Al-Qawaaid Al-Arba' (Kanuni Nne) الْقَوَاعِدُ الأَرْبَع - (Word Doc) Chapisho La 5 - Kimehaririwa 1438H (2017M)

 

Alhidaaya.com

 

Sikiliza Matn Ya Al-Qawaaid Al-Arba’

 

 

 

 

 

 

الْقَوَاعِدُ الأَرْبَع

Al-Qawaaid Al-Arba’ (Kanuni Nne)

 

Mwandishi:

Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab

 

Mfasiri:

Ummu Iyyaad

 

 

Chapisho La 5 – Kimehaririwa 1438H (2017M)

 www.alhidaaya.com 

 

 

YALIYOMO:

 

 

Historia Fupi Ya Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab ……….  5

 

Utangulizi Wa Kanuni Nne ……………………………………………..11

 

Kanuni Ya Kwanza:  ……………………………………………………..14

 

Kanuni Ya Pili …………………………………………………………….15

 

Kanuni Ya Tatu: ………………………………………………………….17

 

Kanuni Ya Nne:  ………………………………………………………….20

 

 

 

 

Historia Fupi Ya Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab[1]

 

 

 Asili yake

 

Jina lake ni Abul-Husayn Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab bin Sulaymaan bin ‘Aliy Musharrif Al-Wuhaybiy. Kabila lake ni Bani Tamiym. Amezaliwa mwaka 1115 H (1704 M) katika mji ya ‘Uyaynah kijiji cha Yamaamah ndani ya Najd, kaskazini Magharibi ya mji wa Riyadhw, Saudi Arabia. Ametoka katika familia ya Wanavyuoni kwani baba yake ‘Abdul-Wahhaab alikuwa ni Mwanachuoni maarufu wa Najd na Qaadhwi wa mji huo.

 

 

Elimu Yake

 

Alijifunza kusoma Qur-aan alipokuwa na umri mdogo na akaihifadhi akiwa chini ya umri wa miaka kumi. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Alimjaalia kuwa na uhodari na akili nzuri, wepesi wa kufahamu na kumaizi jambo au somo. Alipendezewa mno kusoma kazi za Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibnul-Qayyim (رحمهما الله).

Alifanya bidii kwenye masomo yake na kuendelea kujifunza chini ya usimamizi wa baba yake. Akajifunza elimu ya Dini chini ya Wanavyuoni walioko mjini mwake wakiwemo baba yake na ‘ammiy yake. Alisafiri kutoka kwenda Madiynah kusoma chini ya Wanavyuoni wakubwa wa huko wakiwemo; Shaykh ‘Abdullaah bin Ibraahiym bin Ash-Shamariyyi, na Mwanachuoni maarufu wa India Shaykh Muhammad Hayaat Al-Sindi. Alikwenda Makkah pia na alitekeleza Hajj. Hatimaye akaelekea Baswrah (Kaskazini Iraq) kutafuta elimu zaidi akasoma chini ya Wanavyuoni wa huko akawa maarufu kwa mijadala baina yake na Wanavyuoni.

 

 

Harakaat Na Mitihani

 

Watu wa Najd walikuwa katika shirki na bid’ah (uzushi). Walikuwa wakiabudu miungu mingi na kuabudu makaburi, miti, mawe, mapango, majini na mashaytwaan, waja wema waliojulikana kama ni mawalii. Uchawi na unajimu (utabiri wa nyota) ulisambaa pia. Hakuna aliyekataza ‘iIbaadah potofu hizo kwani watu walikuwa katika kuchuma manufaa na starehe za dunia zaidi na wakakhofia kuyapoteza hayo. Hivyo Shaykh akaona umuhimu mkubwa uliohitajika kuwarudisha watu katika manhaj ya Qur-aan na Sunnah. Akaanza kuwalingania watu katika Tawhiyd - kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kumshirikisha na lolote katika ‘ibaadah. Akaazimia kujitumikisha peke yake kwa uvumilivu katika konde. Akajua hakuna lolote kitachofaulu kufanyika ila jihaad katika njia ya Allaah.

