Mume Kumwita Mke Mchawi

SWALI:

 

ASALAM ALEHKU

 

POLENI SANA KWA KAZI NZITO NA HONGERENI SANA MWENYEZI MUNGU ATAWALIPA ZAIDI KWA KUJITOLEA KUTU FAHAMISHA MAMBO AMBAYO ATUYAJUI YA DINI YETU.

 

SWALI LANGU NAOMBA KUJUA NINI HUKU YA MUME ANAE MUITA MKEWE MCHAWI ILE HALI MKEWE HAJUI MAMBO HAYO. MKE ANA BAKI NA SIMANZI KWANI HAJUI KWA NINI MUMEWE ANA MUITA IVYO. KAZI NJEMA

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mume kumuita mkewe mchawi.

Hakika ni makosa kwa Waislamu kuitana majina baada ya kwamba wamejiweka mbali na hayo wanayoitiwa. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Enyi mlioamini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasiotubu, hao ndio wenye kudhulumu” (Al-Hujuraat [49]: 11).

 

Kumwita mtu mchawi katika Uislamu ni jina baya na ni dhambi kubwa, kwani  kwa mwenye kushiriki au kufanya kazi hiyo ya uchawi ni mtu muovu na adui mkubwa wa Dini. Na mwenye kuendelea kufanya jambo kama hilo baada ya kunasihiwa anafaa auliwe kishari’ah.

 

Linalohitajiwa kufanywa hapa katika kesi hii, ni mume kupatiwa mawaidha ya kwamba asirudie tena kumwita mkewe jina hilo kwani ni madhambi na mke naye amsamehe mumewe waweze kuishi kwa amani, utulivu na usalama. Na katika kumnasihi mume kutumike nasaha njema, mawaidha mazuri na hekima na InshaAllaah atakuwa ni mwenye kubadilika.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share