Historia Fupi Ya Al-Ka'abah

 

Historia Fupi Ya Al-Ka’abah

 

 

Muhammad Faraj Salim As-Sa’y (Rahimahu Allaah)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Yaliyomo

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) anawasili Misri

 

Anarudi kwao

 

Anawasili Makkah

 

Anaamrishwa amchinje mwanawe

 

Mama yake Ismaa’iyl na kisima cha Zamzam

 

Watu wa kabila la Jurhum

 

Mwambie abadilishe kizingiti

 

Wananyanyua nguzo za Msikiti

 

Kisa cha Watu wa ndovu (As habul fiyl)

 

Kuujenga upya Al-Ka’abah

 

Wanaishiwa na pesa za halali

 

Mara ngapi umebomolewa na kujengwa upya?

 

Inajengwa tena

 

Hitimisho

 

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) alizaliwa katika mji unaoitwa Aar uliopo kandokando ya mto wa Furaat (Euphrates) Al Kufa - Iraq.

 

Inajulikana kuwa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) aliuhama mji huo na kuishi sehemu iliyokuwa ikiitwa Haraan na hatimaye akahamia nchi ya Palestina na huko ndiko alikofanya makao yake ya kuufikisha ujumbe alopewa na Rabb wake.

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Anawasili Misri

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) akifuatana na mkewe alikwenda kutembelea nchi ya Misri, na huko alipokelewa na mfalme wa Misri aliyewaweka ndani ya qasri yake, na usiku ulipoingia mfalme huyo alijaribu kumdhuru Bibi Sarah mke wa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam), lakini Allaah alimkinga bibi huyo na shari hiyo kwa kuufanya mkono wa mfalme upooze kila anapojaribu kumsogelea.

 

Alipoona dalili za qudra ya Allaah zikimlinda bibi huyo, mfalme akaacha vitimbi vyake na kuamua kumpa Bibi Sarah zawadi, na zawadi hiyo ni binti yake aitwae Hajar, na Sarah akaikubali zawadi hiyo na akamuozesha binti huyo mumewe Ibraahiym (‘Alayhis-salaam).

 

Anarudi kwao

 

Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) akarudi kwao akiwa amefuatana na wake zake wawili, Bibi Sarah na Bibi Hajar, na kutokana na mke mpya, Allaah alimruzuku mtoto wa kiume waliyempa jina la Ismaa’iyl, jambo lililomfanya Bibi Sarah awe na wivu mkubwa juu ya mke mwenzake, na baada ya kuamrishwa na Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa, Nabiy Ibraahiym akamchukuwa Bibi Hajar pamoja na mwanawe Ismaa’iyl aliyekuwa bado mchanga wakati huo, na kufunga nao safari ndefu kutoka Palestina hadi nchi ya Hijazi (Saudia hivi sasa).

 

Anawasili Makkah

 

Alipowasili Makkahh penye bonde baina ya Swafa na Marwa mahali kilipo kisima cha maji ya zamzam hivi sasa, na wakati huo nyumba ya Allaah (Al-Ka’abah) ilikuwa ni sehemu iliyonyanyuka tu juu ya ardhi, ikishambuliwa na upepo mkali pamoja na mikondo ya maji ya mvua iliyokuwa ikizikwanguwa pembe nne za nyumba hiyo.

 

Hapakuwa na mtu anayeishi mahali hapo wala nyumba wala maji isipokuwa mti mmoja alipowaacha mkewe na mwanawe chini yake, akawawekea birika la maji pamoja na chombo alichowatilia tende ndani yake, kisha akageuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Palestina.

 

Mama yake Ismaa’iyl alipomuona mumewe akirudi na kuwaacha mahali hapo walipopafikia baada ya safari ndefu iliyowachukuwa siku nyingi njiani, mahali pasipo na mji wala kijiji. Hapakuwa na hata dalili ya kuwepo mtu mahali popote karibu na hapo, akamfuata mumewe na kumuuliza:

 

“Unatuachia nani mahali hapa pasipo na mtu yeyote?”

 

Akamuuliza hivyo mara nyingi lakini Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) hakumjibu.

 

Mwisho Mama yake Ismaa’iyl akamuuliza:

 

“Allaah ndiye Aliyekuamrisha?”

 

Nabiy Ibraahiym akamjibu:

 

“Naam, ndiyo.”

