04-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Wasemao Kweli Wanaume Na Wanawake

 

Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

04- Wasemao Kweli Wanaume Na Wanawake  

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake [Al-Ahzaab: 35]

 

Sifa ya nne ni: Wasemao kweli.

 

 Inakusudiwa katika usemi wao, vitendo vyao, na niyyah zao kama baadhi ya wafasiri wa Qur-aan walivyonukuu.

 

Vile Vile Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametunasihi tuambatane na wanaosema kweli Anaposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ﴿١١٩﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli. [At-Tawbah: 119]

 

 

Kusema kweli ni alama ya iymaan kama ambavyo kusema uongo ni alama ya unafiki kama anavyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam:

 

 

عَلَيْكُمْ بِالصِّدْقِ فَإِنَّ الصِّدْق يَهْدِي إِلَى الْبِرّ وَإِنَّ الْبِرّ يَهْدِي إِلَى الْجَنَّة وَإِيَّاكُمْ وَالْكَذِب فَإِنَّ الْكَذِب يَهْدِي إِلَى الْفُجُور وَإِنَّ الْفُجُور يَهْدِي إِلَى النَّار وَلَا يَزَال الرَّجُل يَصْدُق وَيَتَحَرَّى الصِّدْق حَتَّى يُكْتَب عِنْد اللَّه صِدِّيقًا وَلَا يَزَال الرَّجُل يَكْذِب وَيَتَحَرَّى الْكَذِب حَتَّى يُكْتَب عِنْد اللَّه كَذَّابًا)) مسلم

 ((Shikamaneni na ukweli, kwani ukweli unapeleka katika wema, na wema unapeleka Peponi. Na jihadharini na uongo, kwani uongo unapeleka kwenye uovu, na uovu hupeleka katika moto. Mtu huendelea kusema ukweli na kujitahidi kuendelea hivyo hadi itarekodiwa na Allaah kuwa ni mkweli. Na mtu huendelea kusema uongo na ataendelea kufanya hivyo hadi itarekodiwa na Allaah kuwa ni muongo)) [Muslim]

 

Baadhi ya Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  hawajapata kusema uongo maishani mwao tokea siku za Ujaahiliyyah (zama za ujinga yaani kabla ya Uislam) wala hawakuwahi kusema uongo katika Uislam. Na mmoja wao ni Abubakar (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  ambaye alipewa sifa hiyo ya: Asw-Swiddiyq.

 

Abubakar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na sababu za kupewa sifa ya Asw-Swiddiyq' (Msema kweli ).

 

 

Al-Imaam An-Nawawiy amesema: "Ummah umekubaliana kwa pamoja bila ya kupingana kwamba amepewa cheo cha 'Asw-Swiddiyq kutokana na kuitikia kwake haraka kumuamini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)   bila ya kusita na kukubali maneno yake kwamba daima ni ya ukweli. Alibakia kuwa mkweli maishani mwake kote wala hajapata kusema uongo  hata mara moja."

 

Ibn Kathiyr amesema: "Kuhusu cheo chake cha   Asw-Swiddiyq inasemekana kwamba alipewa tokea zama za Ujaahiliyyah kutokana na ukweli uliojulikana kwamba alikuwa ni mkweli. Vile vile imesemekana kwamba amepewa cheo hicho kwa sababu alikuwa daima yuko tayari kumwamini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   katika kila jambo alilosema."

 

Baadhi ya matukio yaliyodhihirisha ukweli wake Abu Bakr Asw-Swiddiyq na wepesi wake wa kuamini lolote alilosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na sifa zake nyenginezo:

 

 

 1-Katika kisa cha Israa Wal-Mi'raaj alipobakia thabiti na kuwaambia makafiri kwamba ikiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  mwenyewe ametamka maelezo hayo ya safari ya Israa wal Mi’raaj basi ni kweli!