 

Shaykh alikumbana na mitihani, misukosuko, na vitisho, lakini alikuwa ameshategemea hali hiyo kumfikia na alikuwa tayari kukabaliana nayo kwani alitambua kuwa hilo ni jambo lisiloepukika kwa kila mlinganiaji kwani ndio hali waliyokutana nayo Manabii wote, na Salafus-Swaalih (waja wema waliotangulia).

 

Miongoni mwa mitihani aliyokumbana nayo ni kutokana na Wanavyuoni wadhaifu wasiokuwa na hoja ambao walimpinga na kumfanya akabiliane na misukosuko, vitisho na kukasirikiwa. Pia alikabiliana na misukosuko na mateso chini ya mikono ya madhalimu wa Huraymilaa. Na alipowashawishi watawala wahukumu madhalimu kwa Shariy’ah ya Kiislamu, ilisababisha baadhi ya watu kuyaweka maisha yake hatiani lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Alimnusuru.

 

Aliamua kurudi kwao ‘Uyaynah, ambako kipindi hicho kulikuwa chini ya utawala wa mtoto wa Mfalme ‘Uthmaan bin Muhammad bin Mu’ammar, ambaye alimpokea Shaykh kwa ukarimu na kumuahidi kumuunga mkono na kumsaidia kuwaita watu katika Uislam. Akaendelea kufundisha na kutoa da’wah hatimaye akashawishika kidhati na kwa vitendo kuondoa dini ya miungu mingi pale alipoona baadhi ya watu ni wagumu kurudi katika Uislamu. Aliweza kumshawishi gavana wa mji huo kulivunja zege lililojengewa juu ya kaburi la Zayd bin Al-Khattwaab ambaye alikuwa ni kaka wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنهما). Akavunjavunja mangome mengineyo, mapango, miti n.k. Akaamrisha Shariy’ah ya Kiislamu itekelezwe kama kumpiga mawe hadi afe mwanamke aliyekiri uzinifu.

 

Shaykh aliendelea na harakati zake za kauli na ‘amali ambazo zilimfanya azidi kuwa maarufu. Hatimaye akawa Jaji (Qaadhwiy) wa mji wa ‘Uyaynah. Lakini hakuweza kuendelea hapo kwani Mfalme alishawishiwa na viongozi wa miji ya jirani amuue Shaykh kwa vile hawakupendezewa na da’wah yake. Ikabidi afukuzwe katika mji huo.

Akakaribishwa mji wa Ad-Dir’iyyah ambao ulikuwa ni jirani yake. Huko akakaribishwa ingawa kwanza alitiliwa shaka. Alifikia kwa mja mwema aliyempokea ila alimkhofia kutokukubaliwa na mtoto wa Mfalme Muhammad bin Sa’uwd.  Habari zikamfikia kwanza mke wa Ibn Sa’uwd ambaye alikuwa mkarimu na mwenye taqwa. Akamfahamisha mumewe kwa kumwambia, “H tawfiyq kubwa umeletewa kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) mtu ambaye anawaita watu katika Uislamu, anawaita katika Qur-aan na Sunnah za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Tawfiyq iliyoje? Mkimbilie haraka na umuunge mkono wala usimpinge au kumkataza kwa hayo”. Muhammad Ibn Sa’uwd akakubali ushauri wa mkewe na akaenda kwa Shaykh na akafanya mkataba naye kwamba asiondoke nchini hapo. Ndipo Shaykh akaweka makazi yake hapo na kuendelea na da’wah. Akaendelea na harakati za da’awah hapo Dar’iyyah. Akaheshimika na kupendwa mno na akaungwa mkono na watu. Da’wah yake iliwaathiri na kuwapendezea mno watu. Ikaenea katika nchi za Kiislamu na nyinginezo. Wakimiminika watu kufika hapo Dar’iyyah kujifunza kwake.

