Hufunga Na Kuacha Kuswali Makusudi Ila Ramadhaan

SWALI:

NIMETATIZWA SANA NA FAT'WA YA KWAMBA KILA IBADA INA NGUZO YAKE. NAONA KAMA NI KUCHEZA SHERE. ALLAH SI AMETUAMBIA TUINGIE KATIKA UISLAM WOTE?

 


JIBU:

Shukrani zote anastahiki Allah, Mola  wa walimwengu. Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ali zake na Sahaba zake na watangu wema.

Kwa hakika hili ni swali zuri sana ambalo kila Muislamu anatakiwa azingatie sana. Ni kitu ambacho kinaeleweka na kila Muislamu kuwa kila ‘Ibadah ina masharti na nguzo zake ili ‘Ibadah kama ile iwe ni yenye kusihi. Shahada, Swalah, Zakah, Swawm na Hijjah, kila moja ina nguzo zake. Lakini ni jambo muhimu kuwa tujue ya kwamba lau utaacha ‘Ibadah moja na ufanye nyengine basi kule kukosa kufanya hii moja inavunja ile nyengine. Na ni maadili ya Muislamu kuwa wakati wote anafanya mema na akifanya ovu hujuta, akatubia na kufanya mema.

Katika hilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mche Allah popote ulipo. Na fuatisha jambo baya kwa zuri litalifuta hilo baya” (at-Tirmidhy kutoka kwa Abu Dahrr na Mu‘adh bin Jabal [Radhiya Allaahu ‘anhu]).

Hebu tupige baadhi ya mifano ili tuweze kuelewana vyema zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Amali ya kwanza kuhesabiwa siku ya Kiyama ni Swalah (ya faradhi) ikiwa sawasawa mtu huyo atakuwa amefaulu na lau itakuwa na kasoro basi Allah atauliza kama mja wake ameswali Swalah za Sunnah. Na amali nyengine zitahesabiwa namna hiyo”. Hadithi hii inatuonyesha kuwa amali zote zinategemea Swalah, hivyo ikiwa mtu hakuswali basi hesabu yake itakuwa ni ngumu sana. Na ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Tofauti baina yetu na wao (wasiokuwa Waislamu) ni Swalah”.

Na mtu ikiwa atakuwa anafunga lakini haswali basi funga yake inakuwa haina maana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni wafungaji wangapi ambao hawatakuwa na thawabu yoyote kwa funga zao isipokuwa njaa na kiu na hawatapata chochote kwa kisimamo chao (katika Swalah ya usiku) isipokuwa ukosefu wa usingizi” (an-Nasai, Ibn Maajah na al-Haakim). Na katika ukamilifu huu wa Uislamu na kufungamana baina ya nguzo zake, ndio kilichomfanya Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) apigane na wenye kukataa kutoa Zakah kwa kusema: “Nitapigana na yeyote mwenye kufarikisha baina ya Swalah na Zakah”. Na kwa msimamo huo wa haki Maswahaba wote walikuwa nyuma yake.

Hivyo, ni juu yetu kuingia katika Uislamu wazima wazima bila kubagua baina ya ‘Ibadah ili tupate kufaulu. Allah anasema: “Enyi Mlioamini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za shetani, hakika yeye kwenu nyinyi ni adui aliye wazi” (2: 2008). Hivyo, kuchagua na kufanya baadhi ya ‘Ibadah ni katika kumfuata shetani, nasi inatakiwa tuende kinyume naye ili tupate kufaulu.

Na nguzo za Uislamu ni TANO. Je, Yumkinika nyumba hii iwe imara lau baadhi ya nguzo zitaondolewa? Nyumba hiyo haiwezi kuwa imara kabisa. Na jambo haliingii katika akili kuwa wewe utafanya ‘Ibadah moja kwa kisingizio kuwa umeamrishwa na Allah na kuacha nyingine ambayo tumeagiziwa na Muumba wetu Allah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Nasaha yangu ni kuwa tuwe waangalifu na makini na tutie bidii katika kufanya ‘Ibadah zote kwa uwezo wetu na Allah atatusaidia.

Na Allah Anajua zaidi.

 

 


Share