Kuswali Kabla Ya Wakati

 

SWALI: 

Asalam alaykum.ALLAH  awajaze kheri kwa kufungua website hii mana inatuelimisha sana

Swali langu linahusu sala.je unaweza kusali sala ya ishaa giza linapoingia yaani kabla ya adhana?
 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 Katika shuruti za kuswihi Swalah, moja wapo ni kuingia wakati wake, na wakati wa 'Ishaa ni baada mwanga kupotea  kabisa, kwa hiyo bila ya kuingia wakati wa Swalah, hata kama kiza kimeshaingia, huwezi kuswali hadi uhakikishe kama ni wakati wa 'Ishaa au sivyo Swalah hiyo haitoswihi.

Nyakati za Swalah zote tano ni kama zilivyoelezewa katika Hadiyth ifuatayo:

عن‏ ‏عبد الله بن عمرو ‏أن رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏قال ‏(( ‏وقت الظهر إذا ‏ ‏زالت ‏ ‏الشمس وكان ظل الرجل كطوله ما لم يحضر العصر ووقت العصر ما لم تصفر الشمس ووقت صلاة المغرب ما لم يغب الشفق ووقت صلاة العشاء إلى نصف الليل الأوسط ووقت صلاة الصبح من طلوع الفجر ما لم تطلع الشمس فإذا طلعت الشمس فأمسك عن الصلاة فإنها تطلع بين قرني شيطان))  مسلم  

Imetoka kwa 'Abdullah bin 'Amr رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Wakati wa Dhuhuri unabakia mpaka jua linapopita kilele chake, na kivuli cha mtu kinakuwa ni  sawa na urefu wa mtu  na madamu wakati wa Alasiri bado haukufika. Na wakati wa Alasiri unaendelea kubakia madamu jua halikugeuka kuwa manjano. Na wakati wa Magharibi unabakia madamu rangi nyekundu ingalipo, na wakati wa 'Ishaa unabakia mpaka katikati ya usiku, na wakati wa Alfajiri unaanza baada ya kupambazuka hadi kabla ya jua kuchomoza, acheni kuswali wakati huo kwani jua huchomoza baina ya pembe mbili za shaytwaani)) [Muslim]

Na Anasema Allaah سبحانه وتعالى  

َ(( إِنَّ الصَّلاَةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا))

((Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu)) [An-Nisaa:103]

Ni vizuri kusubiri hadi imalizike Adhaan na uwe unasema kama anavyosema muadhini kisha usome Du'aa yake ujipatie fadhila zake:

Du'aa baada ya Adhaan:

اللّهُـمَّ رَبَّ هَذِهِ الدّعْـوَةِ التّـامَّة وَالصّلاةِ القَـائِمَة آتِ محَـمَّداً الوَسيـلةَ وَالْفَضـيلَة وَابْعَـثْه مَقـامـاً مَحْـمُوداً الَّذي وَعَـدْتَه  

Allaahumma Rabba Haadhihid-Da'awati-taammah Was-Swalaatil-Qaaimah, Aati Muhammadanil-Wasiylata Wal-Fadhwiylah Wab-'ath-hul-Maqaamam-Mahmuudani-lladhi Wa'adtah.

Ee  Allaah, Bwana wa mlingano (mwito) huu Uliotimia, na swala ilio simama, Mpe Mtume Muhammad Wasila, na fadhila, na Mfikishe daraja yenye kusifiwa, ambayo Umemuahidi

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

  

Share