Zakaah Ya Dhahabu Kiasi Gani?

SWALI:

A/alleykum.

Naomba nifafanuliwe zaidi kuhusu zaka ya dhahabu. Mfano mimi nina dhahabu gramu 100, jee natakiwa nitoe zaka shilingi Ngapi za Tanzania?

 

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Shukrani kwa ndugu yetu kuhusu swali lako hilo la Zakaah ya dhahabu.

Kabla ya kuingilia suala lenyewe inafaa sisi tufahamu masharti ya kutoa Zakaah ikiwa ni pesa taslimu, dhahabu au fedha au vito vyengine vya thamani. Miongoni mwa masharti haya ni:

1.    Niswaab: Hiki ni kiwango cha chini ambacho mtu akiwa nacho ni lazima atoe Zakaah ya 2.5%. Ama kwa dhahabu ni gramu 82.5.

2.    Hawl: Kupitiwa hiyo dhahabu na mwaka mzima wa mwandamo ikiwa kwako.

Haya ni masharti ya msingi katika mas-ala hayo ya Zakaah. Tukichukua mfano uliotoa ya kwamba una gramu mia za dhahabu. Kiwango hichi kikipitiwa na mwaka itabidi utoe 2.5%. Asilimia hiyo itakuwa ni sawa na kiwango cha gramu 2.5 ya dhahabu. Upo msemo unaosema kuwa watu wa Makkah wanajua vilivyo kwa watu wao. Nawe ikiwa ni mkaazi wa Tanzania au Kenya utajua maduka ya masonara. Kwa hiyo kabla ya kutoa Zakaah zako unafaa uende ukawaulize gramu moja ya dhahabu ni shilingi ngapi. Ikiwa gramu moja ni 20,000 itabidi baada ya mwaka utoe shilingi 50,000.

Ni bora zaidi kwa kuwa hela hii ni ndogo umpatie anayestahiki mmoja wa kupewa Zakaah ili imsaidie kwa kiasi kikubwa zaidi, kuliko kuigawa na kuwapa wengi kidogo kidogo. Watu wanaofaa kupewa Zakaah wametajwa katika Suratut Tawbah, ayah ya 60: “Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu uliofaridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima”

Nao ni kama wafuatao:

 

1.          Mafakiri.

2.          Masikini.

3.          Wanaozitumikia.

4.          Wanaotiwa nguvu nyoyo zao juu ya Uislamu.

5.          Kuwapa uungwana watumwa.

6.          Kuwasaidia wenye madeni.

7.          Katika njia ya Allaah, na

8.          Kupewa wasafiri walioharibikiwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share