 

Kwa imani iliyothibiti, kwa utiifu mkubwa na kwa moyo uliosalimu amri, Bibi Hajar akamwambia:

 

“Kwa hivyo Hatotupoteza”.

 

Hapo ndipo Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) alipogeuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Sham akimuacha nyuma mkewe na mwanawe wa mwanzo na wa pekee wakati ule, na baada ya kutembea muda kidogo mahali ambapo mkewe hakuweza kumuona, Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) akageuka nyuma na kuomba dua ifuatayo:

 

رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ

Rabb wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria wangu katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, kwenye Nyumba Yako Tukufu. Rabb wetu, ili wasimamishe Swalaah na Ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao na Uwaruzuku mazao ili wapate kushukuru. [Ibraahiym: 37]

 

Anaamrishwa Amchinje Mwanawe

 

Nabiy Ibraahiym alikuwa mara kwa mara akija Makkah kuwazuru mkewe na mwanawe na hapana anayejuwa uhakika wa idadi ya ziara hizo, isipokuwa wanahistoria wameelezea juu ya ziara nne maarufu.

 

Ya mwanzo ni pale alipooteshwa kumchinja mwanawe wa pekee Ismaa’iyl (‘Alayhis-salaam) na mwanawe akakubali kutii amri hiyo, na alipomlaza mwanawe kifudifudi ili asiuone uso wake asije akamuonea huruma, na baada ya Ismaa’iyl (‘Alayhis-salaam) kutoa shahada, na Ibraahiym kusalimu amri kwa Allaah huku akijitayarisha kumchinja mwanawe, Allaah akamfunulia Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) kuwa asimchinje mwanawe na badala yake akamkomboa kwa kondoo.

 

Kisa hicho kimeelezwa ndani ya kitabu cha Allaah Aliposema:

 

فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ. ﴿١٠٣﴾ وَنَادَيْنَاهُ أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ﴿١٠٤﴾ قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا إِنَّا كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ. إِنَّ هَذَا لَهُوَ الْبَلَاء الْمُبِينُ﴿١٠٥﴾ وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ﴿١٠٧﴾

Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza kifudifudi juu ya kipaji. Na tukamwita: ee Ibraahiym. Kwa yakini umesadikisha ndoto. Hakika Sisi hivyo ndivyo Tunavyolipa wafanyao ihsan. Hakika hili bila shaka ni jaribio bayana. Na Tukamtolea fidia kwa dhabihu adhimu. [Asw-Swaffaat: 103-107].

 

Mama Yake Ismaa’iyl Na Kisima Cha Zamzam

 

Bibi Hajar (Mama yake Ismaa’iyl) akawa anakula zile tende alizowekewa na mumewe huku akimnyonyesha mwanawe, lakini haukupita muda mrefu maji yakaanza kupunguwa na hatimaye kumalizika, na mwanawe alipoanza kuona kiu, Bibi Hajar akaanza kuhangaika huku na kule akimtafutia maji.

 

Akaliendea jabali lililokuwa karibu yake - ‘Jabal Swafa’ – na kulipanda, na alipofika kileleni akaanza kutizama huku na kule akitafuta maji au msafara wa watu watakaokuwa na maji, lakini hakuona kitu.

 

Akateremka na kuanza kutembea taratibu penye bonde lililopo baina ya jabali Swafa na jabali Marwa, na alipofika kati kati ya bonde akaanza kukazana huku akiliendea jabali Marwa na kulipanda, na alipofika kileleni akaanza kutizama huku na kule, lakini bila mafanikio yoyote.

 

Anasema Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Hiyo ndiyo Saayi mnayotembea baina ya Swafa na Marwa.”

 

Bibi Hajar aliendelea kufanya hivyo mara saba, na alipokuwa akiliendea jabali Marwa akasikia sauti ngeni ikimsemesha. Alinyamaza kimya ili aisikie vizuri huku akitazama mahali alipo mwanawe, akamuona Malaika amesimama mahali kilipo kisima cha Zamzam hivi sasa, huku akichimba kwa ubawa wake mpaka maji yalipofurika, ndipo mamake Ismaa’iyl alipoyaendea na kuanza kuyachota kwa mikono yake huku akimnywesha mwanawe na kunywa yeye mwenyewe.

 

Alipokuwa akinywa na kumnywesha mwanawe, Malaika akamwambia:

 

“Usiogope - hutopotea, kwani hapa ndipo ilipo nyumba ya Allaah itakayojengwa na mtoto huyu na baba yake."