 

Kama ijulikanavyo kila jema halikosi mitihani. Wakatokeza wapinzani na waliokuwa na chuki naye. Kulikuweko waliompinga da’wah yake ya kuondosha shirki na bid’ah na kuwaita watu katika Tawhiyd. Na wengineo waliompinga kabisa ni kwa sababu ya kuhofu kufukuzwa katika nafasi au vyeo vyao vya kazi. Kwa hiyo wengine walimpinga kwa ajili ya Dini, na wengine walimpinga kisiasa. Wapinzani wake walimzushia ya kumzushia walifika hadi kudai kwamba Shaykh alikuwa ni mfuasi wa Khawaarij. Na mara nyingine wakimlaumu bure bila ya dalili na nje ya upeo wa elimu zao. Hivyo yakaweko malumbano na majibishano yaliyoendelea katika mijadala kadhaa. Shaykh aliwaandikia kuwajibu madai yao, na wao walimrudishia majibu na yeye akawa akiwathibitishia ufahamu wao mbaya wa shariy’ah na Dini kwa ujumla kwa dalili. Ndipo wingi wa maswali na majibu yakawajumuisha watu na wakazidi kuongezeka. Baadhi ya mijadala hiyo iliandikwa na kuchapishwa katika vitabu.

 

 

Athari Ya D’awah Yake

 

Da’wah yake ya takriban miaka 50 imedhihirika na kuleta athari kubwa kwanza kwa Waislamu wa zama hizo. Watu waliacha kuabudu makaburi, miti, mawe, majini, waliacha utabiri wa nyota na kila aina ya shirki. Imewatoa pia watu katika ujinga wa kufuata mila za mababu bila ya dalili.  Maamrisho ya mema na makatazo ya maovu yakalinganiwa katika Misikiti. Na hapo msimamo wa Qur-aan na Sunnah ukahuishwa na shirki na bid’ah zikatoweka. Amani na utulivu ukawafunika watu kila mahali. Na mpaka sasa da’wah yake imekuwa na umuhimu mkubwa katika jamii ya Kiislamu. Vijana khasa kutoka nchi za Magharibi na zaidi wale wanaosilimu wamekuwa na hamasa na shauku kubwa ya kujifunza Dini iliyo sahihi na si ile iliyochanganywa na shirki na bid’ah. Kwa hiyo, mafundisho ya msimamo wake wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah yamekuwa kipaumbele katika lengo la kutafuta elimu kwa Waislamu watakao na wapendao haki.

 

Kazi Zake

 

Ameandika vitabu vingi vya mafunzo mbali mbali lakini alitilia mkazo zaidi katika somo la Tawhiyd na ‘Aqiydah. Na alitumia hikmah ya kuandika vitabu vidogo vidogo lakini vilivyokusanya nukta muhimu kabisa. Vilikuwa ni mukhtasari wa maudhui aliyotaka kuidhihirisha. Na vitabu hivyo vimekuja kufafanuliwa kwa kushereheshwa na ‘Ulamaa kadhaa na vimekuwa vina umuhimu mno katika vyuo vya Kiislamu vinavyofuata mwendo wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah.

Vifuatavyo ni baadhi ya vitabu vyake maarufu. Vinne vya mwanzo ni ambavyo mashuhuri zaidi. Na vinginevyo vimekusanywa na kujumuishwa katika ‘Maj’muw’at Mu-allafaatil-Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab’.

 

1.      Kitaabut-Tawhiyd - kitabu hiki kimekuwa mashuhuri mno na kimeenea sana na somo lake limekuwa ni lenye kutoa mafunzo muhimu kuhusu kumpwekesha Allaah na kuepukana na shirki.

