Kiungo Kilichojificha

 

 

Imekusanywa Na:

Muhammad Faraj Saalim (Rahimahu Allaah)

 

Imepitiwa Na:

Naaswir Haamid

 

Utangulizi

Tawhiyd

Maana Ya Tawhiyd?

‘Ibaadah

Aina Mbali Mbali Za Shirki

Jinni

Jina Lake

Imani Juu Ya Ghayb

Ushahidi Ndani Ya Qur-aan Tukufu

Ushahidi Ndani Ya Sunnah

Wameumbwa Kwa Moto Dalili Katika Qur-aan

Dalili Katika Sunnah

Majini Wanazaliana

Wameumbwa Kabla Ya Binadamu

Uhusiano Baina Ya Jinni Na Shaytwaan

Ibilisi Ni Katika Malaika?

Aina Za Majini

Mahali  Wanapoishi

Wanakula Na Kunywa

Wanaweza Kujigeuza

Wamo Wanawake Na Wanaume

Wanaowa?

Wanakufa?

Wamo Waislamu Na Makafiri

Waislamu Majini Wataingia Peponi?

Wanawaogopa Wanadamu

Wanasikia Habari Za Mbinguni

Uchawi

Nini Maana Ya Uchawi?

Utawezaje Kumjua Mchawi

Uchawi Upo -  Dalili Ndani Ya Qur-aan Na Sunnah

Soma Bahati Yako (Lucky Stars)

Uchawi

Umeanza Zama Za Nabii Sulaymaan ('Alayhis Salaam)?

Uchawi Ni Kufru

Hukumu Ya Uchawi Katika Diyn Ya Kiislamu

Kujikinga Na Shari Zao

Du’a Zinawakumba

Dhikru Llaah

Usiviingize Ndani Ya Nyumba Yako

 

 

 

UTANGULIZI

 

Shukrani zote ni zake Allaah, msaada wote tunamuomba Yeye tu, tunamtegemea Yeye tu, kwa sababu kila kisichokuwa Yeye ni dhaifu na nguvu zote na ufalme wote ni wake Yeye peke yake, milango Yake iko wazi siku zote.

 

Kawaida ya mwanadamu ni kuwa kila unapotaka msaada kutoka kwake, basi yeye hukasirika. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), anaghadhibika usipomuomba Yeye msaada wake.

 

Katika Hadiyth Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

((Yule asiyemuomba msaada Allaah basi hughadhibika naye.))

 

Tunashuhudia kwamba hakuna Mola Anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Mjumbe wake na kipenzi chake, ameufikisha ujumbe na ameituwa amana aliyopewa, amewatoa watu kutoka katika kiza cha kufru na ushirikina na kuwaingiza katika Nuru ya Uislamu kwa idhini ya Mola wake (Subhaanahu wa Ta’ala), amepigana jihaad kama alivyopaswa, basi tunakuomba Mola wetu Umsalie na kumsalimu Mtume wako huyu mtukufu pamoja na ‘Aali yake na Masahaba wake wakarimu.

 

Amma Ba’ad,

 

Nimeona ni vizuri niandike risaalah hii ili niwatahadharishe ndugu zangu Waislamu juu ya ubaya wa kuwaendea wachawi, wapiga ramli na watabiri, nikizingatia juu ya uhusiano huo nilioutaja hapo juu, baina ya Jinni na Mchawi.

 

Baada ya kumaliza kuisoma darsi hii Insha Allaah, tutakuwa tumekwisha ufahamu uhusiano uliopo baina ya Jinni na wachawi pamoja na wapiga ramli na watabiri ili tuweze kuepukana na shari zao.

 

Tunamuomba Allaah Atufungue vifua vyetu tuifahamu darsi hii na aijaalie kazi hii iwe halisi kwa ajili Yake tu - Aamin.

 

 

TAWHIYD

 

Atakayechunguza hali za Waislamu ataona kwamba haziridhishi hata kidogo. Waislamu wanategemea mataifa yasiyokuwa ya Kiislamu katika kila jambo lao. Iymaan zimekuwa dhaifu, Waislamu wameipoteza hata Swalah yao. Wako Waislamu wasioswali, na hata wale wanaoswali, basi wengi wao hawaswali kama inavyopaswa. Ujinga katika mambo ya diyn umeenea, uzushi (bid’ah) umezidi, ushirikina umekuwa ndiyo njia ya kupatia riziki.

 

Kutokana na hayo, umoja baina ya Waislamu ukaanza kutoweka na mapenzi yakageuka kuwa bughudha na heba yao ikaanza kupotea. Haya yote ni kwa sababu ya kutofuata itikadi iliyo sahihi aliyokuja nayo Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nayo ni itikadi ya TAWHIYD.

 

 

MAANA YA TAWHIYD?

 

Kwa ufupi, maana ya Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa kuzielekeza ‘ibaadah zote kwake Yeye tu (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Maulamaa wameigawa ‘ilmu hii yaTawhiyd katika mafungu matatu:

 

1 – Tawhiydur-Rubuubiyyah

 

Nayo ni kuamini kwamba aliyeumba kila kitu, anayeruzuku na kuendesha mambo yote ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Asiye na mshirika na pia kuamini kwamba Ufalme wote ni wake:

 

Allaah Anasema:

{{Sema: "Ni nani Mola wa mbingu na ardhi?" Sema: "Ni Allaah"}} [Suuratur-Raad: 16]

 

Na Akasema:

 

{{Sema: "Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni (kwa kuleta mvua) na katika ardhi (kwa kuotesha mimea) au ni nani anyemiliki masikio na macho? Na nani amtoaye mzima katika mfu na kumtoa mfu katika mzima? Ni nani atengezaye mambo yote? "Watasema:" Ni Allaah", basi sema; "Je! Hamuogopi?"}} [Suuratu-Yuunus: 31]

 

Shirk ya Ar-Rubuubiyyah

 

Mwenye kuamini kwamba yupo mwengine mwenye uwezo wa kumruzuku kwa njia za ghayb au wa kumtengenezea mambo yake asiyekuwa Allaah, huyo anakuwa ametenda kitendo cha Shirk Ar-Rubuubiyyah.

 

Anayewaendea wachawi au watabiri huwa anawategemea wamtengenezee mambo yake na kumwekea vizuri kwa njia za ghayb au kwa nguvu zisizoonekana, na kwa ajili hii anaingia katika shirk hii ya Ar-Rubuubiyyah.

 

2-Tawhiydul-Uluuhiyyah

 

Maana yake ni kuzielekeza ‘ibaadah zote kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Allaah Anasema:

 

{{Sema: "Hakika Swalah yangu, na ‘ibaadah zangu (zote nyengine) na uzima wangu na kufa kwangu, (zote) ni kwa Allaah Muumba wa walimwengu wote, Hana mshirika wake. Na haya ndiyo niliyoamrishwa na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha (kwa Allaah).}} [Suuratul-An ‘aam: 162-163]

 

 

Shirk Al-Uluuhiyyah

 

Mwenye kuelekeza ‘ibaadah zake kwa mwengine asiyekuwa Allaah, kwa kuswali penye kaburi lake, kuapa kwa jina lake, kuchinja kwa ajili yake, kuomba msaada wake, kumuogopa kuliko Mola wake au kufuata sheria zake zinazokwenda kinyume na sheria za Mola wake, n.k, huyo anakuwa amefanya kitendo cha Shirk Al-Uluuhiyyah.

 

Anayemwendea mchawi, hutakiwa kuchinja mnyama kwa ajili ya kuwaridhisha majini, hupewa herizi ambazo yareti kama angeweza kuzifungua na kusoma yaliyomo, basi angeona na kutambua kuwa yaliyoandikwa humo na wachawi hao ni mazungumzo baina yao na majini ya kuwataka wamlinde mtu huyo.

 

Hofu za watu wa aina hii  kwa wachawi huwa ni kubwa sana kuliko hofu yao kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na kuwategemea kwao wachawi hao katika kutengeneza mambo yao ni kwingi kuliko wanavyomtegemea Allaah.

 

Kwa hivyo anayemwendea mchawi au mtabiri anakuwa ametenda kitendo cha Shirik Ar-Rubuubiyyah.

 

 

3-Tawhiydul-Asmaa was-Swifaat

 

Allaah Amejipa majina mazuri mazuri na sifa nzuri nzuri na akawataka waja wake wamuombe na kumtukuza kwa majina na sifa hizo.

 

Allaah Anasema:

 

{{Na Allaah ana majina mazuri mazuri, muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake. Karibuni hivi watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.}} [Suuratul-‘Aaraaf: 180]

 

 

Shirk fiyl Asmaa was-Swifaat

 

Mwenye kuomba kwa majina ya wengine wasiokuwa Allaah, kama vile kuomba kwa majina ya Mitume, majina ya Mawalii n.k. na akayaacha majina hayo matukufu ya MwenyeziMungu, (kwa mfano badala ya kusema "Yaa Qawiyy, = Ewe Mwenye Nguvu, Yaa Maalik, = Ewe Mfalme, Yaa Qaadir = Ewe Mwenye Uwezo - hayo ni katika majina mazuri mazuri ya Allaah, akayaacha majina hayo. Akasema kwa mfano "Ewe Mtume fulani, Ewe Waliy Fulani, Ewe Swahaabah fulani au Ewe Jinni fulani" n.k.), huyo atakuwa ametenda kitendo cha Shirki ya Al-Asmaa was-Swifaat.