 

Watu Wa Kabila La Jurhum

 

Hazikupita siku nyingi na mama yake Ismaa’iyl akajiwa na msafara wa watu wa kabila la Jurhum ambao asili yao ni kutoka Yemen waliokuwa wasafiri waliopiga kambi sehemu ya chini ya mji wa Makkah mbali na hapo, na walikuja baada ya kuwaona ndege wakiruka sehemu aliyopo mama yake Ismaa’iyl wakasema:

 

“Bila shaka ndege hawa wameona maji”, na kwa vile inajulikana kuwa sehemu zile si kawaida kupatikana maji, wakaamua kutuma watumishi wakachunguze sehemu walipoonekana ndege, na walipokiona kisima cha maji ya Zamzam wakarudi kuwajulisha wenzao walioamua kukiendea haraka sana, lakini walipomuona mama yake Ismaa’iyl na mwanawe wakamuomba wakae naye wakamwambia:

 

“Utaturuhusu tukae pamoja na wewe mahali hapa?”

 

Mama yake Ismaa’iyl akawaambia:

 

“Nitakuruhusuni, lakini maji haya ni yangu.”

 

Wakasema:

 

“Tumekubali.”

 

Anasema Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

“Jambo hilo lilimfurahisha sana mama yake Ismaa’iyl, kwani alikuwa mwenye kupenda watu.”

 

Mwambie abadilishe kizingiti

 

Watu wa kabila la Jurhum wakateremka na kuazisha maisha mepya mahali hapo, na Nabiy Ismaa’iyl (‘Alayhis-salaam) akaishi pamoja nao, akajifundisha kwao lugha ya kiarabu, akajifundisha kuwinda, na alipokuwa mkubwa wakamuozesha mmoja katika binti zao.

 

Baada ya kuishi muda aloishi, mama yake Ismaa’iyl akafariki dunia na Ismaa’iyl akaendelea kuishi mahali hapo pamoja na watu wa kabila hilo la Jurhum.

 

Nabiy Ibraahiym alikuja kumtembelea mwanawe katika ziara yake ya pili lakini bahati mbaya hajamkuta nyumbani na badala yake alimkuta mkewe, na alipomuuliza mahali alipo Ismaa’iyl akamwambia:

 

“Ametoka kwenda kututafutia rizki.”

 

Nabiy Ibraahiym akamuuliza juu ya hali zao na mwanamke akamjibu:

 

“Sisi ni wanadamu na hali zetu ni za dhiki na shida.”

 

Akaendela kumshitakia hali zao, na Nabiy Ibraahiym alipoondoka kurudi nchi ya Palestina akamwambia:

 

“Akirudi mumeo msalimie kisha mwambie abadilishe kizingiti cha nyumba.”

 

Aliporudi Nabiy Ismaa’iyl (‘Alayhis-salaam) alihisi kuwa jambo fulani limetokea nyumbani kwake, akamuuliza mkewe:

 

“Alikuja mtu hapa?”

 

Mkewe akajibu:

 

“Ndiyo, alikuja mzee mmoja na wasfu wake ni hivi na hivi, akauliza juu yako na mimi nikamwambia ulipo, akaniuliza juu ya hali zetu, nikamwambia kuwa sisi ni wanadamu na kwamba hali zetu ni za dhiki na shida.”

 

Akamuuliza:

 

“Alikuusia jambo lolote?”

 

Akajibu:

 

“Ndiyo, alinambia ukija nikusalimie kisha nikwambie ubadilishe kizingiti cha nyumba.”

 

Akamwambia:

 

“Yule alikuwa baba yangu na ameniamrisha nifarikiane na wewe, kwa hivyo rudi kwa wazee wako.”

 

Baada ya kumtaliki mkewe wa mwanzo, Nabiy Ismaa’iyl (‘Alayhis-salaam) akaoa mke mwingine, na inasemekana kuwa alikuwa binti wa Mudhaadh bin Amru aliyekuwa Sheikh wa kabila la Jurhum.

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) akaja tena kumtembelea mwanawe katika ziara ya tatu, na safari hii hajamkuta pia, na alipomuuliza mkewe akamwambia:

 

“Amekwenda kutuletea mahitaji yetu.” Na Ismaa’iyl alikuwa mwindaji anayesafiri mara kwa mara sehemu za mbali kwa ajili ya kazi yake hiyo na huchukuwa muda mrefu Swafarini.

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) akamuuliza:

 

“Vipi hali zenu?”

