Skip navigation.
Home kabah

Mirungi - 3 (Mwisho) - Fataawa Za Wanachuoni

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

 

Muhammad Baawazir

 

Fataawa Za Wanachuoni Kuhusu Mirungi

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

“Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashaytwaan (wanamfuata Shaytwaan).  Na Shaytwaan ni mwenye kumkufuru Mola wake.” [Al-Israa: 26-27]

 

“Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo.” [Al-Baqarah: 125]

 

“… na anawahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya…” [Al-'Araaf, 7: 157]

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Allaah Anachukia mambo matatu: kusengenya, kuomba na kupoteza pesa.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Mirungi ni mti mchafu mbaya uliongia katika ardhi ya Waislam, na wameingia katika mitihani baadhi ya Waislam, na unasababisha madhara ya kimali, kimwili, kidini na kiwakati. Vilevile, ulimaji wake husababisha hasara kubwa za kiuchumi kwa sababu ya maji mengi yanayotumika katika ardhi ngumu ambayo inaoteshwewa. Na kwa hivyo, ni HARAAM kulimwa katika ardhi za Waislam, na pia kutafunwa.

 

Matumizi ya Mirungi yanaingia moja kwa moja katika vileo kwani vinamtoa mlaji katika hali yake ya kawaida na kumbadilisha na kuingia katika hali ya kuishi kwenye fikra za kuwazika na ndoto za aliye macho, vilevile mtu kuwa juu juu amehandasika (kalewa), kadhalika ndani yake kuna kuidhuru mtu afya yake, ubadhirifu wa mali na wakati.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu vinywaji fulani vinavyotengenezwa na asali, mahindi, au shayiri kwa njia ya kuvundikwa au kuchanganywa hadi kugeuka na kuwa pombe. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ufupi na uwazi alijibu,

“Kila chenye kulewesha ni pombe, na kila pombe ni Haraam.” (Muslim)

 

Na amesema tena Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Kila chenye kulewesha kikiwa kingi, basi japo kichache ni Haraam.” (Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy). Na kwengine, “Kinacholewesha japo ni ndoo nzima, basi hata muonjo (kuinywa kidogo) wake ni Haraam.” (Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy)

 

Naye ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa amesimama kwenye Minbar ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatangazia,

“Pombe ni chochote chenye kufunika akili” (Al-Bukhaariy Na Muslim)

 

Wanachuoni mbalimbali wametoa fatwa mbalimbali za kuonyesha uharamu wa utumiaji wa Mirungi.

 

Zifuatazo ni Fatawa za Wanachuoni mbalimbali, nimechagua Fatwa tatu za Wanachuoni watatu wa nchi tatu maarufu, Saudiyah. Misr na Yemen. Na badala ya kuzikusanya makumi ya Fatwa kutoka Yemen, au maishirini kutoka Saudiyah au kadhaa kutoka Misr, hizi tatu hapa chini zitakuwa zinawakilisha fatwa nyingi za Wanachuoni wakubwa wa nchi hizo:

 

Mwanachuoni Mkubwa Wa Sa’udiyah Allaamah Ibn Baaz, Aliyekuwa Mufti Wa Sa’udiyah

 

Alipoulizwa:

‘Wengi katika waraibu wa Mirungi, inapofika wakati wa Swalah basi (kwa wale wanaoswali) hutoa midomoni mwao (Mirungi) na kisha huitema kwenye mifuko ya plastiki kisha huswali. Na baada ya Swalah huichukua kutoka kwenye mfuko na kuila tena, je, Mirungi ni najisi? Na nini hukmu ya mtu mwenye kuswali na hali imo kwenye mdomo wake? Na je, inajuzu kwa yule mwenye kuila akachelewesha Swalah hadi amalize kula, kisha aje kulipa Swalah zake?

 

Akajibu:

 

Sina elimu ya chenye kuonyesha kuwa ni najisi, kwani huo ni mti maarufu, na asli kuhusiana na miti na mimea mbalimbali ni kuwa yote ni twahara. Ama utumiaji wake ni HARAAM –kwa kauli sahihi za Wanachuoni- kutokana na madhara yake mengi.

