Mume Haniheshimu Anawadharau Wazazi Wangu Anawatukana Watoto Wangu


 

SWALI:

asalamu aleikum shekh naomba ushauri wako nimejaribu kutaka ushauri kwa watu mbalimbali kutokana na matatizo nilonayo na sasa alhidaaya naamini inaweza kunisaidia kwa uwezo wa Allah nikajaribu kupima nisije nikateleza shekh mimi nikijana wa miaka 25 niliolewa na kijana ambae hatukuelewana nikazaanae watoto 2 Allah akanijaalia kuolewatena kwa kweli sikupenda kuishi mbali na watoto wangu kwa sababu ni wadogo .Baada ya miezi 3 nilimshauri mume wangu nikachukue watoto wangu alikubali tukaishi nao bahati mbaya mume wangu hana uzazi na vilevile mambo hayawezi sasa amebadilika anatukana watoto wangu ,mtoto wa miaka 2 anamuita malaya au mwanaharamu shekh inauma sana mume wangu hanihishimu ingawa mimi namuhishim anawadharau hata wazee wangu sijawahi kumjibu tusi lolote nimewaambia wazee sijapata jibu muafaka kwa kweli sina raha akiwemo ndani mume wangu naomba ushauri wako Ishaallah

 


 

 

JIBU:

 

 

 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunasikitika kuona uko katika hali hiyo na mumeo, jambo ambalo bila ya shaka humfanya mtu awe yuko katika dhiki fulani ya ndoa kama hiyo.

Hatujui sababu khaswa ya kumfanya mumeo awe anafanya hivyo. Ikiwa ni tabia yake tu, basi tunampa nasaha aache tabia hiyo kwani huo si uungwana. Lakini huenda ikawa ni katika kuudhika kwake kutokuweza yeye kuzaa labda ndio humfanya awe na ghadhabu hizo. Hata hivyo Muislamu haimpasi kumdharau mwenzake kabisa kwa aina yoyote na khaswa kudharau wazazi wa mwenziwe mtu au kuwadharau wenzake wowote wengine. Hii hudhihirisha kibri ya mtu na kibri ni dhambi ambayo haimuingizi mtu Peponi, kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

((لا يدخل الجنة من كان في قلبه مثقال ذرة من كبر)) البخاري

((Haingii Peponi yeyote mwenye chembe ndogo cha kibr katika moyo wake)) [Al-Bukhaariy]

 

Kuwatukana watoto wadogo kabisa pia ni jambo ovu kabisa na bila shaka anajichumia mtu dhambi za bure kuwatukana viumbe hao wasiojua kitu wala hawana dhambi zozote.

 

Hivyo tunampa nasaha mumeo aache kuwatukana wazazi wako na watoto wako, na akupe heshima yako kama inavyompasa kwani ndio kutimiza haki za baina ya mke na mume kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

قال رسول الله صلى الله عليه وسلم  عند ما وقف في عرفة في حجة والوداع :(( يآ أيها الناس إن لنسائكم عليكم حقاً ولكم عليهن حق)) أبو داود

 Mtume صلى الله عليه وسلم   alisema aliposimama 'Arafah katika hutuba yake  ya mwisho ya Hajj  ((Enyi watu! Hakika nyinyi mna haki juu ya wake zenu na wake zenu wana haki juu yenu)) [Abu Daawuud]

 

Na katika hikma na faida ya kufunga ndoa ni kupata utulivu na kuoneana huruma na kupeana mapenzi baina ya mke na mume, sasa ikiwa mume hana huruma na mapenzi bila shaka ndoa hiyo itakuwa iko katika hatari kuvunjika. Anasema Allaah سبحانه وتعالى  

((وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَة ًإِنَّ فِي ذَلِكَ لَآ يَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ))

((Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri)). [Ar-Ruum 30:21]

Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema ((Nakuusieni kuwafanyia wema wanawake))  [Al Bukhaariy na Muslim]

 

Vile vile kasema,

((Mbora wenu ni yule aliye mbora  kwa familia yake na mimi ni mbora kabisa kwa familia yangu))   [At-Twabaraniy]

Jambo utakaloweza kufanya wewe labda isaidie, ni kuwa, muulize kwanza mumeo kwa kumuweka kitako wakati yuko katika hali ya furaha, na muulize akuambie mushkila wake na awe muwazi na wewe. Na ikiwa mushkila wake ni watoto, basi jaribu wewe kama unao wazee wako nyumbani na kama watakuwa na uwezo wa kuwalea watoto wako hadi wakuwe wakubwa na wewe uishi na mumeo pekee yenu. Lakini hii ikiwa kama wewe mwenyewe bado una mapenzi na mumeo.

Ama ikiwa huna mapenzi na mume wako na khaswa ikiwa hakutumizii yanayompasa kukutimizia kama kukutimiza haja yako ya matamanio ya kitendo cha ndoa, basi bila shaka hii ndoa haikukamilika na huenda ikakuletea madhara makubwa ya kukupeleka kwengine kuingia katika dhambi. Hivyo  ufikirie kama utaweza kuendelea katika hali hii maisha yako yote. Unavyoonyesha ni bado kijana mwenye umri mdogo, bila shaka hutokosa mume mwengine ambaye atakutimizia mahitajio yako yote pamoja na kuweka heshima yako, ya wazazi wako na watoto wako.

Baada ya kikao na mumeo utaweza kutambua umesimama wapi, na ikibidi unaweza kuwaita wazee wenu wa pande zote mbili kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى

((وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُواْ حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلاَحًا يُوَفِّقِ اللّهُ بَيْنَهُمَا إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا)) 

 ((Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari)) [An-Nisaa: 35]   

 Au vile vile mnaweza kuwaita watu wema kuwatatulia matatizo yenu. Ikiwezekana kutatuliwa matatizo mkarudi kuishi kwa amani ni bora zaidi kuliko kutengana, na ikiwa kila mmoja atachunga na kutimiza haki za mwenzie.

Na ikiwa haikuwezekana kutatua matatizo kutokana na hali ilivyo baina yako na mumeo, basi ndio maana Mola wetu Ametufanyia wepesi wa maisha kwa katuwekea 'talaka' ili tuendelee na maisha yetu katika hali ya kuridhika.

Tunamuomba Allaah Akujaalieni masikilizano mema ili mthibitishe ndoa yenu kwa amani na furaha.   

 Na Allah Anajua zaidi.

 

Share