11-Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Sura Ya Tisa: Wanachuoni Walivyomsifu

 

11- Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Sura Ya Tisa: Wanachuoni Walivyomsifu

 

Alhidaaya.com

 

 

Wanachuoni Walivyomsifu[1]

 

Wanachuoni wengi wa wakati wake na baada ya wakati wake walikuwa wakimsifu Shaykh al-Islaam kwa elimu yake, ikhlaasw yake, hayaa, ucha Mungu wake, na kufuata kwa ukaribu mwendo wa Salaf. Matamko mengi katika haya ya kumsifia yamekusanywa ndani ya kitabu kilichoandikwa na al-Haafidh Ibn Naaswir ad-Diyn kilichopewa jina la ‘Radd al-Waafir’ kikikana dai lililochupa mpaka, lile ambalo linadai kusema kwamba Ibn Taymiyyah, ‘Shaykh al-Islaam’, hakuwa na imani.

 

Baadhi ya maneno haya ya kumsifia na matamko ya kumkubali Imaam huyu hayakuja tu kutoka kwa wanafunzi wake na wafuasi wake, lakini pia kutoka kwa maadui zake waliotoa uhibitisho kwamba amevuka kiwango cha elimu na ufahamu, na halikadhalika wametoa ushuhuda wa jitihada yake, ukarimu na Jihaad yake kwa ajili ya Allaah na kwa ajili ya kuutetea Uislamu. Yanafuatia baadhi ya maneno haya ya kumsifia na kumtamkia:

 

 

-Shaykh Ibn Naaswir ad-Diyn ad-Dimashqiy ameandika kitabu kiitwacho ar-Radd al-Waafir ‘ala man za’ama anna man sammaa Ibna Taymiyyah Shaykh al-Islaam kaafir, ambacho ndani yake amekana Mahanafi waliokithirisha na waliodai kwamba hairuhusiki kumuita Ibn Taymiyyah “Shaykh al-Islaam”, na kwamba yule ambaye atafanya hivyo atakuwa ni kafiri! Ndani yake (kitabu hichi) anataja Imamu themanini na tano (85), wote ambao wamemtaja Ibn Taymiyyah kama ni Shaykh al-Islaam, na kunukuu maneno yao kutoka kwenye vitabu vyao kwa athari hiyo. Pale al-Haafidh Ibn Hajar (Allaah Amshushie rehema zake) aliposoma kitabu hichi – ar-Radd al-Waafir – alikiandikia utangulizi, ambao alisema:

 

Shukrani zote ni za Allaah, amani iwe juu ya waja Wake na ambao Amewachagua.

 

 

Nimekutana na kitabu hichi chenye manufaa na kugundua namna elimu ya ndani ya Imaam (Ibn Taymiyyah) aliyoandika, na namna alivyo mahiri katika matawi mengi ya elimu, hadi kufikia kuwa ni Mwanachuoni mkubwa mwenye kuheshimika na kusifika kwa Wanachuoni. Nafasi yake maarufu aliyokuwa nayo Shaykh Taqiyud-Diyn (Ibn Taymiyyah) kama ni Imaam, ni yenye kuangaza kuliko jua, na jina lake kama ni Shaykh al-Islaam kwa wakati wake limeendelea kubakia hadi leo na litaendelea kubakia hadi kesho. Hakuna anayekataa hilo isipokuwa yule aliyekuwa ni mjinga wa nafasi yake mwenyewe, au asiyekuwa muadilifu. Ni namna gani atakuwa mkosefu yule anayefikiria hivyo na kwa namna gani atakuwa amekwenda mrama. Allaah ni Mmoja Ambaye tunamuomba kutulinda sisi kutokana na maovu ya nafsi zetu na ndimi zetu kwa baraka Zake na uongofu. Iwapo kungelikuwa hakuna ushahidi mwengine wa hadhi kuu ya mtu huyu isipokuwa kutoka kwa yale yaliyoelezewa na al-Haafidh ash-Shahiyr ‘Ilm ad-Diyn al-Barzaaliy ndani ya kitabu chake Taariykh, (pale aliposema):

 

 

 

“Kulikuwa hakuna mtu ndani ya historia ya Uislamu ambaye maziko yake watu walikusanyika kama walivyofanya kwa maziko ya Shaykh Taqiyud-Diyn (Ibn Taymiyyah). Ameweka bayana kwamba maziko ya Imaam Ahmad yalihudhuriwa na mamia kwa maelfu (laki kadhaa), lakini idadi ya Damascus ingalikuwa inalingana na ya Baghdad, au zaidi, basi hakuna mtu ambaye angejaribu kukaa mbali ya maziko yake. Zaidi ya hivyo, wote ambao walikuwepo Baghdad, isipokuwa kwa wachache, wakiamini katika uongozi wa Imaam Ahmad. Mtawala na Khaliyfah wa Baghdad kwa kipindi hicho alikuwa na nafasi kubwa ya mapenzi na heshima kwake. Hii ni tofauti na kesi ya Ibn Taymiyyah, kwa mtawala wa mji kutokuwepo wakati wa kifo chake, na Mafuqahaa walio wengi ndani ya mji huo walijitengea kikundi dhidi yake, na alikufa akiwa kifungoni ndani ya ngome. Lakini juu ya yote, hakuna aliyekaa mbali ya maziko yake au kushindwa kumtakia rehema yeye na kuomboleza, isipokuwa watu watatu tu (waliokuwa na chuki naye) waliokaa mbali kwa hofu ya hamaki za watu wengi.

 

Ingawa idadi hizi kubwa zilifika mazikoni, kulikuwa hakuna msukumo kwa hilo isipokuwa kwamba alikuwa ni mtu mkubwa na hamu yao ya kutaka malipo kwa kuhudhuria maziko yake. Hawakujikusanya kwa amri za watawala au kwa sababu nyengine yoyote. Imesimuliwa kutoka kwenye simulizi sahihi kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nyinyi ndio mashahidi wa Allaah juu ya ardhi”[2]

 

Idadi kadhaa ya Wanachuoni wakimpinga Shaykh Taqiyud-Diyn kwa mara nyingi, kwa sababu ya hoja za kupingana naye ambazo ziliendana na masuala mbalimbali ya msingi na yale madogo. Kesi nyingi zilifunguliwa dhidi yake mjini Cairo na Damascus, lakini hakuna ripoti inayosema kwamba alikuwa ni kafiri na kulikuwa hakuna hukumu inayosema kwamba auawe, ingawa kulikuwa na watu wengi ndani ya serikali kwa wakati huo waliokuwa wakimpinga kwa nguvu zao zote, na alifungwa jena mjini Cairo, kisha baadaye Alexandria. Juu ya yote hayo, wote waliikubali elimu yake pana na hayaa zake za ndani kabisa na ikhlaasw yake, na wakimtambua kama ni mkarimu na mwenye juhudi, halikadhalika kwa kuutetea kwake Uislamu na kuwaita watu kwa Allaah kwa siri na dhahiri. Ni kwanini tusimdumaze yule anayesema kwamba alikuwa ni kafiri au yule anayemuita Shaykh al-Islaam ni kafiri, wakati hakuna kitu chochote kinachoonesha ukafiri wake?

