Mume Anazini Nje, Mke Hakukutana Na Mumewe Kindoa Miaka Minane Kwa Khofu Kuwa Atamtia Maradhi, Je, Ndoa Yao Inasihi Bado?

SWALI:

 

Amani ya Muumba wa Mbingu na Ardhi iwe kwenu!

Nimepata kuulizwa na dada mmoja kama kama kweli bado yupo katika ndoa au laa. Anadai kufikisha takriban miaka minane (8) bila kukutana kimwili wala kulala chumba kimoja na mumewe. Hii inatokana na tabia chafu za mumewe kutoka nje ya ndoa bila haya, kiasi mkewe akapata woga kuambukizwa maradhi. Ndipo alipomueleza kuwa akienda kufanya chafu wake asimkurubie, jambo ambalo lipelekea dada huyu kukabidhiwa chumba chake. Na kwa kuwa washazaa naye basi hupewa matumizi flani kwa ajili ya watoto. Naye kavumilia tu.

 

Sasa auliza VIPI BADO YUANA NDOA au laa na afanyeje maana mumewe hata wazo kama atabadili utaratibu hana.


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kukaa na mume kwa miaka minane bila kukutana kimwili.

Hakika Uislamu una nidhamu yake ya ndoa na talaka. Na ikiwa nidhamu hiyo haijafuatwa basi watu wanaweza kujikuta bado wako katika ndoa nah ali hawapaswi, au watakuwa wameachana na hali bado wapo kwenye ndoa; kwa ujumla itakuwa ni vurugu na uharibifu.

 

Na katika nidhamu ya Uislamu ya talaka ni kuwa lazima mume ima atamke, au atoe ishara yenye kueleweka au aandike kuwa amemtaliki mkewe. Ikiwa hayo hayakufanyika basi mke bado atakuwa yu katika ndoa japokuwa hawajakutana kimwili hata kwa zaidi ya miaka minane.

 

Katika hali hiyo aliyo nayo, dada yetu anaweza kufanya yafuatayo ili kupatikane ufumbuzi wa tatizo lake:

 

1.   Awasiliane na mumewe anaporudi nyumbani ili wazungumze kuhusu yanayowasibu. Itabidi amuweke chini mumewe, na wazungumze naye kwa uwazi bila kuficha chochote. Atumie busara na upole katika kuwasilisha malalamishi yako kwake. Na iwe wazi kuwa anayofanya si sawa, hivyo yeye anaamuaje. Je, bado anataka kuendelea na ndoa au hataki tena? Ikiwa jibu litakuwa ndio basi itabidi achukue majukumu ya kuacha zinaa na arudi katika maelekezo ya Uislamu na aishi kama Muislamu.

2.  Ikiwa huyo mke hukufanikiwa kupata suluhisho itabidi, aitishe kikao ambacho yeye atakuwepo, na mumewe, wazazi wake na wazazi wa mume ili wajadili hilo. Katika kikao hicho inatakiwa iwe wazi kuwa afanyayo ni makosa na hivyo achukue ahadi kimaandishi kuwa ataacha uzinzi na baada ya hapo wasahau yaliyopita na waangalie ya mbeleni. Au akatae kuchukua dhamana hiyo, hivyo amuache kwa wema.

3.  Ikiwa hakukupatika ufumbuzi wa tatizo lake, haifai kwake kukaa katika dhuluma bali inafaa aelekeze mashitaka yako kwa Qaadhi ikiwa yupo hapo anapoishi. Ikiwa hayupo basi inafaa aende kwa Shaykh aliyewaozesha, au Shaykh mwengine mcha Mngu, mwenye elimu na muadilifu ili aweze kuamua matatizo hayo aliyonayo. Kwa shari’ah ya Kiislamu, kule mume kushindwa kumtimizia huyo mke ni sababu tosha ya yeye kuachishwa na mumewe. Ikiwa kutapatikana ufumbuzi, suluhisho hilo akazanie liandikwe na kila mmoja wao awe na nakala ili kuepusha kunyanyaswa na kudhulimiwa tena katika uanandoa.

 

Tunamuombea dada yako kila la kheri katika kupata ufumbuzi wa tatizo hilo kubwa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share