 

2.      Al-Uswuul Ath-Thalaathah – kitabu kitoacho mafunzo kuhusu asili au misingi ya Uislamu.

 

3.      Al-Qawaaid Al-Arba’- kinatoa mafunzo ya kanuni za ufahamu wa shirki kwa ujumla.

 

4.      Kashf Ash-Shubuhaat - kinakanusha hoja zinazojulikana na watetezi wa shirki na bid’ah.

 

5.      Mukhtaswar Al-Inswaaf was-Sharh Al-Kabiyr

 

6.      Mukhtaswar Zaad Al-Ma’aad

 

7.      Mukhtaswar As-Siyrah

 

8.      Mukhtaswar al-Fat-h

 

9.       Masaail Al-Jaahiliyyah

 

10.   Adaab Al-Mashiy ilaa as-Swalaah

 

11.  Nawaaqidhw Al-Islaam

 

 

Wanafunzi Wake

 

Alikuwa na wanafunzi wengi mno. Miongoni mwao ni watoto na wajukuu wake ambao waliendeleza kazi yake ya da’wah na Jihaad katika njia ya Allaah, walifungua vyuo karibu na kwao wakifunza watu masomo ya Dini. Kati ya watoto wake ni Husayn, ‘Aliy, ‘Abdullaah na Ibraahiym. Na kati ya wajukuu wake ni ‘Aliy bin Husayn, na pia ‘Abdur-Rahmaan bin Hasan aliyeandika kitabu cha ‘Fat-h Al-Majiyd Sharh Kitaab At-Tawhiyd’. Wanafunzi wake wengineo ni ‘Abdul-‘Aziyz bin Muhammad bin Sa’uwd, Hamad bin Naaswir bin Mu’ammar na ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Husayn.

Familia Yake

 

Alikuwa na watoto sita; Husayn, ‘Abdullaah, Hasan, ‘Aliy, Ibraahiym, ‘Abdul-‘Aziyz. Shaykh anatokana na kizazi kinachojulikana kwa ‘Aal-Shaykh’ ambacho kimetoa Wanavyuoni kadhaa akiwemo Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aal-Shaykh aliyekuwa Mufti mkuu wa awali Saudi Arabia na Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Aal-Shaykh  ambaye ni Mufti mkuu wa sasa.

 

 

Kifo Chake

 

Alifariki mwaka 1206 H (1792 M) akiwa na umri wa miaka 91. Rahmah za Allaah ziwe juu yake na Allaah Amruzuku Jannah ya Firdaws. Aamiyn.

 

 

 

 

 الْقَوَاعِدُ الأَرْبَع

للإمامِ مُحَمَّد بِن عَبْدِالوَهَّاب

 

AL-QAWAAID AL-ARBA’

(KANUNI NNE)

Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab

 

بِسْــــــمِ اللهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيـــــمِ

أَسْأَلُ اللهَ الْكَرِيمَ رَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ أَنْ يَتَوَلاكَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ. وَأَنْ يَجْعَلَكَ مُبَارَكًا أَيْنَمَا كُنْتَ، وَأَنْ يَجْعَلَكَ مِمَّنْ إِذَا أُعْطِيَ شَكَرَ، وَإِذَا ابْتُلِيَ صَبَرَ، وَإِذَا أذَنبَ اسْتَغْفَرَ. فَإِنَّ هَؤُلاءِ الثَّلاثُ عُنْوَانُ السَّعَادَةِ.

 

Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu.

 

Namuomba Allaah Mkarimu, Rabb wa ‘Arshi Adhimu, Akuhifadhi duniani na Aakhirah, na Akujaalie mwenye baraka popote ulipo, na Akujaalie miongoni mwa wale; anapopewa hushukuru, na anapojaribiwa mitihani husubiri, na anapotenda dhambi huomba maghfirah, kwani mambo hayo matatu ni funguo za furaha.