 

Hapana shaka yoyote kwamba alikuwa ni Shaykh wa Uislamu, na masuala aliyoyapinga yalikuwa si vitu ambavyo amesema kutegemeana na matakwa na mapenzi yake, na wala hakusisitiza kuvizungumzia baada ya ushahidi uliofafanuliwa dhidi ya wakorofi. Vitabu vyake vimejazwa na hoja za kuwakana wale waliohamasisha elimu isiyoyastaarabika na yeye kuwakataa. Lakini hata hivyo, yeye alikuwa ni mwanaadamu ambaye aliweza kupata na kukosea. Yale ambayo alikuwa ni sahihi – ambayo ni mengi, yanaweza kuwa na manufaa, na tunaweza kumuombea rehma kwake kutokana na hayo, na yale ambayo amekosea basi yasifuatwe, lakini anaweza kutolewa udhuru kwa hilo, kwa sababu Imaam wa wakati wake wameshuhudia kwamba alikuwa na kila sifa ya Ijtihaad; hata yule ambaye anampinga kwa nguvu zote na kujitahidi kumsababishia madhara, akiitwa Shaykh Kamaalud-Diyn al-Zamalkaaniy, ameshuhudia juu ya hilo, kama alivyofanya Shaykh Sadrud-Diyn Ibn al-Wakiyl, ambaye alikuwa peke yake aliyeweza kufanya mjadala pamoja na Ibn Taymiyyah.

 

Wala haishangazi kwamba mtu huyu alikuwa mpinzani aliyeaminiwa na wazushi kama vile Raafidhah, Huluuliyyah na Ittihaadiyyah, ambao maandiko juu ya hilo ni mengi na maarufu, ambayo fatwa zao kuhusiana nao ni mengi kuweza kuyahesabu. Ni namna gani wangelikuwa na furaha kutambua kwamba kuna watu wanaomtuhumu kwa kufuru na kusema kwamba yule asiyemtambua kuwa ni kafiri basi ni kafiri. Yule aliyedai kuwa na elimu, iwapo ana sababu ama hisia, basi na apigie mbizi maneno ya mtu huyo ndani ya vitabu vyake, au kusikia kutoka kwa wasimulizi waaminifu na wakweli, ili kwamba aweke mbali yale anayoyaona kuwa ni pingamizi na kuwaonya wengine kwa njia ya ukweli, na kumsifia kwa masuala aliyokuwa sahihi, kama vile tabia ya Wanachuoni wengine walivyokuwa.

 

Iwapo hakuna sifa yoyote nzuri ndani yake yeye isipokuwa kwa ukweli kwamba alikuwa ni mwalimu wa Shaykh Shamsud-Diyn Ibn Qayyim al-Jawziyyah, mwandishi wa vitabu vingi vyenye manufaa, ambavyo kila mtu amenufaika navyo, basi hilo linatosha kuonesha nafasi yake ya juu. Je, ni kwa namna gani pale uweledi wake ndani ya nyanja tofauti za elimu na usomaji wake wa kipekee wa maandiko ulivyothibitishwa na Mashaafi’iy wakubwa wa enzi zake na wengineo, na zaidi kwa Mahanbali?

 

Hakuna haja ya kutilia maanani kwa yule anayemuita kuwa yeye ni kafiri juu ya mafanikio yote, au yule anayemtambua kuwa anayemuita “Shaykh al-Islaam” kuwa ni kafiri, bali atakayedai hivyo adharauliwe kwa mnasaba wa jambo hili; kwa hakika ajibiwe kwa namna ya kumkana kutokana na kusema hivyo, hadi pale atakaporudi katika ukweli. Allaah Anazungumza ukweli na Anawaongoa watu katika njia sahihi; Allaah Anatutoa sisi na Yeye Ndiye bora wa kuyaharibu mambo.[3]

 

Al-Haafidh Ibn Hajar[4] ametoa maelezo mbalimbali katika sehemu tofauti kuhusiana na Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah, ambaye amethibitisha kwamba alikuwa ni mtu wa elimu na mwema aliyeihami Sunnah. Nukta ambazo al-Haafidh Ibn Hajar (Rahimahu Allaahu) amempinga Shaykh al-Islaam zinaweza kutohesabiwa, na kuna wale ambao wamempinga Ibn Hajar yeye mwenyewe katika baadhi ya mambo ya Aqiydah. Isipokuwa tutanukuu yale ambayo yeye amesema kumsifia Shaykh al-Islaam, kwa minaajili ya kuweka bayana makosa ya wale wanaosema kwamba al-Haafidh (Rahimahu Allaahu) hakuwa ni mwenye kumuheshimu Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah.

 

Kinachofuatia ni kuangalia kwa juu juu yale aliyosema al-Haafidh Ibn Hajar (Rahimahu Allaahu) kuhusiana na Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaahu).

 

-Al-Haafidh Ibn Hajar ameandika wasifu mrefu wa Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaahu) ndani ya kitabu chake cha ad-Durar al-Kaaminah, mwanzoni amesema:

 

 

“Baba yake amemchukua kutoka Harraan ndani ya mwaka 667H, na akajifunza kutoka kwa ‘Abdud-Daa’im, al-Qaasim al-Arbiliy, Muslim Ibn ‘Allaan Ibn Abi ‘Umar na al-Fakhr, miongoni mwa baadhi tu. Amesoma mwenyewe na kunukuu Sunan Abi Dawuud, na kusoma ar-Rijaal (wasimulizi wa Hadiyth) na al-ilal (makosa ndani ya Hadiyth). Amepata elimu ya ndani kabisa, na akajitofautisha na kwenda mbele zaidi ya wengine. Ameandika vitabu, kusomesha na kutoa fatwa, na amewashinda wenziwe. Alikuwa na uwezo wa ajabu wa kukusanya tena mara moja; alikuwa ni Mujtahid; alikuwa na elimu ya ndani katika masuala ya maandiko na hoja; na alikuwa na uwezo wa kujadili masuala kwa undani kwa kuegemea maoni ya Wanachuoni wa mwanzo wa baadaye.”[5]

 

- Ibn Hajar amenukuu ndani ya wasifu wake maandiko mengi ya Maimaam waliomsifia Shaykh al-Islaam (Rahimahu Allaahu) na kuuthibitsha usomi wake katika hoja na nyanja za maandiko ya elimu. Kwa mfano, amesema:

 

 

