04-Swabrun Jamiyl: Subira Anaposibiwa Muislamu Na Maradhi

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

04 - Subira Anaposibiwa Muislamu Na Maradhi

 

 

 

Muumini anapopata masaibu na mitihani ya maradhi anapaswa kuvumilia kwa kutegemea fadhila ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ameahidi, pamoja na malipo mema tele, nako ni kwa kuridhika na majaaliwa na si kwa kuchukia na kuhamanika kwani hayatomfaa hayo ila ni kujizidishia maumivu, maradhi na dhiki. Wala haipasi kulaani maradhi kwa vyovyote kwani mja atakuja kukosa fadhila kama alivyofundisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

عَنْ جَابِرُ بْنُ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ دَخَلَ عَلَى أُمِّ السَّائِبِ أَوْ أُمِّ الْمُسَيَّبِ فَقَالَ:  ((مَا لَكِ يَا أُمَّ السَّائِبِ)) أَوْ ((يَا أُمَّ الْمُسَيَّبِ تُزَفْزِفِينَ؟)) قَالَتْ:  "الْحُمَّى لاَ بَارَكَ اللَّهُ فِيهَا"  فَقَالَ: ((لاَ تَسُبِّي الْحُمَّى فَإِنَّهَا تُذْهِبُ خَطَايَا بَنِي آدَمَ كَمَا يُذْهِبُ الْكِيرُ خَبَثَ الْحَدِيدِ)) مسلم

 

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)   kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliingia kwa Ummu As-Saaib au Ummu Al-Musayyib akasema: ((Je, una nini ee Ummus-Saaib?)) Au ((Ee Ummul-Musayyib; unatetemeka?)) Akasema: “Homa Allaah Asiibariki [ilaaniwe]” Akasema: ((Usiitukane homa kwani inaondosha dhambi za mwana Aadam kama moto unavyoondosha takatataka katika chuma)) [Muslim]

 

 

Basi vuta subira ee ndugu Muumini na mshukuru Rabb wako kwa neema tulizoaahidiwa za kusubiri masaibu ili ufutiwe madhambi yako na uzidishiwe mema yako huko Akhera na upandishwe daraja yako mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   kama ilivyothibiti katika Hadiythi zifuatazo:

 

 

1-Kufutiwa Madhambi Na Kupandishwa daraja:

 

 

 عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ابن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه)  قَالَ دَخَلْتُ عَلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَهُوَ يُوعَكُ، فَمَسِسْتُهُ بِيَدِي فَقُلْتُ:  "يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّكَ لَتُوعَكُ وَعْكًا شَدِيدًا" فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((أَجَلْ، إِنِّي أُوعَكُ كَمَا يُوعَكُ رَجُلاَنِ مِنْكُمْ)) فَقُلْتُ:  "ذَلِكَ أَنَّ لَكَ أَجْرَيْنِ؟"  فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((أَجَلْ)) ثُمَّ قَالَ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يُصِيبُهُ أَذًى مِنْ مَرَضٍ فَمَا سِوَاهُ إلاَّ حَطَّ اللَّهُ بِهِ سَيِّئَاتِهِ كَمَا تَحُطُّ الشَّجَرَةُ وَرَقَهَا)) متفق عليه

 

Kutoka kwa ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Niliingia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anaugua homa. Nikamgusa kwa mkono wangu nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika una homa kali?  Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Ndio! Ninaugua kama wanavyougua wawili wenu)). Nikasema: “Je ni kwa sababu utapata thawabu mara mbili?”  Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ((Ndio)) kisha akasema: ((Hakuna Muislamu yeyote anayefikwa na dhara kutokana na maradhi au vingineveyo isipokuwa Allaah Atamfutia     madhambi yake mfano wa majani yanavyopuputika mtini)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Na pia:

 عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((مَا مِنْ مُصِيبَةٍ تُصِيبُ الْمُسْلِمَ إلاَّ كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا عَنْهُ حَتَّى الشَّوْكَةِ  يُشَاكُهَا)) متفق

 

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:    ((Hakuna msiba wowote unaomsibu Muislamu isipokuwa tu Allaah Humfutia madhambi hata mwiba unaomchoma))  [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na pia:

 

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُول:  ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يُشَاكُ شَوْكَةً فَمَا فَوْقَهَا إِلاَّ كُتِبَتْ لَهُ بِهَا دَرَجَةٌ وَمُحِيَتْ عَنْهُ بِهَا خَطِيئَةٌ)) مسلم

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Muislamu hafikwi na (dhara lolote la) kuchomwa mwiba au zaidi ya hivyo isipokuwa Allaah Atampandisha daraja na Atamfutia madhambi kwa ajili yake)) [Muslim]