 

Na inawapasa hao wenye kutumia, wasiitumie kabisa wakati wa Swalah, na wala haijuzu hata kidogo mtu kuchelewesha Swalah kwa ajili hiyo, bali inampasa Muislam aiswali Swalah kwa wakati wake katika Jama’ah pamoja na ndugu zake Waislam Misikitini, kwa kauli yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Atakayesikia Wito wa Swalah (Adhaan) na asiende kuswali, basi hana Swalah ila kwa udhuru.” (Ibn Maajah, Ad-Daara Qutwniy na Al-Haakim kwa Isnaad sahihi)

Na aliulizwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuhusiana na huo ‘udhuru’ ambao umeruhusiwa, akajibu: “Ni khofu au maradhi”’ na matumizi ya Mirungi sio udhuru wa kishari’ah, bali ni jambo la Munkar, na ikiwa mtu atachelewesha Swalah kwa sababu hiyo, basi hiyo itakuwa ni dhambi kubwa sana. Na haifai vilevile kuunganisha Swalah mbili kwa sababu ya Mirungi, kwani huo si udhuru wa kishari’ah unaokubalika…”

 

Kitabu ‘Fataawa Islaamiyah’ kilichokusanywa na Muhammad Al-Musanad, Juz. 3, uk. 445 – Majmu’ Fataawaa wa Maqalaat Mutanawi’ah, Juz. 23.

 

  

 

Shaykh Abu Naswr Muhammad Bin ‘Abdillaah Wa Yemen

 

Katika fatwa yake ndefu ambayo ni risala nzima, hapa tutaifupisha sana.

 

Aliulizwa:

 

Nini hukmu ya Kiislam kuhusu Mirungi; kuliwa, kulimwa, kuiuza, kuinunua na kuitolea zawadi?

 

Akajibu:

 

AlhamduliLlaah was Swalaatu was Salaam ‘alaa RasuuliLlaah wa ‘alaa aalihi waswahbihi waman waalaah, amma ba’ad,

 

Hukmu ya Mirungi kula, kulima, kuuza, kununua na kutolea zawadi yote ni HARAAM kwa dalili na sababu zifuatazo:

 

1.     Zimekuja Dalili za wazi kuhusiana na ubaya na uchafu wa Mirungi kutoka katika kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ambayo imejengeka katika wadhifa aliotumiwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Na anawahalalishia wao vilivo vizuri na kuwaharamishia vibaya” Kutajwa uharamu wa vitu vibaya na vichafu kwenye Aayah hiyo mkabala na kuhalalishwa vilivo vizuri, ni ishara ya kuonyesha kuwa kila kibaya na kichafu ni HARAAM iwe sawa ni chakula, kinywaji, kuingiliana na mengineyo. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatujulisha katika Aayah hii kuwa Mtume wetu anatuharamishia yale yenye madhara, machafu na mabaya. Na hakutuharamishia Mtume wetu kitu ambacho ni kizuri kwa hali yoyote. Na kuharamishwa jambo, huenda kikawa kwa dhati yake chenyewe au kwa kinginecho, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwenye kula kitokanacho na mti huu, basi asiukaribie Msikiti wetu”, Hadiyth hii imekuja kwa mapokezi mengi. Hapa uharamu umekuja kutokana na harufu mbaya inayotokana na viliwavyo kutokana na mti huo ambavyo ni vitunguu maji na vitunguu thawm, na harufu hiyo huwaudhi watu pamoja na Malaika katika nyumba za Allaah (Misikitini).  Na Mirungi haiepukiki kuwa katika fungu hilo la HARAAM kwa dhati yake au kwa dhati ya kinginecho. Baadhi ya watu wanadai kuwa hakuna Aayah wala Hadiyth inayoelezea kwa uwazi uharamu wa Mirungi, watajibiwa kuwa, Aayah hiyo hapo juu imekusanya moja kwa moja Uharamu wa kila kilicho kibaya, kichafu, chenye madhara. Na kwa uwazi kabisa Allaah Ametaja kilicho kibaya mkabala na kilicho kizuri cha halali. Na Wanachuoni wengi kabisa wametaja Aayah hiyo kuwa inaonyesha wazi uharamu wa Mirungi, na hilo liko wazi.

