Kwa Nini Qunuwt Inasomwa kwa Sauti

 

Kwa Nini Qunuwt Inasomwa kwa Sauti

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Nimejadiliana na mwenzangu kuhusu aya hii, akaniuliza swali nimeshindwa kujibu, hivyo nahitaji usaidizi kwenu. Aniuliza mbona Qunut inasomwa katika swala ya witri kwa sauti nazo pia ni dua?

Wa shukran

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hili ni suala kubwa ambalo huwachanganya wengi. Hata hivyo, suala hilo halifai kuwa na utata kwa sababu misingi mikubwa kwetu kufuata ni Qur-aan na Sunnah za Nabiy wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Ibaadah zote ambazo tunazitekeleza ni Tawqiyfiy (kufuata tu kama ilivyofanywa au kuamrishwa na kwetu hatuna maoni yetu wala rai).

Ama Swalaah na du’aa ni ‘Ibaadah ambazo tunafaa sisi kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila kuona tungeweza kufanya hivi au vile. Kuhusu Swalaah, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali[Al-Bukhaariy].

 

Na akasema tena kuhusu kufuata matendo yake:

 

“Mwenye kufanya ‘amali isiyokuwa na hukmu yetu, itakataliwa” [Muslim].

 

Kwa minajili hiyo, tunampata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anaswalisha Swalaah ya faradhi ambazo alikuwa analeta Qunuwt kwa sababu ya balaa, shida au tatizo kama kule kuuliwa kinyama Maswahaba zake sabini alikuwa analeta kwa sauti na Maamuma kuitikia Aamiyn kwa sauti. Mbali na kuwa Qunuwt ni du’aa lakini kumepatikana uthibitisho wa matendo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na hilo la Qunuwt linatofautiana na du’aa za nyakati nyingine. Kwa ajili hiyo mambo hayo mawili hayawezi kulinganishwa.

 

Tufahamu kuwa pia Suwratul-Faatihah ni du’aa, na katika Swalaah ya Adhuhuri, Alasiri, rakaa ya tatu ya Maghrib na rakaa ya tatu na nne ya ‘Ishaa huwa tunasoma lakini si kwa sauti, kwani hivyo ndivyo tulivyopekea katika mafundisho. Kwa minajili hiyo, tutaona kuwa ‘Ibaadah zinatakiwa kufanywa kama zilivyofundishwa na zilivyopokelewa katika Shariy’ah na si kwa kutumia akili zetu kuwa maadam sehemu kadhaa imefanywa hivi basi na kwengineko itafanywa hivyo hivyo. Si lazima hivyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share