 

Akajibu:

 

“Tumesitirika AlhamduliLlaah tumo katika kheri kubwa.”

 

Akawa anasema hivyo huku akimshukuru Allaah.

 

Nabiy Ibraahiym akamuuliza:

 

“Mnakula chakula gani?”

 

Akajibu:

 

“Nyama.”

 

Akamuuliza:

 

“Mnakunywa nini?”

 

Akajibu:

 

“Maji.”

 

Akamwambia:

 

“Allaah vibariki nyama na maji.”

 

Anasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Siku hiyo hawakuwa na chochote nyumbani kwao.”

 

Nabiy Ibraahiym akamwambia:

 

“Akirudi mumeo mpe salamu zangu na umwambie akidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yake.”

 

Aliporudi Ismaa’iyl akauliza:

 

“Alikuja mtu leo?”

 

Akajibu:

 

“Alikuja mzee mmoja mwenye umbo zuri, akataka kujuwa habari zako, nikamjulisha, akaniuliza juu ya hali zetu nikamwambia kuwa tupo katika kheri.”

 

Akamuuliza:

 

“Alikuusia jambo lolote?”

 

Akamwambia:

 

“Ndiyo, yeye anakupa salamu nyingi na anakwambia ukidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yako.”

 

Akamwambia:

 

“Yule alikuwa baba yangu na ananiamrisha nikamatane na wewe.”

 

Wananyanyua Nguzo za Msikiti

 

Nabiy Ibraahiym akaja tena katika ziara yake ya nne, na safari hii Ismaa’iyl alikuwepo nje ya nyumba yake chini ya mti karibu na kisima cha maji ya zamzam akichonga mshale wake, na alipomuona baba yake akamnyanyukia kwa heshima kubwa, akamwamkia kama mtoto anavyoamuamkia baba yake wakakumbatiana kisha Nabiy Ibraahiym akasema:

 

“Allaah amenipa amri.”

 

Ismaa’iyl akamwambia;

 

“Fanya kama ulivyoamrishwa na Rabb wako.”

 

Akamwambia:

 

“Na wewe unisaidie.”

 

Akamwambia:

 

“Nitakusaidia.”

 

Akamwambia:

 

“Allaah Ameniamrisha nijenge nyumba mahali hapa.”

 

Akamuonesha ile sehemu ya ardhi iliyoinuka karibu na kisima cha maji ya zamzam, kisha wote kwa pamoja wakaanza kufanya kazi ya kuzinyanyua nguzo za nyumba na kuijenga Al-Ka’abah, na Ismaa’iyl akawa anamsogezea baba yake mawe huku Ibraahiym akijenga, mpaka nyumba ilipokamilika. Walikuwa wakijenga huku wakiomba dua ifuatayo:

  

“Eee Rabb Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga huu Msikiti.”

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

Na aliponyanyua Ibraahiym na Ismaa’ily msingi wa Nyumba (Al-Ka’abah): Rabb wetu, Tutakabalie, hakika Wewe ni Mwenye kusikia yote,Mjuzi wa yote. [Al-Baqrah:127]

 

Na Akasema (Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa):

  

رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ أَنتَ العَزِيزُ الحَكِيمُ

Rabb wetu, wapelekee Rasuli miongoni mwao atakayewasomea Aayaat Zako na atakayewafunza Kitabu na Hikmah na atakayewatakasa. Hakika Wewe ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al Baqarah:129]

 

Na hii ndiyo tafsiri ya hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa juu ya mwanzo wa amri yake akasema:

  

“Mimi ni dua ya baba yangu Ibraahiym na bishara ya ndugu yangu ‘Iysa (‘Alayhis- salaam).”

 

Anasema Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhu) kuwa baada ya kukamilisha ujenzi wa Msikiti wa Al-Ka’abah, Allaah akamuamrisha Nabiy Ibraahiym awatangazie watu waje kuhiji, na Nabiy Ibraahiym akasema:

 

“Ewe Mola wangu vipi itawafikia sauti yangu.”

 

Akamwambia:

 

“Juu yako ni kutangaza tu, na ni juu Yangu kuifikisha,” ndipo Nabiy Ibraahiym alipopanda juu ya kilele cha mojawapo ya milima ya Makkah na kupaza sauti yake akisema:

 

“Enyi watu mumefaridhishiwa Hijah katika nyumba kongwe,” na tangazo hilo likamfikia kila kiumbe baina ya mbingu na ardhi.

