00-Swabrun Jamiyl: Utangulizi

 

Swabrun Jamiyl (Subira njema)

 

00-Utangulizi

 

 

 

AlhamduliLLaah, Himdi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu wote, Swalaah na salaam zimfikie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jamaa zake, na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na wote waliotangulia kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Muislamu anahitaji subira katika kila jambo zuri au baya na katika kila hali; kwenye furaha na huzuni, siha na maradhi, utajiri na umasikini, neema na dhiki, utiifu na maasi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ

Na Tutakujaribuni kwa mitihani ya shari na kheri. Na Kwetu mtarejeshwa. [Al-Anbiyaa: 35]

 

Dunia ni nyumba ya mtihani ambako mja atakuwa akigeuzwa kukabili hali zote za kheri na shari na hatima yake ni kuelekea kwenye makazi ya malipo kama Anavosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١﴾

Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni Muweza

 

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ﴿٢﴾ 

Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. [Al-Mulk: 1–2]

 

Kwa hiyo Muislamu hana chaguo ila asubiri katika mitihani ili apate fadhila tele Alizoahidi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au sivyo atakuwa miongoni mwa waliokhasirika kama Alivyohukumu Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  katika Suwratul’Aswr. Pia, Muumini atambue kwamba hakuna mtihani ila Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Humteremshia mja Wake rahmah na kwa kumpa faraja Naye Haendi kinyume na ahadi Zake. Anasema:

 

فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٥﴾

Basi hakika pamoja na kila gumu kuna wepesi.

إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٦﴾

 

Hakika pamoja na kila ugumu kuna wepesi. [Al-Inshiraah: 5–6]

 

 

Tumenukuu visa kadhaa vilothibiti ili viwe ni mafunzo kwetu na viweze kumthibitisha Muislamu anaposibiwa na mitihani. Juu ya hivyo, tuna mifano bora kabisa vya Rusuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  waliokumbana na kila aina ya mitihani, Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akawasifu kwa subira zao:

 

وَإِسْمَاعِيلَ وَإِدْرِيسَ وَذَا الْكِفْلِ ۖ كُلٌّ مِّنَ الصَّابِرِينَ ﴿٨٥﴾

Na Ismaa’iyl na Idriys na Dhal-Kifli, wote ni miongoni mwa wenye kusubiri. [Al-Anbiyaa: 85]

 

Akamsifu Nabiy Ayyuwb:

 

إِنَّا وَجَدْنَاهُ صَابِرًا ۚ نِّعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ ﴿٤٤﴾

Hakika sisi Tulimkuta mwenye subira mno, uzuri ulioje wa mja, hakika yeye ni mwingi wa kurudiarudia kutubia. [Swaad: 44]

 

Na Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُولُو الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُل﴿٣٥﴾ِ

Basi subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kama walivyosubiri wenye azimio madhubuti miongoni mwa Rusuli [Al-Ahqaaf: 35]

 

Hao kama walivyokubaliana Wafasiri baada ya kukhitilafiana kwamba ni Nabiy ‘Ibraahiym, Nuwh, Muwsaa, ‘Iysaa (‘Alayhimus-salaam na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Tunamuomba Allaah ('Azza wa Jalla) Ajaalie kazi hii iwe kwa ajili ya kupata Radhi Zake Pekee na Ajaalie iwe yenye manufaa kwa ndugu zetu wa Kiislamu na tunamuomba Atughufurie na Atusamehe kwa makosa yoyote yatakayokuwemo.

 

 

 Wa-Swalla-Allaahu ‘alaa Muhammadin wa ‘alaa aalihi wa-Swahbihi wa sallam.

 

 

19 Swafar 1433H -  13 Januari 2012M

Imehaririwa: 2  Jumaada Al-Uwlaa 1439H - 19 Januari 2018

 

 

 

 

 
Share