 

Ibn Kathiyr amesema: "Al-Hasan Al-Baswriy na Qataadah wamesema: Alijulikana kwa mara ya kwanza kwa cheo hiki asubuhi ya siku ya tukio la Israa." Al-Haakim amesimulia kutoka kwa 'Aishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye amesema: “Washirikina walikuja kwa Abubakar wakamwambia:  Umemsikia rafiki yako anavyodai? Anadai kwamba amesafiri kwenda Baytul-Maqdis kwa usiku mmoja! Akauliza: Je, amesema mwenyewe hivyo?" Wakajibu: "Ndio." Akasema: "Basi amesema ukweli! Naamini ukweli wake katika mambo yaliyo ya ajabu zaidi kuliko hayo, kama habari kutoka mbinguni asubuhi na jioni.”  (yaani wahyi wa Qur-aan). Tokea hapo Abubakar akapewa cheo na sifa ya Asw-Swiddiyq.  [Ibn Kathiyr kasema Isnaad yake ni nzuri].

 

Al-Haakim amesimulia kutoka Nazaal ibn Swabrah ambaye amesema: "Tulimwambia 'Aliy: "Ee kamanda wa Waumini! Tuelezee kuhusu Abubakar.” Akasema: "Ni mtu aliyepewa jina la Asw-Swiddiyq na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kauli ya Jibriyl  ('Alayhis-Salaam)   na kauli ya Muhammad  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Alikuwa ni Khalifa wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Yeye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliridhika naye katika Dini yetu na aliridhika naye katika mambo yetu ya kidunia." [Ibn Kathiyr kasema: Isnaad yake ni nzuri]

 

Na katika vita vya Uhud, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  aliliambia (kwa kulipapasa) jabali  la Uhud lilipotikisika:

 

((أثبت أحد فإنما عليك نبي وصديق وشهيدان))

((Tulia kwani juu yako yumo Nabiy, Asw-Swiddiyq na Mashuhadaa wawili)) (yaani Umar na Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa)) [Al-Bukhaariy]

 

 

2-Kisa maarufu cha kuhama kwake (Hijrah) pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa ameacha familia yake ili abakie na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Maswahaba wote waliruhusiwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhama (Hijrah kutoka Makkah kwenda Madiynah) isipokuwa Abubakar. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwambia abakie ili awe swahibu yake katika Hijrah na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akatimiza pendekezo la Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Katika msafara wa hijrah makafiri walimtafuta Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutaka kumuua wakakimbilia katika pango la At-Thawr. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameteremsha kauli Yake: 

 

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا ۗوَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٤٠﴾

Msipomnusuru (Rasuli), basi Allaah Amekwishamnusuru, pale walipomtoa (Makkah) wale waliokufuru akiwa wa pili katika wawili; walipokuwa katika pango, alipomwambia swahibu yake: “Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi.” Basi Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na Akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona, na Akajaalia neno la waliokufuru kuwa chini. Na Neno la Allaah kuwa ndilo lililo juu. Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah: 40]

 

 

3- Alipolia wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  alisema: ((Hakika kuna mja alipewa uchaguzi na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  baina ya Duniya na Aakhirah, mja akachagua Aakhirah)). Abubakar alijua kuwa huyo mja ni Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alitambua kauli hiyo imemaanisha kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  ataaga duniya karibuni. [Al-Bukhaariy]

 

 

 

4- Alipobakia kuwa thabiti katika kifo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati Maswahaba waliduwaa hawakujua la kufanya, akatoa khutbah ya kuwatuliza.

 

 

 

5- Kuthibitika kwake ingawa alikuwa pekee katika kupeleka jeshi na       kumfanya Usaamah bin Zayd awe mwenye kuongoza jeshi.

 

 

 

6- Kung'angania kwake katika kupigana na watu waliotoka nje ya Uislam baada ya kifo cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

7- Alipomchagua 'Umar ibnil-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Khaliyfah wa      Waislam, jambo ambalo limeainishwa na ‘Ulamaa kuwa ni jambo muhimu la mafanikio.

 

 

 

Share