Makaburi Misikitini

 

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’aiy

 

Kuna baadhi ya kauli zilizotolewa na baadhi ya watu kuwa Haajar na baadhi ya Mitume (‘Alayhimus Salaam) wamezikwa ndani ya Msikiti wa Makkah, na kwamba maneno hayo yameandikwa katika vitabu vya historia.

Bila shaka yoyote mwenye hoja hii anaelewa wazi kabisa kuwa waandishi wa historia hawajiwekea shuruti za usahihi wa Hadiyth zao, pamoja na kufanya tahakiki juu ya mlolongo wa wapokezi wa Hadiyth hizo (narrators), kwani wao hukusanya tu habari na kuziandika. Ama vitabu vilivyo sahihi na vinavyojiwekea shuruti za kuandika Hadiyth sahihi hapana hata kimoja kilichoandika juu ya jambo hilo.

Katika kitabu cha Al-Jaami’ as-Swaghiyr mwandishi wake Al-Manaar anasema;

"Hakuna hata moja katika makaburi ya Mitume yaliyo na uhakika kuwa wamezikwa hapo isipokuwa kaburi la Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) peke yake, ama kaburi la Nabii Muusa na Ibraahiym (‘Alayhimas Salaam) ni dhanna tu, na wala hapana uhakika juu yake".

Kwa hivyo kauli hizo haziwezi kuchukuliwa kuwa ni hoja, hasa katika mambo yanayohusu itikadi za dini.

 

Ama kuhusu kauli kuwa katika kisa cha Asw-haabul Kahf, baada ya kufa kwa watu hao, palisemwa kuwa; ‘Watawajengea Msikiti’, hiyo pia si hoja, kwa sababu katika Aayah hiyo hiyo imeandikwa kuwa; wenzao walisema;

"Jengeni jengo juu yao (wasipate kupita watu kuja kuwachungulia) Mola wao Anawajua vyema (Basi inatosha)"

Wakasema wale walioshinda;

"Bila shaka sisi tutajenga Msikiti juu yao" (yaani katika pango)"

Ukichunguza utaona kuwa waliotaka wajengewe jengo, ndio waliotoa hoja ya Uchaji Allaah kuliko hao walioshinda, na Allaah hakueleza lolote katika hali zote mbili, na maneno haya ndiyo yanayokubaliwa na maulamaa wengi, wa zamani na wa sasa.

 

Isitoshe, hata ikiwa tutakubali kwa ajili ya mjadala tu, basi kauli hii haileti maana yoyote ya kututaka sisi tufuate maneno yao, kwani Allaah Ametuletea Mtume wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akatufundisha yale anayotaka kutoka kwetu, na miongoni mwa aliyotufundisha ni kauli yake (Subhaanahu wa Ta’ala) katika hiyo Suratul Maidah, Sura ambayo ni ya mwisho kuteremshwa, kauli isemayo

"Na kila (Umma) katika nyinyi (binadamu) Tumeujaalia shari’ah yake na njia yake".

Al-Maaidah: 48

 

Kwa hivyo wao walikuwa na shari’ah zao na njia zao, na sisi tuna shari’ah zetu na njia zetu. Kama vile wao walivyokuwa wakiruhusiwa kumsujudia kiumbe mwenzao (Soma Surat Yuusuf) na waliharamishiwa kula baadhi ya nyama na shahamu, wakati sisi tumeruhusiwa kula vyakula hivyo na tumeharamishiwa kumsujudia yeyote mwengine asiyekuwa Allaah.

 

Na kwa vile Sura hii ya Al-Maaidah inajulikana kuwa ni Surah ya mwisho kuteremshwa na kwa ajili hiyo kila kilichoandikwa ndani yake kinahesabiwa kuwa ni hukmu ya mwisho kabisa.

 

Tukirudia katika maudhui yetu ya Kaburi la Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), nilikwishanukuu hapo mwanzo kauli mbali mbali za Maulamaa zinazotofautisha hali baina ya kaburi la Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na yale wanayozikwa watu ndani ya Misikiti au kujengewa juu yake Misikiti.