 

إِعْلَمْ أَرْشَدَكَ اللهُ لِطَاعَتِهِ: أَنَّ الْحَنِيفِيَّةَ مِلَّةُ إِبْرَاهِيمَ: أَنْ تَعْبُدَ اللهَ، وَحْدَهُ مُخْلِصًا لَهُ الدِّينَ

Fahamu, Akuongoze Allaah katika utiifu Wake, kwamba Haniyfiyyah (Kuelemea katika Dini ya haki na kujiepusha na dini potofu) ni Dini ya Ibraahiym, umwabudu Allaah Pekee, ukiwa ni mwenye kumtakasia Dini Yake.

 

كَمَا قَالَ تَعَالَى:

kama Anavyosema Ta’aalaa:

 

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

((Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu))[2]

 

 

فَإِذَا عَرَفْتَ أَنَّ اللهَ خَلَقَكَ لِعِبَادَتِهِ؛ فَاعْلَمْ أَنَّ الْعِبَادَةَ لا تُسَمَّى عِبَادَةً إِلا مَعَ التَّوْحِيدِ، كَمَا أَنَّ الصَّلاةَ لا تُسَمَّى صَلاةً إِلا مَعَ الطَّهَارَةِ.

 

Basi utakapojua kwamba Allaah Amekuumba kwa ajili ya kumwabudu Yeye, basi jua kwamba: ‘Ibaadah haiitwi ‘ibaadah isipokuwa pamoja na Tawhiyd (kumpwekesha Allaah), kama ambavyo Swalaah haiitwi Swalaah isipokuwa pamoja na twahaarah.

 

 

 فَإِذَا دَخَلَ الشِّرْكُ فِي الْعِبَادَةِ فَسَدَتْ، كَالْحَدَثِ إِذَا دَخَلَ فِي الطَّهَاَرِة.

Hivyo basi itakapoingia shirki katika ‘ibaadah inaharibika kama najsi inavyoingia katika twaaharah (inaitengua).

 

 

 فَإِذَا عَرَفْتَ أَنَّ الشِّرْكَ إِذَا خَالَطَ الْعِبَادَةِ أَفْسَدَهَا، وَأَحْبَطَ الْعَمَلَ، وَصَاَر صَاحِبُهُ، مِنَ الْخَالِدِينَ فِي النَّارِ عَرَفْتَ أَنَّ أَهَمَّ مَا عَلَيْكَ مَعْرِفَةُ ذَلِكَ لَعَلَّ اللهَ أَنْ يُخَلِّصَكَ مِنْ هَذِهِ الشَّبَكَةِ.

Na utakapojua kwamba shirki inapochanganyika na ‘ibaadah inaiharibu na inaporomosha ‘amali, na mtendaji huwa ni miongoni mwa watakaodumu motoni, hapo utajua kwamba jambo muhimu kabisa kwako (la kuwajibika) ni utambuzi wa hilo, huenda Allaah Akuepushe katika utando wa utata huu.

 

 

 وَهِيَ الشِّرْكُ بِاللهِ الَّذِي قَالَ الله تَعَالَى فِيهِ:

Navyo ni kumshirikisha Allaah ambayo Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا﴿٤٨﴾

((Hakika Allaah Haghufuri kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae))[3]

 

 

وَذَلِكَ بِمَعْرِفَةِ أَرْبَعِ قَوَاعِدَ ذَكَرَهَا اللهُ تَعَالَى فِي كِتَابِهِ:

Na (utambuzi) huo, ni kwa maarifa manne ya Kanuni Alizozitaja Allaah Ta’aalaa katika Kitabu Chake:

 

 

الْقَاعِدَةُ الأُولَى:

Kanuni Ya Kwanza:

أَنْ تَعْلَمَ أَنَّ الْكُفَّارَ الَّذِينَ قَاتَلَهُمْ رَسُولُ اللهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) مُقِرُّونَ بِأَنَّ اللهَ تَعَالَى هُوُ الْخَالِقُ، الْمُدَبِّرُ، وَأَنَّ ذَلِكَ لَمْ يُدْخِلَهُمْ فِي الإِسْلامِ.

