045-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Mambo Manne Atakayoulizwa Mja Siku Ya Qiyaamah: Umri, Elimu, Mali na Mwili

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 45

Mambo Manne Atakayoulizwa Mja Siku Ya Qiyaamah:

Umri, Elimu, Mali na Mwili

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَبِي بَرْزَةَ الأَسْلَمِيِّ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لاَ تَزُولُ قَدَمَا عَبْدٍ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حَتَّى يُسْأَلَ عَنْ عُمُرِهِ فِيمَا أَفْنَاهُ، وَعَنْ عِلْمِهِ فِيمَ فَعَلَ، وَعَنْ مَالِهِ مِنْ أَيْنَ اكْتَسَبَهُ وَفِيمَ أَنْفَقَهُ وَعَنْ جِسْمِهِ فِيمَ أَبْلاَهُ))  رواه الترمذي وقال: حديث حسن  صحيح

 

Kutoka kwa Abuu Barzah Al-Aslamiyy (رضي الله عنه)  ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Nyayo za mja hazitoondoka [Siku ya Qiyaamah] mpaka aulizwe juu ya umri wake alivyoumaliza, elimu yake alivyoifanyia, mali yake ameichuma kutoka wapi na ameitumia kwa mambo gani, na mwili wake aliutumia kwa kazi gani)). [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Hima ya Muislamu kutumia umri wake katika yale yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

2. Mambo manne hayo ni miongoni mwa neema nyingi za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa mja, anapaswa kushukuru kwa yakini, kauli na vitendo, na ataulizwa kuhusu neema hizo kama Anavyosema:

 

ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ ﴿٨﴾

Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu kuhusu neema. [At-Takaathur: 8]

 

 

3. Himizo la kuchuma mali kutoka njia za halali na kuitumia katika yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى) pamoja na kuitolea Zakaah na sadaka na tahadharisho la chumo la haramu. [Rejea: Al-Baqarah (2: 168), Twaahaa (20: 81].

 

 

4. Kuuhifadhi mwili usitende yaliyo haramu na kuutiisha pamoja na kuutumikia katika utiifu wa Allaah (سبحانه وتعالى), na kufanya ‘Ibaadah kwa wingi.

 

 

5. Kujifunza elimu iliyo na manufaa na aifanyie kazi kwa ikhlaasw anufaike nayo na anufaishe wengineo.

 

 

6. Tanabahisho kwa Muislamu kuwa na ikhlaasw katika ‘amali azitendazo.  Rejea: [Al-Kahf : 110].

 

 

7. Mambo manne hayo ni majukumu ya kila mtu Siku ya Qiyaamah. Hakuna atakayeondoka mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) bila kuulizwa.

 

 

8. Hadiyth hii ni tahadharisho la kujirekebisha, kwa mtu anayekwenda kinyume na yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

9. Uhai na maisha ya dunia ni kama madrasa anayosoma mtu na kufanya juhudi, kisha mtihani wake na malipo ni Siku ya Qiyaamah. Atakayefanya kinyume chake, atapata khasara huko Aakhirah ambako kwenye maisha ya milele.  Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 مَّن كَانَ يُرِيدُ الْعَاجِلَةَ عَجَّلْنَا لَهُ فِيهَا مَا نَشَاءُ لِمَن نُّرِيدُ ثُمَّ جَعَلْنَا لَهُ جَهَنَّمَ يَصْلَاهَا مَذْمُومًا مَّدْحُورًا ﴿١٨﴾

Yeyote anayetaka (starehe za dunia) ipitayo upesi upesi Tunamharakizia humo Tuyatakayo, na kwa Tumtakaye. Kisha Tutamjaalia Jahannam aingie na kuungua hali ya kuwa mwenye kushutumiwa kufukuziliwa mbali (na rahmah ya Allaah).

 

 مَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾

Na anayetaka Aakhirah na akaifanyia juhudi inayostahiki kufanyiwa, naye ni Muumin, basi hao juhudi zao ni za kushukuriwa. 

 

كُلًّا نُّمِدُّ هَـٰؤُلَاءِ وَهَـٰؤُلَاءِ مِنْ عَطَاءِ رَبِّكَ ۚ وَمَا كَانَ عَطَاءُ رَبِّكَ مَحْظُورًا ﴿٢٠﴾

Wote hao Tunawakunjulia; hawa na hao katika hiba za Rabb wako. Na hazikuwa hiba za Rabb wako zenye kuzuiliwa. [Al-Israa (17: 18-20)]

 

Na pia Rejea: [Ash-Shuwraa (42: 20)].

 

10. Umuhimu wa kufanya kazi, na mtu achunge sana kazi atakayofanya, kwa sababu chumo la haramu litampeleka mtu pabaya.

 

 

11. Muislamu anatakiwa katika  Shariy’ah achume chumo la halali na alitumie kwa njia za halali.

 

 

12. Katika riwaayah nyengine ya at-Tirmidhiy badala ya mwili inataja ujana umetumiwe vipi, kumaanisha kuwa kipindi hicho ni muhimu sana katika maisha ya mwana Adamu na ni wakati wa kuchuma mema mengi.

 

 

 

 

 

 

Share