033-Kutoa Zakaah: Kuisafirisha Zakaah

 

Kutoa Zakaah: Kuisafirisha Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

‘Ulamaa wengi wamekubali kuwa mali ya Zakaah (Zakaatul Maal - si Zakaatul Fitwr) inaweza kusafirishwa na kutolewa katika nchi nyingine kwa wanaoistahiki zaidi ikiwa watu wa mji anaoishi mtoaji hawaihitajii zaidi mali hiyo. Ama ikiwa katika nchi hiyo wapo wanaoihitajia, basi zipo Hadiyth zinazotujulisha kuwa Zakaah ya kila nchi wanapewa masikini wake.

 

Katika madhehebu ya Imaam Abu Haniyfah, wao wanasema:

 

"Ni Makruuh kuisafirisha mali ya Zakaah isipokuwa ikiwa kwa ajili ya kumsaidia ndugu wa nasaba mwenye kuihitajia, na hii inatokana na umuhimu wa kuunganisha undugu huo, au pia kwa ajili ya watu wenye shida sana katika watu wa nchi yake, au kwa ajili ya kuiondoa kutoka nchi ya kikafiri na kuipeleka katika nchi ya kiislam."

 

Madhehebu ya Imaam Ash-Shaafi’iy yanasema:

 

"Haijuzu kuisafirisha mali ya Zakaah na inawajibika kutolewa katika nchi iliyochumwa mali hiyo isipokuwa pakikosekana wenye kuihitajia Zakaah hiyo katika nchi hiyo".

 

Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipewa ugavana wa nchi ya Yemen na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alipotawala ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuacha Mu’aadh aendelea kuwa gavana wa nchi hiyo. Lakini Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipompelekea ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) theluthi ya mali ya Zakaah, ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikataa kuzipokea akamwambia:

 

"Sikukupeleka uwe mchotaji (wa mali) wala mpokeaji wa kodi, bali nimekupeleka kwa ajili ya kuchukua mali (ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kuzirudisha kwa masikini wao".

 

Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

"Nisingekuletea ila kwa sababu sikumpata (masikini) anayezistahiki kuzichukua".

 

Share