 

“Hamuoni kuwa watu wanauitikia mwito huo kutoka katika kila pembe ya dunia? Na katika riwaya nyingine; “Na wa mwanzo kuuitikia mwito huo walikuwa watu wa Yemen."

 

Kisa cha Watu Wa Ndovu (Aswhaabul Fiyl)

 

Abraha Mhabeshi aliyekuwa gavana wa An-Najaashiy katika nchi ya Yemeni iliyokuwa ikitawaliwa na Ethiopia wakati huo alikuwa akiona wivu kila anapowaona waarabu wakifunga safari ndefu kwenda kuizuru Al-Ka’abah, na kwa ajili hiyo akaamua kujenga kanisa kubwa kati ya mji wa Sana-a (mji mkuu wa Yemen) kisha akawataka waarabu waache kwenda Makkah na badala yake wakahiji penye kanisa lake.

 

Habari hizo zilimfikia mmoja katika watu wa kabila la bani Kinanah, aliyeamua kuingia kanisani nyakati za usiku na kulipaka mavi, jambo lililomghadhibisha sana Abraha aliyekusanya jeshi kubwa lenye idadi ya askari wanaozidi elfu sitini pamoja na tembo ishirini na mbili na yeye mwenyewe akiwa juu ya tembo mkubwa sana, na kuelekea nalo Makkah kwa ajili ya kuibomoa Al-Ka’abah.

 

Alipokaribia Makkah, penye bonde la Muhsir baina ya Muzdalifa na Mina, tembo mkubwa akapiga magoti na kukataa kuendelea na safari. Ikawa kila wanapomuelekeza kusini au kaskazini anainuka na kutembea, lakini wanapomuelekeza upande wa Makkah anakataa na hupiga magoti.

 

Wakawa katika hali hiyo mpaka pale Allaah alipowapelekea ndege makundi kwa makundi, wakawapiga kwa mawe ya udongo unaounguza.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ ﴿١﴾أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ ﴿٢﴾وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ ﴿٣﴾تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ ﴿٤﴾فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ مَّأْكُولٍ ﴿٥﴾

Je, hukuona (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) jinsi Rabb wako Alivyowafanya watu wa tembo?  Je, Hakujaalia hila zao katika maangamizi?. Na Akawatumia juu yao ndege makundi kwa makundi yafuatanayo? Wakiwarushia mawe ya udongo uliookwa motoni. Akawafanya kama nyasi kavu zilizoliwa. [Al-Fiyl: 1-5]

 

Ndege walikuwa wakiwajia kwa wingi makundi kwa makundi, mfano wa vijumba mshale au zuwarde, kila mmoja akiwa amebeba mawe matatu yenye ukubwa kiasi cha dengu, moja mdomoni na mawili ameyabana mguuni, na kila anayepigwa na jiwe mwili wake hukatika vipande vipande na kufa.

 

Si wote waliopigwa na mawe hayo, walikuwemo wachache walioachwa wakarudi mbio kuelekea makwao huku wakiangukiana. Ama Abraha, Allaah alimsalitishia maradhi yaliyosababisha makucha yake kukatika na kupukutika huku akirudi alikotoka, na alifariki alipowasili mji wa Sana-a mwili wake ukiwa mfano wa kuku aliyenyonyoka manyoa.

 

Makureshi, wao walikimbilia sehemu mbali mbali mbondeni na juu ya vilele vya majabali wakihofia maisha yao, na hawakurudi majumbani mwao mpaka baada ya kumalizika yaliyotokea.

 

Tukio hili lilitokea mwezi wa Muharram kabla ya kuzaliwa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa siku hamsini au hamsini na tano takriban muwafaka wa mwisho wa mwezi February au mwanzo wa mwezi wa March mwaka 571 baada ya Nabiy ‘Iysa.

  

Katika tafsiri ya Suratul Fiyl anasema Ibni Kathiiyr;

 

“Hii ni mojawapo ya neema za Allaah walizopewa Makureshi baada ya kuwalinda na shari walهokuja nayo watu wa ndovu waliokuja wakiwa na azma ya kuibomoa Al-Ka’abah na kuiondoa ili isiwepo tena. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) aliwaangamiza na kuwalazimisha waliobaki warudi wakiwa wameshindwa juu ya kuwa walikuwa watu wanaofuata dini ya Manasara na kwa wakati ule wao walikuwa bora kuliko Makureshi waliokuwa wakiabudu Masanamu, lakini haya yalikuwa ni matayarisho ya kuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa sababu kauli nyingi zinasema kuwa katika mwaka ule alizaliwa.