 

Ndugu zangu Waislam, Hadiyth sahihi ziko nyingi sana na zinaeleza kwa uwazi kabisa kuhusu maudhui yetu haya;

Kutoka kwa bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Ummu Habiybah na Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) walimhadithia juu ya kanisa waliloliona walipokuwa katika nchi ya uhabeshi, ndani yake mna picha nyingi, na bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akamhadithia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

“Watu wale anapokuwa nao mtu mwema baina yao, basi anapokufa mtu huyo wanajenga juu ya kaburi lake msikiti (mahala pa ibada), asha wanachora juu yake picha hizo, hao ni watu wabaya kabisa kwa Allaah”.

Al-Bukhaariy na Muslim

 

Hadiyth nyingine;

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

“Ghadhabu ya Allaah imekuwa kali sana juu ya watu wanaoyageuza makaburi ya Mitume yao na watu wema wao kuwa misikiti”.

Al-Bukhaariy na Muslim

 

Na akasema;

"Mola wangu usilijaalie kaburi langu likawa sanamu linaloabudiwa".

Muslim

 

Na akasema;

"Msiswali kuyaelekea makaburi wala msikae juu yake.”

Muslim

 

Na akasema

"Allaah Amewalaani Mayahudi na Manaswara wamegeuza makaburi ya Mitume yao kuwa Misikiti".

Imepokelewa na Maimamu wa Sunnah wote

 

Imesimuliwa na Abdur-Razaaq katika Musanaf yake kuwa;

"KAULI YA MWISHO KABISA ALIYOITAMKA MTUME (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kuirudisha roho yake iliyotwaharika kwa Mola wake aliyeiumba, alisema;

"Allaah Awaangamize Mayahudi na Manaswara, wameyageuza makaburi ya Mitume yao kuwa mahali pa ibada, pasibaki na dini mbili katika bara ya Arabuni".

Hadiyth hii pia imo katika Muwatwaa ya Imaam Malik

 

Kutokana na Hadiyth zote hizi, ndiyo maana Maulamaa wetu wakatuambia kuwa ni haramu kuswali ndani ya Misikiti iliyo na makaburi ndani yake, yote haya kwa ajili ya kuogopa laana za Allaah zisije zikatusibu kama zilivyowasibu Mayahudi na Manaswara kwa ajili ya kuyageuza makaburi ya Mitume yao kuwa ni mahali pa ibada.

 

Hadiyth za aina hii zilizo sahihi ziko nyingi sana, na tukiendelea kuzitaja tunaweza kujaza kurasa nyingi, isipokuwa ningependa kuongezea jambo moja, nalo ni kuwa, Imam An-Nawawiy amezielezea Hadiyth hizi katika kitabu cha Adhkaar katika mlango wa kutujulisha juu ya watu wanaostahiki kulaaniwa, akawataja hawa wanaotenda mambo haya kuwa ni miongoni mwa watu hao wanaostahiki kulaaniwa.

 

Kwa hivyo ni bora mtu ayakimbie mambo kama haya yenye kutatanisha na yanyomuingiza mtu katika kundi la wanaostahiki kulaaniwa na badala yake kufuata yale yaliyo dahiri na sahihi, yale yanayomkaribisha mja na radhi za Mola wake

 

Watu hawa, wanasema Maulamaa kuwa wanayajengea makaburi hayo kwa niyah njema ya kutaka kuwaigiza katika juhudi zao za kufanya ibada, lakini baada ya kupita miaka mingi wakaja vizazi wasiotambua kusudi la kujengewa, Shaytwaan ataanza kuwatia wasiwasi wake na kuwaambia kuwa wazee wao na babu zao walikuwa wakiwaabudu, kisha na wao wakawaabudu. Na hii ndiyo sababu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatukataza kufanya hivyo ili kuufunga mlango wa fitina tokea mwanzo wake"

Allaah Anasema;

“Wamewafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Allaah, na (wamemfanya) Masihi mwana wa Maryamu, hali hawakuamrishwa isipokuwa kumuabudu Ilaah mmoja, hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Yeye. Ametakasika na yale wanayomshirikisha nayo”.

