28-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maimaam - Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)  

 

28 -  Subira Za Maimaam - Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)

 

 

 

Imaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) alikuwa mwenye Iymaan yenye nguvu, mwenye umbuji, jasiri, mwenye elimu nyingi na kubwa.

 

Wakati wake watu wakiogopa dola iliyokuwa na nguvu. Kwa ushujaa wake watu wengi wakashikamana naye na mara kwa mara wakimzunguka na kuwa pamoja naye.

 

Muda mrefu aliokuwa akiutumia Ibn Taymiyyah ulikuwa ni kufundisha Misikitini, na kuwafungua watu kuhusu mambo ya Dini na kubainisha Alichohalalisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kile Alichoharamisha na kuilinda Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hata hivyo, maadui wake na washindani wake walimfanyia njama mbalimbali ili wamtege na kumchongea na mtawala wa  Misri na Shaam. Akahamishiwa Misri na akahukumiwa mbele ya ma-Qaadhi na viongozi wakuu wa dola. Alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu sehemu iiitwayo, Qal’ah, kisha akatolewa jela na ukawekwa mjadala baina yake na viongozi wengine katika washindani wake. Katika mjadala ule Ibn Taymiyyah alishinda. Hata hivyo hawakumuacha na wakamhamishia Shaam kisha akarudi Misri kwa mara nyingine na akafungwa ambapo alihamishiwa Alexandria na kufungwa huko kwa muda wa miezi minane.

 

Mitihani iliendelea na kuendelea kuteswa hadi aliporudi Misri ambapo ilitolewa amri ya mfalme Naaswir Muhammad Qalawuwn kuhusu kutohusika kwake na tuhuma iliyoelekezwa kwake, na akapewa haki ya kuwaadhibu washindani wake waliokuwa sababu ya kuteswa kwake. Hata hivyo, Imaam Ibn Taymiyyah aliwasamehe! Na hivi ndivyo ilivyo adabu ya watu karimu.

 

Ibn Taymiyyah alibakia Cairo na kueneza elimu, akifasiri Qur-aan Tukufu na akiwalingania watu na kushikamana na Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha akahamia Damascus baada ya kuwa mbali nayo kwa muda wa miaka saba hivi. Alipokuwa kule alitoa Fatwa katika mas-alah fulani na Sultani akamuamrisha abadilishe rai yake kuhusu mas-alah hayo, lakini hakujali amri ile na akashikilia rai yake na akasema: “Siwezi kuificha elimu.” Wakamkamata na kumfunga kwa muda wa miezi sita. Kisha akatolewa jela na akaendela kutoa Fatwa zinazolingana na mafundisho ya Qur-aan na Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mahasimu wake walichukua fursa ya kumfanyia fitna katika fatwa yake inayohusu kufunga safari ya kwenda kutembelea makaburi ya Manabii na waja wema, kwani Ibn Taymiyyah alikuwa na rai kuwa ziara ile si ya wajibu kwa Waislamu. Akafungwa pamoja na nduguye ambaye alikuwa akimhudumia. Pamoja na hayo, hakuacha kuandika, na wakamkataza kufanya hivyo na ndipo alipofungwa na nduguye aliyekuwa akimhudumia kwa hivyo wakataka kuinyamazisha elimu yake isisikike. Vile vile wakamnyang’anya kalamu na karatasi alizokuwa nazo ili asiendelee kuandika elimu yake na kuenea.

 

Azma yake haikuishia hapo kwa kunyang’anywa vifaa vyake akaamua kubadilisha mbinu na kuanza kutumia kuandikia mkaa katika karatasi zilizotapanyika huku na kule.

 

Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) alifariki mwaka 728 Hijriyyah akiwa mwenye kusubiri, Mujaahid akishughulika na elimu. Jeneza lake lilihudhuriwa na Waislamu wapatao laki tano.

Allaah Amruzuku Jannah ya Al-Firdaws. Aamiyn

 

Kwa faida zaidi kuhusu Historia ya Mwanachuoni huyu, soma kitabu hiki muhimu:

 

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Mwanachuoni Wa Wanachuoni (PDF)

 

 

 

Share