 

Atakayejaribu kuzigeuza sifa zake (Subhaanahu wa Ta’ala), au maana yake, au kufananisha sifa hizo ziwe sawa na sifa za binadamu au za kiumbe chochote kile, huyo pia atakuwa ametenda kitendo cha Shirkul-Asmaa was-Swifaat.

 

Anayemwendea mchawi au mpiga ramli, huyo anampa sifa hizo mchawi huyo pamoja na majini wake wanaomtumikia kwa kuamini kwake kwamba wao (majini na wachawi) wana uwezo wa kutengeneza, kudhuru, kubadilisha au kuijua ‘ilmu ya ghayb n.k. Na badala ya kuomba kwa majina mazuri mazuri ya Mola wake anakwenda kuomba kwa majina ya majini hao na mizimu yao n.k. Kwa ajili hivyo anakuwa ametenda kitendo cha kufru ya Al-Asmaa was-Swifaat.

 

 

‘IBAADAH

 

‘Ibaadah katika Uislamu, inakusanya matendo yote anayoyapenda Allaah na kuridhika nayo.

 

‘Ibaadah ziko aina nne:

 

 

1. 

‘Ibaadah za kimwili kama vile kuswali, kufunga, kuhijji, kutufu n.k.

2. 

‘Ibaadah za mali, kama vile kutoa zakkah, kuchinja, kutoa swadaqah n.k.

3. 

‘Ibaadah za Moyo kama vile khushuu katika Swala, kumnyenyekea Allaah, kumtegemea, kumuogopa, kumpenda, kumtukuza n.k. .

4. 

‘Ibaadah za kutamka kama vile kuomba du’aa, kuapa, kumdhukuru Allaah, n.k.

 

Tawhiyd ndiyo Moyo wa diyn ya Kiislamu, na hakuna diyn yoyote duniani inayohubiri Tawhiyd isipokuwa diyn hii tukufu. Lakini kinachosikitisha ni kwamba wapo wajinga wengi wasioijua Tawhiyd wameingiza mambo katika diyn hii hata ikaonekana kwa baadhi ya wasiokuwa Waislamu kama ni diyn ya ushirikina.

 

Wachawi, waganga na watabiri, wote hawa wanajinasibisha na diyn hii kwa kujiita Shaykh Fulani, Alhajj Fulani au Maalim Fulani na hawa wote Uislamu uko mbali kabisa nao.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuja, aliwakuta makuhani na watabiri waliokuwa wakiitwa "Arrafiyn", wakiwa wamejaa penye Al-Ka’abah na kazi zao zilikuwa ni kutabiri, kutisha na kuwadanganya watu kwamba eti wao wanaijua ‘ilmu ya ghayb na kwamba wana uwezo wa kudhuru na kunufaisha.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa na kazi kubwa ya kuwapiga vita waongo hao na kuwabainishia watu kwamba uwezo huo ni wa Allaah Peke Yake, na kwamba atakayewaendea waongo hao kuwauliza jambo, atakuwa amekwisha kufuru.

 

Hii ni kwa sababu Uislamu umekuja kuyapiga vita mambo hayo na umekuja kuwafahamisha watu kwamba hakuna aijuwae ghayb isipokuwa Allaah peke yake.

 

Allaah Anasema:

 

{{"Sema: "Hakuna aliyoko katika mbingu na ardhi ajuaye Ghayb (yasiyotokea) ila Allaah".}} [Suuratun-Naml: 65]

 

Kwa hivyo Malaika hawaijuwi ghayb, wala Mitume, wala hata Majini na watabiri pamoja na wachawi wao. Na mtu anapokutwa na shida au dhiki yoyote ile akawaendea watu wa aina hiyo na kumuacha yule ambaye kwake tu inapatikana faraji na kwake tu inaondoshwa dhiki, basi mtu huyo anakuwa amepotea upotofu mkubwa kabisa na anakuwa ameingia katika shirki itakayomfanya Pepo iwe haramu kwake na Moto uwe ni makaazi yake. Tunamuomba Allaah Atuingize katika Pepo Yake na kutuepusha na Moto Wake - Aamiyn.

 

 

AINA MBALI MBALI ZA SHIRK

 

Shirk ziko aina nyingi na katika sura mbali mbali, na siyo katika sura ya uchawi tu.

 

·         Miongoni mwa shirk ni kwenda katika makaburi ya mawalii na
kutafuta  baraka au kuomba shida zako ziondolewe hapo na kwa uwezo wao.

·         Kuchinja kila mwaka au wakati maalum kwa ajili ya kuilinda nyumba na majini au Shaytwaan.

·         Kuchinja kwa ajili ya Bwana Arusi na Bibi Arusi ili wairuke damu ya mnyama huyo eti Jinni atashughulika na damu hiyo na wasiwadhuru maarusi.

·         Kuvunja yai au kuchinja kwa ajili ya kununua gari jipya na kumwaga damu katika magurudumu.

 

Hayo yote ni baadhi tu za aina mbali mbali za shirk.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Amelaaniwa na Allaah atakayechinja kwa (ajili ya mwengine) asiyekuwa Allaah.))

 

Kutokana na haya nikaona ni bora nikamate kalamu na kuwatahadharisha ndugu zangu Waislamu kwa kadiri ya uwezo wangu ili wajiepushe na mambo haya ya shirk kwa njia ya  kuwadhihirishia uhusiano uliopo baina ya Majini,  Watabiri na Wachawi. Kwa sababu kuwaendea watu hawa ni kitendo cha shirk, na hapana kitendo kibaya Allaah Anachokichukia kuliko kitendo hicho.

 

Pia nimeona ni bora niwafafanulie ndugu zangu ili wakijue Kiungo Baina Ya Majini, Wachawi na Watabiri na jinsi gani watu hawa wanavyojikurubisha na shaytwaan kwa njia za kukufuru ili wapate kutumikiwa nao.

 

Allaah Anasema:

 

{{Hakika wao wametengeneza hila za mchawi tu, wala mchawi hafaulu (hafuzu) popote afikapo.}} [Suuratu-Twaaha: 69]

 

Wanafuata hayo, na kumwacha Allaah ambaye Anasema:

 

{{Je, Allaah hamkifi (hamtoshei) mja wake? Na wanakuogofisha (wanakuhofisha) na wale walio kinyume chake.}} [Suuratuz-Zumar: 36]

 

Kila asiyekuwa Allaah ni dhaifu. Hata hao watu wa Ahlil-Badri waliopigana vita vya Badar idadi yao wakiwa watu mia tatu na kidogo tu dhidi ya makafiri elfu na kuwashinda makafiri, basi Allaah anawataja kuwa ni madhaifu.

 

Allaah Anasema:

 

{{Na Allaah Alikunusuruni katika (vita vya) Badr, hali nyinyi mlikuwa dhaifu.}} [Suuratul-Aali-‘Imraan: 123]

Sasa kwa nini mtu anaacha kumtegemea Allaah Mwenye  nguvu na kuwategemea madhaifu? Kwa nini anaiacha haki na kufuata batili? Kuna nini baada ya kuiacha haki isipokuwa kufuata upotovu tu?

 

MwenyeziMungu Anasema:

 

{{Basi huyo ndiye Allaah, Mola wenu wa haki. Na ni nini kiko baada ya (kuacha) haki, isipokuwa upotofu (upotevu). Basi mnageuzwa wapi?}} [Suuratu-Yuunus: 32]

 

 

 

JINNI

 

JINA LAKE

 

Ameitwa JINNI kwa sababu ya kutokuonekana kwake na watu, na hii ni kwa sababu kila kisichoonekana kwa jicho la binadamu katika lugha ya Kiarabu jina lake hutokana (hutoholewa) na herufi mbili hizi; (Jiym) na (Nuun).

 

Kwa mfano; 'Bustani' huitwa 'janna' kwa sababu ya kuzungukwa kwake na majani kila upande pasiweze kuonekana ndani. Elimu ya uzazi huitwa 'Ilmul ajinna', kwa sababu ya kutokuonekana kwa kile kilichokuwemo tumboni mwa mzazi. Hata mwendawazimu naye huitwa 'majinun' kwa sababu ya kutoweka kwa akili yake. Na Majinni nao wamepewa jina hilo kwa sababu ya kutokuonekana kwao kwa macho ya binadamu.

 

Ukichunguza utaona kuwa maneno yote hayo; 'Janna, ajinna, majinun, jinni', yana herufi ya 'Jiym na Nuun' ndani yake.

 

 

‘IMAAN JUU YA GHAYB

 

Kuamini juu ya ghayb (yasiyoonekana) ni katika misingi ya itikadi ya Diyn.

 

Allaah Anasema:

 

{{ALIF LAAM MYM. Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake. Ni uwongozi kwa wamchao Allaah. Ambao huyaamini yasiyoonekana (maadam yamesemwa na Allaah na Mtume Wake) na husimamisha Swalah na hutoa katika yale Tuliyowapa.}} [Suuratul-Baqarah]

 

Katika aya hizi, Allaah Ametaja baadhi ya sifa za wacha Mungu ikiwemo sifa hii ya kuamini ghayb.

