Kutumia Dawa Za Kuzuia Hedhi Wakati Wa Hijjah
SWALI
Kuna uhalali gani kwa wanawake kuchelewesha au kusogeza mbele siku zao za hedhi kwa kutumia dawa wakati wa hija? Hii inafanyika ili kutimiza ibada nzima ya hija.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Maulamaa wengi wametoa ruhusa mwanamke kutumia dawa za kuzuia hedhi ikiwa anakwenda kutimiza nguzo ya Fardhi ya Hajj, na hoja zao ni zifuatazo:
Inafaa kutumia dawa kuzuia hedhi ili mwanamke aweze kukamilisha nguzo yake ya tano ya Kiislamu ikiwa atakhofu kupatwa hedhi wakati yuko katika taratibu za Hajj, kwa sababu ya kutokana na umbali wa masafa wa kusafiri na gharama zake nyingi ambazo pengine atashindwa tena kurudia kuitimiza nguzo yake miaka mingine.
Hapa inafaa tutaje kuhusu wale wanaotaka kutumia dawa hizo kwa kuwawezesha kufunga mwezi mzima wa Ramadhani:
Rai za Maulamaa kuhusu jambo hili zime ikhtilafiana, kuna wachache waliokubali na wengi wamepinga mwanamke kutumia dawa hizo katika mwezi wa Ramadhani.
Wale waliokubali wamesema kwamba shuruti za kutumia dawa hizo ni kwamba mwanamke apate ruhusa kwa Daktari kuwa akitumia dawa hizo hazitomfanyia madhara yoyote kwani sheria ya dini yetu haipendi madhara kwa mtu.
لا ضرر ولا ضرار
Hakuna kuleta madhara wala kudhuriana" "
Wale waliopinga kabisa kwa kusema kwamba hii na amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) aliyowaandikia binaadamu, kwa hiyo sio sawa kubadilisha maumbile ya mwanamke kama alivyoambiwa bibi 'Aysha (Radhiya Allahu 'anhaa) ilipomjia hedhi wakati wa Hajj kama ilivyo katika hadithi hii:
Imetoka kwa Bibi 'Aishah na Jaabir bin 'Abdillah kuwa katika tarehe nane ya mwezi wa Dhul Hijjah siku ijulikanayo kuwa ni ya 'Tarwiyah' walipokuwa wakielekea Minaa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakaleta talbiya ya Hijja, kisha Mtume akaenda kwa Bi 'Aishah (Radhiya Allahu 'anhaa) akamkuta analia, akamuuliza: ((una nini?)) akajibu (Bi 'Aishah Radhiya Allahu 'anhaa ''Nimepatwa na hedhi na watu wamehirimia na wamefanya twawaaf nami sijafanya vyote hivyo! Na sasa watu wanaelekea kuhiji hivi sasa!!'' Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
فإن ذلك شيء كتبه الله على بنات آدم، فافعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت حتى تطهري
((Hili ni jambo Aliloliandika Allah kwa wanawake (mabint Adam), basi nenda kaoge halafu kahirimie kisha Hiji na fanya yale anayofanya Mwenye kuhiji isipokuwa kutufu na kuswali)). Bi 'Aishah akafanya matendo yote ya Hajj isipokuwa kufanya Twawaaf na Swalah
Vile vile kwa Rahma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametusahilishia dini yetu kwa kuturuhusu kuweza kulipa siku za Ramadhani ambazo mtu akishindwa kufunga ikiwa yuko safarini au ni mgonjwa na hali kama hii ya hedhi ya wanawake kwamba walipe siku zao miezi mingine baada ya kumalizika Ramadhani. Kwa hiyo ni bora zaidi mwanamke kukubali amri ya Allaah Aliyowaandikia kupata hedhi kwani kila majaaliwa ya Allaah juu ya binaadamu bila shaka yana hikma na manufaa makubwa kwetu.
}}فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ {{
((Basi atayekuwa mjini katika mwezi huu naafunge.
Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize
hisabu katika siku nyengine. Allah Anakutakieni
yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize
hiyo hisabu, na mumtukuze Allah kwa kuwa
Amekuongoeni ili mpate kushukuru)) [Al-Baqarah: 185]
Wallaahu A'alam
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