Ujue kwamba makafiri, ambao Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipigana nao, walikiri kwamba Allaah Ta’aalaa ni Muumbaji na Mwendeshaji wa mambo yote. Lakini (kukiri) hivyo hakukuwaingiza katika Uislamu.

 

 وَالدَّلِيلُ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

 قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ﴿٣١﴾

((Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)?  Watasema: “Ni Allaah”; basi sema: “Je basi hamuwi na taqwa?”))[4]

 

 

 

 

الْقَاعِدَةُ الثَّانِيَةُ:

Kanuni Ya Pili:

أُنَّهُمْ يَقُولُونَ: مَا دَعَوْنَاهُمْ وَتَوَجَّهْنَا إِلَيْهِمْ إِلا لِطَلَبِ الْقُرْبَةِ وَالشَّفَاعَةِ.

Kwamba wao (washirikina) wamesema: “Hatukuwaabudu wala kuelekea kwao isipokuwa tu kuomba kukurubia na shafaa’ah (uombezi wa Allaah).

 

فَدَلِيلُ الْقُرْبَةِ؛ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ya kutafuta ukaribu ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

 وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ ﴿٣﴾

((Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi (wakisema): “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie” Hakika Allaah Atahukumu baina yao katika yale waliyokhitilafiana nayo. Hakika Allaah Hamwongoi aliye muongo, kafiri)) [5]

وَدَلِيلُ الشَّفَاعَةِ، قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ya shafaa’ah (uombezi) ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

 وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ ۚ

((Na wanaabudu pasi na Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah”))[6]

وَالشَّفَاعَةُ شَفَاعَتَانِ: شَفَاعَةٌ مَنْفِيَّةٌ، وَشَفَاعَةٌ مُثْبَتَةٌ.

Na ash-shafaa’ah (uombezi) ni aina mbili:

 

i.                    Shafaa’ah iliyokatazwa (iliyoharamishwa katika Qur-aan na Sunnah)[7] 

 

ii.                  Shafaa’ah iliyothibitishwa (inayokubalika katika Qur-aan na Sunnah)[8]

 

فَالشَّفَاعَةُ الْمَنْفِيَّةُ: مَا كَانَتْ تُطْلَبُ مِنْ غَيْرِ اللهِ فِيمَا لا يَقْدِرُ عَلَيْهِ إِلا اللهُ.

Basi Ash-Shafaa’ah iliyokatazwa ni kumwomba asiyekuwa Allaah jambo ambalo hakuna mwenye uwezo nalo isipokuwa Allaah.

 

 وَالدَّلِيلُ قَوْلُهُ تَعَالَى:  

Na dalili ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ۗ وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٢٥٤﴾

((Enyi walioamini! Toeni katika Tulivyokuruzukuni kabla haijafika Siku (ambayo) hakutokuweko mapatano humo wala urafiki wala shafaa’ah (uombezi). Na makafiri wao ndio madhalimu))[9]

وَالشَّفَاعَةُ الْمُثْبَتَةُ: هِيَ الَّتِي تُطْلَبُ مِنَ اللهِ، وَالشَّافِعُ مُكَرَّمٌ بِالشَّفَاعَةِ، وَالْمَشْفُوعُ لَهُ مَنْ رَضِيَ اللهُ قَوْلَهُ وَعَمَلَهُ بَعْدَ الإِذْنِ

Na Ash-Shafaa’ah iliyothibitishwa ni ambayo inaombwa baada ya idhini ya Allaah, na mwombezi amekirimiwa kwa ash-shafaa’ah na anayeombewa ni ambaye Allaah Ameridhika naye kwa kauli zake na vitendo vyake.

