02-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: Maelezo Ya Wachapishaji

 

 

Maelezo Ya Wachapishaji

 

 

 

Tunamhimidi Allaah. Tunamtukuza Yeye, tunamwomba Msamaha na tunaomba hifadhi Yake kutokana na mwelekeo wa kifisadi na kutokana na uovu wa amali mbaya.

 

 

 

Adui mkubwa wa Uislamu ni Shaytwaan. Huja na sura ya hadaa na hutumia juhudi zake zote kuwatoa Waislamu kwenye dini yao na katika misingi na mafundisho yake adhimu. Makafiri wanatishika kwa mwenendo wa maisha ya Waislamu ambao hauna dosari wala usio fedhehesha. Wanajua fika kuwa madhali Waislamu wanashikamana na dini yao, juhudi zote za kuwapotosha hazitofanikiwa kwa sababu Uislamu ndiyo chimbuko la uwezo wao. Uislamu ni dini inayomuinua mtu binafsi kuwa juu na mwenye kuheshimika. Na kwa sababu hii, Uislamu unashambuliwa kwa kila njia na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na wasio kuwa Waislamu (makafiri). Ni jambo rahisi kuwapotosha vijana na kuwatoa katika mambo yenye manufaa na kuwatia katika maangamizi, maisha yaliyo kinyume na Uislamu. Kwa kufuata mwongozo wa Uislamu, tuna muadhimisha Muumba wetu, Allaah na tunakuwa mfano bora kwa binadamu wengine.

 

 

 

Adui (Shaytwaan) ana jaribu kutushawishi tuone ya kuwa maisha ya dunia ndiyo njia pekee ya kupata uwezo na mafanikio. Upotoshaji huo unakusudia kuwashawishi Waislamu waone ya kuwa udhaifu wao una sababishwa na kufuata dini yao, maamrisho yake na misingi yake. Vyombo vya habari pia huitwa viburudishaji, ni vinara vya kuchafua akili za vijana; kwahiyo familia za Kiislamu ziwe macho kutambua uwezo wa viburudishaji kuwapotosha vijana wetu kwa kuwatoa kwenye maadili mema bila wao kujua. Badala ya kuiga haiba ya Mtume Muhammad ambayo haina walakini, bila kujitambua wanaiga tabia mbaya wanazoziona kwenye sinema au runinga, na hivi ndivyo wanavyotekwa na Shaytwaan.

 

 

 

Waislamu imara wana uwezo wa kukhitari kati ya haiba na uigizaji na akabaki na msimamo, ambapo wale dhaifu na wajinga ni rahisi kupotoshwa. Inatupasa kuongeza juhudi hasa katika zama hizi kuzungumza na vijana wetu, na hata sisi watu wazima lazima turejee kwa mashujaa wakuu wa Kiislamu waliopita ambao walijenga utamaduni wenye nguvu na uliotukuka katika tamaduni zingine. Ambao waliitoa jamii kutoka ujahili na kuingiza katika Uislamu ambao ulibadilisha maisha yao kwa kiwango kikubwa. Huu ni utamaduni unaojumuisha shani ya maadili ya Muislamu na maendeleo ya kimaisha sawia.

 

 

 

Tunataka kukiwasilisha kitabu hiki, “LULU ZENYE THAMANI–Wasifu wa Maswahaba kumi waliobashiriwa Pepo.” Kwa vijana wetu kuwa urithi kwao kwa matarajio kuwa wataendelea kutafuta thamani ya kweli ambayo Uislamu unataka kuifikia. Ndani yake kuna mifano ya kuigwa badala ya ubandia, na mafisadi walio wasilishwa kwetu na makafiri.

 

 

 

Abdul Malik Mujahid

 

MENEJA MKUU

 

DARUSSALAM

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Maelezo Ya Wachapishaji (Chapa ya Kiswahili)

 

 

 

Kitabu hiki ni miongoni mwa vitabu muhimu sana kwa wasomaji wa lugha hii ya Kiswahili.

 

 

 

Ni vitabu vichache vinavyozungumzia wasifu wa maswahaba kwa lugha hii ya kiswahili bali ni vichache zaidi vilivyochambua (kwa ushahidi) bila ya ziada ya maneno ya kufurahisha watu wala nuksani.

 

 

 

Hizi ni zama ambazo vigezo bora vimewapotea watu, watu huiga wanavyoviona, wanavyovisoma na wanavyosikia kwa watu. Hakuna kigezo kizuri kama kile alitotuachia Mtume na nyota zilizowakilishwa na maswahaba zake. Hao ndio wa kufuatwa na kuigwa.

 

 

 

Qadhwaa na Qadar ya Allaah ndio iliyowachagua maswahaba zake  kusuhubiana na Mtume Muhammad na usuhuba ule uliwafanya kuwa ni watu walioshiba na kupata maadili yaliyokuwa bora kabisa kutoka kwa mbora wa viumbe vya Allaah. Ilifikia wakati ambao Qur-aan ilikuwa ikionekana katika vitendo vya kila siku katika maisha yao.

 

 

 

Hiyo ndio hali aliyowaachia Mtume na kutuachia kwani yeye kadhalika alikuwa hivyo na Bi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuthibitisha hilo anamwambia Swahaba aliyetaka kujua tabia ya Mtume ilivyokuwa na kumwambia asome Qur-aan kwani ndio ilivyokuwa tabia ya Mtume.

 

 

 

Waislamu hatuna budi kujifunza tabia nyingi nzuri waliotuachia mashujaa wa Ummah huu na kitabu hiki kinawasilisha hayo.

 

 

 

Abu Summayyah

 

 

 

Al-Khansaa Book Center

 

 

Share