01-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Waislamu Wanaume Na Wanawake

 

 Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

01-Waislamu Wanaume Na Wanawake

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

 إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٣٥﴾

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao swadaqah wanaume na wanawake, na wafungao Swawm wanaume na wanawake, wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake; Allaah Amewaandalia maghfirah na ujira adhimu. [Al-Ahzaab: 35]

           

 

Kama tunavyoona katika hiyo Aayah tukufu kuwa hizo ni sifa kumi Alizozitaja Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ambazo pindi Muislamu akizimiliki atapata kughufuriwa madhambi yake na kupata ujira mkubwa kutoka kwa Allaah ('Azza wa Jalla). Hivyo kila mmoja wetu apime nafsi yake na kuhesabu kama yumo katika kumiliki sifa hizi zote kumi.

 

Ikiwa mtu anamiliki sifa mojawapo au zaidi yake, basi ajitahidi kuzifanyia kazi zote ili akamilishe kuwa na sifa hizo.

 

 

Sababu ya kuteremshwa Aayah hii:

 

 

 عن عبد الرحمن بن شيبة، سمعت أم سلمة زوج النبي صلى الله عليه وسلم تقول: قلت للنبي صلى الله عليه وسلم: ما لنا لا نُذْكَرُ في القرآن كما يذكر الرجال؟ قالت: فلم يَرعني منه ذات يوم إلا ونداؤه على المنبر، قالت، وأنا أسَرّح شعري، فلففت شعري، ثم خرجت إلى حُجْرة من حُجَر بيتي، فجعلت سمعي عند الجريد، فإذا هو يقول عند المنبر) يا أيها الناس، إن الله يقول:   إن المسلمين والمسلمات والمؤمنين والمؤمنات)) إلى آخر الآية  (الإمام أحمد)

 

Imetoka kwa 'Abdur-Rahmaan bin Shaybah kwamba: Nimemsikia Ummu Salamah    mke wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema:  “Nilimwambia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Kwa nini sisi wanawake hatutajwi (sana) katika Qur-aan kama wanavyotajwa wanaume? Kisha siku moja bila ya mimi kutambua, alikuwa akiita katika Minbar nami nilikuwa nikichana nywele zangu, nikazifunga nywele zangu nyuma kisha nikaingia chumbani katika vyumba vya nyumba yangu, nikaanza kusikiliza, naye alikuwa akisema kutoka katika Minbar: ((Enyi watu! Allaah Anasema: “Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake na Waumini wanaume  na Waumini wanawake…)) mpaka mwisho wa Aayah. [Imaam Ahmad] 

 

 

Sifa ya kwanza:

 

 إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ

 Hakika Waislamu wanaume na wanawake 

 

 

Zinatambulika nguzo za Kiislamu kuwa ni tano. Muislamu anapaswa kuzitimiza zote ili ukamilike Uislamu wake. Nguzo hizo zimetajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

 عبدالله بن عمر  قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم (( بُنِـيَ  الإِسْلاَمُ علـى خَمْسٍ: شَهادَةِ أنْ لا إِلٰهَ إلا الله وأنَّ مُـحَمَّداً رَسُولُ الله وإِقامِ الصَّلاَةِ وإِيتاءِ الزَّكاةِ وَحَجِّ البَـيْتِ وَصَوْمِ رَمَضَانَ)) البخاري

 

Kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Uislamu umejengeka kwa matano; Kushuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah na kuswali [Swalaah tano], kutoa Zakaah, kuhiji katika Nyumba [Makkah] na Swawm ya Ramadhwaan)) [Al-Bukhaariy]

 

Maana Ya Islaam: 

 

Maana ya ‘Islaam’ ni kujisalimisha na kunyenyekea kwa Allaah, na pia inatokana na neno 'salaam' lenye maana ya  'amani'. Kwa hiyo tunapoamiliana na watu ikiwa ni Waislamu au wasio Waislamu inatupasa tuonyeshe sifa hii yenye maana asili ya Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla), sifa ya usalama na amani kwa sababu Dini hii tukufu ni ya amani na usalama na sio kama inavyodhaniwa na baadhi ya makafiri.

 

Muislamu aweke usalama na amani kwa wasio Waislamu katika kutaamuli nao kwa kutokuwatendea maovu, kutimiza ahadi nao, kutaamuli nao vizuri katika biashara na kadhalika madamu wao hawakufanyia maudhi au kuwasababishia madhara Waislamu kwa lolote.  Dalili ni kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ لِلَّـهِ شُهَدَاءَ بِالْقِسْطِ ۖ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا تَعْدِلُوا ۚ اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾

Enyi walioamini!  Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na taqwa. Na mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo.  [Al-Maaidah: 8]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴿٨﴾

Allaah Hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale wasiokupigeni vita katika Dini, na wala hawakukutoeni kutoka majumbani mwenu. Hakika Allaah Anapenda wafanyao uadilifu. [Al-Mumtahinah: 8]

 

 

Pindi Muislamu atakapotaamuli na asiye Muislamu kama tunavyomarishwa na Allaah ('Azza wa Jalla) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na tukafuata mifano na mwongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyothibiti katika Siyrah yake, basi makafiri watapata kujua maana halisi ya Uislamu na kuupenda na ndio maana utasikia makafiri wengi wanaingia katika Dini ya Kiislamu baada ya kusoma Siyrah na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kutambua tabia zake na jinsi alivyotaamuli na makafiri ikawa ni sababu ya wengi kuingia katika Uislamu. 

 

Ama kwa Waislamu dalili tele zipo mojawapo ni Hadiyth tukufu ifuatayo inayotaja khasa kuhusu kuwekeana usalama na amani:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنهما) قَال: قَال رَسُولُ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((الْمُسْلِمُ مَنْ سَلِمَ الْمُسْلِمُونَ مِنْ لِسَانِهِ وَيَدِهِ  وَالْمُهَاجِرُ مَنْ هَجَرَ مَا نَهَى اللَّهُ عَنْهُ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah in ‘Amr (رضي الله عنهما) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Muislamu ni yule anayeweka amani kwa watu [ambaye Waislamu wenziwe wanasalimika] kwa ulimi na mkono wake. Na mhamaji ni yule anayehama Aliyoyakataza Allaah)).  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

 

Share