02-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Utangulizi

 

 

Utangulizi

 

Kwa hakika shukrani zote zinamstahiki Allaah; tunamtukuza Yeye, tunamwomba msamaha Yeye, na tunatafuta maghfira kwake na msaada. Tunakimbilia kwa Allaah atuhifadhi na uovu wa nafsi zetu na amali zetu mbaya. Yeyote aliyeongozwa na Allaah, hapana awezaye kumpotosha; na yeyote anayepotezwa na Allaah hapana awezaye kumwongoza. Nanakiri ya kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah pekee, na Yeye hana mshirika; na nakiri ya kwamba Mtume wetu Muhammad ni mtumwa Wake na Mjumbe wake.

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.(3:102)

 

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Aliyekuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.” (4:1)

 

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawasawa. 

 

Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na Akusameheni madhambi yenu. Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa.” (33:70-71.)

 

Kwa uhakika, maneno ya ukweli zaidi ni Kitabu cha Allaah, na mwongozo mzuri ni ule wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozushwa (katika Dini), kwani kwa kila jipya linalozushwa ni bida’h, na kila uzushi ni upotevu, na kila upotevu ni kuingizwa Motoni.

 

Katika miaka ya hivi karibuni Waislamu waaminifu, wamekagua hali ya Taifa letu, na walichogundua ni athari za mafanikio ya Shaytwaan, wa amali mbovu, na damu ya majeraha mengi. Waliona kutokupatana, kutokuelewana, mfarakano, mkanganyiko, na wasiwasi. Walipata matokeo mabaya kwa kutokuhukumu kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah, majumbani, sokoni au katika jamii. Waliona matokeo haya mashuleni, vyuo vikuu, vitabuni, magazetini, na vyombo vya habari; kwa uhakika, wanayashuhudia hata katika sehemu ‘adhimu, Misikitini ambapo uzushi unashamiri. Na pia wameona athari za uovu miongoni mwa viongozi wa da’wah (walinganiaji katikaUislamu) na wasomi.

 

Wale wanaojitahidi kufanya amali njema, wanashindana kutafuta tiba kwa Taifa letu na masikitiko yake. Madawa au tiba ya kila kitu yanayotolewa ni mengi, lakini hali haibadiliki – isipokuwa katika maeneo fulani, ambapo juhudi zisizoratibiwa zimefanywa, lakini hazitoshi kufanya mabadiliko kwa ujumla.

 

Iwapo tunataka tiba ya dunia nzima kwa matatizo yetu, lazima tutalii mwongozo wa mwisho uliotolewa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Maswahaba zake na Taifa lake - ambao umeelezewa na Al-Irbaad bin Saariyah (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa khutbah ambayo ilisababisha mioyo ya Maswahaba kutetema na macho kububujika machozi. Kisha, akawapa usia wa mwisho.

 

Nasaha zinaihusu enzi yetu kama ilivyokuwa kwa enzi zote; ni nasaha zinazofaa kwa wakati wa kutopatana na migongano,  wakati  ambao Waislamu wamegawika katika makundi  na vyama; kwa kila kikundi kikisema, “sisi  tuko sahihi na katika yale yaliyo sahihi, na ni wengine ndio waliokwenda kombo.”

 

Kila mmoja anajaribu kuonesha tahadhari zake kwa Waislamu, akijaribu kuwashawishi wajiunge na kundi lake na wajitenge na makundi mengine au vyama. Kila mmoja kwa uwazi au kujitokeza, analaumu wengine kwa kutokuwa na ufahamu kamili wa Uislamu, kwa kutowaalika wengine katika njia inayomridhia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Tunaishi katika zama ambazo kila mmoja wetu anahitaji sana kutafakari juu ya nasaha za mwisho za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Hitajio hilo ndilo lililo nichochea kuandika kitabu hiki kidogo, kwa matarajio ya kupokewa na masikio yanayosikia kwa kuridhia, mioyo inayomcha Mola wao, na nafsi zinazoitikia wito wa kufuata haki.

 

Namwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) azifanye juhudi za kuifanya kazi hii ni ya uaminifu Kwake, na sio kwa jambo jingine lolote. Namwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) auauni Ummah wa Kiislamu kupitia kwangu, kunifanya ufunguo wa wema, na kufuli ya kuzuia maovu. Kwa hakika, Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) ni muweza wa kila kitu.

 

Husayn Bin ‘Awdah al–‘Awayishah

 

Share