 

Kama kwamba uhakika wa mambo unasema; ‘Enyi Makureshi hamkupata nusura hii juu ya Mahabeshi kutokana na ubora wenu, bali kwa ajili ya kuilinda nyumba kongwe itakayopata heshima kwa kuzaliwa hivi karibuni kwa Rasuli wa Allaah Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwisho wa Rusuli."

 

Habari za tukio hili zilienea kila pembe ya ulimwengu wa wakati ule, na kwa vile Wahabeshi walikuwa na uhusiano mzuri na Warumi, Waajemi waliokuwa wakingoja fursa nzuri kama hii wakaingia na kuiteka nchi ya Yemen kwa haraka sana, na dola mbili hizi (Uajemi na Roma) ndizo zilizokuwa dola kubwa za wakati ule, na wakati huo huo tukio hili la kuangamizwa kwa watu wa ndovu liliujulisha ulimwengu juu ya utukufu wa nyumba ile ya Allaah na kwamba Allaah ndiye aliyeitukuza na kuiadhimisha, na kwa ajili hiyo atakapotokea yeyote katika watu wake akasema kuwa yeye ni Nabiy, basi tukio hilo linampa nguvu mtu huyo.

 

Kwa hivyo ndani ya tukio hili mna hekima iliyojificha ya Allaah ya kuwapa ushindi washirikina dhidi ya watu wa imani kwa njia ya kimiujiza.

 

Kuujenga Upya Al-Ka’abah

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano wakati Makureshi walipoujenga upya Msikiti wa Al-Ka’abah, kwa sababu miaka mingi ilikwishapita tokea Nabiy Ismaa’iyl alipoujenga na hapakuwa na kilichobaki katika jengo hilo isipokuwa rundu la udongo lenye urefu wa kiasi cha dhiraa sita, bila ya kipaa, jambo lililowarahisishia wezi kuingia ndani na kuiba hazina zinazowekwa humo.

 

Na kwa vile miaka mingi ilikwishapita tokea kujengwa kwake, kanuni za maumbile zilikwishafanya kazi yake. Kuta zilikuwa na nyufa, na miaka mitano kabla ya kupewa utume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yalitokea mafuriko makubwa yaliyosababisha maji kuingia ndani ya Msikiti na kubomoa sehemu kubwa za Msikiti huo, na kwa ajili ya yote hayo Makureshi wakaamua kuujenga tena Msikiti huo.

 

Wakakubaliana kuwa zisiingizwe katika ujenzi wa jengo hilo pesa zozote za haramu. Zisiingizwe pesa za mahari ya mzinzi, wala pesa za riba, wala pesa alizodhulumiwa mtu n.k.

 

Walikuwa wakiogopa kuubomoa Msikiti na kuanza kuujenga upya wasije wakadhurika, mpaka alipotangulia Al Walid bin Mughiyrah na kuianza yeye kazi hiyo, na wenzake walipoona kuwa hapana kilichomsibu, ndipo nao wakaingia kazini. Wakawa wanaendelea kuubomoa mpaka walipozifikia nguzo zilizosimamishwa na Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam), kisha wakaanza kuujenga upya Msikiti huo, na kila kabila likapewa sehemu yake ya kujenga, na kila kabila lilikuwa likikusanya mawe yake ya ujenzi, na msimamiaji wa ujenzi alikuwa Mrumi aitwae Baqum.

 

Kazi ilikwenda vizuri mpaka ulipofika wakati wa kulirudisha jiwe jeusi mahali pake, ndipo mzozo ulipoanza kila kabila likataka kupewa heshima hiyo ya kulirudisha mahali pake.

 

Mgogoro uliendelea muda wa siku nne au tano na mambo yakawa magumu hata watu wakakaribia kutaka kupigana vita, panga mkononi mpaka pale Abu Umayyah bin Mughiyra Al Makhzumiy alipotoa rai kuwa; wa mwanzo kuingia Msikitini kupitia mlangoni ndiye atakayeamua baina yao, na wote wakaridhika na rai hiyo.

 

Allaah akataka Nabiy wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awe mtu huyo, na walipomuona tu akiingia, wote kwa pamoja wakapiga ukelele wa kuridhika:

 

"Huyu Muaminifu! Sote tumeridhika naye, huyu Muhammad."

