Mke Anaiba Pesa Zangu, Anashawishiwa Na Baba Yake Ujeuri, Je Nina Haki Kumzuia Asiende Kwa Baba Yake?

Mke Anaiba Pesa Zangu, Anashawishiwa Na Baba Yake Ujeuri, Je Nina Haki Kumzuia Asiende Kwa Baba Yake?

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam aleikum! Shaykh

 

Nimewahi kugombana na mke wangu nikafikia kumpiga akakimbilia kwa Baba yake, Baba badili ya kutusuluhisha alikimbilia polisi. Sasa hivi Baba mkwe ameweka utaratibu wa kufanya mkutano na wanae wote wengi ambao wengine wameolewa miongoni mwao ndio mke wangu.

 

Mke wangu nimemzui kuhudhuria vikao hivyo mpaka apate idhini yangu. Sipendi mke wangu ahudhurie vikao hivyo kwa sababu havinatija wala maadili katika familia akija kutoka kwenye vikao vya Baba yake ndipo anakuwa mjeuri sana. Swali. Je ninayo haki kisheria kumzuia kuhudhuria vikao hivyo?

 

Je, mke wangu anahitaji ruhusa yangu kuonana na Baba yake. Je mke wangu na Baba Mkwe wanahaki ya kunipeleka polisi? Kosa kubwa la mke wangu ni kuniibia pesa, yeye anayaita matumizi wakati ninampa matumizi (Yeye system hiyo anaiita kuchuna buzi, yaani anasema lazima anichune, Baba hakemei tabia hiyo) Shekh majibu yako yote yawe na dalili za Aya na hadithi.

 

Wabillah Taufiq.


 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kushawishiwa na baba yake.

Matatizo hayo yote ambayo unayasema yanakukumba sababu kubwa inatokana na wewe mwenyewe.

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na haukusibuni katika msiba wowote basi ni kwa sababu ya yale yaliyochuma mikono yenu, na Anasamehe mengi. [Ash-Shuwraa: 30].

 

Huenda pengine kila mmoja wetu akajiuliza je, nimechuma vipi matatizo kwa mikono yangu? Jibu lipo katika kukengeuka katika maagizo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nasi tumekengeuka vipi maagizo hayo? Katika hilo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Wanawake huolewa kwa sababu zifuatazo: Mali, uzuri, nasaba na Dini. Tafuta mwanamke mwenye Dini” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na pia amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Akikujieni yule ambaye mnaridhia Dini na maadili yake, basi mwozesheni …” [At-Tirmidhiy].

 

Hivyo, mwanamme anatakiwa atafute mwanamke aliye na Dini na maadili. Ni kwa ajili hiyo, tukikosa kufuata agizo hilo tunaingia mashakani.

 

Inavyoonekana hukuchunguza vilivyo wakati ulipotaka kuoa ulikwenda kuingia katika familia gani. Tufahamu kuwa ndoa ni kuunganisha familia mbili sio kuunganisha mume na mke peke yake. Ndio kwa ajili hiyo kukatakiwa muafaka wa walii wa mke na pia idhini ya mume na mke wanaotaka kuoana.

 

Ulichukua hatua mbaya kwa kumpiga mkeo kwani kupigwa mke si katika utaratibu wa mwanzo katika shariy’ah yetu tukufu. Kumpiga mke inakuwa ni hatua ya mwisho katika hatua za kumrekebisha mke asiyesikia maneno ya mume na amevuka mipaka ya Dini, na kupiga si hivyo kulivyokusudiwa, bali ni kuguswa kama kutishwa na si kudhuriwa wala kujeruhiwa wala kuumizwa.

 

Tunaambiwa na Allaah Aliyetukuka:

Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. Na wale ambao mnakhofu uasi wao wa ndoa, basi wanasihini na wahameni katika malazi na wapigeni (kipigo kisichodhuru). Wakikutiini, basi msitafute njia dhidi yao (ya kuwaudhi). Hakika Allaah daima ni Mwenye Uluwa, Mkubwa wa dhati, vitendo na sifa.” [An-Nisaa: 34].

 

 

Na mume anatakiwa aishi na mke wake kwa wema, kwani ni wema ambao unambadilisha mtu muovu kuwa mzuri. Kwa minajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Amesema:

Na mkiwachukia, basi asaa ikiwa mnachukia jambo na Allaah Akalijaalia kuwa lenye khayr nyingi. [An-Nisaa: 19].

 

 

Kwa hiyo, mke akitoka katika utiifu unahitajika kufuata mtindo ufuatao ili kumrekebisha:

1. Kumnasihi kwa njia nzuri.

2. Kumhama katika malazi.

3. Kumpiga kipigo ambacho hakitamuumiza.

4. Ikishindikana basi mtafanya kikao kuhusu tatizo hilo baina yako, mkeo, wazazi wako na wake ili msuluhishe tatizo hilo. [Rejea: An-Nisaa: 35].