“Nimesoma katika maandishi ya al-Haafidh Swalaahud-Diyn al-‘Alaa’iy pale alipoandika kuhusu wasifu wa Shaykh wa ma-Shaykh, al-Haafidh Bahaaud-Diyn ‘Abdullaah Ibn Muhammad Ibn Khalily, yafuatayo: Bahaaud-Diyn huyu amejifunza kutoka kwa Mashaykh wawili, Shaykh wetu, na mtaalamu na kiongozi wa njia ya Allaah, Shaykh mkubwa, yule anayeongoza wafuasi wake katika njia bora, yule ambaye alikuwa na sifa karimu nyingi na ushahidi wa nguvu, ambao mataifa yote wanathibitisha kwamba hawataweza kuorodhesha ushahidi wote huu; Rabb Atujaalie na sisi kusoma kutoka kwenye elimu yake kubwa na kunufaika nayo sisi kwa njia za elimu yake ndani ya dunia hii na Akhera. Huyo ni Shaykh, Imaam, Mwanachuoni, mwalimu, nyota inayong’ara, Imaam wa Imaam, Baraka ya Ummah, kiongozi wa Wanachuoni, mfano wa watu kuufuata, mwangaza wa wasomi, mnyanyasaji wa wazushi, bahri ya elimu, hazina ya wale wanaotafuta manufaa, Mfasiri wa Qur-aan, maajabu ya wakati wetu, asiyeshindwa (kwa hoja sahihi) kwa wakati wetu, Taqiyud-Diyn, Imaam wa Waislamu, ushahidi wa Allaah dhidi ya dunia, ni mmoja wa watu wanaojumuika na watu wa kweli, mfuataji wa waliopita kabla yake, mwenye kuukubali ukweli, alama ya uongofu, muhifadhi wa juu, mwenye hadhi ya juu ya kuzungumza kwa ufasaha, nguzo ya Shari’ah, mwenye kuhodhi elimu bora kabisa, Abul-‘Abbaas Ibn Taymiyyah.”[6]

 

Ingawa hayo maandiko niliyoyanukuu au kuyarejea, yana maneno ya al-Haafidh Ibn Hajar (Rahimahu Allaahu) au ambayo yamenukuliwa na al-Haafidh kutoka kwa wengine, kuzungumzia heshima ya Shaykh al-Islaam na kuweka bayana hadhi yake ndani ya nyanja ya elimu za Diyn, kwamba haimaanishi kuwa al-Haafidh hakupingana na Shaykh al-Islaam hata kidogo ndani ya baadhi ya maeneo ya elimu, au kwamba hakupatapo kumpinga (kielimu), kwa sababu kikawaida inatokezea kwamba Mwanachuoni mmoja hupingana na mwengine, bila ya ulazima wa kumaanisha kwamba yule anayepingana na mwengine hamuheshimu au hakubaliana na hadhi ya huyo mwengine, achilia mbali kumtuhumu kwa uzushi au upotofu. Hapo zamani, Imaam Maalik (Rahimahu Allaahu) alizungumza maneno yake maarufu: “Maoni ya mtu yeyote yanaweza kukubaliwa au kukataliwa, isipokuwa kwa yule aliomo ndani ya kaburi hili” au maneno yenye maana kama hiyo – kwa maana ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Bila ya kujali nani alikuwa sahihi katika suala fulani, iwapo alikuwa ni Shaykh al-Islaam au yule ambaye anayetofautiana naye au amejaribu kupingana naye, al-Haafidh Ibn Hajar au mtu mwengine yeyote, itakuwaje iwapo yule aliyekuwa sahihi katika masuala mengi ambayo wanapingana naye, ni Shaykh al-Islaam? (Rahimahu Allaahu)[7]

 

- Imaam adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaahu) amesema, akiorodhesha mashaykh wake:

 

 

“Ni Shaykh wetu, Shaykh wa Uislamu, asiyeshindwa (na mtu) kwa wakati wetu katika masuala ya kielimu, juhudi, ufahamu, umahiri wa kiroho, ukarimu, ukweli mbele ya Ummah, uamrishaji mema na ukatazaji mabaya, na usomaji wa Hadiyth – ametumia jitihada zake kubwa katika kuitafuta na kuiweka katika maandishi, na amepitia aina ya wasimulizi tofauti na kuipata elimu ambayo hakuna mtu mwengine aliyeipata.

 

Amekithirisha katika kuifasiri Qur-aan (tafsiyr) na amechungua kwa ndani katika upambanuzi wake wa maana. Amefikia tafsiri kutokana nayo ambayo hakuna mwengine yeyote aliyeweza kufanya hivyo kabla yake. Pia amekithirisha katika Hadiyth na uhifadhiji wake; ni wachache mno wamehifadhi Hadiyth nyingi kama alivyofanya yeye. Amezifanyia marejeo Ahaadiyth kwa vyanzo vyake muafaka na wasimuliaji wake, na alikuwa na uwezo mwepesi wa kunukuu chochote anachotaka kuthibitishia ushahidi. Amewapita watu wote katika elimu ya Fiqh na maoni tofauti ya madhehebu mbalimbali, na fatwa za Swahaba na Taabi’iyn, hadi kufikia kwamba pale suala la fatwa linapokuwa haliendani sambamba na maoni ya madhehebu, basi yeye anaegemeza fatwa yake katika maoni ambayo yanakubaliwa kwa ushahidi ulio mzito. Amekithirisha elimu ya lugha ya Kiarabu, na kusoma masuala katika kiwango cha fikra na hoja. Amesoma maoni ya wanafilosofa na kuzipinga hoja zao na kuweka bayana makosa yao na kuwaonya dhidi yao. Ameichukua Sunnah kwa ushahidhi na uthibiti ulio na nguvu. Alidhuriwa kwa ajili ya Allaah na wapinzani wake na kuchunguzwa kwa kukubali kwake Sunnah iliyo safi, hadi pale Allaah Alipomsababishia kuwa bora na kuwafanya waongofu kuungana katika kumpenda yeye na kumuombea du’aa, na kuwakomesha maadui zake na kuwaongoa watu wa makundi na madhehebu mengine kupitia kwake yeye. Allaah Amewafanya wafalme na makamanda kumganda katika kumfuata yeye na kumtii, na ameihuisha Syria – na bila ya shaka Uislamu – kupitia juhudi zake, pale ilipokaribia kushindwa, kwa kujadiliana na watawala kuwakataa Matartar, pale watu walipokaribisha tashwishi kuhusiana na Allaah na Waumini wakajaribiwa na kutikisika kwa mtikisiko mkubwa (rudia al-Ahzaab 33: 10-11) na wanafiki wakawa na nguvu.

 

Sifa zake nzuri ni nyingi, na yeye ni mtu mkubwa kwa mtu kama mimi kuzungumzia maisha yake. Iwapo mimi nitaahidi kula kiapo baina ya Pembe na Maqaam nitaapa kwamba sijapata kuona mtu mfano wake yeye, na kwamba yeye hajaona mtu mfano wake yeye mwenyewe.”[8]

 

-Al-Haafidh ‘Imaadud-Diyn al-Waasitwiy (Rahimahu Allaahu) amesema:

“Naapa kwa Allaah, hakujapatapo kuonekana chini ya kipaa cha juu cha mbingu mtu yeyote mfano wa Shaykh wenu Ibn Taymiyyah kwa elimu, matendo mema, tabia, mambo yake, kushikana kwake na Sunnah, ukaribu, kujizuia na kutenda majukumu ya Allaah pale mipaka Yake mitukufu inapovunjwa; alikuwa ni mtu muaminifu kuliko mtu yeyote, mwenye ufahamu mkubwa zaidi wa elimu, mwenye athari zaidi, mwenye umakini zaidi katika kuutetea ukweli, mwenye ukarimu zaidi, mbora zaidi katika kufuata Sunnah ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hatujapatapo kuona yeyote ndani ya wakati wetu anayefafanua mfano wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Sunnah zake katika maneno na matendo kuliko mtu huyu; mwenye moyo wenye kuelewa atashuhudia kwamba hii ni kufuata Sunnah katika namna sahihi ya neno.”[9]