 

Alipojulishwa juu ya uamuzi huo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (hii ilikuwa kabla ya kupewa utume) alikubali, na kwa utulivu akaomba kiletwe kitambaa, akakitandaza na kuliweka jiwe jeusi juu yake, kisha akawataka viongozi wa makabila yote kila mmoja akamate upande wa kitambaa, kisha wanyanyuwe kwa pamoja. Wakalinyanyua na walipopafikia mahali pa kuliweka, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) akalinyanyua yeye kwa mikono yake miwili na kulirudisha mahali pake.

 

Kwa njia hii Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliweza kulitatua tatizo lililokaribia kuleta umwagaji wa damu mkubwa baina ya Makabila ya Kikureshi, na kila mmoja aliondoka hapo akiwa ameridhika.

 

Wanaishiwa Na Pesa za Halali

 

Makureshi walishindwa kuukamilisha Msikiti baada ya kuishiwa na pesa za halali, wakaamua kupunguza kiasi cha dhiraa sita upande wa kaskazini mwa Al-Ka’abah na hii ni ile sehemu inayojulikana kwa jina la Al Hijr (Hijr Ismaa’iyl) wakashindwa kuunganisha Msikiti pamoja na Hijri Ismaa’iyl ambayo asili yake ilikuwa imekamatana na Msikiti. Wakaunyanyua mlango kiasi cha dhiraa mbili kutoka juu ya ardhi asiweze kuingia isipokuwa wanayemtaka wao tu, na urefu wa jengo ulipotimia kiasi cha dhiraa kumi na tano wakaezeka sakafu juu ya nguzo sita, na baada ya kumalizika kazi hiyo, Al-Ka’abah ikawa na umbo la mraba lenye urefu wa mita kumi na tano, na upande wa jiwe jeusi pamoja na upande wa pili yake (mkabala wake) pande zote mbili kila moja ilikuwa na urefu wa mita kumi.

 

Na jiwe jeusi liliwekwa juu kiasi cha urefu wa mita unusu kutoka juu ya ardhi, na upande wa mlango na upande wa mkabala wake ukawa na urefu wa mita kumi kila upande, na mlango ukanyanyuliwa kiasi cha mita mbili kutoka juu ya ardhi, na upande wa nje ya Al-Ka’abah ikaachwa ikiwa imezungukwa na msingi ulionyanyuka kutoka juu ya ardhi kiasi cha robo mita na upana wa kiasi cha nusu mita.

 

Na sehemu hii ilikuwa ikiitwa Ash Shadherwan, sehemu ambayo asili yake ilikuwa ndani ya jengo la Al-Ka’abah, lakini Makureshi iliwabidi waiache sehemu hii bila kuijenga, na kwa ajili hiyo Msikiti ukawa na umbo la mraba badala ya umbo lake la asili lililofanana na herufi D iwapo utaunganishwa na Hijr kama ulivyojengwa na Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis salaam).

 

Mara Ngapi Umebomolewa na Kujengwa Upya?

 

Inajulikana kuwa Msikiti wa Al-Ka’abah umejengwa kwa mara ya mwanzo na Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

 

Na aliponyanyua Ibraahiym na Ismaa’ily msingi wa Nyumba (Al-Ka’abah): Rabb wetu, Tutakabalie, hakika Wewe ni Mwenye kusikia yote,Mjuzi wa yote.[Al-Baqarah: 127]

 

Imesimuliwa na Imam Muslim katika Sahihi yake na pia ndani ya vitabu vyengine mbali mbali vya elimu ya hadiyth na vya Siyrah katika mlango ya 'Kubomolewa na kujengwa upya Msikiti wa Al-Ka’abah' kama ifuatavyo:

 

Sehemu kubwa ya Msikiti iliungua wakati Al Hajjaj alipoushambulia akitumia 'Manjaniq' (mtambo wa kutupa mawe uliokuwa ukitumika katika vitani vya zamani) akitaka kumuuwa ‘‘Abdullaah bin Az-Zubayr bin ‘Awaam (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na hii ilikuwa wakati wa utawala wa Yazid bin Mu’aawiyah.

 

Mwana wa Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliuacha Msikiti kama ulivyo mpaka ulipoingia msimu wa Hijah wa mwaka ule na watu wakawa wengi, akawakusanya na kuwahutubia, akasema:

 

"Enyi watu! Nataka ushauri wenu juu ya Al-Ka’abah. Niuvunje Msikiti wote kisha niujenge upya au nitengeneze tu sehemu zilizoungua?"