At-Tawbah: 31

 

Imepokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad na At-Tirmidhiy kuwa Uday bin Haatim At-Taaiy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa mkubwa wa kabila la At-Taaiy, kwamba aliposikia juu ya kuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na dini ya Kiislam, alikimbilia nchi ya Shaam, na hii ni kwa sababu kabila lake liliingia katika dini ya Manaswara tokea wakati wa Jahilia (kabla ya kuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Katika mapambano baina ya watu wake Uday bin Haatim At-Taaiy, na majeshi ya Waislam, dada yake aitwae Savanah alikuwa miongoni mwa mateka waliotekwa na Waislam.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipojua kuwa Savanah ni binti wa Haatim At-Taaiy aliyekuwa akijulikana sana na akipigiwa mifano kwa ukarimu wake, akamuacha huru. Aliporudi kwa kaka yake ambaye ni mkuu wa kabila hilo kubwa, alimshikilia sana aingie katika dini ya Kiislam.

 

Wakatoka pamoja kwenda Madiynah ili Uday amuone Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alipokuwa amekaa chumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na msalaba wake alouvaa shingoni pake ukiwa unaning’inia kifuani pake, ikateremshwa Aaayah hiyo hapo juu;

“Wamewafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa ni waabudiwa badala ya Allaah…”

Uday akasema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam);

Lakini hatukuwa tukiwaabudu ewe Mtume wa Allaah”.

 

Uday masikini alikuwa akdhania kuwa ‘Ibada’ ni kumsujudia mtu au kumswalia.

Lakini Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamsahihisha na kumfundisha nini hasa maana ya ibada, akamuuliza;

“Si (hawa wanavyuoni wao na watawa wao) walikuwa wakiharamisha yale aliyohalalisha Allaah na wakihalalisha yale aliyoharamisha Allaah na wao wanawafuata?”

Akasema;

Ndiyo walikuwa wakifanya hivyo”.

Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

Basi huko ndiko kuwaabudu”.

 

Hapa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anatufundisha kuwa kuabudu, si lazima kuwe kwa kusujudu au kuswali tu, bali hata kumfuata mwenye kuhalalisha haramu na kuharamisha halali pia hiyo ni ibada.

Kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia Uday (Radhiya Allaahu ‘anhu);

Ewe Uday! Unasemaje, kwani unadhurika kitu wewe panaposemwaAAllaahu Akbar? Kwani unakijua chochote kingine kilichokuwa kikubwa kuliko Allaah?

Kwani unadhurika wewe panaposemwaLaa ilaaha illa Allaah’. Kwani unamjua mwabudiwa mwengine asiyekuwa Allaah?”

Kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuita katika Uislam na Uday (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaitikia wito wake na akaitoa shahada ya haki.

Katika mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), tutaona anatukataza kuyaabudu makaburi ya watu wema (wachaji Allaah – au kama wanavyoitwa sasa Mawalii).

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema;

Ghadhabu ya Allaah imezidi kwa wale wanaogeuza makaburi ya Mitume yao na wachaji Allaah wao kuwa mahala pa ibada, Mola wangu usijaalie kaburi langu likawa mahali pa ibada”.

Muslim

Na katika riwaya nyingine;

Uslijaalie kaburi langu likawa sanamu linaloabudiwa”.

Juu ya kuwa imeshapita karne nyingi tokea alipofariki Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), inasikitisha kuona kuwa mpaka leo katika nchi nyingi za Waislam bado wapo watu wanaojishughulisha na ibada hizo za makaburi.

 

Ama kuhusu kaburi la Mtume, hali yake inakhitililafiana kabisa na maudhui haya, kwa sababu kwanza Msikiti huo haukujengwa juu ya kaburi hilo, wala Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuzikwa ndani ya Msikiti, isipokuwa katika upanuzi wa Msikiti wakati wa utawala wa Banu Umayyah, kwa vile Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alizikwa ndani ya nyumba yake iliyoambatana na Msikiti, ikabidi kaburi hilo liwe ndani yake, na Maulamaa wakafanya kila njia na kuweza kuuzungushia ukuta na kuutenga mbali na watu wanaoswali.

 

Hili ndilo waliloweza, pamoja na kujenga viti vya saruji mahali ambapo watu wangesimama kwa ajili ya kuswali, na kwa ajili hiyo haiwezekani mtu kusimama na kuswali hapo, na wanaweza kukaa tu na kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na kumuombea du’aa.

 

 

Share