11-Wasiya Wa Mwisho Wa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kukanusha Wale Wanaoigawa Bid’ah Kwenye Makundi Mawili: Bid’ah Nzuri Na Mbaya

 

Kukanusha Wale Wanaoigawa Bid’ah Kwenye Makundi Mawili: Bid’ah Nzuri Na Mbaya

 

Baadhi wanasema ya kuwa kuna bid’ah nzuri na kuna bid’ah mbaya.[1]

Sema, kama inakuridhisha, “Bidah nzuri na bid’ah mbovu, lakini kumbuka haya: Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

“Kwa uhakika kila bida’ni upotovu, na kila upotovu ni Motoni.”

 

Bid’ah zote; ziwe ni nzuri na au mbaya na zote unazoweza kutaja ziko chini ya “yote/kila”, ambayo ilitajwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ilisimuliwa ya kuwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia,

“Kila bid’ah ni upotevu, hata kama baadhi ya watu watachukulia kuwa ni nzuri.[2]

 

Mtu anaposema huu si wakati wa kukataza bid’ah bali ni bora kupiga vita madhehebu zinazokiuka maadili, hayuko sawa – kutokana na sababu zifuatazo:

 

1.     Kwa kutokataza bid’ah, hawatoeneza tu bali wataziongeza, pamoja na hayo, Sunah nyingi (Sunan) zitafutwa. Hali hii itapelekea kuenea kwa upotofu na makosa, kwa sababu, lazima tukumbuke, kila bid’ah ni upotofu (dhwalaalah).

 

2.     Kila Muislamu anawajibu, kama anaweza, kuzuia na kukataza maovu. Iwapo mtu ataona kitendo kiovu kinafanywa mbele ya macho yake, lazima akikataze, bila kujali udogo wake, ukilinganishwa na maovu makubwa yaliyoenea (yaliyo shamiri) – kama vile Ukomunisti, umasonia (Masonry), na itikadi zote potofu.

 

 

Vivyo hivyo, kuwepo kwa madhehebu zilizopotoka kusiwazuie Wanachuoni kuwakumbusha watu juu ya maonyo ya kutowaasi wazazi, kusema uongo, kula Ribaa na vitendo vyote viovu.

 

3.     Ukosefu wa elimu katika jamii, pamoja na bid’ah kunasababisha na kueneza upotovu wa madhehebu. Lakini Maswahaba ambao walisimamisha jamii kinyume na ile tuliyoielezea, walikuwa baidi  (mbali) na bid’ah, kwa hakika, walianzisha jamii safi, ambayo haikuwa na madhehebu zilizopotoka.[3]

 

4.     Hebu tujaalie kuwa tunaelewa vema imani ya makundi mbali mbali yaliyoparaganyika - je, tutafanya nini baada ya hapo? Jibu, bila shaka, ni kuwa tuna haja ya kufafanua kukengeuka kwao, lakini inatubidi tuwe na maarifa, fiqh na mwongozo. Pamoja na hayo, elimu hiyo lazima iwe sahihi na halisi kwa sababu mihemko na ushupavu havitoshi kukanusha waliokengeuka na waliopotoshwa. Yule anayeifahamu Dini ana uwezo mzuri wa kuchanganua upotofu wa madhehebu zilizopotea, na ana uwezo wa kuwakusanya Waislamu kwa lile lililo sawa, katika Imani, Fiqh na mwenendo mzuri.

 [1] Mmoja anaweza kuunga mkono kauli ya ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyosema: “Ubarikiwe uzushi (bid’ah) huu.” Yeye ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema haya katika masimulizi yalitolewa na ‘Abdur- Rahmaan bin ‘Abdil-Qaariy, ambaye alisema, “Wakati wa usiku mmoja wa Ramadhaan, nilikwenda na ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) Msikitini, ambapo watu walisambaa katika makundi, kila kundi lilikuwa na Waumini chini ya kumi, na watu wengine wakiswali kwa makundi. ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoona hali hiyo, yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Nahisi ya kuwa ingekuwa bora kama ningewakusanya wote wawe na Imaam mmoja.” Kisha alidhamiria kulifanya hilo na aliwakusanya nyuma ya Ubay Bin Ka’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu), ‘Abdur-Rahmaan aliendelea kusema, “Nilipotoka naye usiku mwingine (tuliona kuwa) watu walikuwa wakiswali nyuma ya Imaam mmoja, na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema ‘Uzushi (bid’ah) huu ubarikiwe.”

