04-Maamkizi Ya Kiislam: Nidhamu Zake

 

Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake

 

04-Nidhamu Zake

 

 

Alhidaaya.com

   

 

 

Nidhamu za maamkizi ya Kiislamu kuhusu nani wa kuanza kutoa salaam, hali gani za kutoa salaam na kwa nani wanaofaa kutolewa salaam:

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال‏:‏ ‏((‏يسلم الراكب على الماشي، والماشي على القاعد، والقليل على الكثير)) ‏ ‏متفق عليه‏ ‏

وفي رواية للبخاري‏:‏ ((والصغير على الكبير

 

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Aliyepanda (kipando) amsalimie anayetembea, anayetembea amsalimie aliyeketi na wachache wawasalimie walio wengi)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

Na katika Riwaayah ya Al-Bukhaariy ((Mdogo amsalimie mkubwa))

 

Wajibu wa kumsalimia unayemjua na usiyemjua, nayo ni amali iliyo bora katika Uislamu:

 

عن عبد الله بن عمرو بن العاص رضي الله عنهما، أن رجلاً سأل رسول الله: أي الإسلام خير؟ قال: ((تُطْعِمُ الطَّعامَ، وتقرأُ السَّلام علـى مَنْ عَرَفْتَ ومَنْ لَـمْ تَعْرِفْ)) البخاري ومسلـم

 

Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru bin Al-'Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amehadithia kwamba mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Ni amali gani katika Uislamu iliyo bora?” Akasema: ((Ni kulisha chakula na kumtolea salaam unayemjua na usiyemjua)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Aliye bora kabisa mbele ya Allaah ('Azza wa Jalla)  ni mwenye kuanza na maamkizi, na maamkizi bora ni yale ya Kiislamu kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

عن أبي أمامة الباهلي رضي الله عنه قال :قيل يا رسول الله صلى: رجلان يلتقيان أيهما يبدا بالسلام؟   قال: ((أَولاَهما بالله  تعالى )) الترمذي حديث حسن    

Kutoka kwa Abuu Umaamah Al-Baahiliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Watu wawili wanapokutana ni yupi anayepaswa kuanza kutoa salaam?” Akajibu: ((Ni yule aliye mbora kwa Allaah) [At-Tirmidhiy: Hadiyth Hasan].

 

Inapendekezeka kurudia kutoa salaam kwa uliyekutana naye kipindi kifupi nyuma, kama vile umeingia sehemu ukatoka na kisha ukaingia tena, au mathalan kuna ukuta au mti au kizuizi chochote baina yao kimewakinga na kisha wakakutana tena, basi wanaweza kusalimiana tena kwa dalili:

 

عن أبي هريررة رضي الله عنه  عن رسول الله صلى الله عليه وسلم، قال‏: ‏((‏‏إذا لقي أحدكم أخاه، فليسلم عليه، فإن حالت بينهما شجرة، أو جدار، أو حجر، ثم لقيه، فليسلم عليه‏))‏ ‏  ‏رواه أبو داود‏

 

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mmoja wenu atakapokutana na nduguye amtolee salaam, iwapo watazuiwa na mti au ukuta au jiwe kisha akakutana naye basi amsalimie)) [Abu Daawuwd].

 

Mapendekezo ya kutoa salaam unapofika katika majlisi (kikao) na pindi unapoachana na walioketi katika kikao hicho:

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال‏:‏ قال رسول الله صلى الله عليه وسلم‏:‏‏ ‏((إذا انتهى أحدكم إلى المجلس فليسلم، فإذا أراد أن يقوم فليسلم، فليست الأولى بأحق من الآخرة‏))‏ رواه أبو داود، والترمذي وقال‏:‏ حديث حسن

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anapokomea mmoja wenu katika majlisi (kikao) atoe salaam, na atakapotaka kuondoka atoe salaam, kwani salaam ya kwanza si bora kuliko salaam ya pili)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan].

 

Unaweza pia kumtolea salaam mwanamke ambaye ni Mahram wako na pia yule ambaye ni ajinabi (asiye Mahram wako) usipochelea fitna na wao (wanawake) wanaweza nao kutoa salaam kwa wanaume kwa sharti kama hilo:

 

عن سهل بن سعد رضي الله عنه قال‏:‏ كانت فينا امرأة - وفي رواية‏:‏ كانت لنا عجوز- تأخذ من أصول السلق فتطرحه في القدر، وتكركر حبات من شعير، فإذا صلينا الجمعة، وانصرفنا، نُسلم عليها، فتقدمه إلينا‏”‏ ‏- ‏رواه البخاري‏ ‏‏

Kutoka kwa Sahl bin Sa'ad (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesimulia kuwa, “Kulikuwa na mwanamke” – na katika riwaayah nyingine imesema: “Kulikuwa kuna ajuza (mwanamke mwenye umri mkubwa) akichukua mizizi ya kiazisukari (cheupe) akitia sufuriani na akisaga nafaka za shayiri. Tunapomaliza kuswali Swalaah ya Ijumaa na kutawanyika, tulikuwa tukimtolea salaam naye akituitikia.”[Al-Bukhaariy].

