Nikaah Inafaa Kufunga Na Asiye Muislamu? Na Nani Alifungisha Ndoa Za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?

SWALI:

 

Asalaam 3alaikum ya ikhwanu l muslimun, nilikuwa ninataka kujua kuwa Nikaah ya muislamu kuwa inaweza kusomwa na aliyekuwa si muislamu? Na nilitaka kujua nikaah ya habiby l Mustapha Salawatu lla7i 3aly7i ilisomwa na nani?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tafadhali unapotuma maswali kwetu, tumia lugha safi isiyokuwa na herufi za kukatisha zisizokuwa  za kawaida katika matumizi ya lugha ya Kiswahili, ambazo huenda zisifahamike kusudio lake na tukashindwa kufahamu unalotaka kuuliza.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Nikaah kusomwa na asiyekuwa Muislamu.

Hakika khutbah ya Nikaah baina ya Waislamu haiwezi kusomwa na asiyekuwa Muislamu kabisa.

 

Ama khutbah kwa Nikaah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilisomwa na watu tofauti. Mfano ni:

 

Ndoa yake na bi Khadiyjah binti Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha) ilisomwa na ‘ami yake Abu Twaalib kwa kuwa alikuwa hajakuwa Mtume wakati huo.

Ama ndoa yake na Zaynab binti Jahsh (Radhiya Allaahu ‘anha) ilifungwa na Mwenyewe, Allaah Aliyetukuka.

Ama wakeze wengine vitabu vingi vya Siyrah vinatufahamisha kuwa aliwaoa. Na masharti ya ndoa ya Kiislamu ni khutbah na kukubali kwa mume na mke. Na mwenye kuozesha ni walii wa mwanamke au msichana au ampe idhini mtu mwengine aozeshe. Kwa hiyo, yaonyesha Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ndiye aliyesoma khutbah ya harusi ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) na ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisoma khutbah ya bintiye Hafswah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share