 

Hii ni kesi ya upande mmoja hivyo inakuwa ni vigumu kuamua moja kwa moja bila kusikiliza upande mwingine. Hata hivyo, ikiwa hayo unayosema ni kweli, fahamu kuwa mume ana haki kumzuilia mkewe kwenda sehemu ambayo itamfundisha na kumuelekeza katika maadili ambayo si mema hata ikiwa kwa baba yake. Nasaha yetu ni kuwa mtafute suluhisho kwa familia hizo mbili kuweza kuishi pamoja kwa masikilizano mema, mazuri na makubwa. Na lau ikiwa unalosema sivyo basi ni vyema uwe unampa ruhusa kwenda kutazama wazazi wake. Unachoweza kufanya ili kupunguza makali ya ujeuri ni kumpatia ruhusa siku ambayo hakuna mkutano. Inawezekana tabia hizo anazipata kutoka kwa jamaa zake wengine, kama dada zake na sio baba yake.

 

Hatujui kama ndugu yetu ushawahi kuhudhuria vikao hivyo na ukaona kweli havina tija yoyote. Na ikiwa hujahudhuria uliwezaje kujua hayo? Kuwa na dhana nzuri na mkeo ili aweze kurekebishika au huenda ikawa wewe pia unatakiwa kubadilika ili uwe na muamala mzuri na mkeo.

 

Linalohitajika ni kumfanyia Da‘wah kwa njia nzuri na huenda akabadilika, kwani hakuna lisilowezekana. Na Allaah Aliyetukuka Anasema:

Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi. Hakika Rabb wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea njia Yake, Naye Anawajua zaidi walioongoka.” [An-Nahl: 125].

 

Na inafaa uikoe nafsi yako na familia yako na moto wa jahanamu kwa kuwaelekeza katika yaliyo mazuri. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa.” [At-Tahriym: 6].

 

Katika kurekebisha hilo unaweza kufanya yafuatayo:

 

1. Kumpeleka Madrasah ya kinamama aweze kujifunza Dini na hilo litamsaidia katika kuepukana na maadili mabaya.

2. Kumhimiza kuhudhuria darsa za kijumla na zile za kinamama.

3. Muwe mnasoma Qur-aan pamoja na pia kusoma maana yake.

4. Jaribu kuwa kielelezo chema kwake.

5. Mpatie vitabu vya Hadiyth vinavyoeleza kuhusu wake wema waliotangulia na jinsi walivyokaa na waume zao.

 

Tunatarajia kuwa mambo yatakuwa mazuri kwa kufuata nukta hizo na nyinginezo.

 

Ikiwa ulimpiga na ukamuumiza, yaonyesha si mara ya kwanza wewe kufanya hivyo na ndio ikawa wana haki ya kukupeleka polisi japokuwa ingekuwa busara zaidi kwao kuweza kusuluhisha hilo kati yenu. Kama wewe ulivyomkosea ukamtandika mkeo pasi na kuwa na uwezo huo kishariy’ah.

 

Ili iwe funzo kwa wanaume wengine wasiwe ni wenye kuchukua sheria mikononi mwao na kuwadhulumu wanawake wa watu, mara nyingine hatua kama hizo zinafaa zichukuliwe kwa njia kali. Mtoto wa liwali wa Misri alipochukua hatua mikononi mwake na kumchapa Mqibti (Mkiristo), Mqibti huyo alikwenda kushitaki kwa Amiyr wa Waumini, ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Naye Amiyr aliamuru mtoto huyo aletwe na achapwe mbele ya watu na mbele ya Mqibti huyo.

 

Mke hapaswi kuchukua pesa za mume bila ya ruhusa yake. Hata hivyo, shariy’ah imempata mke ruhusa kuchukua kutoka kwa mumewe ambaye hampi masrufu ya kutosha kiasi cha haja, ya kumtosha yeye na watoto wake ikiwa anao. Hii ni kwa Hadiyth ya Hind bint ‘Utbah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipomuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa mumewe ni bakhili na hampi pesa ya kutosha kutumia yeye na watoto wake. Je, kuna makosa kuchukua kutoka kwake. Akaambiwa: Ndio (Anaweza kuchukua), lakini kwa wema (yaani asizidishe zaidi ya yale mahitaji atakayo). [Al-Bukhaariy].

 

 

Hukutueleza unampatia mkeo matumizi yepi? Je, yanamtosha au ni ya kubana bana? Ikiwa unampa ya kutosha itabidi ili kuondoa tabia hiyo uwe unaziweka pesa hizo mbali naye ili asiweze kuzipata. Wakati huo huo unatakiwa uwe ni mwenye kuzungumza naye uharamu wa kufanya kitendo hicho na huku unamsaidia aaache tabia hiyo mbaya.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share