047-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Faida Muhimu Kuhusu Kumswalia Mtume Wa Ummah ‘Swalaatu 'Alan-Nabbiyy’ (Faida Ya Kwanza Na Ya Pili)

FAIDA MUHIMU KUHUSU KUMSWALIA MTUME WA UMMAH ‘SWALAATU 'ALAN-NABBIYY’

 

FAIDA YA KWANZA

 

Kinachoonekana ni kuwa nyingi katika hizi namna mbali mbali za kumswalia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), hakuna utajo wa Ibraahiym pekee bila ya jamaa zake, lakini imo ndani yake: 'kama Swallayta 'alaa aali Ibraahiym' [Kama Ulivyowaswalia jamaa zake Ibraahiym], na sababu ya hii ni kwamba katika Lugha ya Kiarabu, kizazi cha mtu kinajumuisha mtu mwenyewe kama kinavyojumuisha na wenginewe katika wanaomtegemea,  kama katika kauli ya Allaah (تعالى ):

 

((Hakika Allaah Alimteua Aadam na Nuuh na kizazi cha Ibraahiym na kizazi cha 'Imraan juu ya walimwengu wote)). [Al-'Imraan ]

 

((Hakika Sisi Tuliwapelekea kimbunga cha vijiwe, isipokuwa wafuasi wa Luutw. Hao Tuliwaokoa karibu na Alfajiri)). [54: 34]

 

Na katika hayo pia, ni kauli yake : (صلى الله عليه وآله وسلم) ((Ewe Allaah! Waswalie jamaa zake Abu Awfaa)). Pia lipo tamshi la Ahlul-Bayt (watu wa nyumba), kama kauli ya Allaah (تعالى ):

((Rehema ya Allaah na Baraka Zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii!)) [Huud 11: 73]

 

"Kwani hakika Ibraahiym ni katika wao. (amejumuishwa katika 'jamaa zake Ibraahiym) "

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

"Na kwa sababu hiyo, ndio ikaja katika matamshi mengi: 'Kamaa Swallayt 'alaa Aali Ibraahiym' [Kama Ulivyowaswalia jamaa zake Ibraahiym], na 'Kamaa Baarakta 'alaa Aal Ibraahiym' [Kama Ulivyowabariki jamaa zake Ibraahiym]. Na ikaja katika baadhi yake Ibraahiym mwenyewe, na hii ni kwa kuwa, yeye ndiye shina katika Swalah na Utakaso,  na waliobakia katika watu wa nyumbani kwake wanapata hayo kufuatana na hilo. Na imekuja katika baadhi yake kutaja haya, na hii ni kutanabahisha juu ya yote mawili.

Ukisha elewa hayo, kumezagaa maulizano baina ya Maulamaa kuhusiana na namna ya kushabihisha katika kauli yake: 'Kamaa Swallayta 'alaa… mpaka mwisho wake' (kama Ulivyomswalia mpaka mwisho wake), kwani ki kawaida katika kushabihisha ni kuwa anayeshabihishwa huwa si bora kuliko anayeshabihishwa naye. Na kwa hakika, hali hii hapa ni kinyume kabisa na ile ya kawaida, kwani Muhammad  (صلى الله عليه وآله وسلم) ni mbora zaidi kuliko Ibraahiym, na kwa kuwa yeye ni mbora, basi Swalah zinazoombwa zinakuwa ni bora zaidi kuliko Swalah zilizopatikana au zitakazopatikana. Maulaamaa wametoa majibu mengi kuhusu haya yanayopatikana katika Fat-h Al-Baariy na Al-Jalaa Al-Ifhaam. Majibu hayo yamefikia kumi. Baadhi yake ni dhaifu sana kupita kiasi kulinganisha na mengineyo, isipokuwa kauli moja tu ambayo ina nguvu na imependezeshwa na  Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah na Ibn al-Qayyim kwa kusema ni nzuri. Nayo ni ile kauli ya aliyesema:

“Hakika kizazi cha Ibraahiym kinajumuisha Mitume ndani yake, Mitume ambao kama wao hakuna katika jamaa zake Muhammad. Hivyo, inapoombwa Swalah kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na jamaa zake kama Swalah aliyoswaliwa Ibraahiym na jamaa zake ambao kuna Mitume ndani yake, jamaa zake Muhammad wanapata katika hayo yanayolingana nao, kwa vile wao - jamaa zake Muhammad - hawafikii daraja ya Mitume. Hivyo kinachozidi katika kilichoombwa ambacho wanastahiki kupewa Mitume tu akiwemo Ibraahiym, hubakia kuwa cha Muhammad  (صلى الله عليه وآله وسلم). Hivyo yeye hupata heshima ya cheo cha pekee ambacho hawafikii wengineo".  