 

Na maana ya neno 'ghayb', ni yale tusiyoweza kuyaona lakini ametueleza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) au Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

USHAHIDI WA KUWEPO MAJINI KATIKA QUR-AAN TUKUFU

 

Katika Qur-aan Allaah Anasema:

 

{{Na (wakumbushe) tulipokuletea kundi la majini (kuja kwako) kusikiliza Qur-aan.}} [Suuratul-Ahqaaf: 29]

 

Na Akasema:

 

{{(Siku ya Kiama wataambiwa) “Enyi makundi ya majini na wanaadamu! Je, hawajakufikieni Mitume miongoni mwenu kukubainishieni Aya zangu?}} [Suuratul-An-aam: 130]

 

 

USHAHIDI WA KUWEPO KWA MAJINI KATIKA MAFUNDISHO YA MTUME (SWALLA ALLAAHU ‘ALAYHI WA AALIHI WA SALLAM) 'SUNNAH'

 

Katika 'Sunnah', (mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wameelezea Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim katika vitabu vyao vilivyo sahihi kwamba Ibni Abbas amesema:

 

((Majinni waliposhindwa kupata siri kutoka mbinguni na wakawa wanafukuzwa kwa vimondo kila wanapojaribu kuzisogelea mbingu, wakarudi makwao. Na jamii zao walipotaka kujua sababu ya kurudi kwao huko na kushindwa kwao kupata siri za mbinguni, maana kabla ya hapo walikuwa wakiweza kupata baadhi ya habari za huko, wakawajibu: "Pamewekewa vizuizi baina yetu na baina ya (kupata) habari za mbinguni". Wenziwao wakasema: "Bila shaka pana jambo kubwa lililotokea, tembeeni ardhi yote Mashariki na Magharibi mtafute ni kitu gani kilichokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni”.

 

Walipofika mahali paitwapo; “Soko la Akadha”, Waislamu walikuwa wakiswali Swalah ya Alfajiri, na majini hao wakaisikia Qur-aan ikisomwa, ndipo waliposema: "Hii (Qur-aan) WaLlaah, ndiyo iliyokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni".

 

Wakarudi kwa watu wao na kuwaambia: "Enyi jamii yetu! “Hakika sisi tumesikia Qur-aan ya ajabu" Allaah amesema katika Suuratul-Jinn aya ya mwanzo: {{Sema:“Imefunuliwa kwangu kuwa kundi moja la majini lilisikia (Qur-aan) likasema: “Hakika tumesikia Qur-aan ya ajabu.}} [SuuratulJinn: 1]))

 

Hizi ni dalili zilizo wazi za kuwepo kwa viumbe hawa, na kukanusha kuwepo kwao kwa sababu ya kutokuonekana kwao si hoja, maana vitu vingi hatuvioni na tunakubali kwamba vipo kutokana na athari zake. Kwa mfano, joto, baridi, umeme n.k. Hivi vyote hatuvioni lakini tunakubali kuwepo kwake baada ya kuona athari zake.

 

DALILI KATIKA QUR-AAN KUWA JINNI AMEUMBWA KWA MOTO

 

Ndani ya Qur-aan mna dalili nyingi zinazotujuulisha kuwa Jinni ameumbwa kwa moto, na tutazitaja baadhi ya dalili hizo:

 

Allaah Amesema:

 

{{Akasema (Ibilisi): Mimi ni bora kuliko yeye (Mimi) umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.}} [Suuratul-Aaraf: 12]

 

Na Akasema:

 

{{Na akawaumba Majinni kwa ulimi wa moto.}} [Suuratur-Rahmaan: 12]

 

 

DALILI KATIKA MAFUNDISHO YA MTUME (SWALLA ALLAAHU ‘ALAYHI WA AALIHI WA SALLAM) KUWA JINNI AMEUMBWA KWA MOTO

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametujuulisha pia kuwa Majinni wameumbwa kwa moto, na tutataja baadhi ya kauli zake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Wameumbwa Malaika kwa nuru na Majinni kwa ndimi za moto na Adam ameumbwa kwa mliyokwisha elezewa (Udongo).)) [Imepokewa na Muslim].

 

MAJINI WANAZALIANA

 

Allaah Anasema:

 

{{Je! Mnamfanya yeye na kizazi chake kuwa marafiki (zenu) badala yangu hali wao ni maadui zenu? Ni mbaya kabisa kwa madhalimu badala (hii).}} [Suuratul-Kahf: 50]

 

Kauli ya MwenyeziMungu katika aya hii pale aliposema 'na kizazi chake' inamaanisha kwamba majinni wanazaliana.

 

 

WAMEUMBWA KABLA YA BINADAMU

 

Allaah Amesema:

 

{{Na tulimuumba mwanadamu kwa udongo mkavu unaotoa sauti (unapogongwa), unaotokana na matope meusi yaliyovunda. Na majinni tuliwaumba kabla, kwa moto wa upepo wenye joto (kubwa kabisa).}} [Suuratul-Hijr: 26-27]

 

Kwa hivyo majini waliumbwa kabla yetu na waliishi katika ardhi hii hata kabla ya kuumbwa kwa Adam (‘Alayhis Salaam). Na hii ndiyo maana Allaah alipowaarifu Malaika kuwa anataka kuumba viumbe katika ardhi wakasema:

 

{{Utaweka watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu.}} [Suuratul-Baqarah: 30]

 

Malaika waliuliza suala hili si kwa ajili ya kupinga amri ya Allaah au kwa kumuonea wivu mwanadamu, bali waliuliza kwa ajili ya kutaka kuijua hikmah ya kuumbwa viumbe hawa, na hii ni kwa sababu walielewa kutokana na viumbe vilivyotangulia vilivyoishi ardhini, kwamba vina sifa ya ufisadi na umwagaji wa damu.

 

Anasema Ibni Kathiyr (huyu ni katika maulamaa na mfasiri mkubwa wa Qur-aan) kwamba kabla ya kuumbwa kwa wanadamu, Majinni na viumbe wasiokuwa wanadamu walikuwa wakiishi ardhini na kwamba walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa pamoja na umwagaji wa damu.

 

Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

((Majinni waliishi ardhini kabla ya wanaadamu na walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa na MwenyeziMungu akawaondoa na kuwaleta wanadamu.))

 

Maneno kama haya pia yalisemwa na Hassan Al-Basry (Rahimahu Allaah), na akaongeza kusema: ((Hii ndiyo maana Malaika wakamuuliza Mola wao suali hilo.))

 

 

 

UHUSIANO BAINA YA JINNI NA SHAYTWAAN

 

Shaytwaan na Jinni asili yao ni moja, hapana hitilafu baina ya maulamaa kuhusu jambo hili, isipokuwa wamekhitalafiana katika suala: “Je Ibilisi ndiye baba wa Majinni (asili yao)  mfano wa Adam  ambaye ni baba yetu na asili yetu ?)”.

 

Majibu:

 

Iblisi si asili yao, bali yeye ni miongoni mwao.

 

Allaah Anasema:

 

{{Basi wakamsujudia isipokuwa Iblisi, yeye alikuwa miongoni mwa majinni.}} [Suuratul-Kahf: 50]

 

Kwa vile Allaah amemtaja Iblisi kuwa ni ‘miongoni’ mwa majinni, kwa hivyo yeye ni mmoja wao na si asili yao kama mfano wa Adam (‘Alayhis Salaam) alivyokuwa asili ya wanadamu.

 

Tulisema kuwa wameitwa 'Majinni ' kwa sababu ya kutokuonekana kwao na sisi tumeitwa 'Insaan' kwa sababu ya kusahau kwetu, kwani neno 'Insaan', asili yake linatokana na neno 'Nisiyan', na maana yake ni kusahau.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Adam alisahau na vizazi vyake vikasahau.))

 

Ama neno 'Shaytwaan', katika lugha ya Kiarabu maana yake ni 'kila anayeasi na kupinga au kuzuwia au kushawishi viumbe wasiifuate njia ya Allaah', awe Jinni au Mwanadamu.

 

Allaah Anasema:

 

{{Na namna hii tumemfanyia kila Nabii maadui (nao ni) maShaytwaan katika watu na (maShaytwaan katika) majinni. Baadhi yao wanawafunulia wenziwao maneno ya kupambapamba ili kuwadanganya.}} [Suuratul-An-aam: 112]

 

 

IBLISI NI KATIKA MALAIKA?

 

Iblisi si katika Malaika, bali ni miongoni mwa Majinni kutokana na dalili zifuatazo:

 

Allaah Amesema:

 

{{Basi wakamsujudia isipokuwa Iblisi, yeye alikuwa miongoni mwa majini.}} [Suuratul-Kahf: 50]

 

Na Akasema:

 

{{Hawamuasi Allaah kwa amri zake, na wanatenda wanavyoamrishwa (yote).}} [Suuratut-Tahriym: 6]

 

Kutokana na aayah hii, tunapata ushahidi mwingine kuwa; Malaika hawamuasi Allaah. Kwa hivyo Iblisi angelikuwa Malaika, asingemuasi Mola wake bali angetenda kama alivyoamrishwa. Lakini yeye alitenda kinyume na hivyo. Alimuasi Allaah pale alipokataa kumsujudia baba yetu Adam (‘Alayhis Salaam), akasema:

 

{{Akasema (Iblisi): 'Mimi ni bora kuliko yeye (Mimi) umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.}} [Suuratul-Aaraf: 12]

 

Na hapa pia tunapata ushahidi mwingi pia kuwa Iblisi si miongoni mwa Malaika, kwani Malaika wameumbwa kwa Nuru na MaShaytwaan wameumbwa kwa moto.