 

-Al-Haafidh Jalaalud-Diyn as-Suyuutwiy (Rahimahu Allaahu) amesema:

“Ibn Taymiyyah, Shaykh, Imaam, ‘Allaamah (Mwanachuoni mkubwa), muhifadhiaji, mpinganiaji, Faqiyh, Mujtahid, Mfasiri bora kabisa, Shaykh wa Uislamu, kiongozi wa ikhlaasw, asiyeshindwa katika wakati wetu, Taqiyud-Diyn Abul-‘Abbaas Ahmad al-Mufti Shihaabud-Diyn ‘Abdul-Haliym, mtoto wa Imaam na Mujtahid Shaykh al-Islaam Majdud-Diyn ‘Abdus-Salaam Ibn ‘Abdillaah Ibn Abil-Qaasim al-Haraaniy.

 

 

Mmoja miongoni mwa alama za watu wakubwa, alizaliwa Rabiy’ al-Awwak 661 AH, na kujifunza kutoka kwa Ibn Abil-Yasaar, Ibn ‘Abdil-Daaim, na baadhi ya wengine.

 

 

Amechukua hamu ya kujifunza Hadiyth, na kusimulia na kuchagua (Ahaadiyth za maana); amekithirisha katika kusoma wasifu wa wasimuliaji, mapungufu katika Ahaadiyth, Fiqh, sayansi ya Uislamu, ‘Ilm al-kalaam na nyanja nyenginezo. Alikuwa ni mtu mwenye kasi ya kusoma, moja kati ya Wanachuoni wahodari wachache, mwenye ikhlaasw na mtu pekee. Ameandika vitabu mia tatu, na alijaribiwa na kuchunguzwa mara chungu nzima. Amekufa mwishoni mwa mwezi wa Dhu’l-Qa’dah mwaka 628 AH. “[10]

 

-Al-Haafidh al-Bazzaar amesema, akiwaandikia wapinzani wa Ibn Taymiyyah:

 

“Hamtapata kuona Mwanachuoni akimpinga yeye (Ibn Taymiyyah), akimzuia yeye, akiwa na hamaki kwake, isipokuwa kwamba alikuwa na uchu zaidi wa hayo katika kuyakusanya mazuri ya dunia, wenye hila na ujanja zaidi katika kuyapata hayo, mwenye shauku zaidi kuliko wote, mwenye hamu ya sifa… na mwenye kufanya mengi kuliko mwengine katika uongo kwenye ulimi wake.”[11]

 

-Al-Haafidh adh-Dhahabiy amesema:

“Ilikuwa inashangaza pale alipotaja juu ya suala ambalo kuna tofauti ya mawazo, na pale alipotoa ushahidi na kuamua wazo lililo na nguvu – na alikuwa na uwezo wa kuitekeleza Ijtihaad kwa sababu ya yeye kutimiza masharti yake. Sijapata kuona mtu aliyekuwa na kasi kuliko yeye ya kurudia Aayah ambayo imegusa lile suala analolifikia maamuzi, wala mtu aliyekuwa na nguvu katika kurudia maandiko na kutaja vyanzo vyake. Sunnah ilikuwa ipo mbele ya macho yake na katika ncha ya ulimi wake kuna misamiati safi na jicho lililo wazi.

Alikuwa ni alama miongoni mwa alama za Allaah katika tafsiyr na kuielezea. Kwa mnasaba wa msingi wa Diyn na elimu ya hitilafu - ya mawazo (katika suala fulani) basi yeye alikuwa hana mpinzani – hii ni pamoja na ukarimu, juhudi na kutotilia maanani matashi ya nafsi.

 

Na labda kanuni zake za kishari’ah katika aina mbalimbali za sayansi zilifikia vitabu (mijalada) mia tatu (300), au zaidi na mara zote alikuwa akizungumzia ukweli kwa ajili ya Allaah, bila ya kujali malalamiko yaliyomfikia.

Yeyote anayeshirikiana naye na kumtambua vyema  atanituhumu kwa kutokuwa na uaminifu kwa upande wake. Yeyoye anayempinga na kupingana naye atanituhumu kwa kupitilisha mambo, na nimekuwa mkosa kwa pande zote – wafuasi wake na wapinzani wake.

 

Alikuwa na ngozi ya rangi nyeupe na nywele nyeusi na ndevu nyeusi pamoja na nywele za jivujivu. Nywele zake zilifikia ndewe za sikio. Macho yake yalikuwa fasaha (kama) ulimi, na alikuwa na kifua kipana na chenye sauti safi pamoja na usomaji wa haraka. Alikuwa ni mwenye kuhamaki mara moja lakini mwenye kuibatilisha kwa subra na kujizuia.

 

Sijaona mfano wake yeye kwa kumuomba (yeye Allaah) na kutaka msaada Kwake Yeye, na kuwa na hisia sana kwa wenziwe. Hata hivyo, siamini kwamba yeye alikuwa ni mkamilifu, isipokuwa ninapingana naye; msimamo mkali na masuala madogo, kwani yeye – ingawa ana elimu pana, juhudi kubwa, na akili nyingi, na kwa mnasaba wa kuisafisha Diyn – alikuwa ni mtu miongoni mwa watu. Anaweza kupitikiwa na umakini na hamaki ndani ya mjadala, na kuwavamia wapinzani wake (kimaneno) hivyo kuotesha uadui ndani ya nyoyo zao dhidi yake.

 

Kama tu angelikuwa mlaini kwa wapinzani wake basi kungelikuwa na makubaliano kwa ajili yake (angekubalika na wote) – kwani hakika Wanachuoni wakubwa wameikubali elimu yake, wamekubali uwezo wake na ukosefu wa makosa, na kukiri kwamba alikuwa ni bahri isiyokuwa na mipaka na hazina isiyokuwa na mfano. Hata hivyo, wamefikia nafasi ya kujisikia na homa dhidi yake… na kila maneno ya mtu yanaweza kuchukuliwa ama kuachwa.

 

Alikuwa akisimamisha Swalaah na kufunga, kuzitukuza Shar’iah kinje na kindani. Alikuwa hatoi fatwa katika namna ya ufahamu mdogo kwani alikuwa na ufahamu mzuri kabisa, wala kwa namna ya ukosefu wa elimu kwani alikuwa ni bahri inayoelea. Wala hakuwa akiichezea Diyn lakini (akiitumia) kufikia katika ushahidi kutoka kwenye Qur-aan, Sunnah na Qiyaas na kuthibitisha na kujadiliana kwa kufuata nyayo za Maimaam waliomtangulia, hivyo alikuwa na malipo iwapo amekosea na malipo mara mbili iwapo amepatia.