 

Ibn Al-Qayyim amesema:

"Hii ni rai bora kuliko zote (za nyuma), na kilicho bora zaidi ya hii ni kusemwa kwamba Muhammad   (صلى الله عليه وآله وسلم) ni katika jamaa zake Ibraahiym, bali yeye ni mbora wao kama alivyosimulia 'Aliy Ibn Twalha kutoka kwa Ibn 'Abbaas (رضي الله عنهما) kuhusu kauli yake تعالى :

((Hakika Allaah Alimteua Aadam na Nuuh na kizazi cha Ibraahiym na kizazi cha 'Imraan juu ya walimwengu wote)). [Al-'Imraan ]

 

Ibn 'Abbaas amesema: "Muhammad ni katika jamaa zake Ibraahiym". Na hii ni Matini ikiwa wataingia Mitume wengine ambao ni vizazi vya Ibraahiym katika jamaa zake, basi kuingia kwa Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kunafaa zaidi. Hivyo kauli yetu huwa: "… Kama Swallayta 'alaa ali Ibraahiym [kama Ulivyowaswalia jamaa zake Ibraahiym]", inajumuisha kuswaliwa yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuswaliwa Mitume wote wengine waliotokana na kizazi cha Ibraahiym. Kisha Allaah Ametuamrisha kumswalia Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)  na jamaa zake khaswa, kwa kadiri tunavyomswalia yeye (صلى الله عليه وآله وسلم)  pamoja na wengine wote katika jamaa zake Ibraahiym kwa ujumla na yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) ni miongoni mwao.  Kwa hiyo jamaa zake Mtume wanapata yanayowastahiki wao na yanayobakia yote huwa yake yeye  (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Akasema: Wala hakuna shaka kwamba (jumla ya) Swalah wanayoipata jamaa zake Ibraahiym (pamoja) na Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم)  huwa pamoja nao ila  Swalah iliyo bora zaidi na kamilifu kuliko zote huipata Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) pekee. Kwa hiyo, anayoombewa yeye (صلى الله عليه وآله وسلم)  katika Swalah –kuswaliwa- ni hili jambo tukufu ambalo nalo  ndilo lililo bora zaidi kuliko anayoombewa Ibraahiym bila ya shaka yo yote ile.

Na hapo ndipo inapodhihiri ile faida ya kushabihisha na kwamba inakwenda sambamba na asli -kawaida- yake, na kwamba Swalah anayoombewa yeye (صلى الله عليه وآله وسلم)  kwa maneno haya ni ile iliyo tukufu na iliyo bora zaidi kuliko anayoombewa mwengineo. Basi ikiwa kusudio la du'aa ni kuwa yeye(صلى الله عليه وآله وسلم)  kashabihiana na yule anayeshabihishwa naye na kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) anayo sehemu iliyo kubwa zaidi, basi huwa kwake yeye aliyeshabihishwa kusudio zaidi ya aliyopewa Ibraahiym na mwengineo.

 

Na ikiongezewa hayo ni kuwa yule aliyeshabihishwa naye anapata mambo ambayo hawayapati wengineo.  

Kwa hivyo, imedhihirisha fadhila za Muhammad   (صلى الله عليه وآله وسلم) na utukufu wake juu ya Ibraahiym na juu ya kila jamaa zake wakiwemo miongoni mwao  Mitume kama anavyostahiki (utukufu). Ndio ikawa Swalah hii inathibitisha ubora huu na ni kitu kilichoshikamana naye. Na hivyo ndivyo itakiwavyo, kwani hayo ni katika masharti na matakwa yake.

 

‘Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam Tasliyman Kathiyran, Wa Jazaahu ‘Annaa Af-Dhwal Maa Jazaa Nabiyyan ‘An Ummatihi. Allaahumma Swalli ‘Alaa Muhammad Wa ‘Alaa Aali Muhammad, Kamaa Swallayta ‘Alaa Aali Ibraahiym Innaka Hamiydum-Majiyd, Wa Baarik ‘Alaa Muhammad Wa ‘Alaa Aali Muhammad Kama Baarakta ‘Alaa Aali Ibraahiym Innaka Hamiydum-Majiyd’. 

