06-Wasiya Wa Mwisho Wa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Marekebisho Ni Yapi?

 

Marekebisho ni Yapi?

 

”Kisha shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifah wema baada yangu: iumeni (ing’ateni) (yaani Sunnah yangu…) kwa magego yenu.”

 

“Kisha shikamaneni na Sunnah zangu”. Shikamaneni na njia yangu, kwani mwanga, ponyo na rehema; inafafanua Qur-aan na inachota kutoka chemchem yake. Inakuwaje anayepokea kutoka katika Qur-aan na Sunnah kwenda kombo ambapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;

 

“Nimekuachieni mambo mawili; mkishikamana nayo hamtapotea. Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”[1]

 

IliHadiythwa ya kuwa Abu Al-‘Aaliyah alisema, “Ni jukumu lenu kufuata yaliyokuwepo mwanzoni, kabla hawakufarakana.

 

“Kisha mfuate Sunnah yangu.” Lakini  tutajuaje Sunnah yake ni ipi? Njia sahihi ya kuthibitisha lazima ifuatwe na kuhakikisha uhalisi wa Ahaadiyth, na kwa kuwa Wanachuoni wa Hadiyth walifuata njia hiyo, lazima tuwafuate. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

 

 “Litaendelea kuwepo kundi lililoshinda juu ya ukweli katika Ummah wangu; hawadhuriwi na wale walioacha ukweli, mpaka amri ya Allaah itakapokuja (yaani, karibu na Siku ya Qiyaamah, wakati Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) atachukua roho ya kila Muumini mwanaume na mwanamke) nao wakiwa katika hali hiyo.”[2]

 

Kundi la Wanachuoni wanasema kundi hilo ni watu wa Hadiyth. Shaykh wetu, Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi) anawataja wote wenye rai hii katika As-Silsilah as-Swahiyhah (1/541); nao ni:-

1.     ’Abdullaah bin Al-Mubaarak, aliyeizungumzia Hadiyth iliyopita. “Kwa maoni yangu, hao ni watu wa Hadiyth.”

2.     ’Aliy bin Al-Madini. Muhammad bin Ismaa’iyl Al-Bukhaariy alisimulia kuwa ‘Aliy bin Al-Madini alisema,

“Wao na watu wa Hadiyth.”

3.     Ahmad bin Hanbal, alipoulizwa kuhusu maana ya Hadiyth tajwa, alisema, “Iwapo watu wa Hadiyth sio kundi lililofuzu, basi siwajui ni nani.”

4.     Ahmad bin Sinaan At-thiqah Al-Hafidh alisema,

“Ni watu wa elimu na watu wa Hadiyth.”

5.     Muhammad bin Ismaa’iyl Al-Bukhaariy. Wakati Hadiyth tajwa iliposomwa, alisema, “Hii inawarejea watu wa Hadiyth“

 

Katika Sahihi yake, alipokuwa akiitolea maelezo Hadiyth, Al-Bukhaariy alisema, “Na wao ni watu wa elimu.” Hii haikinzani na usemi wake mwingine, kuwa watu wa elimu ni watu wa Hadiyth. Jinsi mtu anapokuwa na maarifa ya Hadiyth anakuwa bora zaidi kuliko yule mwenye maarifa kidogo katika Hadiyth. Katika kitabu chake Khalq–Af’aal Al-‘Ibaad, Al-Bukhaariy anataja Aayah hii,

“Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu…” ( 2:143).

 

Alipokuwa akijadili Aayah hii, kisha alisema, “Ni kundi ambalo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilitaja…” Na kisha alitaja Hadiyth tuliyokuwa tunaijadili hapa.

 

Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliachia ummah wake nuru na mwongozo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

“Kwa uhakika, nimekuachieni weupe unaofanana yaani, juu ya angavu, wazi, ukweli usiopingika. Usiku mweupe ni ule ambao mwezi unaonekana kuanzia mwanzo mpaka mwisho, mchana wake ni usiku wake; hapana anayekenguka kutokana nao isipokuwa yule aliyeangamizwa.”[3]

 

Inaelekea ya kuwa haya ni maelezo ya Aayah ifuatayo:

“Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyonyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya Amekuusieni ili mpate kumcha Mungu.” (6: 153).

 

 

Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema,

 

“Tulikuwa tumekaa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipochora mstari mbele yake na kusema, “Hii ni njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).” Kisha alichora mstari kuliani kwake, na mstari kushotoni kwake, na kusema, “Hizi ni njia za Shaytwaani. Kisha aliweka kiganja chake juu ya mstari wa katikati, alisoma:

 

“Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyonyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya Amekuusieni ili mpate kumcha Mungu.” (6: 153).[4]

 

“Kisha juu yenu ni Sunnah yangu.” Hakusema: Namfuate njia ya Shaykh fulani au Mwanachuoni au mwalimu, kwa hivyo jihadharini na ushabiki wa kuwafuata waliotangulia, bali tuchukue yale wanayotufundisha kutokana na Sunnah na ukweli.

 

“Na Sunnah za Makhalifah waongofu.” Lazima tuelewe Sunnah kama walivyozielewa Makhalifah waongofu, kwani wao walikuwa karibu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mioyo safi, imani thibiti, wakifanya amali njema, na wakishikamana na njia ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Waliyaona mambo kwa macho yao wenyewe, ambapo sisi tunasimuliwa habari zake: “Na kusikia habari si sawa na kujionea kwa macho yako.”[5]

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaelezea ya kuwa waliongozwa vema, tunamjua yeyote baada ya Maswahaba wa Mtume mwenye sifa sawa, ili tumfuate?

 

 [1] Ilisimuliwa na Maalik na Silsila yake ni Mursal, na Al-Haakim kutoka Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa Silsila ya Hasan, kama Shaykh Wetu (Al-Albaaniy)- Allaah Amuwie radhi – alisema katika At-Tawassul Anwa’uhu Wa-Ahkaamuhu (uk.13). (Angalia Tawassul Aina Zake & Hukumu Zake cha Shaykh Al-Albaaniy, Uk. 7.) Ilipigwa chapa na Al-Hildaayah Publishing & Distribution, UK)

[2] Ilisimuliwa na Muslim (1920) na wengineo.

[3] Usahihi wake kwa Silsila nyingi na masimulizi yaliyothibitisha, kama ilivyotajwa katika Kitabus–Sunnah, cha Bin Abi ‘Aaswim (47,48,49).

[4] Imethibitishwa na Hadiyth nyingine, rejea, kitabu As-Sunnah cha Abu ‘Aaswim (16,17).

[5] Ilisimuliwa na Ahmad, at-Twabaraaniy, al-Khaatwib na wengineo, ikiwa na Silsilah Swahiyh, kama ilivyotajwa katika Takhrij al-‘Aqiydah at-Twahaawiyyah (401)

Share