 

Katika aayah iliyotangulia Iblisi alisema: 'Mimi ni bora kuliko yeye (Mimi) umeniumba kwa moto". Angelikuwa yeye ni miongoni mwa Malaika angelisema:  ‘Mimi ni bora kuliko yeye umeniumba kwa Nuru’. Kwa sababu Malaika wameumbwa kwa nuru kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyotangulia:

((Malaika wameumbwa kwa nuru na Majinni kwa ndimi za moto na Adam (ameumbwa) kwa mliyokwisha elezewa (Udongo).)) [Imepokewa na Muslim na Ahmad bin Hanbal].

 

 

AINA ZA MAJINI

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Majinni (wako) namna tatu; namna moja wana mabawa wanaruka na namna (nyengine) majoka na n’ge na namna nyengine hawaishi mahala pamoja na hupenda kuhama.)) [Imepokewa At-Twabaraniy na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaniy ambaye ni mmoja katika maulamaa wakubwa wa ‘ilmu ya tahakiki za Hadiyth.]

 

 

MAHALI  WANAPOISHI

 

Majini wanaishi katika majangwa na katika sehemu za kutupa taka, kwa sababu wao wanakula mabaki ya vyakula vya binadamu.

 

Zimepokelewa Hadiyth nyingi pia kwa njia ya Ibni Abbas na Ibni Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akienda jangwani na kuwasemesha Majinni na kuwalingania katika diyn ya Kiislamu na kuwataka wamuabudu Allaah mmoja wa kweli.

 

Majinni wanapenda pia kuishi vyooni, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha du’aa ya kusoma kabla ya mtu kuigia chooni; akasema: ((Mmoja wenu anapoingia chooni basi aseme: "ALlahumma inniy a’udhu bika minal khubuthi wal khabaaith".)) Na maana yake: “Allaah najikinga kwako kutokana na majinni wanaume na majinni wanawake.” [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Majini pia wanaishi katika mashimo:

 

Kutoka kwa Qataadah kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Mmoja wenu asikojowe ndani ya shimo.)) Na alipoulizwa kuna ubaya gani mtu kukojoa ndani ya shimo akasema: ((Inasemekana kuwa Majinni wanapenda kuishi humo.)) [Imepokewa na An-Nasaaiy]

 

                                                                                                              

WANAKULA NA KUNYWA

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Mmoja wenu anapokula, basi ale kwa (mkono wa) kulia na anapokunywa anywe kwa (mkono wa ) kulia, kwa sababu Shaytwaan anakula kwa kushoto na kunywa kwa kushoto.)) [Imepokwa na Muslim].

 

Na akasema:

 

((Mtu anapoingia nyumbani akasema: 'BismiLlah', na anapokula (akasema BismiLlah), Shaytwaan husema: 'Hatuna makaazi humu (ndani ya nyumba hii), na hatuna chakula cha usiku'. Ama anapoingia asiseme: 'Bismillah', Shaytwaan husema: 'Tumepata makaazi humu', na asiposema BismiLlaah pale anapokula, basi (Shaytwaan) husema: 'Tumepata makaazi na chakula’.)) [Imepokewa na Muslim]

 

 

WANA UWEZO WA KUJIGEUZA

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

((Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinipa jukumu la kulinda (chakula cha) Zakkah ya Ramadhaan, akaja mtu akawa anaiba katika chakula kile, nikamkamata na kumuambia kwamba nitampeleka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akasema: 'Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi na shida nyingi".

 

Anasema Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu):

 

"Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza: ((Ewe Abu Hurairah umefanya nini na mfungwa wako jana?))

 

"Akasema: "Nikamwambia: "Ewe Mtume wa Allaah, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha". Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ama huyu amekudanganya na atarudi)).

 

Nikajuwa kwamba atarudi kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema hivyo. Nikamtegea, akaja tena siku ya pili kuiba chakula, nikamkamata, nikamuambia nitakupeleka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akaniambia: “Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi sitorudia tena”. Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ewe Abu Hurairah umefanya nini na mfungwa wako jana?))

 

Nikamuambia: "Ewe Mtume wa Allaah, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha". Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ama huyu amekudanganya na atarudi)).

 

Nikamkamata mara ya tatu akiwa anaiba (tena) chakula, nikamuambia: "Nitakupeleka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hii ni mara ya tatu na kila mara unasema hutorudia kisha unarudia." Akasema: "Niache nikufundishe maneno Allaah atakufaa nayo". Nikamuuliza: “Maneno gani hayo?" Akasema: “Unapokuwa juu ya tandiko lako soma Aayatul-Kursy - Allahu laa ilaaha illa huwal hayyul qayuum - mpaka mwisho na itaendelea kukuhifadhi aya hii na hatokukaribia Shaytwaan mpaka utakapoamka”. Nikamuacha aende zake.

 

Asubuhi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza: ((Amefanyaje mfungwa wako jana?)) Nikamuambia: "Ewe Mtume wa Allaah amejidai eti amenifundisha maneno ambayo Allaah atanifaa nayo, basi nikamuacha huru". Akaniuliza: ((Ni maneno gani hayo?)) Nikasema: "Ameniambia: ‘Unapokuwa juu ya tandiko lako soma Aayatul-Kursiy mpaka mwisho na Allaah Ataendelea kukuhifadhi nayo na hatokukaribia Shaytwaan mpaka utakapoamka".

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ama yeye amesema kweli ingawaje ni muongo. Unamjua nani uliyekuwa ukizungumza naye siku tatu hizi ewe Aba Hurairah?)) Akajibu: "La simjuwi". Akasema: ((Yule ni Shaytwaan.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy].

 

Kwa vile Shaytwaan huyu aliyekuwa akiiba alikuwa akimjia Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa sura ya binadamu, basi hii ni dalili kwamba majini wana uwezo wa kujibadilisha umbile lao.

 

 

WAMO MIONGONI MWAO WANAWAKE NA WANAUME

 

Katika Hadiyth niliyoitaja hapo juu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

((Anapoingia mmoja wenu chooni, basi aseme: “MwenyeziMungu najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake”)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

WANAOA?

 

Majini wanaoana na kuzaliana, na ushahidi umo ndani Qur-aan katika kauli Yake Subhanahu wa Taala Aliposema:

 

{{Je! Mnamfanya yeye (Ibilisi) na kizazi chake kuwa marafiki (zenu) badala yangu hali wao ni maadui zenu? Ni mbaya kabisa kwa madhalimu badala (hii).}} [Suuratul-Kahf: 50]

 

Hata hivyo Maulamaa wengi hawakubali majini waowane na wanadamu. Pana kisa cha mwanamke mmoja kutoka Yemen alikuwa akidai kwamba anajiwa na jinni na kwamba jinni huyo anataka kumuowa. Alipoulizwa Imaam Maalik kuhusu jambo hili akasema:

 

((Sioni kifungu chochote cha shari’ah kinachoharamisha, isipokuwa nakuogopeeni fitnah (Mitihani).))

 

Maulamaa wamesema kuwa kauli ya Imaam Maalik hii inatujulisha juu ya hofu yake. Kwani mwanamke yeyote anaweza kujipatia mimba kwa njia zisizo za halali, kisha akasema kwamba ameolewa na jinni na kwa njia hii uhuni utazidi na fitnah zitaenea.

 

Maulamaa wengine wamekataa kabisa fikra ya kuoana baina ya majini na wanadamu wakiegemea kauli ya Allaah isemayo:

 

{{Na katika Ishara zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mupate utulivu kwao.}} [Suuratur-Ruum: 21]

 

Na Akasema:

 

{{Na Allaah Amekuumbieni wake katika jinsi yenu na Akakujaalieni kutoka kwa wake zenu watoto na wajukuu.}} [Suuratun-Nahl: 72]

 

Katika aayah hizi Allaah Anatufahamisha kwamba ametuumbia wake zetu katika jinsi yetu, wakati Majinni si katika Jinsi yetu.

 

Na Akasema: “Ili mupate utulivu kwao", wakati mwanadamu hawezi kupata utulivu kwa jinni, maana siku zote mtu hupata utulivu kwa kiumbe aliye mfano wake na majini si mfano wetu.

 

 

MAJINI WANAKUFA?