 

Aliwahi kuumwa ndani ya Qasri (ambalo amefungiwa humo) akiwa na maradhi mabaya mno hadi alipokufa mnamo usiku wa Jumatatu ya 20 ya mwezi wa Dhul Qa’dah, na wakamswalia katika Msikiti wa Damascus. Na baadaye wengi wakamzungumzia kuhusiana na idadi iliyohudhuria mazishi yake, na idadi ya chini iliyotolewa ni alfu hamsini.”[12]

 

-Adh-Dhahabiy pia amesema:

 “Yeye ni zaidi wa ubora kuliko mfano wangu kuelezea sifa zake. Iwapo nitalazimishwa kuapa (kwa Allaah) katika pembe (ya Ka’bah) na sehemu ya (Maqaam Ibraahiym), nitaapa kwamba sijapata kuona kwa macho yangu mawili mfano wake yeye na kwa Allaah, yeye mwenyewe hajaona mfano wake yeye katika elimu.”[13]

 

- Ibn Hajr al-Asqalaaniy amesema:

“Shaykh wa Mashaykh wetu, al-Haafidh Abu al-Yu’mariy (Ibn Sayyid an-Naas) amesema ndani ya wasifu wake wa Ibn Taymiyyah: ‘Al-Mizzi amenisisitiza kuelezea mawazo yangu kuhusiana na Shaykh al-Islaam Taqiyud-Diyn. Nimemuona kuwa anatokana na wale watu walioipata elimu kubwa ndani ya sayansi kama alivyoipata. Alikuwa akikamilisha kuihifadhi na kuifanyia kazi Sunan na Aathaar. Iwapo atazungumzia kuhusiana na tafsiyr basi ataibeba bendera yake, na iwapo atazungumzia fatwa ndani ya Fiqh basi yeye alielewa mipaka yake. Iwapo atazungumzia kuhusiana na Hadiyth basi alikuwa ni Swahaba wa hiyo elimu na utambuzi wa wasimulizi wake. Iwapo atatoa mhadhara wa Diyn na Madhehebu basi hakuna mwengine anayeonekana kuwa na ufahamu au uangalifu kuliko alivyokuwa yeye, amewapita waliopita kabla yake katika kila sayansi, na wewe hutaona mtu yeyote mfano wake yeye, na macho yake mwenye hayajapata kuona mtu mfano wake yeye mwenyewe.

 

Alikuwa akizungumzia kuhusiana na tafsiyr na idadi kubwa ya watu wakihudhuria mikusanyiko yake, na idadi inayokubalika hurudi (wakiwa wamelewa) kwa utamu wake, bahri iliyojaa hazina. Iliendelea namna hii hadi ugonjwa wa uadui ukaingia (ndani ya nyoyo) za watu wa mji wake. Watu wa kutafuta makosa wakajikusanya pamoja na kutoa mambo ambayo hatokubaliana nayo kwa imani yake, na wakayahifadhi baadhi ya matamko yake kwa mnasaba wa hili. Wakamdumaza kwa sababu ya hili na kumuwekea mitego ambayo wangeliweza kumtangazia kuwa yeye ni mzushi. Walifikiria kwamba ameacha njia yao, na kujitoa kwenye dhehebu lao. Hivyo wakajadiliana naye, na yeye kwa wao, na baadhi yao wakakata mahusiano naye, na yeye (akakata mahusiano) pamoja nao.

 

Kisha akajadiliana na kundi jengine ambao lilikuwa likisifika kama ni Fuqaraa (kundi la Kisufi) ambao walidhani kwamba walikuwa na kila chembe ya maelezo ya ukweli wa ndani na juu ya ukweli wake. Na akawawekea wazi Kanuni hizi…

 

Basi hili likawafikia kundi la mwanzo na wakatafuta msaada kutoka kwa wale waliokata mahusiana naye na kumuwekea uovu dhidi yake. Hivyo wakalichukua suala hili kwa watawala, kila mmoja wao akiwa na maamuzi kwamba alikuwa si Muumini. Na kisha wakatayarisha kikao na kuwahamasisha wajinga kueneza neno hilo miongoni mwa Wanachuoni wakubwa. Na wakachukua hatua za kupeleka suala hilo kwa Mfalme wa Misri na hatimaye yeye (Ibn Taymiyyah) akakamatwa na kuwekwa jela. Na mikusanyiko ikaanzishwa kujadili umwagaji wa damu yake, wakiwaita kwa mnasaba wa hili watu kutoka kwenye Misikiti midogo na wanafunzi – wale watu ambao hujadiliana kwa lengo la kuwafanya wengine kuwa na furaha, na wapo wale wengine wenye kujadiliana kuonesha uwerevu wao, na wapo wengine waliotangaza takfiyr na kutangaza kutojumuika (naye). Na Rabb Wako Anajua nini kipo ndani ya vifua vyao na yale waliyoyazusha. Na yule ambaye ametangazia kufr alikuwa sio bora kuliko yule anayejadiliana kuwafurahisha wengine.

 

Na mwiba wa hila zao ukampata, na Allaah Akastawisha kila hila, na kumuokoa katika mikono ya wale Aliowachagua…

 

Basi akaendelea kuhama kutoka mtihani mmoja kwenye mtihani mwengine na katika maisha yake yote hakuondokana na tatizo moja isipokuwa kwenda kwenye tatizo jengine. Kisha ikafuatia lile lililofuatia katika suala la kukamatwa kwake na akabakia kifungoni hadi kifo chake, na kwa Allaah ni marejeo ya masuala yote. Katika siku ya maziko yake mitaa ilifurika watu, na Waislamu wakaja kutoka kila njia ya barabara…”[14]

 

-Ibn Hajr al-Asqalaaniy pia amesema:

“Nimesoma katika maandishi ya al-Haafidh Salaahud-Diyn al-Balaa’iy kwa kukubaliana na Shaykh wa Mashaykh wetu al-Haafidh Bahaaud-Diyn ‘Abdullaah bin Muhammad bin Khaliyl: ‘Shaykh wetu na mtaalamu na Imaam katika masuala ambayo ni baina ya Allaah na sisi, Shaykh wa utafiti (tahqiyq), mkanushaji (wa uzushi), pamoja na wale wanaomfuata yeye, katika njia bora. Mwenye sifa bora na thabati bora ambazo mataifa yote yaliyoridhia ni zaidi ya kuweza kuhesabika. Tunamuomba Allaah Atunufaishe sisi kutokana na yeye ndani ya maisha haya na Akhera. Huyo ndiye Shaykh, Imaam, ‘Aalim anayeelewa mambo, mwenye kujitolea sana, bahri (ya elimu), kiungo cha mwangaza, Imaam wa Maimaam, Baraka kwa taifa la Waislamu, alama kwa Wanachuoni, mrithi wa Rusuli, Mujtahid wa mwisho, ana sifa pekee miongoni mwa Wanachuoni wa Diyn – Shaykh al-Islaam, ushahidi wa Wanachuoni, mfano wa viumbe, ushahidi wa wasomi, mfutaji wa Wanachuoni, panga la wazozaji, bahri ya elimu, hazina yenye manufaa, mfasiri wa Qur-aan, maajabu kwa wakati wetu, mwenye sifa pekee katika enzi hizi na nyenginezo. Hakika Taqiyud-Diyn (Ibn Taymiyyah) ni Imaam wa Waislamu, ushahidi wa Allaah dhidi ya uumbwaji, muunganishi wa mema, ni mtu ambaye ni mfano wa waliomtangulia, mufti wa dhehebu, msaidizi wa ukweli, alama ya uongofu, nguzo ya Huffaadh, Bwana wa maana ya maneno, pembe ya Shari’ah, muanzilishi wa sayansi mpya, Abu al-Abbaas Ibn Taymiyyah.”[15]

