Talaka Ikiwa mume Yuko Mbali Na Mke Muda Mrefu

 

SWALI:

Pili vipi kuhusu mwanamke alieenda safari (Ulaya) na kumuwacha mume wake Afrika kwa muda wa mwaka mmoja, kisha kutokana na mawasiliano kutopatikana mwanamke huyo akaamua kudai talaka, lakini kila akimtafuta huyo mume hapati mawasiliano kabisa, jee suali namna hii huyo mwanamke ameachika?

Na jee mwanamke kama huyo akishauriwa na mwanamume amuoe inajuzu?

Uislam umekuwa ukilitazama jambo hili kwa mwanamme kama kupitia katika ndoa za Mutwa, jee vipi kwa mwanamke akiwa safarini kwa siku nyingi bila ya kupata mawasiliano kwa mume wake, anaweza kuamua kuolewa na mume mwengine?

Natumai masuali yangu yatakuwa yamefahamika na Inshallah Allah atakupeni nguvu kuyajibu kwa hikma kubwa kupitia Qur'an na Hadithi.

Shukran


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Uislamu unaangalia maslahi ya mume na mke wakiwa katika ndoa au ya wanaume na wanawake kwa jumla. Uislamu hautaki mtu yoyote adhuru wengine au adhuriwe yeye. Hivyo, Uislamu haujamruhusu mwanaume kuoa ndoa ya Mut‘ah na hata kupiga ponyeto kumekatazwa. Lakini mwanamme ana nafasi nne katika mas’ala ya ndoa.

Mwanzo ni vyema kwa mwanamme au mwanamke anapowenda safari waelewane na wakaubaliane kabla ya yote ili yasije yakatokea matatizo hayo ya ndoa. Na ni vyema hata kuandikiana jinsi watakavyoendeha maisha yao katika hali hiyo ya kuwa mali na wapiliwako katika maisha – kwa kuwa na mawasiliano, kutumiwa hla mke kwa ajili yamatumizi.

 

Ifahamike kuwa Uislamu una msingi mkuu na mtukufu ambao umewekwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Haifai kudhuru, wala kulipana madhara” (Ibn Maajah na ad-Daraqutniy, na Hadith hii ni Hasan).

 

Uzuri wa ndoa ni kwa mume na mke kufanya bidii kuishi na kusafiri pamoja ikihitajika hivyo ili shida kama hizi zisitokee. Ndio ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu.) akaweka mpango kabambe na madhubuti wa mujahidina kuja kuwazuru wake na familia zao kila baada ya miezi minne ili wasiwadhuru wake zao. Katika hali hiyo ambapo wanandoa wawili wako mbali bila ya mawasiliano inabidi mmoja wao afanye mawasiliano kwa jamaa za mmoja wao wa karibu kujua kinachoendelea na ikiwa bado hapa mawasiliano mbali na kujitahidi kote huku itabidi mke aende kwa kadhi wa sehemu hiyo au Muislamu mwengie anayehusika na mas’ala ya ndoa na talaka katika mji huo. Mwanamke atakuwa bado hajaachika na hivyo hawezi kuolewa na mume mwengine mpaka aombe faskhi nikah (kuifusahi). Na huku ni kutaka kadhi akuachishe kwa sababu ya madhara unayoyapata na kwa hofu ya kuingia katika maasia. Ma-Imaam wametofautiana kwa ule muda ambao mwanamke anaweza kuomba kujifusahi huko. Imam Maalik anasema ni mwaka mmoja na Ahmad anasema miezi 6 kwa sababu ni kipindi ambacho cha juu zaidi ambacho mwanamke anaweza kujizuia na kuwa na subira kwa kutowepo kwa mme. Tabaan hii itatafautiana na uwezo wa mwanamke huyo kujizuilia na uchafu aina yeyote kwa sababu ya kutojua hali ya mumewe. Allaah anasema:



Kisha ni kumweka kwa wema au kumwacha kwa ihsani (2: 229).

Kukaa hivi bila ya kujuana si wema wala ihsani, hivyo kadhi aweza kumwachisha mke na mumewe.

Mwanamke kudai talaka kwa kosa la mume itakuwa ni kumwonea mume kwa sababu hii itakuwa ni kujivua katika ndoa (khul‘) na itabidi arudishe mahari aliyotoa. Hivyo ni vyema aende kwa kadhi atasikiliza kesi hiyo na ataamua nani mkosa. Ikiwa kuna njia ya kuwarudisha tena katika ndoa itakuwa hiyo ni kheri lakini lau haiwezekani basi hapo itabidi ndoa ivunjwe na kadhi. 

 

Na Allaah anajua zaidi.

 

Share