 

Allaah Anasema:

 

{{Kila kilichopo juu yake (ardhi na mbingu) kitatoweka (kitaondoka).}} [Suuratur-Rahmaan: 26]

 

Na Akasema:

 

{{Hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye; kila kitu kitakufa isipokuwa Yeye (MwenyeziMungu basi).}} [Suuratul-Qasas: 88]

 

Inavyojulikana ni kwamba Iblisi yuhai mpaka siku ya Qiyaamah. Allaah Amesema:

 

{{Akasema (Iblisi): “Mola wangu! basi nipe nafasi (nisife) mpaka siku watakayofufuliwa (viumbe) vyote. Akasema (Allaah): “Hakika wewe (nimekwisha kukufanya) katika wale waliopewa nafasi”. “Mpaka siku ya wakati uliowekwa (ukifika wakati huo utakufa)”.}} [Suuratul-Hijr: 36-38]

 

Kwa hivyo Ibilisi ataishi mpaka siku maalum anayoijua Allaah peke yake kisha atakufa, na majini nao pia wanazaliana na watakufa kama sisi.

 

 

WAMO MIONGONI MWAO WAISLAMU NA MAKAFIRI

 

Allaah Amesema:

 

{{Nasi wamo miongoni mwetu waliosilimu na wamo miongoni mwetu wanaokengeuka. Waliosilimu hao ndio waliotafuta uwongofu.}} [Suuratul-Jinn: 14]

 

{{Na hakika katika sisi wamo walio wema na wengine katika sisi ni kinyume cha hayo, tumekuwa njia mbali mbali.}}  [Suuratul-Jinn: 11]

 

Katika kuifasiri aayah hii, anasema Ibni Abbas (Radhiya Allaahu ‘anhu):

 

((Kauli ya Allaah: “Tumekuwa njia mbali mbali”, maana yake ni “Makafiri na Waislamu”.))

 

Baadhi ya maulamaa wanasema:

 

((Diyn mbali mbali na madhehebu mbali mbali.))

 

 

WAISLAMU KATIKA MAJINI WATAINGIA PEPONI ?

 

Katika tafsiri yake Ibni Kathyir amesema:

 

((Waislamu miongoni mwa Majini wataingia Peponi kama Waislamu katika wanadamu.))

 

Na dalili yake pamoja na dalili za maulamaa wengine ni kauli ya Allaah akitujuulisha juu ya hali ya wanawake wa Peponi aliposema:

 

{{Hajawagusa binadamu yoyote kabla yao (hao waume zao) wala jinni.}} [Suuratur-Rahmaan: 74]

 

Na Aliposema:

 

{{Na Mwenye kuogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake atapata mabustani (Pepo) mawili. Basi ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha (kuwa si neema yake)?.}} [Suuratur-Rahmaan: 46-47]

 

MwenyeziMungu Amejaalia jazaa ya majini na binadamu wema kuwa ni Pepo, na majini waliijibu aayah hii kwa kumshukuru Allaah  wakasema:

 

((Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako.))

 

Hii ni Hadiyth iliyosimuliwa na Imaam Attirmidhiy kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba amesema:

 

((Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliisoma Suutratur-Rahmaan mpaka mwisho kisha akasema: ‘Mbona mumenyamaza kimya, Majini wamekuwa bora kuliko nyinyi kwa kujibu kila ninapowasomea aayah hii:  "Basi ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha (kuwa si neema yake)?" Wao huijibu kwa kusema: "Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako".)) [Imesimuliwa na Attirmidhiy na Al-Bazaar na Al-Haakim na pia Ibni Jariyr na Shaykh Al-Albaaniy amesema kwamba Hadiyth hii ni njema.]

 

Dalili inayopatikana kutoka katika aayah hizi ni kwamba; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwapa Majini mafundisho ya Diyn, na kuwafahamisha kwamba pana jaza ya Pepo kwa Mwenye kuogopa.

 

Kama Majini hawatoingia Peponi hapangekuwa na haja ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwatokea na kuwapa mafunzo ya Diyn na kuwajuulisha juu ya Pepo inayowangoja wale wanaomuogopa Allaah.

 

 

MAJINI WANAWAOGOPA WANADAMU

 

Ameeleze Ibn Abi Ad-Dunya kwamba Mujaahid amesema:

 

((Usiku mmoja nilikuwa nikiswali akanitokea mfano wa mtoto mdogo mbele yangu nikamshika kwa nguvu zangu zote akainuka na kuuruka ukuta hata nilisikia kishindo cha kuanguka kwake.))

 

Akaendela kusema: ((Wao (majini) wanakuogopeni kama nyinyi mnavyowaogopa.))

 

Imepokewa kutoka kwa Mujaahid kuwa alisema:

 

((Shaytwaan anakuogopeni kuliko nyinyi mnavyomuogopa akikukaribia usimregezee akakupanda, bali shindana naye na hatimae ataondoka.))

 

 

KUWEZA KWA MAJINI KUSIKIA HABARI ZA MBINGUNI

 

Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba alisema:

 

((Amenihadithia mmoja katika Maswahaabah wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa; usiku mmoja walipokuwa wamekaa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nyota moja ikaanguka na kun’gara. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza: ((Mlikuwa mkisemaje wakati wa ujahilia (kabla ya kuja Uislamu?)) Wakajibu: ((Tulikuwa tukisema: Usiku wa leo amezaliwa mtu mtukufu na amekufa mtu mtukufu.)) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: ((Bali haiangushwi nyota kwa ajili ya kifo cha mtu wala kwa kuzaliwa kwa mtu, lakini Mola wetu aliyetukuka anapotoa amri, Malaika wabebao ‘Arsh husabbih (husema Subhana Llaah), na viumbe vya mbinguni vyote humsabbih Allaah pia. Kisha husabbih viumbe wa mbingu za chini mpaka habari inapofika katika mbingu ya dunia. Majini huzipata habari hizo na huwatupia mabwana zao nazo ni habari za kweli, lakini wao huongeza habari za uongo juu yake.))

 

Kutokana na Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), amesema:

 

((Niliuliza: "Ewe Mtume wa Allaah, makuhani walikuwa wakituelezea baadhi ya mambo na yalikuwa ni ya kweli." Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hiyo ni habari ya kweli ameipokea jini akamtupia bwana wake  na kuongezea uongo mara mia.)) [Imetolewa na Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim na Ahmad na Al-Bayhaqiy]

 

 

UCHAWI

 

 

NINI MAANA YA UCHAWI?

 

Ibn Mandhwuur ambaye ni mtungaji wa kamusi maarafu ya Kiarabu iitwayo “Lisaanul-‘Arabiy” amesema:

 

“Neno “Uchawi”, kwa Kiarabu “As-Sihru”, maana yake ni kitendo cha kujikurubisha na Shaytwaan na kwa msaada wake (Shaytwaan)”, na akasema pia kuwa: “Uchawi ni kulibadilisha jambo mbali na uhakika wake, nako ni kuwadhihirishia watu jambo lisilo la kweli wakaliona kuwa ni la kweli”.

 

Ama Swahaabah Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

((Uchawi ni kuidhirisha batili katika sura ya haki.))

 

Hayo ni katika kamusi za lugha. Amma katika kamusi ya Diyn, maana ya neno ‘uchawi’ (Aa-Sihru), kama alivyofasiri Mwanachuoni mkubwa Fakhruddin Ar-Razi kuwa:

 

"Ni kila jambo lililofichika sababu zake, linalotokeza kwa sababu zisizo za kawaida na ndani yake mna hadaa (khidaa)".

 

Amma Shaykh Wahiyd ‘Abdus-Salaam Baaliy, mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho 'As-Swaarim Al-Bataar Fiy Muhaarabat As-Saharatil Ashraar', na kitabu kiitwacho ‘Al Wiqaayah Minal Jinni Wa Shaytwaan’. Ambaye pia ni mtaalamu maarufu katika ‘ilmu ya majini na maShaytwaan na uchawi na ambaye pia ni katika maulamaa maarufu wanaotoa majini kwa njia ya kusoma Qur-aan, yeye anasema:

 

"Uchawi ni makubaliano baina ya mchawi na Jinni akishurutishwa mchawi kufanya mambo ya haramu au ya shirki, na baada ya kufanya hayo, Jinni anashurutishwa kumsaidia na kumtii mchawi huyo kila anachotaka".

 

Baadhi ya yale ambayo mchawi anatakiwa na Shaytwaan ayatende ili ajikurubishe naye ni:

 

 

·      Mchawi anatakiwa auvae msahafu miguuni na aingie nao chooni

·      Aandike baadhi ya aya za Qur-aan kwa damu ya hedhi

·      Miongoni mwao wanashurutishwa kuandika aya za Qur-aan penye nyayo za miguu

·      Au aiandike Suuratul-Faatihah kinyume nyume

·      Awsali bila ya Wudhuu

·      Wengine hutakiwa kuchinja mnyama bila ya kulitaja jina la Allaah kisha amtupe mnyama huyo mahali maalum anapoamrishwa na Shaytwaan

·      Wamo miongoni mwao wanaozungumza na nyota au kuzisujudia

·      Au hutakiwa kuandika herizi kwa maneno yenye kufru ndani yake

 

Imeelezwa kwamba katika nchi ya Sham kulikuwa na mtu ambaye watu walikuwa wakimpenda na kumheshimu sana wakimdhania kuwa ni mtu mwenye makarama. Mtu huyu alikuwa kila mwaka katika msimu wa Hajji akiwatumikia watu wa mji wake kwa kuchukua barua zao na vitu vyao na kuwapelekea watu wao waliokwenda Saudia kuhijji.

