachotaka wakipata humo.

 

Kila kitu kina expiry date yake, na kwa hakika hata roho ina expiry date yake, seuze nyumba, gari, fanicha na mengineo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameisifu Pepo kwamba ni ya kifakhari kuliko chochote duniani, humo watu wake wataishi milele, daima wa dawaam:

 

{{Kwa yakini watu wa Peponi leo wamo katika shughuli (zao), Wamefurahi. Wao na wake zao wamo katika vivuli, Wameegemea katika viti vya fahari. Watapata humo (kila namna ya) matunda na watapata kila watakavyovitaka. Salama (tu juu yao), ndio neno litokalo kwa Mola (wao) Mwenye Rehema.}} [Suratu-Yaasiyn: 55-58].

 

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameisifu Pepo kwa maneno yafuatayo:

((Hakika wakaazi wa Peponi watakula na kunywa lakini hawatakuwa wanatema, Wala hawendi haja ndogo au kubwa, Wala kutokuwa na uchafu puani. Waliuliza Maswahaba: kitakuwaje chakula? Alijibu Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kitakuwa kitamu kama utamu wa miski na watakuwa wamejazwa na Tasbihi na Tahmidi kama walivyojaaliwa kupumua.)) [Imesimuliwa na Jaabir (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na kupokelewa na Muslim].

 

Enyi makundi ya Waislamu, tusipumbazwe na lahwa za dunia tukasahau neema alizotuahidi Mola wetu Mlezi. Hivyo, tujihimize kumuabudu Yeye bila ya kumshirikisha kwa jambo lolote, insha Allaah tutayakuta yote tuliyoahidiwa, anza leo usisubiri kesho.

 

Share