 Pia:

 عن أم هانئ فاختة بنت أبي طالب رضي الله عنه قالت‏:‏ أتيت النبي صلى الله عليه وسلم يوم الفتح وهو يغتسل، وفاطمة تستره بثوب، فسلمت، وذكرت الحديث  -  ‏رواه مسلم

Ummu Haaniy Faakhitah bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhaa) ambaye amesema: “Nilimuendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya Ukombozi wa Makkah naye anaoga na Faatwimah (binti yake) anamstiri kwa nguo, nikamtolea salaam…” akaendelea mpaka mwisho wa Hadiyth.” [Muslim].

 

Hii ina uhusiano na Hadiyth ifuatayo:

 

عن أسماء بنت يزيد رضي الله عنه عنها أن رسول الله صلى الله عليه وسلم، مر في المسجد يومًا، وعصبة من النساء قعود، فألوى بيده بالتسليم‏.‏ ‏(‏‏(‏رواه الترمذي وقال‏:‏ حديث حسن‏)‏‏)‏‏.‏  

Kutoka kwa Asmaa bin Yaziyd (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipita msikitini siku moja kulikuwa na kundi la wanawake wameketi, akaashiria mkono wake kwa kutoa salaam.” [At-Tirmidhiy na kasema Hadiyth Hasan].

 

Hali hii inachukuliwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijumuisha baina ya kutamka na kuashiria na kinachotilia nguvu ni ile riwaayah ya Abuu Daawuwd inayosema “...akatutolea salaam” Kwa kuunganisha riwaayah hizo mbili, tunapata faida ya kujua kuwa mtu anapoashiria ni bora afutilizie ile ishara yake kwa maneno; kama ni ishara ya kusalimia, basi na atoe salaam mdomoni mwake japo haitosikiwa na aliye mbali.

 

 

Mafunzo Kutoka Katika Kisa Cha Swahaba:

 

 عن الطفيل بن أبي بن كعب أنه كان يأتي عبد الله بن عمر، فيغدو معه إلى السوق، قال‏:‏ فإذا غدونا إلى السوق، لم يمر عبد الله على سقاط ولا صاحب بيعة، ولا مسكين، ولا أحد إلا سلم عليه، قال الطفيل، فجئت عبد الله بن عمر يومًا، فاستتبعني إلى السوق فقلت له‏:‏ ما تصنع بالسوق، وأنت لا تقف على البيع ولا تسأل عن السلع، ولا تسوم بها، ولا تجلس في مجالس السوق‏؟‏ وأقول‏:‏ اجلس بنا هاهنا نتحدث، فقال يا أبا بطن- وكان الطفيل ذا بطن- إنما نغدو من أجل السلام فنسلم على من لقيناه.‏  رواه مالك في الموطأ بإسناد صحيح

Kutoka kwa At-Twufaiyl bin Abiy Ka'ab kwamba 'Abdullaah bin 'Umar alimtembelea kisha akaenda naye sokoni. Walipokuwa njiani hakumpita mtu yeyote asiyeuza au anayeuza, wala masikini wala mtu yeyote ila alimsalimia. Akasema At-Twufayl: “Nikaenda kwa 'Abdullaah bin 'Umar siku moja akanitaka nimfuate sokoni. Nikamwambia: “Utafanya nini sokoni na hali husimami kwa muuzaji wala kuuliza bidhaa, wala kujadiliana nao biashara, wala hukai kikao sokoni? 'Abdullaah bin 'Umar akasema: “Tukae na kuzungumza”. Kisha akasema: “Ee Abaa Batwn” Alikuwa At-Twufayl ni mwenye tumbo! Tunakwenda huko kwa ajili ya kusalimia watu tu, tupate kumsalimia yeyote tunayekutana naye.” [Imaam Maalik katika Al-Muwattwa ikiwa na isnaad Swahiyh].

 

Baada ya kupata mafunzo na fadhila zote hizo kuhusu maamkizi ya Kiislamu tunatumai kwamba tutazingatia umuhimu wa kuamkiana kama ipasavyo, na umuhimu wa kuikamilisha salaam kwenye matamshi na maawasiliano yetu ya kimaandishi. Hali kadhaalika bial kuacha kumsalimia tunayemjua na tusiyemjua.

 

 

Share