 

Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

"Mimi ninayo rai, naona ni bora usiubomoe, bali utengeneze tu na uiache kama ilivyo nyumba waliosilimu watu juu yake, na mawe waliosilimu watu juu yake, na alitumwa kwa ajili yake nyumba hiyo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)."

 

Mwana wa Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

  

"Mmoja wenu ikiungua nyumba yake hatoridhika kuiacha ilivyo (bila shaka atapenda kuijenga upya), vipi basi nyumba ya Rabb wenu? Mimi nitaswali Istikhaarah mara tatu kisha nitaamua."

 

Na baada ya kukamilisha tatu akaamua kuubomoa, lakini kila mmoja aliogopa kupanda na kuianza kazi hiyo asije akadhurika, mpaka alipopanda mtu mmoja na kunyanyua jiwe, akalitupa chini, na watu walipomuona hajadhurika wakaingia na wao kazini na kuianza kazi ya kuubomoa Msikiti mpaka walipozifikia nguzo, kisha mwana wa Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akazinyanyua nguzo na kuujenga upya, na alipomaliza akaishonea Al-Ka’abah pazia, akaujenga Msikiti kama ulivyokuwa wakati wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) kisha akasema:

 

"Nilimsikia khale yangu (Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akisema kuwa amemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) akisema:

 

"Ingelikuwa watu hawakutoka hivi karibuni tu katika ujahilia na ningelikuwa na pesa za kutosha kuujenga vizuri Msikiti, ningeongeza dhiraa tano na kuuganisha na Hijri (Ismaa’iyl) kisha nikajaalia mlango kwa ajili ya watu kuingia ndani yake na mlango wa kutokea."

 

Na katika riwaya nyingine:

 

"Makureshi walipoijenga nyumba walishindwa kuikamilisha kwa sababu waliishiwa na pesa."

 

Na katika riwaya nyengine kupitia kwa ‘‘Abdullaah bin Abi Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"Na ningejenga milango miwili, mmoja mashariki na mmoja magharibi ikawa juu ya ardhi kisha ningeunganisha Msikiti na Hijri Ismaa’iyl."

 

Akasema ‘‘Abdullaah bin Zubair (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

"Mimi leo ninazo pesa na siwaogopei watu."

 

Akaongeza dhiraa tano na akajenga milango miwili, mmoja kwa ajili ya watu kuingia na mwengine wa kutokea.

 

Inajengwa Tena

 

Alipouliwa ‘‘Abdullaah bin Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Al Hajjaj akamuandikia ‘Abdul-Malik bin Marawan aliyekuwa Khalifa wa Waislamu wakati huo na kumjulisha juu ya mabadiliko aliyofanya mwana wa Az-Zubayr katika Msikiti, na ‘Abdul Malik akamjibu:

 

"Urefu alouongeza mwana wa Az-Zubayr uache na sehemu aloongeza katika Hijri ibomowe na milango aloiongeza izibe."

 

Al Hajjaj akafanya kama alivyoambiwa.

 

Hitimisho

 

Riwaya zinazokubalika zilizopokewa na 'Ulamaa zinasema kuwa Msikiti umejengwa mara nne.

 

  • Ya kwanza ulipojengwa na Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam).

 

  • Ya pili wakati wa ujahilia kabla ya Uislamu, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) alishiriki katika ujenzi huo na wakati huo alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano na katika riwaya nyingine alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano.

 

  • Ya tatu ulipojengwa na mwana wa Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

  • Ya nne ulipojengwa tena na Al Hajjaj baada ya kupewa amri na ‘Abdul Malik bin Marwaan ya kubomoa zile sehemu zilizoongezwa na mwana wa Az-Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Imepokelewa pia kuwa Haaruun Ar-Rashiyd alitaka ushauri wa kuujenga upya Msikiti huo na kuzirudisha zile sehemu zilizojengwa na ‘‘Abdullaah mwana wa Zubayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), lakini Imam Maalik akamnasihi kwa kumwambia:

 

"Kwa ajili ya Allaah ewe Amiri wa Waislamu, tafadhali iache nyumba kama ilivyo, na usiifanye ikawa mchezo kwa wafalme, kila mmoja akaja kubomoa na kuujenga upya atakavyo, na mwisho wake haiba ya nyumba itaondoka ndani ya vifua vya watu."

 

Share