030-Kutoa Zakaah: Walioharimishwa Kupewa

Kutoa Zakaah: Walioharimishwa Kupewa

 

Alhidaaya.com

 

 

1.    Kafiri

 

Katika Hadiyth iliyotangulia, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Zichukuliwe kutoka kwa matajiri Wao na kurejeshewa masikini Wao"

  

Na maana yake ni kuwa:-

 

Zichukuliwe kutoka kwa matajiri wa Kiislam na kupewa masikini wa Kiislam.

 

 

2.    Bani Hashim

 

Nao ni watoto wa Aliy na Aqiyl na Jaafar na Al ‘Abbaas na Al Harith (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

Nabiy (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

"Swadaqah haijuzu kupewa kwa watu wa Muhammad". [Muslim]

 

‘Ulamaa wamekhatalifiana juu ya ukoo wa Bani Al Muttalib, iwapo nao pia hawapewi katika mali ya Zakaah au wanapewa. Imaam Ash-Shaafi’iy amesema kuwa hawa nao wasipewe katika mali ya Zakaah, na hii inatokana na Hadiyth iliyotolewa na Imaam Ash-Shaafi’iy na Imaam Ahmad na Imaam Al-Bukhaariy kutoka kwa Jubair bin Mut’am aliposema:

 

"Siku ya Khaybar (baada ya kumalizika vita hivyo), Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliikusanya upande mmoja sehemu ya ngawira ya watu wa ukoo wake katika Bani Haashim na ya Bani Al-Muttwalib na akawaacha (watu wa kabila lake) katika Bani Nawfal na Bani ‘Abdu Shams. Tukamwendea mimi na ‘Uthmaan bin ‘Affaan na kumuuliza:

 

"Ee Rasuli wa Allaah hawa ni Bani Haashim na sisi hatukanushi fadhila zao kutokana daraja yako mbele ya Allaah, lakini vipi hawa ndugu zetu katika Bani Al Mutwalib, umewaingiza wao ukatuacha sisi wakati nasaba yao na yetu juu yako ni sawa sawa?"

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"Sisi na Bani Mutwalib hatujafarikiana katika ujahilia wala katika Uislaam, bali sisi na wao ni kitu kimoja". Akaviingiza vidole vyake vya mkono wa kulia ndani ya vidole vya mkono wa kushoto na kuvichanganya."

 

Kutokana na ushahidi huu, baadhi ya maulamaa wakasema; 'Bani Mutwalib nao pia wanaingia katika kuharamishiwa kupewa katika Mali ya Zakaah".

 

 

3.    Baba Na Watoto

Haijuzu mtu kumpa katika mali ya Zakaah baba yake, mama yake, watoto wake na babu zake, na hii ni kwa sababu mtoaji Zakaah anawajibika kuwatizama watu hao na kuwapa katika mali yake, na kwa ajili hiyo, watu hao wanalazimika kuwa matajiri kutokana na utajiri wake.

 

 

4.    Mke

Haijuzu mtu kumpa mkewe katika mali ya Zakaah, na jambo hili linakubaliwa na ‘ulamaa wote na hii ni kwa sababu mtu anawajibika kumtizama na kumpa mkewe katika mali yake kama anavyowajibika kuwapa wazee wake wawili akiwa anao uwezo huo.

 

Anasema Ibnul Mundhir:

 

"Isipokuwa kama mke ana deni, basi hupewa Zakaah katika ile sehemu ya kuwasaidia wenye madeni kwa ajili ya kulipa deni hilo".

 

Ama ikiwa mke ni tajiri mwenye uwezo wa kutoa Zakaah, basi yeye anarushusiwa kumpa mumewe katika mali ya Zakaah kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

"Amesema kweli Ibn Mas’uud, mumeo na mwanao wanastahiki zaidi kuwapa Swadaqah". [Al-Bukhaariy]

 

 

5.  Haijuzu kuitumia mali ya Zakaah kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah kama vile kujenga misikiti, kununua misahafu, kununua vifaa vya kusaidia kuosha maiti nk. Na hii ni kwa sababu Allaah kwa hekima yake keshazitaja na kuzisherehesha njia za kutoka Zakaah katika aya iliyotangulia ya Suwrah At-Tawbah na akaikamilisha aayah hiyo kwa kusema;

 

  ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah: 60]

 

Share