 

‘Basi Allaah Amswalie pamoja na jamaa zake, na Amshushie amani juu yake, maamkizi mengi ya amani, na Ampe jazaa njema kutokana na sisi (du'aa zetu) jaza bora kuliko zote Alizompa Mtume yeyote kutokana na Ummah wake. Ee Allaah! Mswalie Muhammad na jamaa zake Muhammad kama Ulivyowaswalia jamaa zake Ibraahiym, hakika Wewe ni Mwenye kusifika Mtukufu. Na Mbariki Muhammad na jamaa zake Muhammad kama Ulivyowabariki jamaa zake Ibraahiym, hakika Wewe ni Mwenye kusifika Mtukufu.’

 

 

FAIDA YA PILI

 

Msomaji mtukufu ataona kwamba matamshi haya yote ya Swalah juu ya tofauti ya aina zake, yote yana kuswaliwa kwa jamaa zake Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), wake zake, kizazi chake pamoja na yeye mwenyewe (صلى الله عليه وآله وسلم). Kwa hiyo basi, sio katika Sunnah wala mtu hatokuwa anatekeleza amri ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) ikiwa atafupisha kwa kusema tu: 'Allaahumma Swalli 'alaa Muhammad' pekee, bali hakuna budi kuleta aina mojawapo ya Swalah hizi kwa ukamilifu kama ilivyokuja kutokana na yeye  (صلى الله عليه وآله وسلم), wala hakuna tofauti baina ya Tashahhud ya kwanza na ya mwisho. Hii ni matini kutoka kwa Imaam Ash-Shaafi'iy katika Al-Umm akisema:  "Tashahhud katika ya kwanza na ya pili ni sawa sawa  -tamshi moja- hayatofautiani. Na maana ya kauli yangu “Tashahhud” ni “Tashahhud was Swalaatu ‘alaan Nabiyyi“ ni kushuhudia na kumswalia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), haitoshi moja bila ya nyingine."

 

Na katika maajabu ya zama hizi na katika fujo za kielimu ni kuwa  baadhi ya watu -naye ni Ustaadh Muhammad Is-'aaf An-Nashaashiyby katika kitabu chake 'Al-Islaamus-Swahiyh' (Uislamu Sahihi),- wana ushupavu wa kukanusha kuwaswalia jamaa zake Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati wa kumswalia yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya kuthibiti hayo katika Swahiyhayn (Al-Bukhaariy na Muslim), na kwengineko na kutoka kwa kundi la Maswahaba  mbali mbali wakiwemo Ka'ab bin 'Ujrah, Abu Humayd As-Saa'idy, Abu Sa'iyd Al-Khudriyy, Abu Mas'uud Al-Answaariy, Abu Hurayrah na Twalha bin 'Ubaydullaah. Na katika Hadiyth zao (imeonekana kwamba) walimuuliza Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم): "Vipi tukuswalie?" Akawafundisha(صلى الله عليه وآله وسلم) aina hizi. Na hoja ya An-Nashaashiyby katika kukanusha ni kwamba Allaah تعالى Hakutaja katika kauli Yake mtu mwengine yeyote yule pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم):

إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

((Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Mtume. Enyi mlioamini! Mswalieni na muombeani rahma)). [Al-Ahzaab: 56].

 

Kisha akaendelea kukanusha bali alipindukia mipaka katika kukanusha kwamba Maswahaba wamemuuliza   (صلى الله عليه وآله وسلم) swali kama hilo, kwa sababu ya maana ya 'Swalah' ilijulikana kwao, nayo ni 'du'aa'. Hivyo, itakuwaje wamuulize?!   