 

Ibn Hajr pia amesema:

“... Ile misimamo yake ambayo imekataliwa kutokana naye haikusemwa kwa sababu ya matakwa yake na utashi wake tu na wala hakuwa ni mwenye kuendelea nayo na kung’ang’ania nayo baada ya kupatiwa ushahidi unaoonesha dhidi yake. Zifuatazo ni kazi zake zikiwa zimejaa na pingamizi kutoka kwa wale wanaosimamia tajsiyim ingawa yeye ni mtu mwenye kufanya makosa na pia ni mwenye kupata. Hivyo, kwa yale ambayo amepatia – na hayo ndio mengi – yapatiwe manufaa na Rehma za Allaah ziombwe kwa ajili yake kwa sababu ya hilo, na kwa yale ambayo hakuwa sahihi yafuatwe kwa upofu. Kwa hakika, amesamehewa kwa makosa yake kwa sababu yeye ni moja wa Maimaam wa wakati wake na imeshuhudiwa kwamba amekamilisha masharti ya Ijtihaad...

 

Miongoni mwa sifa za kustaajabisha za mtu huyu ni kwamba alikuwa miongoni mwa mtu mwenye nguvu kabisa dhidi ya Watu wa Uzushi, Rawaafidhah, na Huluuliyyah, na Ittihaadiyyah, na kazi zake katika hili ni nyingi na ni maarufu, na fataawaa zake katika hayo hazina hesabu, je namna gani yale macho ya wazushi yalivyokuwa na furaha pale yaliposikia wale walipomtangazia kuwa yeye ni kafiri! Na ni kwa shangwe gani wamekuwa walipoona wale wasiomtambua yeye kuwa ni kafiri wao wenyewe wakabandikwa jina la ukafiri! Ni wajibu kwa yule ambaye amejivalisha joho la elimu na kuwa na ufahamu kwamba, ayakadirie maneno ya mtu yaliyoegemezwa na vitabu vyake maarufu au kutoka kwa ndimi za wale waliomuamini kufikisha maneno yake kwa usahihi – kisha kujitenga nayo yote haya kwa yale yaliyokanwa na kuwatahadharisha wao kwa lengo la kutoa ushauri wa ukweli na kumsifia kutokana na sifa zake bora na kwa yale aliyokuwa sahihi kama ilivyo njia ya Wanachuoni.

 

Iwapo hakuna sifa zozote za Shaykh Taqiyud-Diyn isipokuwa kwa mwanafunzi wake maarufu Shaykh Shams ad-Diyn Ibn al-Qayyim al-Jawziyyah, mwandishi wa kazi nyingi, ambazo kutoka kwa pande zote za wapinzani wake na wafuasi wake wamenufaika nazo, basi inatosha hili kuonesha nafasi yake (Ibn Taymiyyah) kubwa kabisa. Na kwa nini iwe vyenginevyo kwa kuwa Maimaam wa Kishaafi’y na wengineo, bila ya kuwazungumzima Mahanbaliy, kwa wakati wake kuthibitisha kutokana na umashuhuri katika sayansi (za Kiislamu)...”[16]

 

-Ibn Kathiyr amesema:

 

 “Jambo dogo ambalo anaweza kulifanya pale anaposikia kitu ni kukihifadhi na kisha kuwa na mshughuliko wa kukisoma. Alikuwa na ufahamu na alijifunga kuhifadhi sana na hivyo, akawa ni Imaam katika tafsiyr na kilichofungamana nayo. Alikuwa na elimu (kubwa) katika Fiqh; ilisemwa kwamba alikuwa na elimu zaidi ya Fiqh katika madh-hab kuliko wafuasi wake wa yale madh-hab wanayoyafuata katika wakati wake na wakati mwengine. Alikuwa na fahamu tosha ya mawazo tofauti ya Wanachuoni. Alikuwa ni Mwanachuoni wa Uswuul, matawi ya Diyn, sarufi, lugha na sayansi nyengine za maandiko na ufahamu. Hakupatapo kuchukuliwa katika kikao na hakuna Mwanachuoni maarufu kuzungumza naye katika sayansi fulani isipokuwa kwamba kuona kwamba sayansi hii ilikuwa ni elimu maalumu (takhasus) ya Ibn Taymiyyah na humuona yeye kama ni mwenye maarifa ya kutosha katika hilo na kuipambisha... Ama kwa Hadiyth basi alikuwa ni mbebaji wa bendera yake, muhifadhi wa Hadiyth, na mwenye uwezo wa kupambanua jepesi kutokana na zito, akiwa na maelezo kamili ya wapokezi na kuwa ni mtaalamu katika hili...”[17]

Pia amesema,

“Alikuwa, Rehema za Allaah ziwe juu yake, kutoka katika Wanachuoni wakubwa kabisa, pia kutoka kwa wale wenye kufanya makosa na kupatia. Hata hivyo, makosa yake kwa mnasaba wa zile hukumu zilizo sahihi ilikuwa ni kama vile tone katika bahari kubwa na hayo (makosa) yanasamehewa kama ilivyosimuliwa kwa usahihi na [al-Bukhaariy], “pale Kiongozi anapotoa hukumu, na yupo sahihi basi anapatiwa malipo mara mbili, na iwapo atakosea basi analipwa moja.’”

 

Pia ameelezea kwamba pale Wanachuoni wa wakati wake wanapokusanyika kwa kikao pamoja na Ibn Taymiyyah kwa ajili ya kujadili kazi yake Aqiydah al-Hamawiyyah’ kwamba majibu yake kwa madai yao hayawezi kukanushwa.[18]

Vivyo hivyo ametaja kwamba pale Wanachuoni wanapokaa kujadiliana naye kwa mnasaba wa ‘Aqiydah al-Waasitiyyah yake, mjadala humalizikia kwa wao kukubaliana na yote yaliyokuwemo ndani ya kitabu hicho kama ilivyo ndani ya kitabu cha (Mjalada) 14 cha al-Bidaayah’ chini ya mada ya ‘Aqd al-Majaalis ath-Thalaathah.’

