016-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Athari ya Kuelekeza Kwenye Hidaayah Na Upotofu

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 16  

 Athari ya Kuelekeza Kwenye Hidaayah Na Upotofu

www.alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((مَنْ دَعَا إِلَى هُدًى كَانَ لَهُ مِنْ الأَجْرِ مِثْلُ أُجُورِ مَنْ تَبِعَهُ, لاَ يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْئًا, وَمَنْ دَعَا إِلَى ضَلاَلَةٍ كَانَ عَلَيْهِ مِنْ الإِثْمِ مِثْلُ آثَامِ مَنْ تَبِعَهُ لاَ يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ آثَامِهِمْ شَيْئًا)) رواه مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Atakayelingania katika hidaayah, atapata ujira mfano wa aliyemfuata, bila ya kupunguziwa chochote katika ujira wao. Na atakayelingania katika upotofu, atapata dhambi mfano wa dhambi za waliomfuata bila ya kupunguziwa chochote katika dhambi zake)) [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 1. Fadhila za mlinganiyaji ni nyingi mno kwa kufuatwa anayoyalingania, na thawabu zake zinazidi hata baada ya kufariki kwake kwa kila atakayefuata. Rejea Hadiyth namba (54), (76), (77), (78), (80).

 

 

2. Ulinganiaji Dini ni katika mema yatakayoendelea baada ya kufariki kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ أَمَلًا ﴿٤٦﴾

  Mali na watoto ni pambo la uhai wa dunia. Na mema yanayobakia ni bora mbele ya Rabb wako, kwa thawabu na matumaini.   [Al-Kahf  (18: 46)]

 

 

Rejea pia: Maryam  (19: 76).

 

 

3. Fadhila za elimu na da’wah, nazo hazipatikani ila kwa kuwa na elimu ya Dini, na si kwa kufuata watu au matamanio. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٨﴾

  Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya nuru za elimu na umaizi, mimi na anayenifuata.  [Yuwsuf (12: 108)]

 

 

 

4. Umuhimu wa kujifunza elimu sahihi, la sivyo kuna hatari nyingine, nayo ni kujitayarishia makazi ya motoni. Rejea Hadiyth namba (76).

 

 

5. Mlinganiyaji mema au maovu na mtendaji wake, watapata malipo sawasawa, mazuri au mabaya.

 

 

6. Mlinganiyaji atahadhari anayoyalingania, kwani akilinganiya maovu ataacha athari nyuma yake na atabeba dhambi zake na kila atakayemfuata. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ ﴿١٢﴾

Hakika Sisi Tunahuisha wafu, na Tunaandika yale waliyoyakadimisha na athari zao na kila kitu Tumekirekodi barabara katika daftari bayana. [Yaasiyn: 12]

 

 

 Na pia Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۙ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ﴿٢٥﴾

Ili wabebe mizigo (ya madhambi) yao kamili Siku ya Qiyaamah, na mizigo ya wale waliowapoteza bila ya elimu. Tanabahi!  Uovu ulioje wanayoyabeba. [An-Nahl (16: 25).]

 

 

7. Muislamu atahadhari kufuata mafunzo ya ubatili na ajiepushe na wabatilifu wanaopotosha watu katika Dini.

 

 

8. Rusuli walipowalinganiya watu wao wasimshirikishe Allaah (سبحانه وتعالى) jibu la wengi wao lilikuwa kwamba wamewafuata mababa zao. Na hali imekuwa ni hivihivi kwa walio wakaidi katika jamii pindi mtu anaponasihiwa ache upotofu na uzushi. Rejea: Al-Baqarah (2: 170), Al-Maaidah (5: 104), As-Swaaffaat (37: 69-70), Az-Zukhruf (43: 22-23).

 

 

Share