 

Alikuwa akipeleka na kurudi kwa muda wa siku moja au mbili tu, na watu walimpenda sana na kuamini kwamba alikuwa ni Waliy. Siku moja mtu huyo aliumwa sana, akamuita mwanawe na kumwambia kuwa kama atakufa, basi aende mahali fulani wakati wa usiku na atamkuta ngamia wa aina fulani na ampande na kufuata amri zote atakazopewa na ngamia huyo.

 

Alipofariki dunia, mwanawe alifanya kama alivyoambiwa na baba yake, akaondoka peke yake wakati wa usiku na kuelekea jangwani kule alikoambiwa na baba yake kuwa atamkuta ngamia. Akamkuta ngamia kama alivyoambiwa, akampanda na alipokuwa anaenda, ngamia akaanza kusema na kumtaka kijana yule ashuke na amsujudie.

 

Yule kijana alishtuka sana kusikia ngamia akisema na pia akashangazwa na amri zake, akamwambia: "Vipi nikusujudie, kweni wewe ni nani?" Ngamia akajibu: "Ikiwa unataka nifuate amri zako kama nilivyokuwa kwa baba yako, na nikupeleke popote utakapo duniani, basi unisujudie kama alivyokuwa akinisujudia baba yako."

 

Yule kijana akajibu: "Mimi ninamsujudia Allaah peke yake, amma wewe la, siwezi kukusujudia". Yule ngamia akamrusha kijana yule kutoka juu ya mgongo wake na kumwangusha chini, na kijana yule akatoka mbio mpaka nyumbani kwa mama yake na kumuelezea yote aliyoyaona na kwamba baba yake alikuwa akimsujudia Jinni ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kusafiri kila anapotaka kwenda kwa kupaishwa na jinni yule.

 

Kwa haya inatubainikia kuwa Jinni hamsaidii wala hamhudumii mchawi wala mtu yeyote isipokuwa naye kwa mkabala wake anatumikiwa kwa kutendewa matendo ya kufru, na Maulamaa wanasema kuwa:

 

"Kila mchawi anapokufuru zaidi, basi Shaytwaan humtumikia kwa nguvu zaidi, na mchawi akitaka apate huduma ya hali ya juu kabisa kutoka kwa masultani wa majinni au kwa Kiarabu wanaitwa "Maradatul-Jinni", basi inambidi afanye kufuru kubwa zaidi. Kwa ajili hiyo, mchawi anapotaka nguvu juu ya wenzake inamlazimikia akufuru zaidi".

Kutokana na haya tunafahamu kwamba mchawi na Shaytwaan ni marafiki na washirika katika kumuasi Allaah.

 

Allaah Anasema:

 

{{Na (wakumbushe) siku atakapowakusanya wote (akawaambia): "Enyi makundi ya majinni! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu". Na marafiki wao katika wanaadamu (watagombania) waseme:  "Mola wetu! Tulinufaishana sisi na wao na tumefikia muda wetu uliotuwekea". Basi (Mungu) Atasema: "Moto ndio makazi yenu, mtakaa humo milele", ila apende MwenyeziMungu (kuwarehemu), hakika Mola wako ndiye Mwenye hikima (na) ndiye ajuaye.}} [Suuratul-An’ Aaam: 128]

 

 

VIPI UTAWEZA KUMJUA MCHAWI?

 

Zifuatazo ni dalili zitazokuwezesha kutofautisha baina ya mganga na mchawi. Utakapoona mojawapo ya dalili zufuatazo utambuwe kuwa huyo ni mchawi bila shaka yeyote na wala si Shaykh au mganga (daktari).

 

Dalili hizo ni:

 

 

·         Mchawi huuliza jina la mgonjwa na jina la mamake

·         Huchukua baadhi ya vitu vya mgonjwa kama vile nguo za nje au za ndani au kitambaa cha kufutia jasho n.k.

·         Hutaka mnyama mwenye sifa maalum au rangi maalum ili achinjwe na hapigiwi BismiLlaah anapochinjwa

·         Huandika hirizi

·         Husema maneno yasiyojulikana

·         Humtaka mgonjwa aepukane na watu muda maalum na akae katika chumba kisichofikiwa na jua

·         Mara nyengine humtaka mgonjwa asiguse maji muda wa siku arubaini hivi (anasema Shaykh Wahiyd Abdus-Salaam Bali kwamba akikutaka ufanye hivyo ujue kwamba Jinni anayemtumikia mchawi huyo ni mkiristo)

·         Humpa mgonjwa vitu ili avifukie ardhini

·         Humpa mgonjwa karatasi aziunguze kisha ajifukize na moshi wake

·         Mara nyengine humwambia mgonjwa jina lake na mji anaoishi

·         Huandika maneno katika karatasi na kumwambia mgonjwa azichemshe na kunywa maji yake

UKIONA DALILI HIZI KWA MGANGA UMJUE HAPO HAPO KUWA NI MCHAWI NA UEPUKANE NAYE

 

Anasema Shaykh Wahiyd ‘Abdus-Salaam Baliy:

 

"Ukiutizama uso wa mchawi utakiona kiza cha kufru kilivyotanda katika uso huo mfano wa mawingu meusi”.

 

Anaendelea kusema Shaykh huyo:

 

“Kwa wale wanaowajua wachawi, wanawaona siku zote wakiwa katika dhiki, shida, matatizo katika siha zao, matatizo na wake zao au watoto wao na siku zote hawana raha wala utulivu”.

 

Allaah Anasema:

 

{{Na hakika kulikuwa na wanaume miongoni mwa wanaadamu wakijikinga kwa wanaume miongoni mwa majini kwa hivyo wakawazidishia taklifu (taabu).}} [Suuratul-Jinn: 6]

 

Na Anasema:

 

{{Na atakayejiepusha na mawaidha yangu basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki.}} [Suuratut-Twaaha: 124]

 

 

DALILI KUWA UCHAWI UPO,  KUTOKA KATIKA QURANI NA KATIKA SUNNAH - MAFUNDISHO YA MTUME (SWALLA ALLAAHU ‘ALAYHI WA AALIHI WA SALLAM)

 

Katika Suurat-Yuunus aayah ya 77 Allaah Anasema:

 

{{Akasema Muusa: "Mnasema (hivi) juu ya haki ilipokujieni, (kuwa) Huu ni uchawi? (Mbona umefaulu basi) Na wachawi hawafaulu".}}

 

Hii ni dalili kwamba uchawi upo na Allaah anatufundisha katika aayah hii kwamba uchawi haufaulu.

 

Na katika Suuratul-Falaq Akasema:

 

{{Na (najikinga na) shari ya wale wanaopuliza mafundoni.}}

 

Katika kuifasiri aayah hii, mmoja katika maulamaa wakubwa wa tafsiri ya Qur-aan Imaam Al-Qurtubiy amesema:

 

"Maana ya neno "Naffaathaat", ni wachawi wanapopuliza katika nyuzi huku wakizipiga fundo.

 

Na Ibni Kathiyr katika tafsiri yake akinukuu kutoka kwa Ikrimah na Mujaahid na Al-Hassan Al-Basry (Rahimahuma Allaah) amesema:

 

"Hawa wanaopuliza mafundoni ni wachawi, na Allaah anatuamrisha tujiepushe na shari zao.

 

Amma Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinazotufahamisha kwamba uchawi upo na kwamba uchawi ni katika madhambi makubwa sana, ni hizi zifuatazo:

 

Kutoka kwa Abi Huraira (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Jieupusheni na (mambo) saba yaangamizayo. Wakasema: 'Ni yepi hayo ewe Mjumbe wa Allaah?" Akasema: "Kumshirikisha Allaah, Uchawi, kuiuwa nafsi iliyoharimishwa na Allaah ila kwa haki yake, kula riba, kula mali ya yatima, kurudi nyuma (kukimbia) katika vita vya Jihaad (huku ukiwaacha wenzio wanapigana), na kuwasingizia uwongo wanawake wema wasio na makosa".)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ndugu yangu Muislamu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema kuwa mambo hayo 'yanayomuangamiza', maana yake ni kuwa yanamuangamiza mtu katika moto wa Jahannam.

 

Ukirudia kuisoma tena Hadiyth hiyo utaona kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameutanguliza uchawi kabla ya dhambi ya kuuwa, ingawaje kuuwa ni dhambi kubwa sana, na Allaah Anasema katika Suuratun-Nnisaa aayah ya 93:

 

{{Atakayemuuwa Muislamu kusudi, basi jazaa yake ni Jahannam atakuwa humo milele na Allaah Ataghadhibika naye na Atamlaani na amemtayarishia adhabu kubwa.}}

 

Juu ya ukubwa wa dhambi hiyo ya kuuwa, lakini Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameipa uzito zaidi dhambi ya uchawi kwa kuiweka nafasi ya pili baada ya shirki na kabla ya dhambi ya kuuwa.