Alichokusudia ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kusema bid’ah (uzushi) ni maana ya kilugha (isimu) ambayo ina maana ya upya au ugeni, kile ambacho hakikufahamika mwanzo. Yafuatayo ni kiini cha aliyosema mwandishi wa Jami’ Al-‘Uluum Wal-Hikam: Baadhi ya watangulizi wetu watukufu walipopasisha baadhi ya bid’ah (uzushi), ulikuwa uzushi kwa maana ya kilugha (isimu) na si uzushi kwa maana ya Shari’ah. Mfano mmoja wapo ni yale aliyosema ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) usiku wa manane walipokuwa wakiswali katika mwezi wa Ramadhaan: “Bid’ah hii imebarikiwa.”

Alichokusudia Yeye (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni kuwa kitendo kile makhsusi hakikuwahi kufanywa katika utaratibu ule kabla ya wakati ule; hata hivyo, kilikuwa na mzizi katika Shari’ah. Mathalan, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasihi Waislamu wasimame na kuswali Taaraawiyh (tarawehe) katika mwezi wa Ramadhaan. Hata wakati wa uhai wa Mtume, watu walisimama kwa makundi au mmoja mmoja, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe aliwaswalisha Maswahaba Taaraawiyh katika mwezi wa Ramadhaan zaidi ya mara moja. Ni kweli ya kuwa baadaye Mtume alikataa kufanya hivyo, lakini alieleza kwa nini aliacha; alichelea ya kuwa ingefaradhishwa kwao na kuwa wangeshindwa kuidumisha. Kwa kuwa Swalah ya Taaraawiyh ingefaradhishwa tu wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)-baadaye wakati wa Ukhalifah wa ‘Umar –hapakuwa na sababu ya kuogopa alichoogopa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lazima tukumbuke ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru tufuate Sunnah za Makhalifah waongofu, na Swalah ya Taaraawiyh kwa jamaa moja ilikuwa Sunnah ya Khalifah mwongofu, hivyo watu walijumuika kutimiza Sunnah ile wakati wa kipindi cha ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu), ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu), na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Shaykh wetu, Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi) alisema katika Swalaat at-Taaraawiyh (Uk. 43), Kauli ya ‘Umar ‘Bid’ah hii imebarikiwa’, haikukusudiwa bid’ah kwa mujibu wa maana yake katika Shari’ah: kuanzisha jambo katika Dini bila ya kuwa na umuhimu au tukio la mfano wake. Kama inavyofahamika ya kuwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuanzisha jambo jipya, lakini alihuisha zaidi ya Sunnah moja, tunajua kuwa kwa bid’ah alikusudia ile ya maana ya kiisimu: mpya na ngeni ambayo haikujulikana kabla ya kuwepo. Hapana shaka ya kuwa Swalah ya Taaraawiyh nyuma ya Imaam mmoja haikufahamika wala haikufanyika wakati wa Ukhalifah wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na nusu ya Ukhalifah wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa mtazamo huo ni mpya. Lakini kwa maoni inayoafikiana na aliyofanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni Sunnah, si bid’ah, ambayo ndio sababu pekee ilifanya ielezwe kuwa ni nzuri. Na hayo ni maelezo ya Wanachuoni maarufu kuhusu kauli ya ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). ‘Abdul-Wahhaab As-Subkiy, katika Ishraaq Al-Masaabiyh … Alisema ya kuwa Ibn ‘Abdil-Barr alisema, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuanzisha Sunnah hii kwa sababu yeyote nyingine kuliko kuanzishwa Sunnah hii na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe, kwani aliipenda, aliridhishwa nayo, na hakuacha kuitekeleza mara kwa mara kwa sababu yoyote ile zaidi ya kuchelea kufanywa faradhi kwa Ummah wake. Yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mrehemevu kwa ummah wake. ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alijifunza kutoka kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akijua ya kuwa vitendo vya faradhi haviwezi kuongezwa wala kupunguzwa baada ya kifo cha Mtume –alifufua Sunnah ya Mtume inayohusu Swalah ya Taaraawiyh katika mwaka wa 14H, rehema aliyopewa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Allaah na ambayo hakumfunulia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kufanya hivyo, japokuwa, alikuwa kwa ujumla, alikuwa bora na makini zaidi kufanya ‘amali njema kuliko ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). Kila mmoja kati ya wawili hao alikuwa na sifa za kipekee nazo hazikupatikana kwa mwengine. Aidha As-Subkiy alisema, “Kama haikuwa Swahiyh ingekuwa bid’ah kama ‘amali njema zinapopandishwa katika nusu ya Sha’abaan au Ijumaa ya mwanzo ya Rajab, kwa hali yoyote ilikuwa lazima kukana kitendo cha kuwakusanya pamoja kwenye Swalah ya Taaraawiyh.”