 

  كَمَا قَالَ تَعَالَى:

Kama Anavyosema Ta’aalaa:

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ

((Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake))[10]

 

 

 

 

الْقَاعِدَةُ الثَّالِثَةُ:

 

Kanuni Ya Tatu:

أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) ظَهَرَ عَلَى أُنَاسٍ مُتَفَرِّقِينَ فِي عِبَادَاتِهِمْ، مِنْهُمْ مَنْ يَعْبُدُ الْمَلائِكَةَ، وَمِنْهُمْ مَنْ يَعْبُدُ الأَنْبِيَاءَ وَالصَّالِحِينَ، وَمِنْهُمْ مَنْ يَعْبُدُ الأَشْجَارَ وَالأَحْجَارَ، وَمِنْهُمْ مَنْ يَعْبُدُ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ، وَقَاتَلَهُمْ رَسُولُ اللهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) وَلَمْ يُفَرِّقْ بَيْنَهُمْ.

 

Kwamba

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuta watu wakitofautiana katika ibaada zao. Kuna waliokuwa wanaabudu Malaika, wanaoabudu Manabii na Swalihina (waja wema), wanaoabudu miti na mawe, na wanaoabudu jua na mwezi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akapigana nao na wala hakutofautisha baina yao (katika walivyoviabudu).

 

وَالدَّلِيلُ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ ۚ

((Na piganeni nao mpaka kusiweko fitnah (shirki na mateso) na Dini yote iwe kwa ajili ya Allaah))[11]

وَدَلِيلُ الشَّمْسِ وَالْقَمَرِ؛ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ya jua na mwezi (kuabudiwa) ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ ﴿٣٧﴾

((Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake, ni usiku na mchana, na jua na mwezi.  Msisujudie jua wala mwezi; bali msujudieni Allaah Ambaye Aliyeviumba ikiwa Yeye Pekee mnawambudu))[12]

وَدَلِيلُ الْمَلائِكَةِ؛ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ya Malaika (kuabudiwa) ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

 وَلَا يَأْمُرَكُمْ أَن تَتَّخِذُوا الْمَلَائِكَةَ وَالنَّبِيِّينَ أَرْبَابًا ۗ

((Na wala hakuamuruni kuwachukua Malaika na Manabii kuwafanya miungu))[13]

وَدَلِيلُ الأَنْبِيَاءِ؛ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ya Manabii (kuabudiwa) ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

 وَإِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ ۚ إِن كُنتُ قُلْتُهُ فَقَدْ عَلِمْتَهُ ۚ تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ ۚ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ ﴿١١٦﴾

((Na (kumbuka) Allaah Atakaposema: “Ee ‘Iysaa mwana wa Maryam!  Je, wewe uliwaambia watu: “Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu miwili badala ya Allaah?” (‘Iysaa) Atasema: “Subhaanak Utakasifu ni Wako! Hainipasi mimi kusema yasiyokuwa haki kwangu; ikiwa nimesema hayo basi kwa yakini Ungeliyajua; Unayajua yale yote yaliyomo katika nafsi yangu; na wala mimi sijui yale yaliyomo katika Nafsi Yako; hakika Wewe ni Mjuzi wa ghayb))[14]

وَدَلِيلُ الصَّالِحِينَ؛ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ya Swalihiyna (kuabudiwa) ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

 أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ ۚ

((Hao wanaowaomba (wao wenyewe) wanatafuta kwa Rabb wao njia ya kujikurubisha, yupi miongoni mwao awe karibu zaidi na wanataraji rahmah Yake, na wanakhofu adhabu Yake)) [15]  

 

وَدَلِيلُ الأَشْجَارِ وَالأَحْجَارِ؛ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ya miti na mawe (kuabudiwa) ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ ﴿١٩﴾ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ ﴿٢٠﴾

 ((Je, mmeona Laata na ‘Uzzaa?  Na Manaata mwengine wa tatu?))[16] 

وَحَدِيُث أَبِي وَاقٍد اللَّيْثِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: خَرَجْنَا مَعَ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) إِلَى حُنَيْنٍ وَنَحْنُ حُدَثَاءُ عَهْدٍ بِكُفْرٍ، وَلِلِمُشْرِكِينَ سِدْرَةٌ، يَعْكُفُونَ عِنْدَهَا وَيُنَوِّطُونَ بِهَا أَسْلِحَتَهُمْ، يُقَالَ لَهَا ذَاتُ أَنْوَاطٍ، فَمَرَرْنَا بِسِدْرَةٍ فَقُلْنَا: يَا رَسُولَ اللهِ اجْعَلْ لَنَا ذَاتَ أَنْوَاطٍ كَمَا لَهُمْ ذَاتُ أَنْوَاط ... الحَدِيثَ  