 

 

 

SOMA BAHATI YAKO (NYOTA YAKO) LUCKY STARS

 

Katika Hadiyth ifuatayo iliyosimuliwa na Abu Dawuud na Ibni Maajah, Hadiyth ambayo Shaykh Al-Albaaniy ameitaja kuwa ni "Hadiyth njema", na Hadiyth hii pia ni dalili kwamba ‘ilmu ya kutabiri kwa nyota ambayo huandikwa katika magazeti na watu hupenda kusoma kwa kutaka kujua bahati zao, kitendo hiki ni haramu na yeyote atakayesoma nyota yake, basi Swalah zake hazikubaliwi kwa muda wa siku arobaini. Hii ikiwa anasoma na huku haziamini, amma akisoma na huku anaziamini, basi anaingia katika hukumu ya aliyemuendea mtabiri na kumuuliza jambo, na anakuwa amekwisha kufuru yote yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Atakayejifunza sehemu ya ‘ilmu ya nyota (utabiri) amejifunza sehemu ya uchawi, akiongeza atakachoongeza (katika uchawi au nyota).))

 

Na hii ni kwa sababu wanaosoma ‘ilmu ya nyota (utabiri) wanaamini kwamba katika nyota wanaishi majini ambao ni masultani na wakuu, na wanaitakidi kuwa mambo yetu yote husababishwa na harakati za nyota hizo kila zinapotaharaki kutoka mahali kuelekea pengine. Kwa ajili hiyo wao huzingoja nyota hizo masaa mengi ya usiku ili wapate kuandika talasimu zao, na huku ni sawa na kuziabudu nyota hizo.

(Pana tofauti baina ya ‘ilmu ya anga za juu (Astronomy) ambayo haina ubaya wowote ndani yake, na ‘ilmu ya nyota (Astrology) - utabiri - ambayo ni haramu).

 

Ushahidi mwengine unapatikana katika Hadiyth iliyosimuliwa na ‘Umraan bin Hussaiyn (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Hayuko pamoja nasi mwenye kuamini juu ya nukhsi (ukorofi) [Waarabu walikuwa wanapotaka kusafiri humrusha ndege na akielekea upande wa kulia basi husafiri, amma akielekea upande wa kushoto huamini ni ukorofi na kuivunja safari yake], na pia hayuko pamoja nasi mwenye kupiga ramli au mwenye kupigiwa, na atakayemuendea mtabiri na akamsadiki asemayo basi kesha kufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).)) [Imepokewa na Al-Bazaar]

 

Katika Hadiyth hizi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatukataza tusiwaendee wachawi wala watabiri wa aina yoyote ile kwa kuwauliza juu ya jambo lolote lile, hata kama atajibadilisha na kujiita Al-Hajj Fulani au Shaykh Fulani au Maalim Fulani au Mganga Fulani na hii ni kutokana na kufru zao wanazozifanya kwa kuwasujudia majini na kuridhishana nao ili wawatumikie.

 

Na hii ni dalili kwamba uchawi upo, maana kama haupo, basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asingetukataza kufanya kisichokuwepo.

 

Pia Hadiyth hizi zinatufahamisha kwamba mambo haya ni haramu na atakayeyatenda anakuwa amekwishayakanusha yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kwamba hapana aijuwae ghaibu isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Hadiythi ziko nyingi sana, lakini hizi pamoja na aya zilizotangulia zinatosha kuwa ni dalili kwamba yote hayo yametajwa katika Qur-aan na katika mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

UCHAWI UMEANZA ZAMA ZA NABII SULEIMAN ('ALAYHIS SALAAM)?

 

Wachawi wanaposoma talasimu zao huwadanganya watu kwa kuanza kusoma baadhi ya aayah au sura ndogo ndogo za Qur-aan na kulitajataja jina la Nabii Sulaymaan na utawasikia daima wanamnasibisha Mtume huyu (‘Alayhis Salaam) na kufru zao hizo ili wajinga wanaowafuata wadhani kwamba hayo yamo katika diyn.

 

Uchawi haujaanza zama za Nabii Sulaymaan kama wachawi wanavyozuwa na kumsingizia Nabii huyu wa Allaah. Bali ulikuwepo kabla yake kwa miaka elfu nyingi.

 

Uchawi ulikuwepo tokea zama za Nabii Swaalih (‘Alayhis Salaam) aliyekuja kabla ya Nabii Sulaymaan kwa miaka elfu nyingi.

 

Allaah Anasema:

 

{{Wakasema: (kumuambia Nabii Swaalih): "Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa".}} [Suuratush-Shu’araa: 153]

 

 

UCHAWI NI KUFRU

 

Wachawi na wafuasi wao hupenda kumsingizia Nabii Sulaymaan kwa kuinasibisha na kufru yao hiyo na Mtume huyu mtukufu ambaye Allaah Alimpa ufalme ambao hajaupata mwengine baada yake, kwa sababu alimpa uwezo wa kuwatiisha majini, upepo, na alipewa uwezo wa kujua lugha za wanyama n.k.

 

Allaah Anasema:

 

{{Basi tukamtiishia upepo unaokwenda pole pole kwa amri yake, anakotaka kufika (unamfikisha). Pia tukamtiishia maShaytwaan, kila ajengaye na azamiaye (lulu). Na wengine wafungwao minyororoni (wanapokhalifu amri zake).}} [Suuratus-Sa’d: 36-38]

 

Katika tasfiri yake, Ibni Kathiyr amenukuu kauli ya Ibni Abbas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

 

"Asif - alikuwa mwandishi wa Nabii Sulaymaan na alikuwa akilijuwa jina tukufu la Allaah (Al-Ismul-a’adham), na alikuwa akiandika kila kitu katika daftari kwa amri ya Nabii Sulaymaan na kulificha daftari hilo chini ya kiti cha Nabii Sulaymaan. Alipofariki Nabii Sulaymaan, majini wakayatoa maandishi hayo wakachanganya na kuandika baina ya kila mistari miwili uchawi na kufru yao, kisha wakawaambia watu wao kuwa hayo ndiyo maandishi ya Nabii Sulaymaan na ndiyo aliyokuwa akiyatenda, na Mayahudi wakayasadiki maneno hayo, wakawa wanamtangazia Nabii huyu kuwa ni mchawi.“

 

Mpaka alipokuja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuteremshiwa aayah ya 102 katika Suuratul Baqarah:

 

MwenyeziMungu Anasema:

 

{{Wakafuata yale waliyoyafuata mashaytwaan (wakadai kuwa yalikuwa) katika ufalme wa (Nabii) Sulaymaan; na Sulaymaan hakukufuru (kwa sababu uchawi ni kufru) bali mashaytwaan ndio waliokufuru wakiwafundisha watu uchawi (waliokuwa wakiujua wenyewe tangu zamani) na (uchawi) ulioteremshwa kwa Malaika wawili Haruta na Maruta katika (mji wa) Babil (Babylon). Wala (Malaika hao) hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie "Hakika sisi ni mtihani (wa kutazamwa kutii kwenu); basi usikufuru." Wakajifunza kwao ambayo kwa mambo hayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe (na mengineyo). Wala hawakuwa wenye kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya Allaah. Na wanajifunza ambayo yatawadhuru wala hayatawafaa. Na kwa yakini wanajua kwamba aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera. Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia (starehe za) nafsi zao (za Akhera). Laiti wangalijua, (hakika wasingefanya hivi)".}}

 

Anasema Shaykh ‘AbduLlaah Swaalih Al-Faarsiy katika tafsiri yake kwamba aayah hii inaonesha wazi kuwa:

 

 

a.     Uchawi ni amali ya ukafiri

b.     Mchawi hawezi kumdhuru mtu ila kwa idhini ya Allaah

c.      Mchawi mwenyewe anadhurika kwa uchawi wake

 

Katika aya hii Allaah anatufahamisha pia kuwa uchawi ulikuwepo kabla ya Nabii Sulaymaan kwa miaka mingi. Tokea zama za ustaarabu wa Babiloni walipoteremshwa Malaika wawili, Haruta na Maruta ili kuwaonyesha watu na kuwafahamisha nini uchawi, wapate kuujuwa mara watakapouona na wasiufuate, na hii ni kwa sababu uchawi ni kufru.

 

Watu waliacha kufuata nasaha za Malaika hao na wakajifunza yale ambayo yatawadhuru na wala hayatawafaa, ingawaje walikuwa wakijuwa kuwa aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera. Wachawi mpaka hivi sasa wanajaribu kuunasibisha uchawi wao na Nabii Sulaymaan pamoja na Malaika hawa wawili.

 

Tatizo kubwa hupatikana pale wachawi wanapofanya uganga wao pale wanaposema maneno yao ya kichawi. Wao huchanganya maneno hayo na baadhi ya aayah za Qur-aan na wanaofanyiwa uganga hudhania kwamba Qur-aan ndiyo inayosomwa na kwa ajili hiyo na kutokana na ujinga wao, huhadaika na kujiingiza nao katika shirki.

 

 

HUKUMU YA UCHAWI KATIKA DIYN YA KIISLAMU

 

Anasema Imaam Maalik (Rahimahu Llaah) katika kitabu chake Al-Muwattaa kwamba:

 

((Mchawi anayefanya uchawi mwenyewe, hukumu yake ni kuuwawa, ama yule anayemuendea mchawi, huyo hauwawi.))

 

Ibni Qudaamah naye anasema: "Hukumu ya mchawi ni kuuawa."