 

Katika Fatwa yake, mwanachuoni Ibn Hajr al-Haythamiy alisema, “Kuwaondosha Mayahudi na Wakristo kutoka Ghuba ya Uarabu na kuwapiga Waturuki… Hayakuwa matendo ya bid’ah, japokuwa hayo hayakujiri wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposema, “Bid’ah hii imebarikiwa”, alikuwa na maana ya bid’ah katika maana yake halisi katika lugha ya Kiarabu. Na katika hali hiyo bid’ah inatumika kwa mujibu wa maana ya kilugha (isimu) katika Aayah ifuatayo:

“Sema: Mimi si bid’ah (kiroja, kilichozuka) miongoni mwa Mitume...” (46: 9).

 

Mifano yote iliyopita ni bid’ah katika lugha, na bid’ah kwa wajibu wa maana yake kishari’ah ni upotevu. Kwa hiyo wanazuoni wanaposema kuwa bid’ah nzuri na mbaya, wameigawa bid’ah kwa mujibu wa maana ya asili ya lugha ya Kiarabu. Na wanaposema ya kuwa kila bid’ah ni upotofu, wanakusudia ile ambayo Shari’ah inaipa maana ya bid’ah. Huoni kuwa Maswahaba na Taabi’iyn walipozuia Adhana kwa Swalah ambazo si Swalah tano za kila siku kwa mfano, Swalah za ’Iyd mbili, japokuwa hapana zuio la hilo. Na walichukizwa na Shami’an mbili za kona ya Ka’bah kukumbatiwa na kubusiwa baada ya Sa’ay kati ya Swafaa na Marwaa …Vivyo hivyo, kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijitenga kufanya tendo kwa sababu, hivyo kuacha tendo hilo ni Sunnah, na kulitekeleza ni bid’ah. Tuliposema, ‘kwa sababu’ hiyo haihusu kuwaondoa Mayahudi na kuikusanya Qur-aan katika Kitabu kimoja. Aidha, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliacha kuwakusanya watu kwa ajili ya Swalah ya Taaraawiyh kwa sababu, na sababu hiyo ilipotoweka, ilikuwa Swahiyh kwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwajumuisha watu kwa Swalah…”

[2] Hadiyth hii ina Silsilah Swahiyh, kama ilivyotajwa katika Iswlaah al-Masaajid (Uk. 13) kilichoandikwa na Shaykh wetu, Al-Albaaniy (Allaah Amuwie radhi).

[3] Pamoja na hayo, wakati wao, kulikuwa na shirk, ukafiri, uovu na upagani. Hata hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliwaauni Waumini wakapata ushindi, kwa upanga na mkuki vile vile kupitia uthibitisho na ushahidi.

Share