Na Hadiyth ya Abuu Waaqid Al-Laythiyy (رضي الله عنه) amesema: “Tulitoka pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwenda (vitani) Hunayn nasi ndio kwanza tumetoka katika ukafiri, na washirikina walikuwa na mkunazi wakijisabilia nao kufanya ‘ibaadah na walikuwa wakitundika silaha zao (kutafuta baraka). Wakiuita ‘Dhaatu-Anwaatw’. Tukapita mbele ya mkunazi tukasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Tufanyie nasi Dhaatu-Anwaatw kama walivyokuwa nao (makafiri) Dhaatu-Anwaatw” …  Al-Hadiyth

 

 

 

 

 

الْقَاعِدَةُ الرَّابِعَةُ:

Kanuni Ya Nne:

أَنَّ مُشْرِكِي زَمَانَنَا أَغْلَظُ شِرْكًا مِنَ الأَوَّلِينَ، لأَنَّ الأَوَّلِينَ يُشْرِكُونَ فِي الرَّخَاءِ، وَيُخْلِصُونَ فِي الشِّدَّةِ، وَمُشْرِكُو زَمَانَنَا شِرْكُهُمْ دَائِمٌ فِي الرَّخَاءِ وَالشِّدَة.

 

Kwamba washirikina wa zama zetu ni waovu zaidi katika shirki zao kuliko washirikina wa zamani kwa sababu, wa zamani walimshirikisha Allaah katika raha, lakini walitakasa (‘ibaadah zao) wakati wa shida. Ama washirikina wa sasa, shirki zao ni za kuendelea daima wakiwa katika raha au katika shida.

 

وَالدَّلِيلُ قَوْلُهُ تَعَالَى:

Na dalili ni kauli Yake Ta’aalaa:

 فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ ﴿٦٥﴾

((Wanapopanda merikebu humwomba Allaah wakiwa wenye kumtakasia Yeye Dini, lakini Anapowaokoa katika nchi kavu, tahamaki hao wanamshirikisha))[17]

 

 

 

تمت وَصَلَّى اللهُ عَلَى مُحَمَّدٍ وعلى َآلِهِ وَصَحْبِهِ وَسَلَّمَ.

Tammat Wa-Swalla Allaahu ‘alaa Muhammadin wa ‘alaa aalihi

 wa Swahbihi wa sallam.

 

 

 

[1]  Marejeo: Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab Da’watuhuu wa Siyraatuhu - Shaykh Ibn Baaz.

 

[2]  Adh-Dhaariyaat (51: 56)

[3]  An-Nisaa (4: 48, 116)

[4]  Yuwnus (10: 31)

[5]  Az- Zumar (39: 3)

[6]  Yuwnus (10: 18)

[7] Uombezi unaoombwa bila ya idhini ya Allaah (سبحانه وتعالى) nao ni wa washirikina (wanaomshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى)

[8] Uombezi unaoombwa baada ya idhini ya Allaah (سبحانه وتعالى) na ni watu wa Tawhiyd (wanaompwekesha Allaah سبحانه وتعالى)

[9]  Al-Baqarah (2: 254).

[10]  Al-Baqarah (2: 255)

[11]  Al-Anfaal (8: 39)

[12]  Fusswilat: (41: 37)

[13]  Aal-‘Imraan (3: 80)

[14]  Al-Maaidah (5: 116)

[15]  Al-Israa (17: 57)

[16]  An-Najm (53: 19-20)

[17]  Al-‘Ankabuwt (29: 65)

 

 

Share