2.     Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakuna kujidhuru wala kudhuriana (kusababisha madhara)”, Hadiyth hii ambayo imesimuliwa na Maswahaba nane ni hoja nzuri kabisa. Aliposema, “La Dhwarar” hakuna madhara inafafanua kupita kiasi kuliko angesema, “La tadhwuruu” msidhuru, na Hadiyth hii ni msingi wa jumla unaojengea masuala mengi yasiyo na idadi, maana kauli yake “La Dhwarar wala Dhwiraar” maana yake ni msijidhuru nafsi zenu au msijiletee madhara nyinyi wenyewe na wala msidhuru nafsi nyinginezo au msipeleke madhara kwa wengine. Na inafidisha Hadiyth hii kuwa kila chenye kuleta madhara kwa nafsi au kinachopelekea madhara kwa nafsi nyingine ni HARAAM ila tu pale kutakapotokea dalili ya kuonyesha kinyume chake. Na imepokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad na Abu Daawuud na Al-Bayhaqiy na wengineo kutoka kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kila chenye kulewesha.”

 

Akaendelea Shaykh kuelezea kwa kirefu madhara yake yanayompata mtu binafsi na yale yanayoikumba Taifa zima kutokana na ulaji wake na kilimo na mengine ya kidini, kiafya, kiuchumi, upotezaji wakati na kutopatikana uzalishaji, kuenea umaskini, wizi, rushwa, uongo, kupotea haki za watu na mengi mengineyo.

 

Akamalizia Shaykh kwa kutaja Wanachuoni wengi walioharamisha Mirungi, miongoni mwao ni:

Shaykh Ahmad bin Hajar Al-Haytamiy katika kitabu chake “Tahdhiyr Ath-Thuqaat Min Aklil Kuftati Wal Qaat”, na Al-Faqiyh Abu Bakr bin Ibraahiym Al-Muqriy Al-Haraaziy Ash-Shaafi’iy katika kitabu chake, “Tahriym Al-Qaat”, na wengineo ni Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aal Shaykh, na Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz, na Shaykh Abul Hasan Mustwafaa bin Ismaa’iyl As-Sulaymaaniy na Maulamaa wengine.

Ama Shaykh Muqbil bin Haadiy Al-Waadi’iy (ambaye ni mwalimu wake), yeye amewafikiana na Fatwa hii. Na kumetungwa vitabu mbalimbali kuharamisha Mirungi ambavyo vimetaja ndani yake madhara na mafaasid yanayopatikana katika ulaji Mirungi, miongoni mwa vitabu hivyo ni, “Kashfu Ash-Shubuhaat ‘An Adhwraaril Qaat” cha Dkt. Ibraahiym bin ‘Abbaas, na kitabu “Al-Qaat” cha Dkt. Al-Marzuuqiy na Dkt. Abu Khutw-wah, na kitabu “Shahaadaatu Ath-Thuqaat ‘Alaa Adhwraaril Qaati” cha Shaykh ‘Aaidhw bin ‘Aliy Mismaar, na kitabu “Al-Qaatu Wal Mujtama’” cha Abu Ibraahiym Atw-Twayriy.

(Mwisho wa kumnukuu)

 

 

Tunamalizia makala hii ya Mirungi kwa wito kwa walaji wote wamche Allaah na wajiepusha na jambo hilo chafu, baya, lenye madhara makubwa ya kidini, kimwili, kiafya, kimali na kiuchumi, na watumie muda wao huo mkubwa wanaoupoteza kufanya yenye manufaa kwa dunia na Akhira yao. Na wakumbuke wataulizwa siku ya masiku kwa muda wao walioupoteza, na kwa mali yao walivyotumia.

 

Na wale wanausuhubiana na walaji, wito kwao wajiepushekusuhubiana na watu hao wasije nao kuingia kwenye balaa na afa hilo miongoni mwa maafa makubwa yaliyomo katika jamii ya Kiislam, wakumbuke pia mwenye kusuhubiana na mfua chuma, basi ima akuunguzie nguo yako au akutie harufu mbaya ya moshi wake. Hiyo ni tahadhari tuliyopewa na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa hiyo tuizingatie sana inshaAllaah.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ajaalie risala hii iwe khaaliswan Liwajhih na iwe na taathira kwa walaji Mirungi na inshaAllaah iwe ndio sababu ya kuachana kwao na uraibu huo.

 

 

MWISHO

 

 

Rudi Juu