 

Huku ni kuchanganyikiwa kuliko wazi kabisa, kwani swali lao -Maswahaba- halikuwa kuhusu maana ya kumswalia yeye   (صلى الله عليه وآله وسلم) hata akajibu alivyotaja, bali lilikuwa ni vipi kumswalia yeye  ,(صلى الله عليه وآله وسلم) kama ilivyothibiti katika riwaayah zote zilizotangulia kuashiriwa. Na wakati huo hapatokuwa na la kushangaza, kwani walimuuliza (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu namna ya utekelezaji kishari’ah -kama ilivyo katika Shari’ah- jambo ambalo hawawezi kulielewa isipokuwa kwa njia ya uongofu kutoka kwa Mjuzi na Mwenye Hikima na Muwekaji wa Shari’ah. Na hii ni kama lau walimuuliza kuhusu vipi utekelezaji wa Swalah ya Faradhi kutokana na kauli ya Allaah تعالى:

وََأَقِيمُوا الصَّلَاةَ

Kwani elimu yao ya maana ya asili ya Swalah katika lugha haiwatoshelezi kuuliza kuhusu vipi unakuwa utekelezaji wake kishari’ah, na hii ni dhahiri kabisa.

 

Ama hoja yake -An-Nashaashiyby- iliyohusishwa si lolote, kwani ni jambo linaloeleweka vizuri miongoni mwa Waislamu kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) ndie mbainishaji wa maneno ya Mola wa Walimwengu kama Anavyosema:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

((Nasi Tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyo teremshwa kwao, wapate kufikiri))  [An-Nahl: 44]

 

Hivyo Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amebainisha wazi namna gani aswaliwe na ndani yake imejumuisha kutaja jamaa zake. Hivyo ni wajibu kukubali hivyo kutokana na yeye (صلى الله عليه وآله وسلم), na kwa kauli yake Allaah:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ

 

((Na anachokupeni Mtume chukueni, …)) [al-Hashr: 7]

 

Na kwa kauli yake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth Swahiyh mash-huur([1]): ((Nimepewa Qur-aan pamoja na iliyofanana nayo)).([2])

 

Nashangazwa na wala sielewi ni nini hasa anachotaka kusema An-Nashaashiyby na kila aliyedanganyika na uongo wa maneno yake yenye majivuno. Itakuwaje kwa anaekanusha Tashahhud katika Swalah kabisa, au kukanusha mwanamke mwenye hedhi kuacha kuswali na kufunga akiwa katika masiku yake, yote kwa hoja kwamba Allaah (تعالى) Hakutaja Tashahhud kwenye Qur-aan; bali Ametaja kisimamo na kusujudu tu, na kwamba Yeye (تعالى) katika Qur-aan Hakumuondoshea mwanamke mwenye hedhi kuswali na kufunga, bali ni wajibu juu yake -mwenye hedhi– kuzitekeleza! Hivyo, wanakubali na hoja kama hizi ambazo zinakwenda sambamba na hoja zake za asili au sivyo. Je, wanakubaliana naye huyu mkanushaji katika kukanusha kwake, au wanapingana nae? Wakiwa wanakubaliana naye jambo ambalo hatulitarajii, basi watakuwa kwa uhakika wamepotea upotofu wa mbali, na wamefarikiana na Waislamu. Na ikiwa wanapingana naye, basi watakuwa wamewafikishwa na wamesibu na walichomjibu mkanushaji. Na sisi ndio jawabu letu kwa An-Nashaashiybiy, na tumekubainishia hivyo.

 

Basi tahadhari ewe Muislamu kujaribu kufahamu Qur-aan bila ya kurejea kwenye Sunnah, kwani hakika hutoweza kufanya hivyo hata kama utakuwa katika lugha (Ya Kiarabu) ni Siybawayh([3]) wa zama zako. Huu hapa mfano mbele yako. Huyu An-Nashaashiybiy alikuwa ni mmoja kati ya Wataalamu bingwa na wakubwa wa lugha ya Kiarabu wa zama hizi, na wewe unamuona namna alivyopotoka baada ya kughururika kwa elimu yake katika lugha bila ya kutafuta msaada wa Sunnah katika kuweza kuifahamu Qur-aan, bali yeye ameikanusha hiyo Sunnah kama unavyoelewa. Na kuna mifano mingi tu kwa haya tuyasemayo, lakini hakuna nafasi ya kuitaja, (lakini) na katika tuliyoyataja yatatosheleza. Na Allah Ndie Muwafiqishaji.   

[1] Ni Hadiyth ambayo idadi ya wapokezi wake haijafikia idadi ya wapokezi wa Hadiyth ya Mutawaatir.

[2] Abu Daawuud na Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.

[3] Mwanasarufi mashuhuri na bingwa wa lugha ya Kiarabu katika karne ya pili Hijriyah.

 

Share