106-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Mwanamke Aliyeadhibiwa Kwa Ajili Ya Kumtesa Paka

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 106

 

Mwanamke Aliyeadhibiwa Kwa Ajili Ya Kumtesa Paka

 

 

 

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((عُذِّبَتْ امْرَأَةٌ فِي هِرَّةٍ حَبَسَتْهَا حَتَّى مَاتَتْ جُوعًا فَدَخَلَتْ فِيهَا النَّارَ، لاَ هِيَ أَطْعَمْتِهَا  وَسَقَيْتِهَا إِذْ هِيَ حَبَسْتِيهَا وَلاَهِيَ تَرَكَتْها تَأكُلُ مِنْ  خَشَاشِ الأرْضِ)) متفق

 

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mwanamke fulani aliadhibiwa kwa sababu ya paka aliyemfungia mpaka akafa kwa njaa, akaingia motoni [kwa sababu] alipomfungia hakumpa chakula wala hakumnywesha maji wala hakumwacha aende akale vidudu ardhini)).  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Tisho kwa wanaotesa wanyama wanaowafuga kwa kuwafungia na kutokuwapa chakula au maji kwamba adhabu yao ni kuingizwa motoni.

 

 

2. Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) ni pana mno hata kwa viumbe Vyake vyote, mpaka wanyama wadogo. Kila kiumbe kapatiwa rizki Yake, kama Anavyosema:

 

 وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا ۚ كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴿٦﴾

 

Na hakuna kiumbe chochote kitembeacho katika ardhi isipokuwa riziki yake iko kwa Allaah; na (Allaah) Anajua mahali pake pa kustakiri na pa kuhifadhiwa kwake. Yote yamo katika Kitabu kinachobainisha. [Huwd (12: 6)]

 

 

3. Kwa hiyo haipasi bin Aadam kumzuilia mnyama chakula chake.

 

 

4. Funzo kwamba wanyama wanapaswa kupewa haki zao kama viumbe vinginevyo.

 

 

5. Bainisho la ruhusa ya kufuga baadhi ya wanyama nyumbani kama paka. 

 

 

6. Muislamu ni lazima awe kielelezo chema katika kuwatendea viumbe wote wema na kuwapatia haki zao kikamilifu.

 

 

 

Share