‘Aqiyqah – Je Ni Lazima Mnyama Achinjwe Nyumba Anayoishi Na Lazima Mtoto Anyolewe Nywele?

SWALI:

Assalam  alaykum..: nina watoto wawili mapacha...wenye umri wa mwaka mmoja...nimewafanyia haqyika kwa kufuata yale yote nikiyopata kuyasoma humu katika toleo la 16 Rajab1435H..lakin nimeingiwa na wasiwasi huwenda sikufanya kama vile inavyo takiwa kwa maana..:
1:sikuweza ifanya hiyo haqyika katika nyumba ninayoishi mimi lakin ndani ya kijiji hichohicho..nilifanyia kwa rafiki yangu
2:siku hiyo sikuweza kuwanyoa nyele...je kwa kufanya hivi nitakuwa nimeharibu hiyo haqyika..!!? Na kama nimeharibu naweza kurejeza tena kuwafanyia...
wahadha salam a'laykum


JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunashukuru kwa utekelezaji wako wa Sunnah ya ‘Aqiyqah baada ya kupata mafunzo kutoka kwetu. Hakika hii inatuzidishia iymaan kwamba ndugu zetu mnafuata mafunzo haya na juhudi zetu si za bure. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Azidi kutuelimisha na kutuongoza.

Ama kuhusu ‘Aqiyqah uliyoifanya kwa kukosekana mambo mawili uliyoyataja, ni kwamba haikuharibu ‘Aqiyqah yako kwa sababu hakuna dalili kwamba ‘Aqiyqah lazima itekelezwe katika nyumba anayoishi mtu au lazima mtoto anyolewe nywele. Kwa hiyo huna haja kurejea kutekeleza tena bali inatosheleza na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akutakabalie na Awajaalie watoto wawe waja wema na wenye taqwa.

Itambulike kwamba kumnyoa nywele moto, ni katika Sunnah iliyopendekezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyokuja dalili katika Hadiyth ya Abu Rafi‘i (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa al-Hasan bin ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhuma), mama yake, ambaye ni Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) alitaka kumfanyia ‘Aqiyqah ya kondoo wawili. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Usifanye ‘Aqiyqah, lakini mnyoe nywele zake, halafu utoe sadaka ya fedha yenye uzito wa nywele hizo”. Kisha akazaliwa al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhuma), akafanya mithili ya hivyo” (Ahmad). 

Ni dhahiri kwamba kuna hikma na faida ya kumnyoa mtoto nywele na anayeweza kutekeleza ni kheri kwake na kwa mtoto. Ama asiyejaaliwa kutekeleza hana ubaya bali atakuwa amekosa faida zake tu, na mtu hulipwa kwa niyyah yake.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share