 

-Al-Haafidh al-Mizzi amesema:

“Sijaona mfano wake yeye, na jicho lake mwenyewe halijapata kuona mfano wake yeye. Na sijapata kuona mtu mwenye ufahamu zaidi yake yeye katika Kitabu na Sunnah ya Rasuli Wake, au yule mwenye kuzifuata hizo kwa ukaribu zaidi.”[19]

 

-Al-Haafidh Ibn Daqiyq al-‘Iyd amesema:

“Pale nilipokutana na Ibn Taymiyyah, niliona mtu akiwa na sayansi zote mbele ya macho yake, alichukua kutokana na sayansi hizo chochote anachopenda na kuacha chochote akipendacho.” [20] Baada ya hili akasema, “Naapa kwa Allaah sijafikiria kama yupo aliyebakia mfano wako wewe.” [21]

 

- Qaadhiy wa Qaadiys Ibn al-Huriyriy amesema:

“Iwapo Ibn Taymiyyah alikuwa si Shaykh al-Islaam basi yeye ni nani?”[22]

 

-Al-Haafidh al-Bazzaar amesema:

“Sikupatapo kumuona akitaja anasa na vivutio vya dunia hii, hakujichimbia katika mijadala ya kidunia na wala hakupatapo kuulizia aina yoyote ya makaazi yake. Isipokuwa aliipeleka akili na mijadala yake katika kuitafuta Aakhirah na lile ambalo litamuweka karibu na Allaah.”[23]

 

-Al-Shaykh Mullaa ‘Aliy al-Qaariy amesema:

 “Itaonekana wazi kwa yule anayesoma ‘Madaarij as-Saalikiyn’ (cha Ibn al-Qayyim) kwamba hawa wawili (Ibn Taymiyyah na Ibn al-Qayyimj) ni wakubwa katika Ahlus Sunnah wal Jamaa`ah, na ni Awliyaa wa taifa hili.” [24]

 

-Muhammad bin ‘Abdil-Barr as-Subkiy amesema:

“Naapa kwa Allaah, hakuna mtu anayemchukia Ibn Taymiyyah isipokuwa kwa mtu mjinga au mwenye kubeba matamanio ambayo yamemgeuza kutoka katika ukweli baada ya kuutambua (ukweli).”[25]

 

-Abu Hayyan al-Andalusiy amesema:

“Naapa kwa Allaah, macho yangu mawili hayajapata kuona mfano wa Ibn Taymiyyah.”[26]

 

-Al-Haafidh ‘Abdur-Rahmaan Ibn Rajab al-Hanbaliy amesema:

“Yeye ni Imaam, Mwanashari’ah, Mujtahid, Mwanachuoni wa Hadiyth, Haafidh, Mfafanuzi wa Qur-aan, Mpwekeshaji, Taqiyud-Diyn Abu al-‘Abbaas Shaykh al-Islaam, mwenye ufahamu bora katika wenye ufahamu bora, haiwezekani kukithirisha umaarufu wake pale anapotajwa... yeye, Rehma za Allaah ziwe juu yake, alikuwa na sifa pekee katika wakati wake kwa mnasaba wa ufahamu wa Qur-aan na elimu ya ukweli wa imani.”[27]

 

-Imaam wa Hanafi, Badrud-Diyn (Mahmuud bin Ahmad) al-‘Ainiy amesema:

 

“Yeyote anayesema kwamba Ibn Taymiyyah ni kafiri basi ukweli ni kwamba yeye mwenyewe ni kafiri, na yule anayemtuhumu kwa upotofu basi yeye mwenyewe ni mpotofu. Itawezekanaje kuwa hili (ni ukweli) wakati kazi zake zinapatikana kwa mapana na hakuna alama ya kuonesha upotofu wala fitnah zilizokuwemo ndani ya kazi hizo.”[28]

 

Pia amesema:

"Yeye ni Imaam, muongofu, mtaalamu, mcha Mungu, msafi, mwenye kujitolea, mtaalamu katika sayansi ya Hadiyth na tafsiyr, Fiqh na misingi miwili (yaani Kitabu na Sunnah) pamoja na ukali wa akili na umakini. Yeye ni upanga ulio mkali dhidi ya wazushi, mtawala, aliyeanzisha mambo ya Diyn na kamanda mkuu wa mema na mkatazaji wa maovu. Alikuwa na (ustaarabu wa) hisia, ushupavu na kuendeleza lile ambalo linatisha na kukatisha tamaa. Alikuwa ni mwenye kufanya dhikr sana, kufunga, kuswali na kuabudu.” [29]

 

-Shaykh Kamaal ad-Diyn Ibn az-Zamlakaaniy, ambaye alihojiana naye Ibn Taymiyyah, katika kikao zaidi ya kimoja, amesema:

“Popote anapoulizwa kuhusiana na nyanja fulani ya elimu, yule anayeshuhudia na kusikia (jibu hilo) huhitimisha kwamba hakuwa na elimu nyengine yoyote katika nyanja nyengine na kwamba hakuna mwengine mwenye kuwa na elimu kama hiyo. Wanachuoni wa makundi yote, popote wanapokaa pamoja naye, hunufaika naye kwa mnasaba wa fikra za madhehebu yao katika maeneo ambayo hapo kabla hawakuwa ni wenye kuyafahamu. Haifahamiki kwamba alikuwa ni mwenye kujadiliana na yeyote ambapo mjadala hufikia kusimama au kwamba chochote anachozungumzia katika eneo fulani ya elimu – iwapo inahusiana na sayansi ya Shar’iah au nyengineyo – basi kwa hapo hawatong’ara kwa wataalamu wa eneo hilo na wale wanaoungana nayo.”[30]

 

Pia amesema: “Masharti ya Ijtihaad yalijumuika ndani yake katika namna ambayo ilitakiwa, alikuwa na uwezo mkubwa wa kuandika vizuri kabisa na kufanya vyema kabisa katika kutamka, kupanga, kugawanya na kuelezea.”[31]

 

-As-Suyuutwiy ananukuu kutoka kwa az-Zamlakaaniy ambaye amesema:

“Mtaalamu wetu, Shaykh wetu, Imaam, Mwanachuoni, Mpekee (wa aina yake), Haafidh, Mujtahid, Mwenye Ikhlaasw, Mwenye kuabudu (‘Aabid), Mfano, Imaam wa Imaam, mfano wa Taifa, alama ya Wanachuoni, mrithi wa Mitume, Mujtahid wa Mwisho, Mwanachuoni pekee wa Diyn, Barka kwa Uislamu, Hoja ya Wanachuoni, Hoja ya Mutakallimiyn, muharibifu wa wazushi, mwenye kuikamata na kuing’arisha sayansi ya maajabu kabisa, mwenye Kuihuisha Sunnah. Ni yule ambaye Allaah Amemfadhilisha juu yetu, na kujenga ushahidi dhidi ya maadui Zake... naye ni Taqiyud-Diyn Ibn Taymiyyah...”