 

 

 

2-Kuvumilia ili kupata Jannah:  

 

 

عن عَطَاءُ بْنُ أَبِي رَبَاحٍ قَالَ قَالَ لِي ابْنُ عَبَّاسٍ أَلاَ أُرِيكَ امْرَأَةً مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ؟ قُلْتُ بَلَى. قَالَ: هَذِهِ الْمَرْأَةُ السَّوْدَاءُ أَتَتْ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَتْ:   إِنِّي أُصْرَعُ وَإِنِّي أَتَكَشَّفُ فَادْعُ اللَّهَ لِي. قَالَ:  ((إِنْ شِئْتِ صَبَرْتِ وَلَكِ الْجَنَّةُ وَإِنْ شِئْتِ دَعَوْتُ اللَّهَ أَنْ يُعَافِيَكِ)) فَقَالَتْ: أَصْبِرُ فَقَالَتْ: إِنِّي أَتَكَشَّفُ فَادْعُ اللَّهَ لِي أَنْ لاَ أَتَكَشَّفَ. فَدَعَا لَهَا  - متفق عليه

 

Kutoka kwa ‘Atwaa bin Abi Rabaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: “Ibn ‘Abbaas aliniambia: “Je nikuonyeshe mwanamke miongoni mwa watu wa Jannah?” Nikasema: “Ndio” Akasema: Huyu mwanamke mweusi alimwendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akasema: “Hakika mimi nina kifafa nami hukashifika   [ninapoanguka] basi niombee kwa Allaah”. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akasema: ((Ukitaka usubiri utapata Jannah, au ukitaka nimuombe Allaah Akuafu)) Akasema: Nitasubiri” Akasema tena: Hakika mimi nakashifika [nikianguka] basi mwombe Allaah nisikashifike” Akamuombea” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

3-Anayepotelewa na macho jazaa yake ni Jannah:

 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه)  قَالَ: سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((إِنَّ اللَّهَ قَالَ: إِذَا ابْتَلَيْتُ عَبْدِي بِحَبِيبَتَيْهِ فَصَبَرَ عَوَّضْتُهُ مِنْهُمَا الْجَنَّةَ)) يُرِيدُ عَيْنَيْهِ-  البخاري

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu)   amesema: Nilimsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema ((Hakika Allaah Amesema: Nitakapomjaribu mja Wangu kwa kukosa vipenzi vyake viwili [macho yake] Nitambadilishia Jannh badala yake)) [Al-Bukhaariy].

 

 

Na kuumwa kuna faida zake ambazo ni:

 

  • Yanampofika maradhi mtu, humfanya atambue kwamba yeye ni dhaifu, hana uwezo wa kujiondoshea dhara inapomfika isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hapo ndipo hutambua Qadar ya  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na pia hukumbuka Majina  Yake Mazuri na Sifa Zake mbali mbali; mfano wa sifa mojawapo ya Allaah ni Ash-Shaafi’ [Mwenye Kuponyesha]

 

  • Humfanya mtu aliyekuwa katika ghaflah ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  arejee kwa Rabb wake kwa vile Ndiye anayemhitaji zaidi wakati huu, kwani Yeye Subhaanahu wa Ta’aalaa ni Pekee Atakayeweza kumwondoshea dhara. Tajiri awe tajiri vipi lakini yanapomfika maradhi huenda madaktari wakashindwa kumtibu hata kama atatumia mali yake yote ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Hakutaka apate hiyo shifaa; kwani hakuna shifaa ila shifaa Yake. Hivyo Muumini huwa karibu zaidi na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa du’aa zake anazomkabili kumwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amuondoshee maradhi.

 

  • Muumini anapopatwa na maradhi humfanya atambue neema ya umri wake wa nyuma alipokuwa na afya, na hilo ni jambo la kushukuriwa anapotambua neema ya afya aliyokuwa nayo awali. Na hawezi kutambua na kushukuru yeyote isipokuwa Muumini tu.

 

  • Anapata kujifunza na kujua fadhila za kuugua na maradhi akatambua neema na mazuri aliyoahidiwa kama kufutiwa madhambi n.k. na hapo huzidishia iymaan yake na yaqini kuhusu Aliyoahidi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).    

 

Subira ya hali ya juu kabisa ni subira ya Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-Salaam) ambaye alifikwa na mtihani wa kusibiwa mali, watoto na siha. Kwa kuvumilia kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Alimrudishia yote aliyoyapoteza. Hiyo ilikuwa ni subira ya aina ya pekee. Pia tunayo mafunzo ya subira kutokana na visa vya Manabii wengineo, Salaf Swaalih [wema waliopita] n.k. 

 

 

 

Share