025-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Wanyonge Na Masikini Watakuwa Jannah, Ama Wababe Wajeuri Na Wenye Kiburi Watakuwa Motoni

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 25

Wanyonge Na Masikini Watakuwa Jannah,

Ama Wababe Wajeuri Na Wenye Kiburi Watakuwa Motoni

www.alhidaaya.com

 

 

 

 

 

 

 عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((احْتَجَّتْ الْجَنَّةُ وَالنَّارُ فَقَالَتْ النَّارُ: فِيَّ الْجَبَّارُونَ وَالْمُتَكَبِّرُونَ.  وَقَالَتْ الْجَنَّةُ: فِيَّ ضُعَفَاءُ النَّاسِ وَمَسَاكِينُهُمْ: فَقَضَى الله بَيْنَهُمَا: إِنَّكِ الْجَنَّةُ رَحْمَتِي أَرْحَمُ بِكِ مَنْ أَشَاءُ.  وَإِنَّكِ النَّارُ عَذَابِي أُعَذِّبُ بِكِ مَنْ أَشَاءُ.  وَلِكِلَاكُمَا عَلَيَّ مِلْؤُهَا)) رواه مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy(رضي الله عنه)  amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Jannah na moto zilihojiana. Moto ukasema: Kwangu kunapatikana wababe wajeuri na wenye kiburi.  Jannah ikasema: Kwangu kunapatikana watu madhaifu na masikini wao.  Allaah Akahukumu baina yao (Akisema): Wewe Jannah ni Rahma Yangu, Nitamrehemu kwa sababu yako Nimtakaye. Na wewe moto ni adhabu Yangu, Nitamwadhibu Nimtakaye kwa sababu yako, na nyote Nitawajaza)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Allaah (سبحانه وتعالى) Anawaacha watu wawe huru kutenda wayatakayo baada ya kuwaonyesha njia ya haki na ya ubatilifu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٢﴾ إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا ﴿٣﴾

 

Hakika Sisi Tumemuumba bin-Aadam kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili Tumjaribu; Tukamjaalia mwenye kusikia na kuona. Hakika Sisi Tumemuongoza njia; ima awe mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.   [Al-Insaan (67: 2-3)]

 

Rejea pia: Al-Balad (90: 8-10).

 

 

2. Hikma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuwajaalia baadhi ya watu kuwa ni masikini, wanyonge na wengineo kuwa ni matajiri wenye nguvu.

 

Rejea: An-Nahl (16: 71).  

 

Hata Manabii wamefadhilishwa wengine juu ya wengine kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ ۚ وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ ۗ

Hao ni Rusuli, Tumewafadhilisha baadhi yao juu ya baadhi. Miongoni mwao kuna aliyesemeshwa na Allaah, na Akawapandisha baadhi yao vyeo. Na Tukampa ‘Iysaa mwana wa Maryam hoja bayana na Tukamtia nguvu kwa Ruwhil-Qudus (Jibriyl (عليه السلام.   [Al-Baqarah 2: 253].

 

 

 

3. Ujuzi wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba baadhi ya waja Wake watakuwa ni wema japokuwa wao ni dhaifu, maskini na wanyonge, na hivyo hatima yao itakuwa ni kuingia Jannah. Na wengineo watakuwa wenye kutakabari na wababe wajeuri juu ya kuwa ni matajiri, hivyo hatima yao itakuwa ni kuingia motoni.   [Hadiyth: ((Wataingia Jannah Waislamu masikini kabla ya matajiri wao kwa nusu siku ambayo ni miaka 500)). [Swahiyh At-Tirmidhiy ya Al-Albaaniy]

 

 

4. Bishara njema ya Jannah kwa walio wanyonge duniani, na tisho la moto kwa wenye kutakabari na wababe wajeuri.

Rejea Hadiyth namba (55), (59), 60).

 

 

5. Hadiyth hii inatufunza kuwa kufaulu Aakhirah hakutegemei uwezo wa kifedha hapa duniani.

 

Share