 

-Kisha as-Suyuutwiy anafuatizishia hili kwa kusema:

“Nimenukuu wasifu huu kutoka kwa maandiko ya ‘Allaamah, mtu aliyekuwa na sifa za kipekee katika enzi zake, Shaykh Kamaal ad-Diyn az-Zamlakaaniy, Rehma za Allaah ziwe juu yake, ambaye alikuwa ni mwenye kusema, ‘yule ambaye amehifadhi zaidi kuliko yeye hakupata kuonekana katika miaka mia tano iliyopita.” [32]

 

-As-Suyuutwiy amesema katika hali ya kuujadili wasifu wake:

“Shaykh al-Islaam, Haafidh, Faqiyh, Mujtahid, Mufassir wa kipekee, adimu kwa wakati wake, Mwanachuoni mwenye Ikhlaasw” [33] 

 

Tuna uwezo wa kutaja Wanachuoni wengi zaidi ambao walimsifu, lakini in shaa Allaah kwa yale tuliyoweza kunukuu hapo juu yanatosha kuipaka rangi picha ya Imaam huyu kwa uadilifu na ukweli. Ama kwa wale Wanachuoni ambao wametumia jina la ‘Shaykh al-Islaam’ kwake yeye, basi wapo wengi na inahitaji vitabu vingine kuwaorodhesha. [34]

 

 

 

 

 

 

 

 

 

[2] Al-Bukhaariy na Muslim

[3] (Imesemwa na kuandikwa na Ahmad Ibn ‘Aliy Ibn Muhammad Ibn Hajar ash-Shafi’iy, Allaah Amsamehe, siku ya Ijumaa ya mwezi 9 wa Rabiy’ al-Awwal, mwaka 835H. Shukrani zote ni za Allaah, na tunamuomba Allaah amtumie Swala na salamu juu ya Rasuli wake Muhammad na familia yake.) Al-Radd al-Waafir cha Imaam Ibn Naaswirid-Diyn ad-Dimashqiy (uk. 145, 146), al-Haafidh al-Sakhaawiy – mwanafunzi wa Ibn Hajar – amenukuu maneno ya Shaykh wake ndani ya kitabu chake cha al-Jawaahir wad-Durar (2/734-736). 

[4] Al-Haafidh Ibn Hajar al-‘Asqalaaniy ni Imaamu maarufu aliyefariki mnamo mwaka 852H; ambaye ni mwandishi wa vitabu vyenye manufaa kama vile Fat-h al-Baariy Sharh Swahiyh al-Bukhaariy, al-Talkhiys al-Habiyr, Tahdhiyb at-Tahdhiyb na vinginevyo.

[5] Ad-Durar al-Kaaminah fi A’yaan al-Mi’ah al-Thaaminah (1/168). 

[6] Ad-Durar al-Kaaminah (186-187).

[7] Masuala mengi ambayo Shaykh al-Islaam amekuwa akipingwa, haswa na Ibn Hajar al-Haythamiy, ambaye tumemtaja hapo juu, zinaweza kuelezewa kwamba ni zile ambazo zimeandikwa na Shaykh Nu’maan Khayr ad-Diyn Ibn al-Aluusiy (Rahimahu Allaahu) ndani ya kitabu chake chenye manufaa cha Jala’ al-‘Aynayn fi Muhaakamah al-Ahmadayn, kwa maana ya Ahmad Ibn Taymiyyah na Ahmad Ibn Hajar al-Haythamiy (Rahimahu Allaahu). 

Hili linaweza pia kupatikana ndani ya kitabu cha Da’awa al-Munaawi’iyn li Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah, ambacho ni utafiti wa kisomi uliofanywa na Dr. ‘Abdullaah Ibn Swaalih al-Ghusuun. Angalia pia: Islaam Q&A ya Shaykh Muhammad bin Swaalih al-Munajjid.

 

[8] Dhayl Tabaqaat al-Hanaabilah cha Ibn Rajab al-Hanbaliy (4/390).

[9] Al-‘Uquud al-Durriyyah, uk. 311.

[10] Twabaqaat al-Huffaadh, uk. 516, 517.

[11] Al-A`laam al-‘Aliyyah, uk. 82

[12] Ad-Durar al-Kaaminah’ cha Ibn Hajr al-Asqalaaniy chini ya wasifu wa Ibn Taymiyyah

[13] Ar-Radd al-Waafir, uk. 59 (katika matoleo mengine ipo ukurasa wa 35).

[14] Ad-Durar al-Kaaminah’ cha Ibn Hajr al-Asqalaaniy chini ya wasifu wa Ibn Taymiyyah

[15] Ad-Durar al-Kaaminah’ cha Ibn Hajr al-Asqalaaniy chini ya wasifu wa Ibn Taymiyyah. Kwa kitabu hichi kuchukuliwa kama kilivyo, ni vigumu kufahamu maoni ya Ibn Hajr kuhusiana na Ibn Taymiyyah. Kwani kikubwa alichokifanya ni kukusanya vitu vyote anavyoweza kupata kuhusiana na Shaykh na kisha kuanza kupambanua kwa Wanachuoni wote walioandika dhidi yake, na kumalizia na Wanachuoni wote waliomkubali. Inaonesha kwamba msimamo wa Ibn Hajr unaendana na wale aliomaliza nao katika wasifu wake, kwa sababu ya wao kuwa ni Mashaykh wake. Hoja hii inakubaliwa na nukuu inayofuatia kutoka kwa Ibn Hajr. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

[16] Kutoka ridhaa ya Ibn Hajr katika ‘Radd al-Waafir’ iliyopo mwisho wa kitabu.

[17] Al-Bidaayah wan Nihaayah, Ibn Kathiyr (14/118-119)

[18] Al-Bidaayah wan Nihaayah, Ibn Kathiyr (14/5)

[19]  Hayaat Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah, Shaykh Bahjah al-Baytaar, uk. 21, na ar-Radd al-Waafir, uk. 59.

[20] Min Mashaahiyr al-Mujaddidayn, Shaykh Swaalih al-Fawzaan, uk. 26.

[21] Al-Bidaayah wan Nihaayah, Ibn Kathiyr (14/27), na Dhail `alaa Twabaqaat al-Hanaabilah, Ibn Rajab (2/392).

[22] Hayaat Shaykh al-Islaam, (uk. 26)

[23] Al-A`laam al-Aliyyah fiy Manaaqib Ibn Taymiyyah, al-Bazzaar, (uk. 52).

[24] Mirqaat al-Mafaatiyh, (8/251-252) ufafanuzi wake kwa Mishkaat al-Maswaabiyh, kama ilivyonukuliwa ndani ya Shubuhaat Ahl al-Fitnah, (uk. 442) cha ‘Abdur-Rahmaan Dimishqiyyah.

[25] Ar-Radd al-Waafir (uk. 95) cha Ibn Naaswirid-Diyn

[26] Ar-Radd al-Waafir, uk. 63.

[27]  Adh-Dhail `alaa Twabaqaat al-Hanaabilah, Ibn Rajab (2/387-392).

[28] Ar-Radd al-Waafir, (uk. 245).

[29] Ar-Radd al-Waafir, uk. 159.

[30] Ar-Radd al-Waafir, uk. 58.

[31] Ar-Radd al-Waafir, uk. 58.

[32] Al-Ashbaah wa an-Nadwhaair an-Nahwiyyah, (3/681), angalia pia ‘Dhail alaa Twabaqaat al-Hanaabilah’ (2/392-393)

[33] Tabaqaat al-Huffaadh, (uk. 516 nam. 1144), na al-Asbaah wa al-Nadhaa’ir, as-Suyuutiy (3/683).

[34] Kama ilivyofanywa na baadhi ya Wanachuoni, miongoni mwao ni Ibn Naasir ad-Diyn ndani ya kitabu kilichotajwa cha ar-Radd al-Waafir.

Share