 

Hukmu kama hizi pia zimepokelewa kutoka Maswahaabah mbali mbali kama vile ‘Umar, ‘Uthmaan, Ibni ‘Umar na wengineo (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Hukmu hii ya kuuwawa kwa mchawi pia ameitamka Imaam Ahmad bin Hambal (Rahimahu Llaah).

 

Na imepokelewa kutoka kwa Maswahaabah mbali mbali kwamba ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwaandikia Maswahaabah kuwaamrisha wamuuwe kila mchawi mwanamke au mwanamume.

 

Anasema mmoja katika Maswahaabah kwamba baada ya kupata maandishi hayo waliwakamata na kuwaua wachawi watatu.

 

Amma Imaam Shaafi’iy (Rahimahu Llaah), yeye anaona kuwa mchawi asiuliwe isipokuwa akikiri mwenyewe kwamba ameuwa kwa uchawi wake.

 

Kutokana na yaliyotangulia infahamika kwamba Maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum) pamoja na maulamaa wengi wanaona kwamba hukumu ya mchawi ni kuuliwa. Isipokuwa Imaam Shaafi’iy (Rahimahu Llaah), yeye anaona kuwa auliwe tu ikiwa mchawi huyo atakiri kwamba ameuwa kwa uchawi wake.

 

 

KUJIKINGA NA SHARI ZA WACHAWI NA MAJINI WAO

 

Zifuatazo ni baadhi ya njia za kujikinga na waovu hao:

 

KUSAFISHA NIYAH

 

Iblisi alipohukumiwa kupotea kwa sababu ya kuasi kwake, aliahidi kuwapoteza viumbe wote isipokuwa wale waliosafika kikweli.

 

Iblisi akasema kumwambia Allaah: "Isipokuwa wale waja wako waliosafika kweli kweli".

 

Kusafisha nia (Al-Ikhlaasw), maana yake ni kuzihusisha ‘Ibaadah zote kwa moyo wote kwa ajili ya Allaah peke yake. Sio kujionesha mbele za watu kuwa ni Mcha Mungu na unapokuwa peke yako unamuasi.

 

Al-Junaid, mmoja katika maulamaa wakubwa wa wakati wake amesema:

 

"Allaah ana waja wake wenye akili, walipopata akili wakaifanyia kazi, walipofanya kazi wakaitakasa kazi hiyo na kule kuitakasa kwao kukawaingiza katika milango ya kheri yote".

 

KUTIA WUDHUU:

 

Katika Hadiyth nyingi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha juu ya umuhimu wa kubaki na Wudhuu kila mtu anapoweza kwa ajili ya kupata thawabu na kwa ajili ya kujikinga na kila shari.

 

SWALAH KATIKA JAMA’AH:

 

Kuswali Swalah za jamaa msikitini, maana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kwamba mbwa mwitu (Shaytwaan) huwala kondoo wanaotembea mbali na wenzao.

 

SWALAH ZA SUNNAH:

 

Swalah za Sunnah uzisali nyumbani, usiiache nyumba yako ikawa kama kaburi, na unaposali nyumbani Shaytwaan hulia na kutoka nje ya nyumba yako huku akisema: "Sina pa kulala humu, wala sina pa kula humu".

 

KUMUOMBA ALLAAH:

 

Kumuomba Allaah kila mara Shaytwaan anapotaka kukuchezea na kila unapoingia mahali pachafu.

 

Kwa mfano:

 

Unapoingia chooni uisome dua hii: "Allahumma inniy a’udhu bika minal khubuthi wal khabaaith”. Na maana yake: (Allaah mimi najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake).

 

Kabla ya kulala usome Suuratul-Ikhlaasw, Suuratul-Falaq na Suuratun Naas pamoja na Aayatul-Kursiy. Maana Hadiyth sahihi tuliyoitaja mwanzo wa darsi hii inasema kuwa anayeisoma aayah hii, Allaah Anaendelea kumhifadhi mpaka asubuhi anapoamka.

 

Ni vizuri pia kuzisoma aayah tano za mwanzo za Suuratul-Baqarah kisha Aayatul-Kursiy. Kisha kuzisoma aayah tatu za mwisho za Suuratul-Baqarah na Allaah atakulinda na majini pamoja na uchawi katika siku nzima.

 

Kuzisoma dua mbali mbali kama vile:

 

A’uwdhu bikalimaati Llaahi ttaammaati min kulli shaytwaani wa haammah wa min kulli ‘aynin laammah”. Na maana yake ni: "Najikinga kwa Allaah kutokana na kila Shaytwaan na (kila) mdudu anayesota (kama vile nge na nyoka n.k. na kwa kila jicho linalodhuru).

 

Bismillahi lladhiy laa yadhuru ma-‘a smihiy shay un fil ardhi walaa fiy ssamaa wahuwa ssamiy’ul ‘aliym”.

 

Unapotoka nje ya nyumba usome: “BismiLlaah tawakkaltu ‘ala Llaah walaa haula walaa quwwata illa biLlaah.”

 

KUSOMA QUR-AAN

 

Qur-aan ni kinga kubwa sana, na Muislamu anatakiwa daima awe anaisoma nyumbani kwake. Hapana kitukufu anachokiogopa Shaytwaan kuliko Qur-aan, du’aa, pamoja na ‘Ibaadah zinazokusogeza karibu na Mola wako. Na kila mtu anapokuwa mbali na Mola wake katika kumuasi, basi atambuwe kuwa anajiweka mbali na Mola wake na kwa ajili hiyo anampa Shaytwaan fursa ya kumsogelea na kumtawala.

 

Kwa kupiga mfano: Mtu anapita njiani akakumbana na mbwa mkali anayebweka huku akiwa amemzuwilia njia. Bila shaka mtu huyo atashindwa na hila ya kumuondosha ili apite na zake; bali ataogopa asitafunwe na mbwa huyo. Lakini mtu huyo mara atakapotambua kuwa mwenye mbwa huyo yupo karibu, na kwamba akimuomba amwondoe njiani basi kwa ukelele wake mmoja tu, mbwa huyo ataondoka taratibu na kumpisha apite, bila shaka atamuomba msaada wake.

 

Mfano huu ni mfano wako wewe binadamu unapomuomba Mola wako akukinge na mashaytwaan.

 

 

DU’AA ZINAMKUMBA SHAYTWAAN

 

Kama vile Shaytwaan anavyoweza kuwakumba wanadamu walioghafilika na kumdhukuru Allaah, Shaytwaan naye pia hukumbwa na du’aa za wanaomdhukuru MwenyeziMungu:

 

Imeelezwa na maulamaa kuwa, Shaytwaan anapojaribu kumsogelea Mcha Mungu mwenye kumdhukuru Mola wake kila wakati kwa ajili ya kumkumbuka, basi du’aa zake humkumba Shaytwaan huyo na kumuangusha chini. Kisha mashaytwaan wenzake hukusanyika na kuulizana: "Amepatwa na nini huyu?" Wenzao huwajibu: "Amekumbwa na binadamu".

 

DHIKRU LLAAH

 

Kwa kumaliza napenda kujikumbusha nafsi yangu kwanza na pia kuwakumbusha ndugu zangu Waislamu pia kwamba, hakuna kinga kubwa inayomkinga mtu na kila balaa baada ya Qur-aan kama kumdhukuru Allaah.

 

Kumdhukuru unapolala, unapoamka, unapotoka nyumbani, unapositushwa na jambo, unapofurashishwa. Katika kila jambo lako jema au lisilo jema, bali hata katika kumuasi Mola wako unapomkumbuka Allaah na kukumbuka uwezo Wake juu yako na neema Zake juu yako mara utayaacha maasi hayo.

 

Na ukumbuke kwamba kwa msaada wake Yeye tu (Subhaanahu wa Ta’ala) utaweza kujikinga na kila balaa.

 

 

USIINGIZE NDANI YA NYUMBA YAKO VIFUATAVYO:

 

Mwisho kabisa ningependa kukumbusha kuwa ndani ya nyuma yako usije ukaingiza yafuatayo:

 

·         Usitundike picha [ya viumbe hai] yeyote ile.

 

·         Usisikilize nyimbo.

 

·         Usiweke baraza za kusema watu au kutukana watu.

 

·         Usitizame filam za sinema n.k.

Hayo yote yanakaribisha mashaytwaan katika nyumba yako na yanafukuza Malaika.

 

MwenyeziMungu Anasema:

 

{{Na kama wasiwasi wa Shaytwaan ukikusumbua basi sema (A’udhu biLlaahi), jikinge kwa Allaah (na kuchezewa na Shaytwaan), Bila shaka Yeye ndiye asikiaye na ajuaye. Hakika wale wanaomuogopa (Allaah) zinapowagusa pepesi za Shaytwaan, mara hukumbuka, tahamaki wamekweshaona njia. Na ndugu zao (wale walioasi) wanawavutia katika upotofu (upotevu kisha wao hawaachi).}} [Suuratul-A’Aaraaf: 200-202]

 

Hivi ndivyo ilivyo, wale wanaoasi daima hawapendi kuona wenziwao wanaokoka na wanajaribu kila njia kuwavutia katika maasi. Lakini mwenye kuomba msaada wa Allaah basi Mola wake Atamuokoa.

 

 

 

Share